Saturday 31 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

EMIRATES CUP: Yaanza leo!
Celtic 2 Lyon 2
Arsenal 1 AC Milan 1
Lile Kombe la Emirates ambalo huchezwa kila Mwaka Uwanja wa Emirates, nyumbani kwa Arsenal, kabla Msimu haujaanza ili kuzipa mazoezi Timu shiriki, leo limeanza kushindaniwa na Timu 4.
Katika Mechi ya kwanza Celtic ya Scotland ilitoka sare 2-2 na Lyon ya Ufaransa.
Lyon ndio walikuwa wa kwanza kupata mabao yao kupitia Michel Bastos dakika ya 28 na kwenye dakika ya 54 Harru Novillo akapachika bao la pili.
Celtic wakajitutumua na kupata bao la kwanza dakika ya 82 Mfungaji akiwa Gary Cooper na dakika ya 89 Georgios Samaras akasawazisha.
Wenyeji Arsenal walitinga kupambana na AC Milan katika Mechi ya pili na Mchezaji mpya Marouane Chamakh ndie aliefunga bao lao lakini Straika hatari wa AC Milan Alesandro Pato akasawazisha.
Kesho Jumapili Agosti 1, AC Milan v Lyon na Arsenal v Celtic.
Chicharito namba ipo Man United!
Javier Hernandez, maarufu Chicharito, ambae alijiunga Manchester United akitokea Klabu ya Mexico, Deportivo Chivas Guadalajara kabla ya Fainali za Kombe la Dunia kuanza, alidhaniwa kuwa amekwenda Old Trafford kujaza idadi tu lakini Soka lake kwenye Kombe la Dunia na kiwango chake kwenye Mechi mbili alizocheza Man United kimeonyesha atapata namba kwenye Kikosi cha Kwanza.
Hilo limeungwa mkono na Sir Alex Ferguson ambae amesema: “Amecheza na Timu pinzani ngumu na ameonyesha kiwango cha juu. Anamudu vizuri kukontroli mpira na kuumiliki na hivyo ni vitu muhimu kwenye Ligi Kuu.”
Mafowadi wanaogombea namba huko Man United ni Rooney, Berbatov, Hernandez, Michael Owen, Mame Biram Diouf, Federico Macheda na Danny Welbeck.
Lakini Welbeck yuko mbioni kujiunga na Sunderland kwa mkopo.
Mido kuikomoa Boro!
Inadaiwa Mchezaji kutoka Misri Mido amekasirishwa na Klabu yake Middlesbrough kuikataa ofa ya Pauni Milioni 2 ili ahamie Ajax huko Uholanzi waking’ang’ania walipwe zaidi.
Mido, ambae alihamia Boro 2007 akitokea Tottenham, amedaiwa kusema yuko tayari kubakia hapo Boro kwa Miezi 12 iliyobaki kwenye Mkataba wake bila kuchezeshwa na kisha aondoke kama Mchezaji huru na hivyo kuikosesha Boro ada ya uhamisho.
Mido, Miaka 27, anaelipwa Mshahara wa Pauni 40,000 kwa Wiki, amedai: “Siondoki mpaka ofa nzuri ipatikane na siondoki mpaka wanilipe bonasi zangu ninazostahili! Hii si mara ya kwanza kukataa kunilipa!”
Mido pia amekasirishwa na kitendo cha Kocha Gordon Strachan kumuacha kwenye ziara ya Ireland na Ujerumani kwa madai hayuko fiti na ikabidi abaki Klabuni afanye mazoezi zaidi.
CAS yaruhusu Wachezaji wa Northern Ireland kuchezea Republic of Ireland
CAS [Court of Arbitration for Sport], Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, imetupilia mbali Rufaa ya Chama cha Soka cha Northern Ireland iliyodai kuwa Republic of Ireland ‘ilimteka’ Fowadi Chipukizi Daniel Kearns.
Kearns, Miaka 18, alizaliwa Belfast, Northern Ireland na akaichezea Nchi hiyo kwenye michuano ya Kimataifa ya Vijana lakini akahamia kuichezea Republic of Ireland [Mji Mkuu ni Dublin] mwanzoni mwa Mwaka huu na hilo limewakera Northern Ireland na wakakata Rufaa FIFA ambao waliibwaga Rufaa hiyo na kumruhusu Kearns kuchagua Nchi ya kuchezea kwa vile amezaliwa Visiwa vya Ireland vyenye Nchi hizo mbili.
Ndipo Northern Ireland wakakata Rufaa CAS ambako nako wamebwagwa.
Ingawa Northern Ireland imesikitishwa na uamuzi huo lakini wameukubali kwa shingo upande.
Wachezaji wengi wa Northern Ireland huamua kuichezea Republic of Ireland na mfano ni Darron Gibson wa Manchester United ambae Wazazi wake walizaliwa Northern Ireland lakini yeye ameamua kuichezea Republic of Ireland.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Chicharito aifunga Man United!!!
Katika mechi iliyochezwa Alfajiri ya leo Jumamosi, Julai 31 kwenye ufunguzi wa Uwanja mpya wa Club Deportivo Guadalajara, Klabu ya zamani ya Mchezaji mpya wa Manchester United, Javier Hernandez aka Chicharito, Estadio Omnilife, Mexico, Chicharito alicheza Kipindi cha kwanza akiwa Klabu hiyo ya Mexico na kufunga bao la kwanza dakika ya 8 na Kipindi cha pili akavaa jezi ya Man United na kucheza kwa Robo Saa.
Kila ‘Chicha’ alipopata mpira alikuwa akishangiliwa Uwanja mzima.
Katika mechi hiyo Club Deportivo Guadalajara ilishinda bao 3-2.
Mabao mengine ya Club Deportivo Guadalajara yalifungwa na Bautista dakika ya 38 na Hector Reguoso dakika ya 58.
