Saturday 29 May 2010

Cameroun 1 Slovakia 1
Mechi za majaribio kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Cameroun zimezidi kuwa ngumu baada ya leo tena kulazimisha sare ya 1-1 walipocheza na Slovakia ambao pia wako kwenye Fainali hizo wakishiriki kwa mara ya kwanza.
Hii ni mechi ya pili kwa Cameroun kutoka sare baada ya kwenda suluhu 0-0 na Georgia majuzi.
Katika mechi hii ya leo iliyochezwa Nchini Austria, Slovakia ndio walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 6 kwa mzinga wa Mita 18 wa Kamil Kopunek.
Cameroun, wakicheza bila ya Samuel Eto’o aliepumzishwa, walisawazisha kupitia kwa Eyong aliefunga dakika 7 kabla mchezo kwisha.
Cameroun wapo Kundi E kwenye Kombe la Dunia pamoja na Denmark, Japan na Uholanzi.
Mechi inayofuata ya majaribio kwa Cameroun ni Juni 1 huko Covilha, Ureno watakapoikwaa Ureno ambayo pia iko matayarishoni kwa Kombe la Dunia, kisha watacheza na Serbia Juni 5 huko Belgrade.
Fergie ni Mhusika Mkuu kuteua Mrithi wake
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson ndie Mhusika Mkuu wa kumchagua nani amrithi endapo ataamua kustaafu na hilo limetamkwa na Mkurugenzi Mkuu David Gill.
Ferguson amekalia wadhifa wake kwa Miaka 23 na kuisaidia Man United kunyakua Vikombe 34 vikiwemo 11 vya Ubingwa wa Ligi Kuu England na viwili vya Klabu Bingwa Ulaya.
David Gill amesistiza ushauri wa Ferguson ni muhimu katika uteuzi wa Mrithi wake lakini mpaka sasa hawajui ni lini Ferguson atang’atuka.
Gill pia ameongeza kuwa wakati Ferguson akiamua kustaafu wataunda jopo litalowashirikisha yeye, Sir Bobby Charlton, Sir Alex Ferguson na Wamiliki wa Klabu hiyo, Familia ya Glazer, ili kumtafuta Mtu atakaefaa kuwa Meneja.
Kuhusu habari zinazodai kuwa Jose Mourinho akitua Real Madrid anataka kumchukua Wayne Rooney huko, Gill amepuuza habari hizo kwa kusema: “Hawezi kwenda huko. Hatakubali kwenda huko. Hizi ni kelele tu. Sizijali!”
MECHI YA KIRAFIKI: Kesho England v Japan
Kesho England inacheza mechi yake ya mwisho ya majaribio kabla Kikosi chake hakijapunguzwa na kubakisha Wachezaji 23 watakaowasilishwa FIFA hapo Jumanne, Juni 1.
England, ambao wako kambini huko Austria, watacheza na Japan Jumapili, Mei 30 Uwanja wa UPC Arena Mjini Graz, Austria katika mechi itakayoanza saa 9 na robo mchana, saa za bongo.
Kocha wa England, Fabio Capello, inasemekana atafanya mabadiliko katika Kikosi chake kwa kuwaanzisha Tom Huddlestone wa Tottenham na Darren Bent wa Sunderland.
Vilevile, Wachezaji wa Chelsea John Terry, Ashley Cole na Frank Lampard watacheza mechi hiyo baada ya kuikosa mechi ya Jumatatu iliyopita England walipocheza na Mexico huko Wembley na kushinda 3-1.
Vikosi vinategemewa kuwa:
England:
David James, Glen Johnson, John Terry, Rio Ferdinand, Ashley Cole, Theo Walcott, Tom Huddlestone, Frank Lampard, Aaron Lennon, Wayne Rooney, Darren Bent.
Japan:
Narazaki, Uchida, Nakazawa, Tanaka, Nagatomo, Tamada, Endo, Hasebe, Nakamura, Okazaki, Honda.
Eto’o atishia kujitoa Kombe la Dunia!!!
Samuel Eto'o amedokeza huenda akajitoa kwenye Kikosi cha Cameroun cha Kombe la Dunia kufuatia lawama alizobebeshwa na Mkongwe Roger Milla.
Roger Milla, alieng’ara Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 1990 huko Italia, amedai Eto’o hajitumi ipasavywo anavyochezea Nchi yake kama anavyojitutumua alipokuwa FC Barcelona na sasa Inter Milan.
Milla alikaririwa akisema: “Amefanya mengi kwa Barcelona na Inter Milan lakini hajafanya lolote kwa Cameroun!”
Eto'o ndie anaeonekana nyota na mkombozi wa Cameroun na ndie anaeongoza katika historia ya Cameroun kwa kuwa Mfungaji Bora akiwa na Mabao 44 katika Mechi 94 za Nchi yake.
Kauli ya Milla imemchukiza Samuel Eto’o na mwenyewe amedai analalamikiwa bila sababu na Watu wenye uchungu usio na msingi.
Eto’o, ambae wikiendi iliyokwisha aliisaidia Klabu yake Inter Milan kutwaa Klabu Bingwa Ulaya walipoifunga Bayern Munich 2-0, amehoji: “Hivi kuna faida yeyote mie kwenda Kombe la Dunia?”
Eto’o akaongeza: “Nina siku kadhaa za kutafakari kama kuna umuhimu mimi kucheza Fainali hizo. Siku zote kabla Mashindano makubwa wanaibuka Watu wenye kinyongo!”
Huku akionekana mwenye uchungu alipohojiwa na Kituo cha TV Canal Plus, Eto’o alisema: “Yeye Milla kaifanyia nini Cameroun? Hajashinda Kombe la Dunia! Alifika tu Robo Fainali na Kikosi kizuri! Si kwa sababu waliweka historia kwa kucheza Kombe la Dunia wakiwa na Miaka 40 ndio waanze kusema Watu!”
Mwishowe, Eto’o akahoji: “Unashangaa, unajiuliza: hivi hawa ni Watu wangu? Ni kweli Watu wangu? Kuna faida kwenda Kombe la Dunia?”
Real kumtangaza ‘El Especial’ J’Tatu
Jumatatu Real Madrid itamsimika Jose Mourinho kama Kocha wao mpya kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini aliefukuzwa Jumatano iliyopita na hatua hii inafuatia makubaliano yaliyofikiwa jana kati ya Marais wa Klabu za Inter Milan na Real Madrid, Massimo Moratti wa Inter Milan na Florentino Perez wa Real, ya jinsi Inter itakavyolipwa fidia kwa Mourinho kuukatisha Mkataba wake unaotakiwa kwisha 2012.
Katiba Mkataba huo wa Mourinho, anaesifika kama The Special One’ na sasa anaitwa ‘El Especial’ huko Spain ikimaanisha ‘Mtu Spesheli’, na Inter kuna kipengele kinachotaka Inter ilipwe Pauni Milioni 13.5 ikiwa Mkataba utakatishwa.
Mourinho alijiunga na Inter Septemba 2008 na Jumamosi iliyokwisha aliiwezesha Inter kuchukua UEFA CHAMPIONS LIGI pamoja na Makombe ya Coppa Italia na Serie A na hivyo kuweka historia ya kuwa Klabu ya kwanza Italia kushinda Trebo [Vikombe vitatu].
MECHI YA KIMATAIFA YA KIRAFIKI:
Republic of Ireland 3 Algeria 0
Algeria ambao wako Fainali za Kombe la Dunia jana huko Dublin walipigwa bao 3-0 na Republic of Ireland Uwanjani Croke Park.
Mabao ya Ireland yalifungwa na Paul Green dakika ya 31 na mbili kupitia Nahodha wao Robbie Keane, dakika ya 52 na 85, kwa penalti.
Ireland walikosa kucheza Fainali za Kombe la Dunia walipotolewa na Ufaransa kwa bao la utata mkubwa wakati Thierry Henry alipokontroli mpira kwa mkono na kumpasia William Gallas aliefunga bao la kusawazisha na hivyo kuifanya Ufaransa ifuzu.
LEO MECHI ZA KIRAFIKI ZA MATAIFA:
Jumamosi, 29 Mei 2010
[saa za bongo]
Azerbaijan v FYR Macedonia, [saa 12 jioni]
Congo DR v North Korea
Hungary v Germany, [saa 3 usiku]
Iceland v Andorra, [saa 4 usiku]
New Zealand v Serbia, [saa 12 na robo usiku]
Norway v Montenegro, [saa 11 jioni]
Poland v Finland, [saa 12 jioni]
Slovakia v Cameroon, [saa 9 mchana]
Spain v Saudi Arabia, [sa 1 usiku]
Sweden v Bosnia-Hercegovina, [saa 2 usiku]
Ukraine v Romania, [saa 2 na nusu usiku]
United Arab Emirates v Moldova, [saa 2 usiku]
USA v Turkey, [saa 3 usiku]

