Saturday 17 April 2010

Ni siku njema kwa Man United!!!
Chelsea yashindiliwa, Man United wawaliza Mahasimu sekunde ya mwisho!!
Katika dabi ya Manchester iliyochezwa City of Manchester Stadium, Manchester United waliwatungua Mahasimu wao wakubwa Manchester City kwa bao 1-0 bao lililofungwa na Paul Scholes katika sekunde za mwisho za gemu hiyo.
Katika mechi iliyofuata baadae, wamepata pigo kubwa walipowashwa na Tottenham bao 2-1 Uwanjani White Hart Lane na kufanya wawe pointi moja tu mbele ya Man United huku kukiwa kumebaki mechi 3.
Ushindi wa Tottenham umewafanya washikilia nafasi ya 4 na sasa wana pointi 64 na Man City wako nafasi ya 5 wakiwa na pointi 62.
Mabao ya Tottenham yalifungwa na Jermaine Defoe kwa penalti na Bale akafunga bao la pili.
Hakika ni siku tamu kwa Man United kwa matumaini yao ya kutwaa Ubingwa tena kufufuliwa tena.
MATOKEO KAMILI MECHI ZA LEO:
Birmingahm 0 Hull City 0
Blackburn 2 Everton 3
Fulham 0 Wolves 0
Man City 0 Man United 1
Stoke 1 Bolton 2
Sunderland 2 Burnley 1
Tottenham 2 Chelsea 1

Friday 16 April 2010

DABI YA MANCHESTER: Ni utamu Msimu huu!
Vigogo wa Manchester, Manchester City na Manchester United, wanavaana Jumamosi Uwanja wa City of Manchester, kwenye mechi ya Ligi Kuu ambayo ina umuhimu mkubwa mno.
Siku zote huwa ni pambano linalongojewa kwa hamu lakini msimu huu kuna vikorombwezo vingi ndani yake.
Ingawa Manchester United yuko mbele sana kupita Man City kimafanikio lakini Wadau wanadai pengo kati yao linaanza kupungua baada ya Man city kununuliwa na Matajiri wakubwa.
Man City Msimu huu, kwa mara ya kwanza katika historia yao, wananyemelea kupata nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Man United wao wapo hatarini kushindwa kuutetea Ubingwa wao Msimu huu wakiwa wanataka kuchukua Ubingwa kwa mara ya 4 mfululizo lakini hadi sasa kukiwa kumebaki mechi 4 tu wako pointi 4 nyuma ya Chelsea ambao wako kileleni.
Ushindi kwa Man United dhidi ya Mahasimu wao wakubwa ni kitu cha lazima mno ikiwa wanataka kutwaa Ubingwa.
Lakini Man City nao pia ni lazima washinde mechi hii ili wajichimbie nafasi ya 4 ambayo pia inawaniwa vikali na Tottenham walio pointi moja myuma yao.
Msimu huu, Man City ishawahi kuifunga Man United Uwanjani hapo City of Manchester bao 2-1 katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling lakini kwenye marudiano huko Old Trafford, Man City walitandikwa bao 3-1 na kubwagwa nje ya Kombe hilo ambalo hatimaye lilichukuliwa na Man United walipoitwanga Aston Villa 2-0 kwenye Fainali.
Kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Msimu huu huko Old Trafford mwezi Septemba, Man United waliibamiza Man City 4-3 katika mechi iliyokuwa vuta ni kuvute.