Mabao ya Man United yalifungwa na Chris Smalling dakika ya 10 na Nani dakika ya 80.
Kikosi cha Man United kilikuwa:
Kuszczak; De Laet (Rafael 65), Smalling, O’Shea, Fabio; Gibson (Nani 46), Scholes (Giggs 65), C.Evans (Fletcher 75), Cleverley; Berbatov (Hernandez 46, Welbeck 65), Diouf (Macheda 65
Wenger: ‘Sheria mpya Wachezaji 25 itavuruga Soka!”
Ingawa Sheria mpya ya kusajili Wachezaji 25 tu na kati yao 8 wawe ‘wamelelewa’ katika Klabu za ama England au Wales kwa Miaka mitatu kabla hawajafikisha umri wa Miaka 21, haiwaathiri sana Arsenal, Meneja wao Arsene Wenger ameiponda kuwa Sheria hiyo itakayoanza kutumika Msimu huu mpya wa 2010/11 kuwa itavuruga Soka.
Licha ya Arsenal kuwa na lundo la Wachezaji ambao ni Wageni, yaani si Raia wa England kama vile Nahodha Cesc Fabregas, Denilson, Gael Clichy, Nicklas Bendtner na Alex Song, lakini hao pamoja na Waingereza Theo Walcott, Jack Wilshere, Aaron Ramsey na Kieran Gibbs, kwenye Sheria hiyo mpya wanafuzu kama Wachezaji ‘waliolelewa’ nyumbani kwa vile walianza kuichezea Arsenal tangu wadogo.
Wenger amedai: “Mie si Shabiki wa Sheria hiyo. Kwanza itawafanya Wachezaji wengi kukosa Klabu! Pili, Klabu zitadhoofika kwenye Soko la Uhamisho wa Wachezaji kwani ukiwa na Wachezaji 25 na ukanunua mmoja unajua sasa una 26 na ni lazima uuze mmoja!”
Wadau wamedai kuwa Wachezaji wengi walio na Miaka 21 na zaidi na ambao hawakuwepo England au Wales kwa Miaka mitatu kabla hawajafikisha umri wa Miaka 21, watajikuta wakipigwa shoka na kukosa Klabu huko England.

Friday 30 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Wenger awania Sentahafu
Baada ya kuwapoteza Masentahafu Sol Campbell, William Gallas, Mikael Silvestre na Sendoros, Arsenal imebakiwa na Masentahafu watatu tu na hilo limemfanya Bosi wa Arsenal Arsene Wenger kusaka Beki mmoja mpya.
Masentahafu waliobaki Arsenal ni Thomas Vermaelen, Mchezaji mpya Laurent Koscielny na Johan Djourou.
Wenger ametamka: “Tunasaka Mabeki wapya kwani tunahitaji tuwe na jumla ya Masentahafu watano. Inabidi tumpate mmoja kwa sababu tunao Wachezaji wanaoweza kucheza kwa dharura kama Sentahafu. Wapo tunaowalenga lakini kwa sasa siwezi kusema ni nani.”
Ufaransa Bingwa Ulaya Chini ya Miaka 19
Timu ya Taifa ya Ufaransa Chini ya Miaka 19 leo imewafunga Spain 2-1 na kutwaa Ubingwa wa Ulaya katika Fainali iliyochezwa Stade Michele d’Ornano Mjini Caen, Kaskazini ya Ufaransa.
Hadi mapumziko, Ufaransa ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 kwa bao la Rodrigo.
Kipindi cha pili, Ufaransa iligeuka mbogo na kusawazisha dakika ya 49 kupitia Sunu na Alexandre Lacazette akafunga bao la ushindi dakika ya 85.
CHEKI: www.sokainbongo.com

David James ahamia Bristol City
Bristol City imefanikiwa kumsaini Kipa Mkongwe David James aliekuwa Portsmouth kwa Mkataba wa Mwaka mmoja huku kukiwa na kipengele cha nyongeza ya Mwaka mmoja.
David James, anaekaribia Miaka 40, ataanza kuichezea Bistola City, iliyo Daraja la Coca Cola Championship, Agosti moja.
James alikuwa pia akitakiwa na Klabu za Celic ya Scotland na Sunderland lakini alishindwa kufikia makubaliano na Klabu hizo.
David James amewahi kuwa Kipa katika Klabu za Liverpool, Aston Villa, West Ham na Manchester City.
Fergie adai zigo kwa Rooney litatuliwa na ‘Chicha’ na Macheda
Sir Alex Ferguson, Bosi wa Manchester United, amedai hana wasiwasi na Javier Hernandez, maarufu kama Chicharito, na Federico Macheda, kwa sababu Wachezaji hao ndio watakaosaidia sana Msimu ujao kumpunguzia mzigo wa kuibeba Timu Wayne Rooney ambao ulimwelemea Msimu uliopita.
Chicharito na Macheda walifunga mabao matamu katika mechi ya Jumatano Man United ilipoinyuka MLS All Stars 5-2 huko Houston, Marekani.
Chicharito alikuwa akicheza Mechi yake ya kwanza kwa Man United.
Ferguson pia alitoboa kuwa wanafikiria kuwatoa Washambuliaji wengine Chipukizi, Danny Welbeck na Mame Biram Diouf, kwa mkopo ili wapate uzoefu.
Ferguson alisema licha ya Chicharito na Macheda kuwa na vipaji pia wana sifa muhimu ya kuwa na nia na ari wakiwa Uwanjani na vitu hivyo ndivyo vimewafanya wawepo Man United.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Redknapp aponda upangaji Ratiba
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amelaumu jinsi Ratiba ya Msimu mpya ilivyopangwa na kuwepo kwa mechi za kirafiki kwa Timu za Taifa siku chache kabla Msimu haujaanza.