Friday 28 May 2010

Ufaransa Mwenyeji EURO 2016
Ufaransa leo imechaguliwa kuwa Mwenyeji wa Fainali za Mashindano ya EURO 2016 Michuano inayoshirikisha Mataifa ya Ulaya itakayokuwa na Nchi 24 na kuchezwa jumla ya Mechi 51.
Ufaransa iliibwaga Uturuki kwa kura moja na Italia ilitupwa nje katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo.
Kampeni za Ufaransa za kuwania nafasi hiyo ziliongozwa na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na Staa wa zamani Zinedine Zidane huko Makao Makuu ya UEFA Nchini Uswisi.
Serikali ya Ufaransa imesema itatoa dhamana ya Pauni Bilioni 1.45 ili zitumike kujenga na kukarabati Viwanja mbalimbali kwa ajili ya Michuano hiyo.
Katika maombi yao ya kuwa Wenyeji Ufaransa ilipendekeza Viwanja 12 ukiwemo ule uitwao Stade de France ambako Ufaransa waliifunga Brazil Mwaka 1998 na kutwaa Kombe la Dunia.
Vingine ni Uwanja wa Klabu ya Paris Saint Germain uitwao Parc des Princes, Lens, Lille, Bordeaux, Nice, Toulouse, Marseille, Lyon, Strasbourg, Saint Etienne na Nancy.
Kabla ya Fainali hizo za EURO 2016, zitafanyika Fainali za EURO 2012 kwa pamoja Nchini Poland na Ukraine na zitashirikisha Nchi 16.
Familia ya Glazer yasema Man United haiuzwi!!!
Familia ya Kimarekani ya kina Glazer imetoa taarifa rasmi leo iliyotamka Klabu yao Manchester United haiuzwi na wao hawana nia ya kumsikiliza Mtu yeyote mwenye azma ya kutoa ofa ya kuinunua.
Tamko hilo ni la kwanza rasmi toka kwa Wamiliki hao tangu ulipoanza upinzani dhidi yao toka kwa Kikundi kinachojiita ‘Wakombozi Wekundu’ ambacho ni Kikundi cha Watu Matajiri Mashabiki wa Manchester United na Kikundi kingine ni cha Masapota kinachoitwa MUST [Manchester United Supporters Trust] ambacho pia kinataka Familia ya Glazer ing’oke Manchester United.
Vikundi hivyo viwili, Red Knights na MUST, vilisema vitakusanya nguvu zao kwa pamoja ili kushinda vita yao.
Wakati MUST ilikuwa ikikusanya nguvu na kuendesha upinzani kwa Mashabiki kuvaa Rangi za Dhahabu na Kijani katika mechi za Man United ambazo ndizo zilikuwa Rangi za Klabu anzilishi ya Man United iliyoitwa Newton Heath, ‘Wakombozi Wekundu’ walikuwa wakikusanya nguvu ya kifedha ili kutoa ofa kwa kina Glazer.
Taarifa hiyo ya Familia ya Glazer imesema Klabu inaendeshwa vizuri na inazalisha fedha nyingi licha ya kuwa na deni kubwa ambalo hata hivyo linalipwa kama ilivopangwa na halisumbui uendeshaji.
Vilevile, taarifa hiyo ilidokeza jinsi Wadhamini wapya, wanaolipa pesa nyingi, wanavyozidi kumiminika na kuwa Timu inategemewa kufanya ziara yenye faida kubwa kifedha huko Marekani na Canada katika Majira ya Joto kabla Msimu mpya wa 2010/11 kuanza hapo Agosti 8. 
Daktari wa Argentina: Soka na Ngono Ruksa!!!
• Maradona kukimbia uchiii!!!
Daktari wa Timu ya Argentina ya Kombe la Dunia, Dr. Donato Vallani, amesema Wachezaji wa Timu hiyo ruksa kupata unyumba na Mapatna wao wa kawaida wakiwa huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Dr. Vallani amesema: “Wachezaji wako huru kufanya ngono na Wake zao na Wachumba zao! Wao si Viumbe toka Dunia nyingine! Lakini si kufanya hivyo saa 8 za usiku wakinywa pombe na kuvuta Sigara!”
Daktari huyo pia amesema Wachezaji ruksa kula Nyama Choma na glasi ya mvinyo ambavyo hupendwa sana huko Argentina lakini kukata Kilaji kwa kupindukia hairuhusiwi.
Argentina wanategemewa kutua Afrika Kusini leo na wapo Kundi B pamoja na Nigeria, Korea Kusini na Ugiriki.
Nigeria ndio wapinzani wa kwanza wa Argentina hapo Juni 12.
Wakati huo huo, Kocha wao Diego Maradona ameahidi kukimbia uchi katikati ya Jiji la Buenos Aires, Argentina endapo Nchi hiyo itatwaa Kombe la Dunia.
Maradona alikuwa Nahodha wa Argentina Mwaka 1986 walipochukua Kombe la Dunia.
Majaribio ya Waamuzi Watano kwa Mechi……………..
UEFA imeongeza muda wa kutumia Marefa Watano katika kila mechi na Msimu ujao yatahusisha pia Mashindano ya Klabu ya UEFA CHAMPIONS LIGI na yale ya Mataifa ya EURO 2012 baada ya kuanza kutumika Msimu uliopita kwenye EUROPA LIGI.
Mtindo huo wa Marefa Watano hutumia Marefa Watatu wa kawaida, yaani Refa Mkuu anaekuwa katikati Uwanjani akisaidiwa na Washika Vibendera Wawili wakiwa pembezoni ya Uwanja, huku nyuma ya kila mstari wa goli huwepo Refa Msaidizi mwingine mmoja na kufanya jumla ya Waamuzi kuwa Watano.
Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka [IFAB=The International Football Association Board] ambao ndiyo yenye mamlaka ya kubadili sheria za Soka Duniani na inayoundwa na Waawakilishi toka FIFA, Vyama vya Soka vya England, Scotland, Wales na Ireland, Vyama ambavyo ndivyo Waanzilishi wa Soka Duniani, ilibariki kutumika kwa mtindo wa Marefa Watano kwa mechi kwa UEFA na Vyama vingine vya Soka Duniani.
Mwezi Machi, IFAB iligoma kupitisha mapendekezo ya kutumika utaalam wa kisasa wa elektroniki kwenye mistari ya magoli ili kuwasaidia Marefa kuamua kama mpira umevuka mstari na hivyo ni goli au la.
Lakini mtindo huo wa Marefa Watano uliojaribiwa kwenye EUROPA LIGI Msimu uliopita ulipokewa kwa hisia tofauti na Makepteni wa Timu zilizoshiriki EUROPA LIGI ambao walipiga kura kupitia Chama chao cha Wachezaji wa Kulipwa, Fifpro, na Asilimia 70 waliona hamna kilichosaidia kwa kutumika Marefa Watano katika mechi moja.
Lakini UEFA wana mtizamo tofauti na wameona IFAB kubariki kutumika Mtindo huo na kuendelezwa kwa Majaribio kuhusisha UEFA CHAMPIONS LIGI na EURO 2012 ni kuukubali.
Nae Refa wa zamani wa Ligi Kuu England, Graham Poll, anahisi kubadili mfumo wa utumiaji Marefa una matatizo na alisema kuna wakati Marefa hao Watano kwa mechi moja walifanya kazi nzuri na akatoa mfano Dirk Kuyt alipoifungia goli Liverpool kwenye mechi na Benfica na Refa Msaidizi [Mshika Kibendera] akaashiria ni Ofsaidi lakini Refa Msaidizi mwingine aliekuwa nyuma ya goli, aliona Mchezaji aliekuwa ofsaidi hakuugusa na wala hakuingilia mchezo na hivyo ni goli halali na Refa Mkuu akalikubali.
Graham Poll akatoa mfano mwingine uliohusu Marefa Watano kwenye mechi ya EUROPA LIGI ya Fulham ambao, kwa pamoja, walifanya makosa makubwa ya kutaka kumtoa kwa Kadi Nyekundu Mchezaji ambae si mkosaji na ikabidi yule Mchezaji mkosaji akiri yeye ndie mwenye kosa na si yule alietaka kutolewa.
Poll amesema: “Siku zote makosa ya Kibanadamu yapo hata ukiweka Marefa wangapi! Lazima tukubali hilo au tuseme hatutaki na kutumia teknolojia!”
Matokeo Mechi za Kirafiki:
Alhamisi, 27 Mei 2010
Belarus 2 v Honduras 2
Denmark 2 v Senegal 0
South Africa 2 v Colombia 1