Ifuatayo ni Historia ya Mechi kati yao kwenye Ligi Kuu zilizochezwa nyumbani kwa Man City tu (Wafungaji kwenye mabano):
30 Novemba 2008
Man City 0 Man Utd 1 (Rooney)
19 Agosti 2007
Man City 1 (Geovanni) Man Utd 0
5 Mei 2007
Man City 0 Man Utd 1 (Ronaldo)
14 Januari 2006
Man City 3 (Sinclair, Vassell, Fowler) Man Utd 1 (Van Nistelrooy)
13 Februari 2005
Man City 0 Man Utd 2 (Rooney, Dunne og)
14 Machi 2004
Man City 4 (Fowler, Macken, Sinclair, Wright-Phillips) Man Utd 1 (Scholes)
9 Novemba 2002
Man City 3 (Anelka, Goater 2) Man Utd 1 (Solskjaer)
18 Novemba 2000
Man City 0 Man Utd 1 (Beckham)
6 Aprili 1996
Man City 2 (Kavelashvili, Rosler) Man Utd 3 (Cantona, Cole, Giggs)
11 Februari 1995
Man City 0 Man Utd 3 (Cole, Ince, Kanchelskis)
7 Novemba 1993
Man City 2 (Quinn 2) Man Utd 3 (Cantona 2, Keane)
20 Machi 1993
Man City 1 (Quinn) Man Utd 1 (Cantona)
Mancini apatikana na hatia, akwepa kifungo,apigwa Faini
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amepatikani na hatia kwa kosa la kutokuwa na mwenendo mzuri na hivyo kupigwa Faini ya Pauni Elfu 20 na FA kufuatia mshikemshike kati yake na Meneja wa Everton, David Moyes, uliotokea Machi 24 Man City ilipoikaribisha Everton City of Manchester Stadium na Refa wa mechi hiyo akalazimika kuwatoa wote wawili Uwanjani.
Mancini alikiri kosa lake na akaomba adhabu ndogo kwa vile ni kosa lake la kwanza na pia alikwisha kumuomba msamaha David Moyes mara baada ya mechi hiyo.
Faini ya Mancini imesitishwa hadi mwishoni mwa Msimu wa 2011/12 ili kumwangalia asifanye kosa hadi wakati huo.

Thursday 15 April 2010

Wenger Mikono juu Ubingwa!!
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema Timu yake iusahau Ubingwa kufuatia kichapo cha Jumatano cha 2-1 mikononi mwa Tottenham kilichowafanya wawe pointi 6 nyuma ya vinara Chelsea na mechi zikiwa zimebaki 4.
Wenger amesema: “Ubingwa basi! Sisi tufikirie kumaliza juu kadri tuwezavyo!”
Wenger amekiri Timu yake haijakomaa na hilo limeonekana walipofungwa na Tottenham kwani mechi hizo ndizo za kushinda ili kuonyesha umekomaa.
Hata hivyo, Wenger amesisitiza wao wataendelea kupigana hadi mwisho ingawa sasa nafasi yao ya Ubingwa ni finyu.
Pia, Wenger alionyesha kufurahishwa na kurudi Uwanjani kwa Straika wake mahiri Robin van Persie alieingizwa mwishoni baada ya kupona enka iliyomweka miezi mitano nje.
Wenger alisema alipoingia Van Persie Arsenal ilibadilika na kuwa na uhai mbele.
Barca yaisuta Arsenal
Barcelona wamegoma kuwa wana makubaliano na Arsenal ya kutomrubuni Cesc Fabregas na hilo linapingana na kauli ya Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood, ambae alitamka kuwa wana makubaliano na Barcelona ya kuitaka Klabu hiyo ya Spain isimrubuni Nahodha Wao Cesc Fabregas ambae amekuwa akivumishwa kwa muda mrefu kuwa yuko njiani kwenda Barcelona Msimu ujao.
Hill-Wood alisema: “Tuna makubaliano na Barca ya kuwataka wasimfuate Fabregas ila baadae wanaweza kuja kwetu moja kwa moja."
Lakini Katibu wa Ufundi wa Barcelona Txiki Begiristain amesisitiza hawana makubaliano yeyote na Arsenal na kama wakimtaka Fabregas wataongea na Arsenal.
Begiristain amesema: ‘Hatujasema hatutamsaini. Tukimtaka tutaanzisha mazungumzo!”