Tottenham jana ilifungwa na Villareal 4-1 na Jumanne ijayo itacheza na Benfica kisha Fiorentina Agosti 7 zote zikiwa mechi za kujipima nguvu.
Baada ya hapo, Tottenham itawakosa Wachezaji wengi watakaokuwa na Timu za Taifa huku England ikipangiwa kucheza na Hungary Agosti 11.
Tottenham itacheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England Agosti 14 kwa kupambana na Manchester City na kati ya Agosti 17 na 18 itacheza Mechi ya Kwanza ya Raundi ya Mchujo ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Redknapp alisema: “Huu ni wehu! Tumelundika mechi nyingi! Tunachohitaji ni kufanya mazoezi tu lakini sasa hamna ni mechi baada ya mechi na Wachezaji hupumzika kidogo tu na kucheza mechi nyingine bila mazoezi mazuri!”
Meneja huyo wa Tottenham akaongeza: “Kuna sababu gani kucheza Mechi ya Kimataifa kabla Msimu haujaanza? Hawa walikuwa pamoja Kombe la Dunia na sasa wiki nzima ntawakosa wako Timu ya Taifa na wanarudi Ijumaa na Jumamosi tunacheza na Man City! Hii si sawa!”
Real yamsaini Khedira
Klabu ya Bundesliga Sttugart imethibitisha Mchezaji wao Kiungo Sami Khedira anahamia Real Madrid baada kukubaliana ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 14.
Khedira, Miaka 23, ameshakubaliana maslahi binafsi na Real na atapimwa afya yake na kukamilisha kusaini Mkataba wa Miaka mitano.
CHEKI: www.sokainbongo.com

EUROPA LIGI: Ngog aibeba Liverpool!
Bao mbili za David Ngog zimewapa Liverpool ushindi wa ugenini wa 2-0 dhidi ya Rabotnicki ya Macedonia katika mechi ya kwanza ya Raundi ya 3 ya Mtoano wa EUROPA LIGI iliyochezwa usiku Alhamisi Julai 29.
Liverpool ilicheza bila Mastaa wao ambao walipewa likizo ndefu kidogo baada ya sulubu za Kombe la Dunia.
Timu hizi zitarudiana Anfield Agosti 5.
Timu:
Rabotnicki: Bogatinov, Belica, Sekulovski, Dimovski, Todorovski, Gligorov, Tuneski, Fernando Lopes, Ze Carlos, Da Silva, Wandeir.
Akiba: Kandikijan, Marcio, Mojsov, Adem, Roberto Carlos, Petkovski, Sinkovic.
Liverpool: Cavalieri, Kelly, Kyrgiakos, Skrtel, Agger, Spearing, Aquilani, Lucas, Jovanovic, Ngog, Amoo.
Akiba: Gulacsi, Darby, Shelvey, Dalla Valle, Eccleston, Ayala, Ince.

Thursday 29 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Robinho kurudi Man City
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amesema Robinho atarudi tena Klabuni hapo hivi karibuni baada ya kumalizika Mkataba wake wa mkopo na Santos ya huko kwao Brazil.
Mancini amesema yeye hana tatizo kumkaribisha tena Robinho ambae alilazimisha kurudi kwao Brazil kwa vile hakuwa na furaha hapo Manchester.
Baada ya kurudi Santos, Robinho aliibuka na fomu mpya na pia kung’ara na Brazil huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia.
Anelka alishitaki Gazeti kwa kumdhalilisha
Nikolas Anelka, ambae alitimuliwa toka Kikosi cha Ufaransa huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia, yuko mbioni kufungua mashitaka kwa Gazeti la kila siku la huko Ufaransa la Michezo, L’Equipe, kwa kumchafulia jina katika stori ya Gazeti kuwa alimtukana aliekuwa Meneja wa Ufarnasa Raymond Domenech.
Ingawa Anelka hajakana kuwa alimtukana Domenech wakati wa hafutaimu wa Mechi ya Kombe la Dunia Juni 17 dhidi ya Mexico, amedai kuwa GAzeti L’Equipe limepotosha maneno yake.
Wachezaji wengine wa Ufaransa waliokuwa huko Afrika Kusini wakati wa sakata la Anelka, akiwemo Thierry Henry, wamedai L’Equipe limetia chumvi mno.
Hata hivyo Gazeti hilo linadai stori yao ni sahihi
CHEKI: www.sokainbongo.com

WATAHAMA, HAWAHAMI?
1. Fernando Torres
Ingawa fomu yake imeshuka kwa muda sasa, Torres anaendelea kuhusishwa na kuihama Liverpool huku Chelsea na Manchester City zikitajwa kama Timu ambazo atajiunga nazo.
Lakini Meneja wa Liverpool, Roy Hodgson, amepuuza habari hizo na kudai Torres anabaki Liverpool.
2. Cesc Fabregas
Bado kuna mvutano kati ya Barcelona na Arsenal kuhusu Nahodha huyu wa Arsenal.
Barcelona walishatoa ofa ya Pauni Milioni 29 na ikakataliwa na Ze Gunners na sasa Arsenal haitaki kuzungumza lolote kuhusu Fabregas ambae mwenyewe alishaonyesha nia ya kurudi Barca ambako ndiko alikoanzia Soka.
3. Javier Mascherano
Kiungo huyu kutoka Argentina ameshatamka bayana anataka kuihama Liverpool.
Mascherano anataka aende Inter Milan ili aungane tena na Meneja Rafael Benitez.
4. Mario Balotelli
Kuna kila dalili Supa Mario yuko mbioni kujiunga na Manchester City.
Kocha wa Man City, Roberto Mancini, anamtaka Chipukizi huyu kutoka Italia Klabu ya Inter Milan kwa udi na uvumba.