Thursday 27 May 2010

Pellegrini asikitishwa!
Baada ya kumwaga unga Real Madrid, Manuel Pellegrini, ameelezea masikitiko yake kwa jinsi alivyotendewa na jinsi alivyovunjika moyo kwa kutofanikisha matarajio yake.
Pellegrini alilalamika: “Nlikuja hapa na matumaini makubwa na fahari kubwa ya kuiongoza Timu. Lakini bahati mbaya sikufanikiwa na nilikuwa na tofauti kubwa na Uongozi wa Klabu.”
Pellegrini alitoboa kuwa kulikuwa na tofauti kubwa ndani ya klabu na akatoa mfano wa yeye kutaka Wachezaji Wesley Sneijder na Arjen Robben wabaki Real kwa vile ni wazuri lakini Uongozi ulitaka wauzwe.
Sneijder akatimkia Inter Milan na Robben akatua Bayern Munich.
Bosi huyo wa zamani wa Real anaetoka Chile, alijiunga hapo Mwezi Juni 2009 akitokea Villareal na alitua hapo kumbadili Juande Ramos lakini alishindwa kuiongoza Timu na haikufika hata Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIG, ikatolewa Copa del Rey na Timu ndogo na ikaukosa Ubingwa wa Spain uliochukuliwa na Mahasimu wao FC Barcelona licha ya Klabu kutumia zaidi ya Pauni Milioni 200 kuwanunua Masupastaa Ronaldo, Kaka, Benzema na Alonso.
Pellegrini aliongeza kuwa alikuwa haongei na Rais wa Real Madrid Florentino Perez ambae alizungumza nae kwa mara ya mwisho mwezi Agosti Mwaka jana.
Pelligrini alikiri ameumizwa sana roho kwa jinsi mrithi wake alivyotafutwa na hilo analiona si jambo la utu na si uungwana hata chembe.
Hata hivyo, Pellegrini, amemtakia kila la heri Jose Mourinho.
Essien kwa heri World Cup
Michael Essien hatacheza Fainali za Kombe la Dunia kwa vile hawezi kupona goti lake kabla ya mwisho wa Julai.
Essien, ambae ni Mchezaji wa Ghana, aliumia goti akichezea Nchi yake kwenye mechi za awali za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mwezi Januari huko Angola na tangu wakati huo hajachezea hata Klabu yake Chelsea.
Fainali za Kombe la Dunia zitaanza huko Afrika Kusini Juni 11 na kumalizika Jula11.
Kila Nchi iliyo Fainali hizo inatakiwa kuwasilisha Kikosi chake cha Wachezaji 23 kwa FIFA ifikapo Juni 1.
Ghana wako Kundi D pamoja na Ujerumani, Australia na Serbia.
Chicharito apata Kibali kucheza Man United
Straika toka Mexico Javier Hernandez, Miaka 21, amepewa Kibali cha Kazi Nchini England cha kuichezea Manchester United na rasmi atahesabika kama Mchezaji wa Klabu hiyo Julai 1.
Hernandez, maarufu kama Chicharito, alichukuliwa na Man United Aprili kutoka Klabu ya Chivas Guadalajara ya Mexico lakini usajili wake ulitegemea kupata Kibali cha Kazi ambacho kilikuwa na utata kwa vile alikuwa hajafikisha kuchezea mechi Asilimia 75 za Nchi yake Mexico katika Miaka miwili iliyopita kama kanuni za Kazi zinavyotaka kwa Wachezaji Soka wa Kulipwa watokao nje ya Jumuia ya Ulaya.
Hivyo ilibidi Man United waombe Kibali hicho cha Kazi kwa kutuma Maombi spesheli yaliyosisitiza kuwa Kijana huyo ana kipaji pekee ambacho ni ngumu kupatika katika Nchi za Ulaya kwa dau waliomnunulia.
Jopo la FA ambalo linasimamia Vibali hivyo kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya England liliafikiana na ombi la Man United na kumruhusu Javier Hernandez aka Chicharito kuanza kuichezea Klabu yake mpya.
Chicharito siku ya Jumatatu iliyopita aliichezea Mexico Kipindi cha pili ilipocheza mechi ya kirafiki na England Uwanjani Wembley.
Jana Chicharito aliichezea tena Mexico walipokutana na Uholanzi na alifunga bao la Nchi yake katika mechi ambayo Holland waliifunga Mexico 2-1.
Katika Fainali za Kombe la Dunia, Mexico wapo Kundi A pamoja na Wenyeji Afrika Kusini, Ufaransa na Uruguay.
Yuko njiani Real, Mourinho awataka Cole, Maicon Real!!
Jose Mourinho, anaetegemewa kutangazwa kama Mrithi wa Manuel Pellegrini alietimuliwa jana ndani ya Masaa 24 yajayo, tayari ameshaanza kudokeza mikakati yake Real Madrid kwa kusema anataka akiwa hapo acheze mtindo wa kuwa na Mabeki wanne na kati yao Mafulbeki wawili wenye staili ya kupanda na kushambulia kama walivyo Ashley Cole, aliekuwa Mchezaji wake Chelsea, na Maicon ambae wako wote Inter Milan.
Kitu pekee kinachochelewesha Mourinho asitangazwe ndie Meneja mpya wa Real ni kipengele cha Mkataba wake kinachotaka Inter Milan walipwe Pauni Milioni 13.2 ikiwa Mkataba utakatizwa kabla ya mwisho wake Mwaka 2012.
Mourinho amenena: “Napenda kucheza na Mabeki wanne ingawa nimeshashinda mechi nyingi na Mabeki watatu. Kawaida nacheza na Difensi ya Mabeki wanne na wawili ni wale wa pembeni wanaopanda kushambulia kama wanavyofanya Maicon na Cole.”
Mourinho ndie aliemchota Ashley Cole kutoka Arsenal Mwaka 2006 kwenda Chelsea wakati alipokuwa Meneja wa Chelsea na kumtaja kwake Cole kumeleta hisia atamchukua Real akitua huko.
Mourinho pia alidokeza kuwa Frank Lampard na Steven Gerrard ni Wachezaji wanaofaa kwa Real.
MECHI ZA KIMATAIFA ZA KIRAFIKI
[saa za kibongo]
Alhamisi, 27 Mei 2010
Belarus v Honduras, [saa 1 na nusu usiku]
Denmark v Senegal, [saa 3 na robo usiku]
South Africa v Colombia, [saa 3 dak 35 usiku]
________________________________________
Ijumaa, 28 Mei 2010
Rep of Ireland v Algeria, [saa 3 dak 45 usiku]
________________________________________
Jumamosi, 29 Mei 2010
Azerbaijan v FYR Macedonia, [saa 12 jioni]
Congo DR v North Korea
Hungary v Germany, [saa 3 usiku]
Iceland v Andorra, [saa 4 usiku]
New Zealand v Serbia, [saa 12 na robo usiku]
Norway v Montenegro, [saa 11 jioni]
Poland v Finland, [saa 12 jioni]
Slovakia v Cameroon, [saa 9 mchana]
Spain v Saudi Arabia, [sa 1 usiku]
Sweden v Bosnia-Hercegovina, [saa 2 usiku]
Ukraine v Romania, [saa 2 na nusu usiku]