PFA yatoa Listi ya Wagombea Mchezaji Bora wa Mwaka
Straika wa Manchester United na England, Wayne Rooney, yumo katika Listi ya Wagombea wanne na ndie anaepewa nafasi kubwa ya kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora ya PFA [Chama cha Wachezaji wa Kulipwa wa Soka].
Wengine kwenye Listi hiyo ni Kiungo wa Arsenal Cesc Fabregas, Didier Drogba wa Chelsea na Carlos Tevez wa Manchester City.
Rooney na Fabregas pia wamo kwenye Listi kama hiyo lakini ya Vijana na wanaungana na James Milner wa Aston Villa na Kipa wa Birmingham Joe Hart kwenye Listi hiyo.
Ikiwa Rooney atashinda Tuzo hiyo hii itakuwa ni mara ya 4 mfululizo kwa Mchezaji wa Manchester United kuinyakua.
Wachezaji wengine wa Man United walioshinda Tuzo hiyo ni Cristiano Ronaldo alieshinda mwaka 2007 na 2008 na mwaka jana Ryan Giggs ndie alieinyakua.
Rooney na Fabregas washawahi kushinda Tuzo hii kwa Vijana hapo nyuma wakati Rooney alipoinyakua mwaka 2005 na 2006 na Fabregas kushinda 2008.
Ze Gunners yabondwa, Chelsea njia nyeupeeee…….!!!
Jana, Uwanjani White Hart Lane, Tottenham waliibonda Arsena kwa bao 2-1 katika dabi ya Ligi Kuu England ambayo huenda ndio imemaliza kabisa ile kiu ya Arsenal ya angalau kupata Kikombe kimoja Msimu huu na kuumaliza ule ukame wao wa kutokuwa na Kikombe tangu 2005 kwani sasa wako nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi 6, nyuma ya Man United kwa pointi 2 na mechi zimebaki 4 tu.
Ushindi huu kwa Tottenham bado unaweka hai matumaini yao ya kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya 4 na hivyo kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao kwani sasa wako nafasi ya 5 pointi moja tu nyuma ya Manchester City walio nafasi ya 4 huku Timu hizo mbili zikiwa zimebakiza mechi 5 kila mmoja.
------------------------------------------------
MSIMAMO LIGI KUU [Kwa Timu za juu]:
1. Chelsea mechi 34 pointi 77
2. Man United mechi 34 pointi 73
3. Arsenal mechi 34 pointi 71
4. Man City mechi 33 pointi 62
5. Tottenham mechi 33 pointi 61
6. Liverpool mechi 34 pointi 56
7. Aston Villa mechi 33 pointi 55
8. Everton mechi 34 pointi 51
9. Birmingham mechi 34 pointi 46
10.Stoke mechi 33 pointi 43
11.Blackburn mechi 34 pointi43
-----------------------------------------------
Alikuwa ni Mchezaji aliekuwa akicheza Ligi kwa mara ya kwanza, Danny Rose, aliipeleka Tottenham mbele kwa mzinga wa mita 30 kwenye dakika ya 10.
Dakika moja baada ya haftaimu, Gareth Barry akaipatia Spurs bao la pia alipopokea pasi toka kwa Jermain Defoe.
Kipa wa Spurs, Heurelho Gomes aliokoa michomo mitatu ya Arsenal lakini baadae akashindwa kumzuia Niklas Bendtner wa Arsenal kuifungia Timu yake bao.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Tottenham kwa Arsenal katika Ligi tangu Novemba 1999 na mechi 20 zimepita kati yao tangu wakati huo.