5. James Milner
Kuna mvutano wa dau la uhamisho kutoka Aston Villa kwenda Manchester City kwa Kiungo huyu Mwenye Miaka 24 huku Man City wakitoa ofa ya Pauni Milioni 24 lakini Villa wanataka Milioni 30.
6. Luis Suarez
Tottenham ndio wameonyesha nia ya kumchota mbaya huyu wa Ghana kutoka Uruguay ambae alisababisha Ghana itolewe Kombe la Dunia huko Afrika Kusini alipodaka mpira na kuwanyima Ghana bao la wazi.
Klabu yake Ajax Amsterdam ya Uholanzi inasemekana inataka Pauni Milioni 30.
7. Ricardo Carvalho
Beki huyu Mkongwe toka Ureno anataka kwenda Real Madrid ili kuungana tena na Meneja wake wa zamani huko Porto na Chelsea, Jose Mourinho.
8. Rafael van Der Vaart
Kiungo huyu wa Uholanzi hana namba ya kudumu huko Real Madrid na hilo limemfanya atake kuhama na Klabu za Liverpool na Chelsea ndizo zinamwania.
9. Mesut Ozil
Ni mmoja wa Wachezaji waliong’ara mno huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani na kuna msululu wa Klabu zinazodaiwa kumwania ingawa Tottenham ndio ipo mbele. Nyingine ni Arsenal, Manchester United na Real Madrid.
Klabu yake Werder Bremen inataka Pauni Milioni 15.
10. Sami Khedira
Kiungo huyu wa Ujerumani ni Mchezaji mwingine aliewika huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia na Real Madrid ndio wanaotegemewa sana kumnasa kwa uhamisho wa Pauni Milioni 15.
UEFA CHAMPIONS LIGI: Raundi ya 3 Mtoano
MATOKEO Mechi za Jumatano Julai 28
Aktobe [Kazakstan] 1 Hapoel Tel-Aviv FC [Israel] 0
FC BATE Borisov [Belarus] 0 FC Kobenhavn [Denmark] 0
FC Sheriff Tiraspol [Moldova] 1 NK Dinamo Zagreb [Croatia] 1
Debreceni VSC [Hungary] 0 FC Basel 1893 [Switzerland] 2
BSC Young Boys [Switzerland] 2 Fenerbahce [Turkey] 2
AIK Solna [Sweden] 0 Rosenborg BK [Norway] 1
FK Partizan [Serbia] 3 HJK Helsinki [Finland] 0
Ajax Amsterdam [Netherlands] 1 PAOK FC [Greece] 1
Braga Sporting [Portugal] 3 Celtic [Scotland] 0
CHEKI: www.sokainbongo.com


Man United 5 MLS All Stars 2
• Chicharito acheza mara ya kwanza na kufunga!
Mchezaji mpya wa Manchester United kutoka Mexico, Javier Hernandez aka Chicharito, jana alicheza mechi yake ya kwanza na kumudu kufunga bao katika ushindi wa 5-2 wa Man United dhidi ya MLS All Stars ambayo ni Kombaini ya Wachezaji wa Ligi ya huko Marekani MLS.
Mechi hiyo ilichezwa mbele ya Mashabiki 71,000 Uwanjani Reliant, Houston.
Macheda ndie alieipatia Man United bao la kwanza sekunde ya 22 tu baada ya kuinasa pasi ya Beki Kevin Alston kwa Kipa wake.
Macheda aliongeza bao la pili kwa kichwa kufuatia kona ya Nani.
Dakika ya 63, MLS All Stars walipata bao kupitia Brian Ching lakini Man United wakaongeza bao mbili Wafungaji wakiwa Darron Gibson na Cleverly.
Chichariti alifunga bao lake la kwanza kwa Man United dakika ya 84 baada ya pande tamu la Fletcher.
MLS All Stars walipata bao lao la pili dakika ya 90 Mfungaji akiwa De Rosario.
Vikosi:
Manchester United: Van der Sar; Rafael, Brown, J Evans, Fábio (Scholes, 72); O'Shea; Obertan (Cleverley, 23), Fletcher, Giggs (Gibson, 52), Nani (Hernández, 62); Macheda (Welbeck, 62).
MLS All-Stars: Ricketts (Rimando); Alston (De Rosario,), Olave (Gonzalez, ht), Marshall (Conde, 63), Pearce (Donovan, 74); Joseph (Davis, 74); Le Toux (Convey,), Morales (Moreno, 63), Schelotto (Ferreira,), Pappa (Larentowicz,); Angel (Ching,).
Maradona alaumu usaliti!
Baada ya kukosa kuendelea kuwa Kocha wa Argentina, Diego Maradona, ameilaumu AFA, Chama cha Soka cha Argentina, kwa kusema uongo na kuwa wasaliti.
Maradona pia alimlaumu Meneja wa Timu ya Brazil, Carlos Bilardo, kwa kula njama yeye asipewe Ukocha Argentina.
Maradona aligoma kutii amri ya AFA ya kumtaka awaache baadhi ya Wasaidizi wake ikiwa atataka Mkataba mpya na hivyo AFA ililazimika kumtema.
Pia Maradona amedai Rais wa AFA, Grondona alimdangaya.
Kocha wa Timu ya Taifa ya Vijana wa Chini ya Miaka 20, Sergio Batista, ndie ameteuliwa kuwa Kocha wa Muda wa Argentina.
Fulham kumtangaza Mark Hughes Meneja mpya
Fulham inategemewa kumtangaza Mark Hughes kuwa Meneja mpya ndani ya Masaa 48 yajayo kuchukua nafasi ya Roy Hodgson aliehamia Liverpool.
Mark Hughes alitimuliwa kutoka Manchester City Desemba 2009 na kabla aliwahi kuwa Meneja wa Blackburn Rovers na Timu ya Taifa ya Wales.