United Arab Emirates v Moldova, [saa 2 usiku]
USA v Turkey, [saa 3 usiku]
________________________________________
Jumapili, 30 Mei 2010
Belarus v South Korea, [saa 10 jioni]
Chile v Northern Ireland, [saa 5 usiku]
Japan v England, [saa 9 na robo mchana]
Mexico v Gambia, [saa 12 jioni]
Nigeria OFF Colombia, [saa 3 usiku]
Paraguay v Ivory Coast, [saa 3 usiku]
Tunisia v France, [saa 3 usiku]
Venezuela v Canada, [saa 8 na nusu usiku]
________________________________________
Jumatatu, 31 Mei 2010
Chile v Israel, [saa 11 alfajiri]
South Africa v Guatemala, [saa 3 na nusu usiku]
________________________________________
Jumanne, 1 Juni 2010
Australia v Denmark, [saa 9 na nusu usiku]
Netherlands v Ghana, [saa 3 na nusu usiku]
Portugal v Cameroon, [saa 3 na nusu usiku]
Switzerland v Costa Rica, [saa 3 na robo usiku]
Ni rasmi, Brazil kucheza Bongo!!!
Taifa Bora kwa Soka Duniani na ambao wanashika rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia kwa kujitwika nalo mara 5, Brazil, watacheza mechi za kirafiki na Zimbabwe Juni 2 na Juni 7 watakuwa Dar es Salaam kucheza na Taifa Stars.
Mikataba kwa ajili ya mechi hizo mbili tayari imeshasainiwa na tayari Timu hiyo iko Afrika Kusini ilipowasili jana ikitokea kwao Brazil.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga, akithibitisha ujio wa Brazil, alitamka kwa furaha: “Unazungumzia Timu Bora Duniani. Hii ni njia bora ya kuitangaza Nchi yetu. Na hii ni moja ya hatua tunazopasa kuchukua kukuza Soka letu. Italeta furaha Nchini na kuwapa moyo Vijana wetu.”
Brazil wataanza kampeni yao kwenye Kombe la Dunia Juni 15 kwa kucheza na Korea Kaskazini na wapo Kundi moja pamoja na Ivory Coast na Ureno.
UEFA yaweka kibano kwa Klabu za LIGI KUU
UEFA inategemewa kupitisha sheria mpya ambazo zitazibana sana Klabu za England za Ligi Kuu na huenda ikazifanya zisishiriki Mashindano ya Ulaya kama vile UEFA CHAMPIONS LIGI na EUROPA LIGI.
Sheria hizo zinategemewa kupitishwa Alhamisi Mei 27 na Kamati Kuu ya UEFA na ni mkakati wa dhahiri wa Mfaransa Rais wa UEFA Michel Platini ambae ni mpinzani mkubwa wa Klabu za Uingereza hasa England.
Sheria hizo, ambazo zitaanza kazi rasmi Msimu wa Mwaka 2012/13, zinataka Klabu zipunguze na kuweka kiwango katika Mishahara ya Wachezaji, Klabu ziwe zinajiendesha kwa faida na pia kutopewa ruzuku na Wamiliki wake.
Hivi sasa huko England Klabu nyingi zina Mishahara ya kupindukia ya Wachezaji, nyingi zinaendeshwa kwa hasara na kukumbwa na Madeni makubwa na kadhaa wa kadhaa zinategemea ruzuku za Wamiliki wake ili kujiendesha.
Katika Msimu wa Mwaka 2008/9, ambao Klabu nyingi walikamilisha na kukaguliwa Mahesabu yao, kati ya Klabu 20 za Ligi Kuu, 14 zilipata hasara na moja, Blackburn Rovers, ilipata faida ya Pauni Milioni 3.6 lakini baada ya kupewa mkopo wa Pauni Milioni 5 na Mwenye Klabu, kitendo ambacho kitapingana na Sheria mpya za UEFA.
Klabu nyingi Ligi Kuu zinapewa ruzuku na Wamiliki wao na zinazoongoza kwa hili ni Chelsea na Manchester City ambazo Wamiliki wake Roman Abramovich kwa Chelsea na Koo ya Kifalme ya Abu Dhabi kwa Man City, walifuta Madeni makubwa ya Pauni Milioni 47 kwa Chelsea na Pauni Milioni 93 kwa Man City kwa kutoa ruzuku kwa Klabu zao.
Hilo nalo halitakiwi na UEFA katika sheria mpya za Michel Platini ambazo pia zitawataka Wamiliki wawekeze kwenye Klabu kwa kununua Hisa lakini si kukopesha au kutoa ruzuku na pia kujenga Miundombinu kama Viwanja vya Mazoezi na Vyuo vya kuendeleza Vijana badala ya kuwa wanalipa Mishahara minono kwa Wachezaji au kununua Wachezaji kwa bei mbaya.
Mwenyewe Platini anadai sheria hizi ni suala la kufa na kupona kwa Soka hasa kwa vile Klabu zinakabiliwa na Madeni makubwa.
Katika Ligi Kuu, ukiondoa Chelsea na Man City, Aston Villa walipewa ruzuku na Mmiliki wake lakini walikuwa na hasara ya Pauni Milioni 46 kwa Mwaka 2008/9, Sunderland hasara ya Pauni Milioni 26, Liverpool hasara ya Pauni Milioni 55.
Kwa Manchester United, Mahesabu yao yameonyesha kupata faida kwa sababu tu walimuuza Cristiano Ronaldo kwa dau la Pauni Milioni 81 na kabla ya hapo Klabu hiyo ilikuwa ikionyesha kila Mwaka hasara tu tangu inunuliwe na Familia ya kina Glazer.
Kwenye Vikao vya UEFA, Ligi Kuu ilikuwa ikipigania kwa Klabu zake ziruhusiwe kupokea ruzuku toka kwa Wamiliki wake lakini walishindwa nguvu na Wanachama wengi wa UEFA waliopinga hilo.
Endapo Klabu itashindwa kutekeleza sheria hizo mpya haitaruhusiwa kucheza Mashindano ya Klabu za Ulaya.
Uholanzi 2 Mexico 1
Kwenye mechi ya kirafiki, Robin van Persie wa Holland alifunga bao mbili dhidi ya Mexico iliyopigwa 3-1 juzi Jumatatu na England huko Wembley, London.
Uholanzi, chini ya Kocha Bert van Marwijk ilicheza bila Mastaa Mark van Bommel, Arjen Robben, Wesley Sneijder na Nigel de Jong ambao wana maumivu kidogo.
Rafael van der Vaart, ambae dakika ya 8 alipiga fataki iliyogonga posti, alimtengenezea Van Persie kufunga bao la kwanza dakika ya 17 na dakika 3 baada ya mapumziko Van Persie akafunga bao la pili.
Katika dakika ya 74, Javier Hernandez, maarufu kama Chicharito, ambae ni Mchezaji mpya wa Manchester United, akaipatia Mexici bao lake moja.
MATOKEO MECHI ZA KIRAFIKI:
Jumatano, Mei 26
Azerbaijan 1 v Moldova 1
Estonia 0 v Croatia 0
France 2 v Costa Rica 1
Uholanzi 2 v Mexico 1
Uturuki 2 v Northern Ireland 0
Uruguay 4 v Israel 1
Chile 3 v Zambia 0
RATIBA MECHI ZA KIMATAIFA ZA KIRAFIKI:
Alhamisi, Mei 27
[saa za kibongo]
Belarus v Honduras [saa 1 na nusu usiku]
Denmark v Senegal [saa 3 na robo usiku]
Afrika Kusini v Colombia [saa 3 dak 35 usiku]