Wote, Tottenham na Arsenal, waliingia kwenye dabi ya jana wakitoka kwenye vipigo vitakatifu pale Tottenham alipobwagwa nje ya FA Cup na Timu hoi bin taabani Portsmouth walipochapwa 2-0 kwenye Nusu Fainali Uwanjani Wembley Jumapili na Arsenal kupata kipigo cha mbwa kachoka huko Nou Camp cha bao 4-1 toka kwa mtu mmoja tu, Lionel Messi, kilichowafanya Barcelona waisokomeze Arsenal nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Arsenal, kwa mara nyingine tena, walipata pigo pale Beki wao Thomas Vermaelen aliposhindwa kuendelea na mechi na kutoka nje akichechemea na nafasi yake kuchukuliwa na Mkongwe Mikael Silvestre alieungana na Mkongwe mwingine Sol Campbell kama Masentahafu.
Lakini Arsenal walipata faraja kidogo walipomwona Straika wao Robin van Persie akiingizwa na kucheza baada ya miezi mitano nje akiuguza enka na kuingia kwake kulimfanya Kipa wa Spurs Gomes aokoe mipira miwili hatari toka kwake.
Aston Villa 2 Everton 2
Bao la kujifunga mwenyewe la Phil Jagielka katika dakika za majeruhi zimewapa sare Aston Villa wakiwa nyumbani Villa Park walipocheza na Everton kwenye Ligi Kuu hapo jana.
Tim Cahill wa Everton ndie aliepachika bao la kwanza kwa Everton kufuatia krosi ya Leighton Baines na kichwa cha Gabriel Agbonlahor kiliwasazishia Villa lakini haikuchukua muda mrefu Tim Cahill akafunga bao la pili kwa Everton.
Sare hii si matokeo mazuri kwa Timu zote hizo mbili, Villa wakipoteza matumaini ya kupata nafasi ya 4 na Everton sasa wanabanwa kuipata nafasi ya kucheza EUROPA LIGI.
Wigan 0 Portsmouth 0
Kwenye mechi ya Ligi Kuu hapo jana, Wigan jana ilishindwa kuifunga Timu hoi bin taabani Portsmouth ambayo tayari ishashushwa Daraja na jana iliingia Uwanjani ikiwa Timu ya kuungwaungwa tu huku Meneja wao Avram Grant akishindwa kukamilisha idadi ya Wachezaji wa Akiba wanaoruhusiwa kuwa benchi ya Wachezaji 7 pale alipolazimika kuwa na Wachezaji wanne tu benchi kutokana na matatizo ndani ya Klabu hiyo.
Portsmouth walibadilisha Wachezaji wanane toka Kikosi kilichoifunga Tottenham 2-0 Jumapili na kuwafikisha Fainali za Kombe la FA lakini Wigan walishindwa kuwafunga.
Sare hii imewafanya Wigan wawe pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho ambazo zipo eneo hatari la kushushwa Daraja.

Wednesday 14 April 2010

Arsenal wakataa kutaka kumuuza Fabregas Msimu ukiisha
Mwenyekiti wa Arsenal Peter Hill-Wood ametamka kuwa wana makubaliano na Barcelona ya kuitaka Klabu hiyo ya Spain isimrubuni Nahodha Wao Cesc Fabregas ambae amekuwa akivumishwa kwa muda mrefu kuwa yuko njiani kwenda Barcelona Msimu ujao.
Hill-Wood amesema: “Tuna makubaliano na Barca ya kuwataka wasimfuate Fabregas ila baadae wanaweza kuja kwetu moja kwa moja."
Mwenyekiti huyo alitilia mkazo imani yake kuwa makubaliano hayo hayawezi kuvunjwa na akasisitiza kwamba Arsenal na Barca walikutana Aprili 6 kulijadili hilo kwa mara nyingine na kukubaliana tena.
Fabregas ana Mkataba na Arsenal hadi mwaka 2014.
Lakini kila siku kumekuwa na uvumi kuwa Fabregas atarudi Barca Klabu aliyoanza kuichezea tangu akiwa mtoto.
Juve yampa siku 10 Rafa
Rafael Benitez amepewa siku 10 na Juventus aamue kama bado anataka kuhamia Klabu hiyo kwa Msimu ujao ili watayarishe listi yao ya nani wana nia ya kufanya kazi Juve.