Serie A kuanza Agosti 28
Mabingwa Watetezi wa Serie A huko Italia, Inter Milan, ambao pia ni Mabingwa wa Ulaya, wataanza kampeni yao ya utetezi wa Ubingwa wao kwa mechi ugenini dhidi ya Bologna.
Mechi za Wikendi ya Agosti 28 na 29:
Bari v Juventus
Chievo v Catania
Milan v Lecce
Parma v Brescia
Roma v Cesena
Sampdoria v Lazio
Uudinese v Genoa
Palermo v Cagliari
Bologna v Inter
Fiorentina v Napoli

Wednesday 28 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Liverpool kuanza EUROPA LIGI bila Mastaa
Roy Hodgson ameruka na Kikosi chake cha Liverpool kwenda Macedonia kupambana na FK Rabotnicki kwenye mechi ya kwanza ya Raundi ya 3 ya Mtoano wa EUROPA LIGI hapo kesho bila Mastaa wake wakubwa kama Nahodha Steven Gerrard, Jamie Carragher na Mchezaji mpya Joe Cole ambao wote walikuwa Timu ya England kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na ambao ndio kwanza wamerudi mazoezini baada ya kupewa muda zaidi kupumzika.
Kikosi cha Liverpool cha Wachezaji 20 kilichosafiri kina Chipukizi kina Jonjo Shelvey, Nathan Eccleston, Martin Hansen, Peter Gulacsi, David Amoo, Lauri Dalla Valle na Tom Ince.
Wachezaji wazoefu waliokuwemo ni Martin Skrtel, Daniel Agger, Sotirios Kyrgiakos, pamoja na Wachezaji wapya Milan Jovanovic na Danny Wilson.
Kikosi kamili ni: Cavalieri, Aquilani, Agger, Jovanovic, Kyrgiakos, Lucas, Wilson, Ngog, Spearing, Darby, Shelvey, Kelly, Skrtel, Eccleston, Ayala, Hansen, Gulacsi, Amoo, Dalla Valle, Ince
Drogba si biashara!
Mkurugenzi Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay, ameufuta uvumi kuwa Didier Drogba anahama Stamford Bridge kufuatia kauli ya Wakala wake, Thierno Seydi, kudai Drogba huenda akatua Manchester City.
Gourlay amesema Drogba, mwenye Miaka 32 na mwenye Mkataba na Chelsea hadi 2012, atabakia hapo Msimu huu na kwamba wao wamezoea wakati kama huu kila Msimu kusikia kuhama kwa Mastaa wao.
Bosi huyo wa Chelsea, ambayo tayari imechukua Wachezaji wapya wawili, Yossi Benayoun toka Liverpool na Tomas Kalas, amesema Meneja wao Carlo Ancelotti yuko huru kuongeza Wachezaji akihitaji.
Raul atua Bendsliga na Schalke 04
Mkongwe na Staa wa Real Madrid ambae ameondoka Klabu hiyo ya Spain amesaini Mkataba wa Miaka miwili na Klabu ya Ujerumani Schalke 04.
Raul alidumu Real kwa Miaka 18 na kuchezea mechi 741 na kufunga magoli 323.
CHEKI: www.sokainbongo.com


Maradona baibai Argentina
Chama cha Soka cha Argentina, AFA, kimetamka hakitaongeza Mkataba kwa Diego Maradona kuendelea kuwa Kocha wao ingawa walitaka aendelee lakini kukawa na kutokubaliana kuhusu kuwepo kwa baadhi ya Wasaidizi wa Maradona.
Maradona alikiri kuwa yuko tayari kuendelea kama Kocha lakini hakutaka kuwabadilisha baadhi ya Wasaidizi wake ambao AFA ilikuwa haiwataki.
Rais wa AFA, Julio Grondona, ametamka: “Ili kuwa ngumu kukubaliana kuhusu kuondolewa kwa Wasaidizi wake.”
Argentina sasa itakuwa chini ya Kocha wa muda, Batista, ambae kazi yake ya kwanza itakuwa kuisimamia Nchi hiyo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Ireland hapo Agosti 11 huko Dublin, Ireland.
El Chicharito angojewa kushangiliwa na Jamii ya Kimexico Houston!!!
Javier Hernandez, Miaka 22, leo anategemewa kucheza mechi yake ya kwanza kwa Klabu yake mpya Manchester United huko Houston, Marekani dhidi ya Kombaini ya Mastaa wa MLS, Ligi ya Marekani, Jijini Houston ambako kuna Watu wa asili ya Mexico wengi sana na wenye hamu ya kumuona Staa wao alieifungia Mexico bao 2 huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Hernandez, aka ‘El Chicharito’ yaani njegere ndogo, amejiunga na Man United kutoka Klabu ya Mexico Chivas Guadalajara.
Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson, amesema wataangalia kama Hernandez yuko fiti kwa vile alijiunga jana tu na Kikosi chake akitokea likizo lakini huenda akacheza kidogo kwenye mechi hiyo na Mastaa wa MLS kwa vile Wamexico wengi wanataka kumuona.
Baba Mzazi na Babu yake Hernandez walikuwa Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mexico na jina la ‘El Chicharito’ limetokana na jina la utani la Baba yake aliekuwa akiitwa ‘El Chicharo’ yaani njegere.
Wenger: “Fabregas hauzwi, Barca ni wapiga kelele tu!”
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema Arsenal haina nia ya kumuuza Nahodha wao Cesc Fabregas licha ya Barcelona kuonyesha nia ya kumtaka.
Barcelona walitoa ofa ya Pauni Milioni 29 lakini Arsenal wakaikataa na baada ya hapo Arsenal wamekataa kabisa kufanya mazungumzo na Barcelona.
Wenger amesisitiza msimamo wa Arsenal kwa kusema: “Hizo ni kelele zao, sisi hatuna nia kumuuza! Yeye ni Mchezaji muhimu kwetu na ni Kepteni wetu.”