Wednesday 26 May 2010

Brazil kutua Bongo njiani kwenda Bondeni?
[BOFYA KWA HABARI ZAIDI]

Pellegrini afukuzwa Real Madrid
Real Madrid imemtimua Kocha wake Manuel Pellegrini na kuiacha njia nyeupe kwa Kocha wa Inter Milan Jose Mourinho kuchukua wadhifa huo kama ilivyokuwa ikivumishwa.
Bodi ya Real ilikaa leo na kuto uamuzi wa kumtimua Pellegrini na Rais wake Florentino Perez ndie alietangaza maamuzi ya Bodi hiyo.
Huko Italia, Inter Milan wameshakata tamaa kumbakisha Mourinho na Rais wa Klabu hiyo Massimo Moratti ameshasema hategemei kama Kocha huyo machachari atabaki Inter.
Pellegrini alikuwa tayari amekalia kuti kavu huko Real baada ya Klabu hiyo kutumia zaidi ya Pauni Milioni 200 kuwanunua Mastaa kina Cristiano Ronaldo, Kaka, Karim Benzema na Xabi Alonso na mwishoni mwa Msimu kuambua patupu baada ya kuukosa Ubingwa wa la Liga, uliobebwa na Mahasimu wao FC Barcelona, kutupwa nja ya UEFA CHAMPIONS LIGI ambayo Fainali yake ilifanyika nyumbani kwa Real Uwanja wa Santiago Bernabeau na pia kubwagwa nje ya Copa del Rey na Timu ndogo sana na masikini sana.
FIFA kupima Wachezaji 256 kabla Fainali Kombe la Dunia
FIFA itawapima Wachezaji wanane toka kila Timu katika Nchi zote 32 zilizo Fainali za Kombe la Dunia kabla Fainali hizo kuanza huko Afrika Kusini Juni 11.
Jumla ya Wachezaji 256 watapimwa mkojo na damu kabla ya Fainali ili kuchunguza kama wanatumia madawa yaliyopigwa marufuku.
Pia, wakati wa Fainali hizo, Wachezaji wawili toka kila Timu watapimwa baada ya kila mechi katika mechi zote 64 za Fainali za Kombe la Dunia.
Fainali za Kombe la Dunia zimekuwa tulivu bila Wachezaji kugunduliwa kutumia madawa yaliyopigwa marufuku isipokuwa ile Fainali ya Mwaka 1994 wakati Diego Maradona wa Argentina alipogundulika akitumia mchanganyiko wa madawa marufuku na akatimuliwa kwenye Fainali hizo.
LISTI YA UBORA YA FIFA: Brazil Nambari Wani, Bongo bado nafasi ya 108!!!
Brazil wataanza Fainali za Kombe la Dunia huku wakiwa ndio Timu ya kwanza kwa Ubora kufuatia listi mpya ya FIFA.
Timu iliyo nafasi ya pili ni Spain wakifuatiwa na Ureno, Holland na Italy.
Katika Afrika Nchi iliyo juu kabisa ni Misri ambao wako nafasi ya 12. Katika Nchi za Afrika zilizo Fainali ya Kombe la Dunia Cameroun ndio wako juu kabisa wakiwa nafasi ya 19 na Wenyeji wa Kombe la Dunia Afrika Kusini wako nafasi ya 83.
Tanzania bado wameng’ang’ania nafasi ya 108.
Msimamo kwa Timu za juu ni:
1 Brazil
2 Spain
3 Portugal
4 Holland
5 Italy
6 Germany
7 Argentina
8 England
9 France
10 Croatia
11 Russia
12 Egypt
13 Greece
14 USA
15 Serbia
Mmiliki wa zamani Liverpool ajuta kuiuza!
David Moores amepasua kuwa anajuta sana kuiuza Liverpool kwa Wamarekani George Gillett na Tom Hicks na amewataka waiuze Klabu hiyo.
Moores aliiuza Liverpool Mwaka 2007 lakini Wamarekani hao wawili walioinunua wameitumbukiza Klabu kwenye Madeni makubwa.
Moores amewaambia: “Msiwaadhibu Washabiki! Uzeni Klabu!”
Gillett na Hicks walinunua Liverpool kwa Pauni Milioni 200 toka kwa Moores lakini utawala wao haukuwapendeza Washabiki na pia kuitumbukiza Klabu kwenye deni la zaidi ya Pauni Milioni 350 ndio kero kubwa ya Washabiki hao.
Pia kushindwa kwa Liverpool kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao kwa vile wamemaliza nafasi ya 7 kumewaudhi mno Wadau.
Gillett na Hicks walitangaza Mwezi Aprili kuwa wataiuza Liverpool lakini mpaka sasa hakuna Mnunuzi aliejitokeza.
Merida wa Ze Gunners atimkia Atletico
Kiungo wa Arsenal Fran Merida anarudi Spain baada ya kusaini Mkataba na Atletico Madrid akiwa Mchezaji huru.
Merida alikuwa Arsenal tangu 2006 aliposainiwa kutoka FC Barcelona lakini uchezaji wake ulikuwa wa nadra sana.
Straika Dindane ajiunga na Klabu ya Qatar
Straika wa Portsmouth Aruna Dindane amejiunga na Lekhwiya ya Qatar kwa Mkataba wa Miaka mitatu.
Dindane alikuwa Portsmouth kwa mkopo wa Mwaka mmoja akitokea Lens ya Ufaransa.
Klabu ya Lekhwiya pia imemsaini Bakary Kone toka kwa Mabingwa wapya wa Ufaransa Marseille.
Wote Dindane na Kone ni Wachezaji kutoka Ivory Coast na wamo kwenye Kikosi cha Nchi hiyo kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.