Inaaminika listi ya Mameneja wanaotakiwa na Juventus ni pamoja na Kocha wa Brazil, Dunga, lakini Klabu hiyo kigogo ya Italia inamwona Benitez kama chaguo lao la kwanza.
Juventus ilimtimua Kocha wao Ciro Ferrara mwezi Januari na kumweka Kocha wa muda Alberto Zaccherano waliposhindwa kumchota Benitez wakati huo ingawa inadaiwa kulikuwa na makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Inasemekana Benitez ameahidiwa donge nono la kununua Wachezaji, kitu ambacho hakipati Liverpool, na pia Juve kuhamia kwenye Uwanja mpya Makao Makuu yao Mjini Turin.
‘Wakombozi Wekundu’ wanakamilisha ofa ya Man United
Habari zimeibuka kuwa lile Kundi la Matajiri wanaotaka kuiondoa Manchester United mikononi mwa Familia ya Kimarekani ya kina Glazer, Kundi linaloitwa “Wakombozi Wekundu’, wanategemewa kukamilisha ofa yao ya kuinunua Klabu hiyo wiki hii.
Ingawa Wamiliki wa Manchester United, Familia ya Glazer, imekuwa ikidai Klabu hiyo haiuzwi, ‘Wakombozi Wekundu’ wana imani ofa yao itawafanya Wamarekani hao waisikilize na kusogea mezani kujadiliana.
Kundi hili pia limepata nguvu baada ya Man United kutolewa nje ya Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LIGI na hivyo thamani ya Klabu kushuka chini.
Bolton wadai Chelsea wanabebwa!!!
Meneja wa Bolton Owen Coyle amemlaumu Refa Lee Probert kwa kuwanyima penalti mbili katika mechi ya jana ya Ligi Kuu ambayo Chelsea waliifunga Bolton 1-0 Uwanjani Stamford Bridge na kujichimbia uongozi wa Ligi wakiwa pointi 4 mbele.
Coyle amedai Drogba aliunawa mpira kipindi cha kwanza na John Terry nae aliucheza mpira kwa mkono kipindi cha pili na zote zilikuwa ni penalti za wazi.
Coyle amelalamika: “Hatukuhitaji bahati leo, tulihitaji Marefa waamue kwa haki!”
Coyle amedai Msaidizi wa Refa alisema ttukio la Terry mpira ulimgonga begani lakini Coyle amesisitiza alicheza wazi wazi kwa mkono.
Chelsea haooo..............!!!!!!
Chelsea 1 Bolton 0
Chelsea wamechanja mbuga na wako pointi 4 mbele katika uongozi wa Ligi kukiwa kumebaki mechi 4 Ligi kwisha baada ya kuitungua Bolton Wanderers bao 1-0.
Wakicheza kwao Stamford Bridge, Chelsea hawakuonekana kuwa kwenye fomu lakini Nicolas Anelka aliwapa ushindi dakika tatu kabla ya haftaimu alipofunga kwa kichwa baada ya krosi ya Didier Drogba.
Chelsea sasa wana pointi 77, Man United 73 na Arsenal 71 lakini leo wapo White Hart Lane kuikwaa Tottenham na ushindi kwao utawafanya wachupe nafasi ya 2.
Mechi za leo ni:
Jumatano, 14 Aprili 2010
[saa 3 dak 45 usiku]
Aston Villa v Everton
Wigan v Portsmouth
[saa 4 usiku]
Tottenham v Arsenal

Tuesday 13 April 2010

Chelsea kakamata usukani lakini njia ni Mahandaki matupu!!!
Mbio za kuelekea Ubingwa wa Ligi Kuu na ile vita ndogo ya kuchukua nafasi ya 4 vimepamba moto na kimsimamo Chelsea wako kwenye usukani katika kuwania Ubingwa na Manchester City wanaelekea kuinyakua nafasi ya 4 itakayowafanya wacheze UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Sare ya Manchester United kwa Blackburn na Man City kuibamiza Birmingham ndio vimefungua pazia kuona wazi wazi mwelekeo wa Ligi ulivyo.