Fabregas, Miaka23, alijiunga na Arsenal akiwa na Miaka 16 tu Mwaka 2003 akitokea Barcelona na mpaka sasa ameshaichezea Arsenal Mechi 267 na kufunga mabao 48.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Barca imo kwenye lindi la Deni kubwa!!!
Ukaguzi mpya wa Mahesabu wa Mabingwa wa Spain, FC Barcelona, umefichua kuwa Klabu hiyo ipo kwenye Deni kubwa la Pauni Milioni 369.5 na sio Pauni Milioni 11 kama ilivyotangazwa awali na pia Mahesabu hayo yameonyesha Barca imepata hasara ya Pauni Milioni 64 Msimu uliokwisha.
Hivi karibuni, Barcelona ilibidi ikope Pauni Milioni 125 baada ya kushindwa kulipa Mishahara ya Wachezaji ya Mwezi Juni.
Barca wagomewa na Ze Gunners!!!
Msemaji wa Barcelona, Toni Freixa, amesema kuwa mpaka sasa Arsenal hawataki kujadiliana na wao kuhusu kumuuza Cesc Fabregas kwao.
Barcelona walitoa ofa ya Pauni Milioni 29 kumnunua Fabregas Mwezi Juni lakini Arsenal wakaikataa na baada ya hapo kila walipojaribu kuanzisha mazungumzo Arsenal wamegoma kusikiliza chochote.
Freixa ametamka: “Arsenal hawataki kukaa chini na sisi! Tatizo sio sisi au Fabregas, tatizo hawataki kuongea lolote!”
Fabregas bado ana Mkataba wa Miaka mitano na Arsenal ingawa ameshatamka anataka kuichezea Barcelona Klabu ambayo alianzia Soka akiwa mtoto.
Licha ya Klabu yenyewe Barca kujaribu kumrubuni Fabregas, Wachezaji wa Barca ambao Fabregas hucheza nao Timu ya Taifa ya Spain, kina Andres Iniesta, Xavi na David Villa, wamenukuliwa wakimshawishi Fabregas aondoke Ze Gunners na kwenda Barca.
Hata hivyo, licha ya mazungumzo kati ya Barca na Arsenal kukwama hakuna anaejua Barcelona watamudu vipi kumnunua Fabregas hasa ukizingatia hali yao ya kifedha hivi sasa.

Tuesday 27 July 2010

CHEKI: www.sokaingongo.com

Campbell kutua Newcastle
Mkongwe Sol Campbell huenda akasaini na Newcastle ikiwa leo atafaulu upimaji wake wa afya baada ya Mkataba wake na Arsenal kumalizika.
Campbell, Miaka 35, alikuwa bado anatakiwa na Arsenal na pia Klabu za Sunderland na Celtic lakini chaguo lake mwenyewe ni Newcastle Timu iliyopanda Daraja Msimu huu baada ya kuporomoka kutoka Ligi Kuu Msimu wa 2008/9.
Ikiwa usajili wa Campbell utakamilika, yeye atakuwa Mchezaji wa tatu kwa Meneja wa Newcastle, Chris Hughton, kusajili kwa ajili ya Msimu mpya, wengine wakiwa ni Dan Gosling kutoka Everton na James Perch toka Nottingham Forest.
Brazil yawaita Rafael na Lucas
Beki wa Manchester United Rafael da Silva nam Kiungo wa Liverpool Lucas Leiva wameitwa kwenye kikosi cha Brazil kitakachocheza Mechi ya kirafiki na USA hapo Agosti 10.
Kikosi hicho cha Brazil ndio uteuzi wa kwanza wa Meneja mpya wa Brazil, Mano Menezes, na Rafael na Lucas ni Wachezaji pekee kutoka Ligi Kuu England.
Menezes amewachukua Wachezaji wanne tu toka Kikosi cha Brazil kilichocheza Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ambao ni Dani Alves, Ramires, Thiago Silva na Robinho.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rafael kuitwa kuichezea Brazil lakini Lucas itakuwa mara yake ya tatu.
Wachezaji 11 kati ya 24 waliotajwa na Menezes kwa ajili ya Mechi hiyo na USA itakayochezwa New Jersey, Marekani, ni wapya kwa Brazil.
Kikosi kamili ni:
Makipa: Jefferson (Botafogo), Renan (Avai), Victor (Gremio) Mabeki: Andre Santos (Fenerbahce), Dani Alves (Barcelona), Marcelo (Real Madrid), Rafael da Silva (Manchester United), David Luis (Benfica), Henrique (Racing Santander), Rever (Atletico Mineiro), Thiago Silva (AC Milan)
Viungo: Carlos Eduardo (Hoffenheim), Ederson (Lyon), Paulo Henrique Ganso (Santos), Hernanes (Sao Paulo), Jucilei (Corinthians), Lucas Leiva (Liverpool), Ramires (Benfica), Sandro (Internacional)
Mafowadi: Alexandre Pato (AC Milan), Andre (Santos), Diego Tardelli (Atletico Mineiro), Neymar (Santos), Robinho (Santos, on loan from Manchester City)
Hodgson: “Mascherano anataka kuhama Liverpool!”
Meneja wa Liverpool, Roy Hodgson, amethibitisha kuwa Javier Mascherano anataka kuhama lakini amethibitisha Fernando Torres atabaki.
Mascherano, Miaka 26, amehusishwa sana na kuhamia Inter Milan ili kuungana tena na aliekuwa Meneja wa Liverpool, Rafael Benitez, ambae ndie Kocha mpya wa Klabu hiyo ya Italia.
Hodgson amesema: “Ndio anataka kuondoka. Alitaka kuhama tangu Msimu uliokwisha. Lakini bado ana Mkataba na Liverpool hivyo uamuzi wa kuhama ni wetu na si yeye.”