Tuesday 25 May 2010

MATOKEO MECHI ZA KIRAFIKI:
Jumanne, Mei 25
Armenia 3 v Uzbekistan 1
Ukraine 4 Lithuania 0
Georgia 0 v Cameroun 0
Greece 2 v Korea Kaskazini 2
Montenegro 0 v Albania 1
Nigeria 0 v Saudi Arabia 0
Republic of Ireland 2 v Paraguay 1 
USA 2 Czech Republic 4
RATIBA MECHI ZA KIMATAIFA ZA KIRAFIKI
Jumatano, Mei 26
Azerbaijan v Moldova [saa 1 usiku]
Estonia v Croatia [saa 1 usiku]
France v Costa Rica [saa 4 usiku]
Uholanzi v Mexico [saa 3 usiku]
Uturuki v Northern Ireland [saa 2 na nusu usiku]
Uruguay v Israel [saa 4 usiku]
SHAKIRA NA 'TIME FOR AFRICA', 'WIMBO WA TAIFA KOMBE LA DUNIA' BONDENI!! [Bofya hapa kwa Taarifa Zaidi]

Barca yapiga domo tu bila ofa ya Fabregas!!
Barcelona imesema wameongea na Arsenal na kuwafahamisha nia yao ya kutaka kufanya mazungumzo ili wamnunue Cesc Fabregas lakini hamna ofa yeyote iliyotolewa.
Fabregas aliiambia Arsenal wiki iliyokwisha nia yake ya kurudi Barca Timu aliyoanzia kucheza mpira akiwa mtoto kabla kujiunga na Arsenal.
Hata hivyo dalili zinaonyesha Arsenal hawatamwachia kirahisi Nahodha wao.
Mkurugenzi Mkuu wa Barcelona, Joan Oliver, amesema: “Bado hatujatoa ofa ila tumewajulisha nia yetu kufanya mazungumzo. Hatuna haraka.”
Nae Baba yake Mzazi Fabregas, Francesc Fabregas, amesema mjadala wa Arsenal na Barca utachukua muda mrefu kwa vile ishu yenyewe ni ngumu.
Baba huyo amekiri kuwa wao siku zote wanaishukuru Arsenal kwa kumkomaza Cesc kutoka Mtoto hadi kuwa Mwanaume kamili.
Fabregas ana Mkataba na Arsenal hadi 2012.
Ufaransa yataja Kikosi cha mwisho cha Wachezaji 23
Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech ametangaza Kikosi chake cha Wachezaji 23 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia na majina hayo ndiyo yatawasilishwa FIFA Juni 1.
Ufaransa, iliyokuwa na Wachezaji 24 kambini, ilipata pigo pale Kiungo Lassana Diarra alipoumia na Domenech amesema haongezi Mtu na Kikosi kilichobaki ndicho cha mwisho na kitaenda Kombe la Dunia.
Kikosi kamili:
Makipa: Hugo Lloris (Olympique Lyon), Steve Mandanda(Olympique Marseille), Cedric Carrasso (Girondins Bordeaux)
Walinzi: Bacary Sagna (Arsenal), Patrice Evra (Manchester United), William Gallas (Arsenal), Eric Abidal (Barcelona), Sebastien Squillaci (Sevilla), Marc Planus (Girondins Bordeaux), Gael Clichy(Arsenal), Anthony Reveillere (Olympique Lyon)
Viungo: Alou Diarra(Girondins Bordeaux), Jeremy Toulalan (Olympique Lyon), Florent Malouda (Chelsea), Yoann Gourcuff (Girondins Bordeaux), Abou Diaby (Arsenal), Franck Ribery (Bayern Munich)
Mafowadi: Thierry Henry (Barcelona), Nicolas Anelka (Chelsea), Andre-Pierre Gignac (Toulouse), Sidney Govou (Olympique Lyon), Djibril Cisse (Panathinaikos), Mathieu Valbuena (Olympique Marseille)
England 3 Mexico 1
Wakicheza mechi yao ya kwanza ya kujipima nguvu tangu waweke kambi Nchini Austria kwa ajili ya Kombe la Dunia wiki moja iliyopita, England waliweza kuilaza Mexico, ambayo nayo pia iko Fainali za Kombe la Dunia, kwa bao 3-1.
Hadi mapumziko, England walikuwa mbele kwa bao 2-1.
Bao la kwanza la England lilifungwa dakika ya 17 baada ya kona ya Gerrard kumkuta Crouch aliepiga kichwa na kumfikia Ledley King aliemalizia kwa kichwa.
Bao la pili alifunga Peter Crouch baada kichwa cha Wayne Rooney kupanguliwa na Kipa Perez na mpira kugonga mwamba wa juu na kumbabatiza Crouch mkononi na kutinga wavuni.
Mexico walipata bao lao Mfungaji akiwa Franco kwenye dakika ya 48 baada ya kona.
Kipindi cha pili Mexico walimwingiza Mchezaji mpya wa Manchester United, Javier Hernandez aka Chicharito, kuchukua nafasi ya Franco alieumia.
England walifunga bao la 3 dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza baada ya Beki wa Kulia, Glen Johnson, kupanda na kuachia fataki iliyopinda hadi wavuni.
Vikosi vilivyoanza:
England: Green, Glen Johnson, Ferdinand, King, Baines, Walcott, Gerrard, Carrick, Milner, Crouch, Rooney.
Akiba: Hart, James, Carragher, Dawson, Upson, Warnock, Lennon, Parker, Huddlestone, Wright-Phillips, Adam Johnson, Heskey, Defoe
Mexico: Perez, Juarez, Aguilar, Marquez, Salcido, Osorio, Torrado, Rodriguez, Giovani, Franco, Vela.
Akiba: Ochoa, Michel, Barrera, Castro, Blanco, Hernandez, Moreno, Guardado, Magallon, Torres, Bautista, Medina, Jonathan.
MATOKEO MECHI ZA KIRAFIKI:
Jumatatu, Mei 24
Argentina 5 v Canada 0 
Australia 2 v New Zealand 1
England 3 v Mexico 1
Japan 0 v Korea Kusini 2
Ureno 0 v Cape Verde 0
Afrika Kusini 1 v Bulgaria 1
RATIBA MECHI ZA KIRAFIKI:
Jumanne, Mei25
[saa za bongo]
Armenia v Uzbekistan [saa 12 jioni]
Georgia v Cameroun [saa 1 usiku]
Greece v Korea Kaskazini [saa 3 usiku]
Montenegro v Albania [saa 3 na robo usiku]
Nigeria v Saudi Arabia
Republic of Ireland v Paraguay [saa 3 dak 45 usiku]
Ukraine v Lithuania [saa 1 usiku]