Endapo Chelsea leo usiku watawafunga Bolton watakuwa pointi 4 mbele kileleni na labda wapate matokeo mabovu mno kwenye mechi 4 zitakazobakia ndio waukose Ubingwa.
Huku mechi zikizidi kuyoyoma, kauli mbiu kwa Wadau imekuwa ni kuweka presha lakini Man United na Arsenal, hivi karibuni, zimeshindwa kuipa presha Chelsea.
Lakini siku zote hakuna alie na Ubingwa hadi umelitwaa Kombe mkononi na kwa Chelsea inabidi washinde mechi zao ili wawe Mabingwa.
Mara kadhaa Msimu huu, Chelsea wamekuwa wakishika hatamu na mara kadhaa wamekuwa wakiteleza.
Ingawa mechi zinazidi kuyoyoma, nani anasema hilo haliwezi kutokea tena hasa kwa vile wana mechi ngumu za ugenini na Tottenham ikiwa ni dabi ya London na ile ya Anfield na Liverpool?
Hata hivyo, ili wanufaike na kuteleza kwa Chelsea, ni lazima Manchester United na Arsenal washinde mechi zao.
Hilo kwa Man United linamaanisha lazima wakienda kwa Mahasimu wao wakubwa Manchester City, ndani ya Uwanja wa City of Manchester Jumamosi, ushindi ndio kitu pekee wanachotakiwa kukipata.
Wakifungwa mechi hiyo, basi Ubingwa bai bai Msimu huu.
Man United wakishinda mechi hiyo ya Jumamosi, presha itahamia kwa Chelsea wanaocheza baadae siku hiyo na Tottenham kwani wanajua Man United wako nyuma kwa pointi moja tu [hii ikiwa Chelsea ataifunga Bolton leo] na kila mtu anajua ukiwa na presha ni rahisi makosa kufanyika na lolote kutokea.
Lakini, hata kama Man United wataifunga Man City, Ubingwa bado mgumu kwani njia yao pekee ni kwanza kushinda mechi zao zote na pili Chelsea wateleze.
Arsenal nao wako kama Man United- ni lazima washinde mechi zao zote na Chelsea wateleze.
Arsenal wanaanza Jumatano kwa dabi ya Timu za London ya Kaskazini watakapoenda White Hart Lane kucheza na Tottenham ambao nao bado wanalilia nafasi ya 4.
Ni lazima Arsenal ashinde mechi hii na asiposhinda ni balaa.
Na hata wakishinda, mbele wana vigingi vingine navyo ni Man City watakaokwenda Emirates na pia safari ya Arsenal kwenda Ewood Park, Uwanja ambao Chelsea na Man United waliambua droo tu walipocheza na Blackburn.
Mbali ya sakata hilo na mahesabu hayo makali ya Nani Bingwa kati ya Chelsea, Man United na Arsenal, pia utamu upo kwenye kitimtim cha nani atachukua nafasi ya 4 na hivyo kuungana na Chelsea, Man United na Arsenal kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Man City ndio wanaishikilia nafasi hiyo ya 4 na inaelekea wao ndio watainyakua labda wavurunde.
Wengine wanaoiwania nafasi hiyo, na kimahesabu bado wamo kwenye vita hiyo, ni Tottenham, Liverpool na Aston Villa.
Kwa Liverpool na Aston Villa huenda ikawa finyu kuinyakua nafasi hiyo lakini Tottenham bado matumaini makubwa yapo ingawa njia yao ni ngumu kwani inabidi wacheze na Arsenal, Chelsea na Man United.
Ni mahesabu makali lakini bora tukae na kusubiri nini kitatokea kuanzia sasa hadi Mei 9 Ligi itakapofika tamati.
Berbatov nje?