Kuhusu Torres, Hodgson amesema bado yuko likizo na atajiunga na Liverpool Jumatatu ijayo lakini atabakia hapo kwa vile bado anaifurahia Anfield.

Monday 26 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Man City mbioni kumnasa Supa Mario
Kuna taarifa, ingawa zimepingwa na Wakala, kwamba Mchezaji wa Inter Milan, Mario Balotelli, Miaka 19, yuko mbioni kuungana tena na Roberto Mancini, Kocha ambae ndie aliemwinua na kumwingiza Inter Milan bado akiwa Kinda Mwaka 2006 wakati Mancini akiwa ndie Meneja wa Inter.
Mancini amesema wana nia ya kumchukua Balotelli lakini hawako tayari kulipa dau kubwa kuliko thamani ya Mchezaji huyo.
Tayari Man City imeshawachukua kwa ajili ya Msimu mpya Jerome Boateng, Aleksandar Kolarov, Yaya Toure na David Silva.
Mascherano arudi mazoezini Liverpool
Huku akivumishwa yuko njiani kwenda kujiunga na Meneja wa zamani wa Liverpool, Rafael Benitez, huko Inter Milan, Kiungo Javier Mascherano amerudi Liverpool na kujiunga na wenzake mazoezini kwa ajili ya Msimu mpya ambao kwa Liverpool unaanza mapema mno kwa Mechi ya Mtoano ya EUROPA LIGI ambako Alhamisi Julai 29 watacheza na Rabotnicki ya Macedonia Uwanja wa Anfield na marudio ni Agosti 5 huko Macedonia.
Meneja mpya wa Liverpool, Roy Hodgson, alijaribu kuwasiliana na Mascherano kwa simu alipokuwa likizo lakini hakumpata na mara baada ya Mchezaji huyo kutoka Argentina kutua Liverpool walifanya mazungumzo ili kuwekana sawa kuhusu hali ya baadae.
Hata hivyo haijulikani nini kilifikwa kwenye mazungumzo hayo.
Cudicini arudi kilingeni baada ya ajali mbaya
Kipa wa Tottenham, Carlo Cudicini, ameanza tena kuonekana golini Miezi 8 baada ya kupata ajali mbaya sana ambapo pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na Gari na yeye kuvunjika mikono yote miwili pamoja na mfupa wa kwenye kiuno.
Cudicini, Miaka 36, aliidakia Tottenham kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Bournemouth na pia jana walipotoka sare 2-2 na Sporting Lisbon.
Cudicini aliekuwa Chelsea kabla ya kujiunga Tottenham anategemewa kugombea Ukipa Nambari wani hapo Klabuni na Mbrazil Heurelho Gomes ambae ndie Namba moja.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Raul kuondoka Real
Baada ya Miaka 18 ya utumishi kwa Real Madrid, Straika Raul amedai yuko njiani kuondoka na huenda akaangukia England kwenye Ligi Kuu.
Raul, Miaka 33, alitegemewa kujiunga na Klabu ya Ujerumani Schalke lakini mwenyewe ameziruka habari hizo.
Katika Mechi 741 alizoichezea Real, Raul alifunga mabao 323 na ameichezea Spain Mechi 102 na kufunga bao 44.
Raul alianza kuichezea Timu ya Kwanza ya Real Mwaka 1994 akiwa na Miaka 17 na alijiunga hapo Mwaka 1992.
Akiwa na Real ameweza kunyakua Ubingwa wa Ulaya mara 3 na La Liga mara 6.
Raul amesema baada ya siku chache atajua kama atacheza Bundesliga au Ligi Kuu England.
Ripoti ya Majeruhi wa Man United
Wakati Kikosi cha Manchester United kipo ziarani huko Marekani na baadae wataenda Mexico kwa mechi kadhaa, Wachezaji kadhaa wamebaki huko Manchester wakifanya mazoezi binafsi baada ya kupona maumivu yao.
Nahodha Gary Neville na Antonio Valencia wameanza mazoezi ya nguvu. Rio Ferdinand na Michael wameanza mazoezi mepesi.
Kuhusu majeruhi wa muda mrefu Anderson na Owen Hargreaves, Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amedokeza kuwa Anderson, alieumia goti Mwezi Februari Mwaka huu, anategemewa kuonekana Septemba na Owen Hargreaves ataendelea kubaki Marekani kwa Daktari aliempasua magoti yake mawili huko nyuma hadi waridhike na hali yake.
Man United yafungwa Marekani
Jana katika Uwanja wa Arrowhead, Kansas City, Marekani, Manchester United ilifungwa bao 2-1 na Kansas City Wizards.
Kansas City Wizards walifunga bao lao la kwanza dakika ya 11 kwa bao la David Arnaud na dakika ya 39 walipata pigo pale Jimmy Conrad alipotolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
Berbatov aliisawazishia Man United kwa penalti dakika ya 41 lakini dakika mbili baadae Kei Kamara alipachika bao la pili na la ushindi kwa Kansas City Wizards.
Man United wanasafiri kwenda Jijini Houston kucheza na Mastaa wa Ligi ya huko Marekani MLS hapo Jumatano Julai 28.

Sunday 25 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Man City kulizwa na sheria mpya ya Usajili Wachezaji
Sheria mpya inayoanza kutumika Msimu huu ya kutaka kila Klabu ya Ligi Kuu England isajili Wachezaji 25 na kuwasilisha majina yao ifikapo Septemba Mosi huku Wachezaji 8 kati ya hao 25 ni lazima wawe ‘wamelelewa’ kwenye Klabu za England au Wales kwa Misimu mitatu mfululizo kabla hawajatimiza Umri wa Miaka 21, huenda ikawakata maini Manchester City.
Sheria hiyo itawafanya Manchester City waathirike mno na huenda wakalazimika kuwatema hadi Wachezaji 12 kabla Dirisha la Uhamisho halijafungwa hapo Agosti 31.