Monday 24 May 2010

Hatma ya Mourinho Masaa 24 yajayo
Jose Mourinho anategemewa kumjulisha Rais wa Inter Milan, Massimo Moratti, uamuzi wake wa kujiunga na Real Madrid katika Masaa 24 yajayo.
Licha ya kuwa na Mkataba na Inter Milan hadi Juni 2012, kuna kipengele kwenye Mkataba huo kinachomruhusu Mourinho kuhama kabla kwisha.
Msemaji wa Mourinho amethibitisha atakutana na Moratti ndani ya Masaa 24 ili kuwekana sawa.
Wakati kuna taarifa za Wakala wa Mourinho, Jorge Mendes, kuwa Mjini Madrid akikamilisha mambo huko Milan, Meya wa Milan, Letizia Moratti, ambae ni Shemeji yake Massimo Moratti, Rais wa Inter Milan, amewalaumu Wanahabari wa Italia kwa kuondoka kwa Mourinho.
Mama huyo Meya amelalamika: “Naomba Wanahabari wajaribu kumbembeleza Mourinho abaki kwani ni kosa lao! Anaondoka kwa sababu kwingineko Ulaya Waandishi hawapondi Watu ovyo!”
Leo England v Mexico Uwanjani Wembley
Matayarisho ya England kwa ajili ya Kombe la Dunia leo yatapata mtihani Uwanja wa Wembley Jijini London watakapocheza na Timu ngumu Mexico kuanzia saa 4 usiku saa za bongo.
England walikuwa kambini Nchini Austria ambako watarudi tena baada ya mechi hii.
Inategemewa leo Fabio Capello, Kocha wa England, atawapumzisha Mastaa kama kina John Terry, Frank Lampard na Ashley Cole kwa vile walicheza Fainali ya FA Cup wiki moja iliyopita na badala yake watachezeshwa kina Joe Hart, Ledley King, Tom Huddlestone na wengineo ambao hucheza England kwa nadra ili kuwapa nafasi waonekane kabla Kikosi hakijapunguzwa kutoka Wachezaji 30 hadi 23 ifikapo Juni 1 kama inavyotakiwa na FIFA.
Hata hivyo Mexico si Timu ya kuibeza na ikiongozwa na Kocha Javier Aguero pia iko matayarishoni kwa Kombe la Dunia na wapo Kundi A pamoja na Afrika Kusini, Ufaransa na Uruguay.
Mexico inao Wachezaji stadi kama vile Andres Guardado Winga anaechezea Deportivo, Giovani Dos Santos, Mchezaji wa Tottenham aliekopeshwa nje, Carlos Vela wa Arsenal, Guillermo Franco wa West Ham na Mchezaji mpya wa Manchester United, Javier Hernandez maarufu kama Chicharito.
Difensi yao inaongozwa na Rafael Marquez wa Barcelona akishirikiana na Ricardo Osorio.
Vikosi vinategemewa kuwa:
England: Hart, Johnson, King, Ferdinand, Baines, Lennon, Huddlestone, Milner, Gerrard, Crouch, Rooney.
Mexico: Ochoa, Salcido, Marquez, Osorio, Juarez, Guardado, J Dos Santos, Torrado, G Dos Santos, Franco, Blanco
Mnigeria ang’aka kutaka kuinunua Ze Gunners
Bilionea wa Nigeria Aliko Dangote alietangazwa kutaka kununua Hisa za Arsenal za Asilimia 16 amekanusha habari hizo na kudai hana nia hiyo.
Ripoti zilidai Dangote atanunua Hisa za Mama Nina Bracewell-Smith ambae ameziweka sokoni Hisa zake za Asilimia 16 zenye thamani ya Pauni Milioni 160.
Dangote amesema ingawa aliwahi kufanya mazungumzo siku za nyuma kuhusu kuwekeza Klabu ya Arsenal hivi sasa hana nia hiyo.
Dangote anakadiriwa kuwa na Fedha kiasi cha Pauni Bilioni 2.3.
Wadau wakubwa wa Arsenal ni Mmarekani Stan Kroenke mwenye Hisa Asilimia 29.88 na Mrusi Alisher Usmanov mwenye Asilimia 26.29.
Kuuzwa kwa Hisa za Mama Bracewell-Smith kumeibua hisia kuwa Wamiliki hao wakubwa watapigania kununua Hisa hizo ili kuiimiliki Klabu hiyo kwani Sheria zinasema kuwa Mdau mwenye Hisa Asilimia 30 anatakiwa kutoa ofa ya kuinunua Klabu yote.
Hadi sasa Wadau hao, Kroenke na Usmanov, hawajabainisha nia zao.

Sunday 23 May 2010

Kibopa wa Nigeria ataka hisa Ze Gunners!!!
Bilionea mmoja wa huko Nigeria anaesifika kuwa ni tajiri wa kupindukia anataka kuzinunua Hisa za Klabu ya Arsenal za Asilimia 16 ambazo inadaiwa zitauzwa na Mmiliki wake Mama Nina Bracewell-Smith na inasemekana Tajiri huyo, Aliko Dangote, amekazania kuzitwaa.
Mpaka sasa ndani ya Arsenal kuna mvutano mkubwa kati ya Wamiliki wake wakuu wawili wa Hisa zake, Mmarekani Stan Kroenke na Mrusi Alisher Usmanov, ambao wanavuta nikuvute ya kutaka kuzoa Hisa nyingi ili wadhibite Klabu.
Dangote ni Mmiliki wa Kampuni kubwa ya Uzalishaji huko kwao iitwayo Dangote Group na ashawahi kuwa Mkuu wa Soko la Hisa huko Nigeria.
Shea za Mama Nina Bracewell-Smith zinauzwa kwa thamani ya Pauni Milioni 160 na Dangote yumo katika Listi ya mwisho ya Watu wanaofaa kuzinunua.
Rio yu tayari kwa Unahodha!!
Rio Ferdinand amesema yuko tayari kwa kila kitu ili kuiongoza England kama Kepteni kwenye Kombe la Dunia ingawa amekuwa na Msimu mbaya kwenye Klabu yake Manchester United kufuatia kuandamwa na maumivu ya mara kwa mara yaliyomfanya aichezee Klabu yake mechi 21 tu Msimu wote wa 2009/10 ulioisha Mei 9.
Rio amekuwa akisumbuliwa na tatizo la mgongo Msimu wote lakini amesema yuko fiti na anajisikia freshi sana kwa vile alizoea kucheza mechi 40 mpaka 50 kwa Msimu lakini Msimu huu amecheza mechi chache mno.
Rio alikuwemo kwenye Kikosi cha England cha Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 1998 huko Ufaransa na England wakatolewa Raundi ya Pili na Argentina lakini yeye hakucheza hata mechi moja.
Rio, aliechukua Unahodha wa England baada ya John Terry kutimuliwa baada ya skandali, alicheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2002 na 2006 ambazo zote walitolewa Robo Fainali na Brazil na iliyofuatia na Ureno.
England wataanza kampeni yao ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini Juni 12 kwa kucheza na USA Mjini Rustenburg.
Rio ametamka: “Kuwa Nahodha ni heshima kubwa na ni wajibu ambao nauhusudu! Lakini hili haliwezi kunibadili! Ntabaki vilevile tu! Kabla sijawa Kepteni Wachezaji Chipukizi walikuwa wanajua mie ni mtu rahimu wanaeweza kumfuata wakiwa na tatizo na hilo ni muhimu kuliko kuwa Nahodha!”
Gerrard azua utata kubaki Liverpool!!!!!
Steven Gerrard ameididimiza Liverpool katika utata mkubwa aliposema hatma yake kubaki au kuondoka Klabu hiyo itajulikana baada ya Fainali za Kombe la Dunia.
Gerrard yuko kambini Nchini Austria pamoja na Kikosi cha England kinachojitayarisha na Kombe la Dunia.
Liverpool, baada ya kumaliza Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 7, wamekosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao na hilo limemvunja moyo Gerrard na kuzua mjadala kuwa Nahodha huyo wa Liverpool atahama.
Gerrard, mwenye miaka 29 ambae Mwaka 2004 nusura asaini Chelsea lakini akabadili mawazo dakika za mwisho, amesema: “Sitafikiria wala kuamua lolote mpaka baada ya Kombe la Dunia. Baada ya hapo huwa tunakuwa na Wiki 3 au 4 za holidei na huo ni wakati mzuri kuamua hatma yako!”
MECHI ZA KIMATAIFA ZA KIRAFIKI
Nchi nyingi zipo kambini kwa matayarisho ya Kombe la Dunia litaloanza Juni 11 huko Afrika Kusini na maandalizi hayo yanajumuisha mechi mbalimbali za kujipima.
Ifuatayo ni Ratiba ya baadhi ya mechi hizo kwa Wiki hii:
Jumatatu, Mei 24
[saa za bongo]
Argentina v Canada [saa 4 na nusu usiku]
Australia v New Zealand [saa 6 na nusu mchana]
England v Mexico [saa 4 usiku]
Japan v Korea Kusini [saa 7 dak 20 mchana]
Ureno v Cape Verde [saa 3 dak 20 usiku]
Afrika Kusini v Bulgaria [saa 3 dak 35 usiku]
Jumanne, Mei25
Armenia v Uzbekistan [saa 12 jioni]
Georgia v Cameroun [saa 1 usiku]
Greece v Korea Kaskazini [saa 3 usiku]
Montenegro v Albania [saa 3 na robo usiku]
Nigeria v Saudi Arabia
Republic of Ireland v Paraguay [saa 3 dak 45 usiku]
Ukraine v Lithuania [saa 1 usiku]
Jumatano, Mei 26
Azerbaijan v Moldova [saa 1 usiku]
Estonia v Croatia [saa 1 usiku]
France v Costa Rica [saa 4 usiku]
Uholanzi v Mexico [saa 3 usiku]
Uturuki v Northern Island [saa 2 na nusu usiku]
Uruguay v Israel [saa 4 usiku]
USA v Czech Republic [saa 9 usiku]
Alhamisi, Mei 27
Belarus v Honduras [saa 1 na nusu usiku]
Chile v Zambia
Denmark v Senegal [saa 3 na robo usiku]
Afrika Kusini v Colombia [saa 3 dak 35 usiku]
Mourinho yuko njiani kwenda Real!!
Kocha wa Inter Milan Jose Mourinho, ambae jana aliweka historia ya kuchukua Trebo, yaani kunyakua Vikombe vitatu kwa mpigo katika Msimu mmoja vikiwa ni Ubingwa wa Serie A, Coppa Italia na Klabu Bingwa Ulaya, amesema Real Madrid itakuwa nyumba yake ya tatu akimaanisha ataondoka Inter.
Jana Mourinho aliingia kwenye historia ya kuwa Meneja wa tatu kutwaa Ubingwa wa Ulaya akiwa Klabu mbili tofauti baada ya Diego Milito kupiga bao mbili na kuwaliza Bayern Munich na kuwafanya Inter wanyakue Kombe la UEFA CHAMPIONS LIGI.
Mourinho amesema: “Inter ni kwangu kama ilivyokuwa Chelsea. Ilikuwa ngumu kuhama Chelsea na nikihama Inter ni ngumu lakini hayo ni maisha, ndio Soka! Nilikuwa na nyumba mbili, Chelsea na Inter na sasa ntakuwa nay a tatu-Real Madrid!”
Alipoulizwa kwa nini anavutiwa na Real, Mourinho alijibu: “Ndio Klabu pekee inayonitaka!”
Inter Bingwa Ulaya!!!!!!
• Inter 2 Bayern 0
Diego Milito amedhihirisha yeye ndie Mfungaji Bora wa Inter Milan alipopachika bao 2 na kuwapa Inter Ubingwa wao wa kwanza wa Ulaya katika Miaka 45 walipoifunga Bayern Munich bao 2-0 katika Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI iliyochezwa Uwanja wa Santiago Bernabeau, Madrid, Spain.
Katika mechi hii, Bayern walionekana kuutawala mchezo lakini walishindwa kuipenya ngome iliyoongozwa na Lucio na dhahiri walionyesha kumkosa Franck Ribery.
Milito alifunga bao la kwanza dakika ya 35 na la pili dakika ya 70.
Bao la la kwanza la Inter lilianza kwa Kipa Julio Cesar aliepandisha mpira wa juu mbele na Diego Milito akaupoza kwa pasi ya kichwa kwa Sneijder na Sneijder hakuchelewesha akapenyeza pasi kwa Milito aliekuwa kachomoka kuingia ndani ya boksi na Straika huyo toka Argentina hakufanya ajizi akamchambua Kipa wa Bayern, Butt, na kutingisha wavu.
Bao la pili lilitokana na pande la Samuel Eto’o kumkuta Milito nje ya boksi na akawahadaa Van Buyten na Demichelis kisha kumdanganya Kipa Butt kwa shuti la kifundi.
Vikosi vilivyoanza:
Bayern Munich: Butt; Lahm, Badstuber, Van Buyten, Demichelis; Altintop, Van Bommel, Schweinsteiger, Robben; Olic, Muller.
Inter Milan: Cesar; Maicon, Lucio, Samuel, Zanetti; Cambiasso, Pandev; Eto’o, Sneijder, Chivu; Milito.
Refa: Howard Webb (England).
Powered By Blogger