Sheria hiyo mpya inaruhusu Klabu kuwa na zaidi ya Wachezaji 25 ikiwa tu hao Wachezaji wa ziada wako chini ya Miaka 21 na ‘wamelelewa’ England au Wales kwa Misimu mitatu mfululizo.
Wachunguzi wanahisi Wachezaji walio hatarini kutemwa na Man City ni kundi la kina Roque Santa Cruz, Craig Bellamy, Jo, Felipe Caicedo, Micah Richards, Michael Johnson, Vincent Kompany, Shaun Wright-Phillips, Stephen Ireland, Nigel De Jong, Kelvin Etuhu, Pablo Zabaleta na Nedum Onuoha.
Meneja wa Man City Roberto Mancini amekiri kuwepo kwa tatizo hilo: "Najua lazima tuwauze baadhi ya Wachezaji. Inabidi tuwe na listi ya Wachezaji 25.”
Hodgson akiri Torres ni kitendawili
Meneja mpya wa Liverpool, Roy Hodgson, licha ya kumtaka Straika Staa Fernando Torres abakie Liverpool kama mwenzie Steven Gerrard, ameonyesha wasiwasi kama Mhispania huyo atabaki Anfield.
Hodgson alikutana na Torres wiki iliyokwisha lakini amedokeza kuwa Nyota huyo anasita kutoa msimamo thabiti kama atabaki Liverpool.
Hodgson amesema: “Bahati mbaya sina cha zaidi cha kufanya. Torres ana bifu na Klabu na si mimi. Yeye ameniambia ana madai na Klabu ya tangu siku za nyuma hivyo mimi sina uwezo kuhusu hilo.”
Ancelotti adai Cole haendi Real
Huku kukiwa na uvumi mzito kwamba Ashley Cole yuko njiani kwenda Real Madrid kuungana tena na Jose Mourinho, Mtu ambae ndie aliemrubuni ang’oke Arsenal na kuhamia Chelsea wakati Mourinho yuko Chelsea, Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti ameonyesha imani yake kuwa Fulbeki huyo atabaki Stamford Bridge.
Ancelotti ametamka: “Cole ni Mchezaji wa Chelsea na hakuna anaetaka kumuuza. Yeye ni Mchezaji bora Duniani kwenye nafasi yake na yuko na furaha hapa. Haongoki ng’o!”
Mwalimu wa Viungo akimbizwa toka Marekani kwenda kuwanoa Rooney na Wenzake!!!
Wachezaji wa Manchester United waliocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kupewa likizo ndefu na kutakiwa warudi Manchester Julai 28, watakuwa chini ya Mwalimu Mkuu wa Mazoezi ya Viungo, Strudwick, ambae yupo kwenye ziara ya Man United huko Marekani na ataruka toka huko Jumapili jioni kurudi Manchester.
Wachezaji hao ni Wayne Rooney, Michael Carrick, Patrice Evra, Nemanja Vidic na Ji-sung Park.
Kocha wa Manchester United amesema hataki kuwaharakisha Wachezaji hao Mastaa kucheza hadi wawe fiti na hivyo hawatacheza mechi na Chelsea kugombea Ngao ya Hisani hapo Agosti 8.
Kocha huyo wa Viungo, Strudwick, amesema: “Kitu muhimu kwanza ni kujua wapo katika hali gani. Tutawapa programu kulingana na kiwango alicho fiti kila Mchezaji.”
Man United leo usiku wanacheza huko Kansas City, Marekani na Kasas City na baadae wataruka hadi Houston kucheza na Kombaini ya Nyota wa MLS siku ya Jumatano.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Guti aondoka Real baada ya Miaka 25
Kiungo wa Real Madrid Guti ametangaza anahama Real Madrid baada ya kuwa na Timu hiyo tangu Mwaka 1985 akiwa Timu ya Vijana na kisha kuitumikia Timu ya Kwanza kwa Miaka 15.
Guti, Miaka 33, amebakiza Mwaka mmoja kwenye Mkataba wake na Real lakini sasa anafikiria kuhamia huko Uturuki.
Guti amesema amepewa ofa nzuri na Besiktas ya Uturuki.
Katika Kikosi cha sasa cha Real Madrid, ni Raul pekee ndie aliedumu hapo muda mrefu kupita Guti.
Rio nje hadi mwishoni Agosti
Beki wa Manchester United, Rio Ferdinand, atalazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kupita ilivyokadiriwa na sasa anategemewa kurudi tena mwanzoni mwa Septemba badala ya katikati ya Agosti.
Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson, ametoboa: “Rio atarudi baada ya Wiki 6.”
Kuchelewa kurudi kwa Rio kutamfanya pia azikose mechi za England za kuwania kufuzu kuingia Fainali za EURO 2012 zitazochezwa Septemba dhidi ya Bulgaria na Uswisi.
Pia atazikosa mechi za Ligi Kuu za Man United v Newcastle hapo Agosti 16, hii ikiwa mechi ya ufunguzi, na zile zinazofuata za Agosti 22 dhidi ya Fulham na Agosti 28 na West Ham.
Ferdinand aliumia goti huko Afrika Kusini mazoezini kwenye Kikosi cha England kilichokuwa kipo kwa Fainali za Kombe la Dunia na alipata maumivu hayo baada ya kugongana na Emile Heskey.
Fergie furahani
Wakati huo huo, Sir Alex Ferguson ameonyesha kufurahishwa kwake kwa Beki wake Nemanja Vidic kukubali kusaini Mkataba mpya.
Fergie ametamka: “Siku hizi ni ngumu kuwafanya Wachezaji wazuri kusaini Mkataba mpya na hasa Wachezaji watokao nje ya England. Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu Vidic. Tumefurahi amesaini tena! Yeye ni Sentahafu mzuri sana!”
Powered By Blogger