Wadau wengi wanadai Dimitar Berbatov hajafanya lolote Manchester United tangu atue hapo Septemba 2008 kwa dau la Pauni Milioni 31 kutoka Tottenham na kuna tetesi za Magazetini kuwa mwishoni mwa Msimu atatemwa.
Ukweli ni kuwa tangu aanze kuchezea Man United, Berbatov amekuwa chaguo la pili katika mechi zote kubwa na pale alipokuwa chaguo la kwanza, ameshindwa kuwika na amekuwa akiwakera Washabiki wengi.
Inadaiwa Sir Alex Ferguson ameshachoshwa na atamuuza ili kuwanunua David Silva kutoka Valencia na Karim Benzema wa Real Madrid.
Hata hivyo, Wachunguzi wanaamini Berbatov hatauzwa kwa sababu Man United hawako tayari kumpoteza Straika mwingine baada ya kuwapoteza Cristiano Ronaldo na Carlos Tevez kwa mpigo na pia hata wakiamua kumuuza Berbatoz dau lake litakuwa chini mno na hiyo ni hasara kwa Klabu.
Adebayor astaafu Togo
Nahodha wa Timu ya Taifa ya Togo, Emmanuel Adebayor, anaechezea Manchester City, ametangaza rasmi kustaafu kuichezea Nchi yake Togo.
Timu ya Togo ilipata maafa Januari 8 iliposhambuliwa kwa risasi ikiwa kwenye Basi wakitokea Congo na kuingia Jimbo la Cabinda, Angola kwenda kushiriki Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika na Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa Togo wakauawa.
Togo ilijitoa Mashindanoni na baadae CAF ikaifungia Miaka minne.
Adebayor ametaja maafa hayo kuwa ndio yaliyochangia kwenye uamuzi wake.
Chelsea kuchanja mbuga?
Leo usiku, Chelsea wana nafasi ya kuongeza tofauti ya pointi kati yao na Manchester United, walio nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, kufikia pointi 4 watakapoikaribisha Bolton Wanderers Stamford Bridge.
Juzi, Man United walishindwa kuipiku Chelsea walipotoka sare 0-0 na Blackburn na hilo limemfanya Sir Alex Ferguson kukiri Ubingwa ni mgumu kwao na pia kusema mechi ya leo ni ubwete kwa Chelsea kauli iliyochekwa na Meneja wa Bolton, Owen Coyle, aliesema wao lengo lao ni kugangamara.
Van Persie kurudi Jumatano?
Arsenal Jumatano wapo kwenye dabi ya Timu za London ya Kaskazini watakaposafiri kwenda White Hart Lane kuivaa Tottenham katika mechi ya Ligi Kuu na hiyo ni mechi muhimu kwao kwani ushindi utaifanya waichomoe Manchester United toka nafasi ya pili lakini kwa Washabiki wa Ze Gunners kumuona Straika wao mahiri Robin van Persie akiwa Uwanjani ndio kutaleta furaha kubwa.
Van Persie yuko nje ya Uwanja tangu Novemba alipoumia enka akichezea Nchi yake Uholanzi mechi ya kirafiki na Italia.

Monday 12 April 2010

Pompey kukata rufaa ili wacheze Ulaya
Portsmouth watakata rufaa kwa FA ili waruhusiwe kupata leseni ya UEFA itakayowafanya waweze kecheza michuano ya Ulaya ya EUROPA LIGI Msimu ujao.
Kwa kuingia Fainali ya Kombe la FA, Portsmouth ambao wameshushwa Daraja, wamefuzu kucheza mechi za EUROPA LIGI kwa vile Chelsea, watakaocheza nao Fainali ya Kombe la FA, moja kwa moja watacheza UEFA CHAMPIONS LIGI kwa kumaliza Ligi Kuu nafasi 3 za juu.
Lakini kwa sababu Portsmouth iko chini ya Msimamizi Maalum alieteuliwa ili kuinusuru Klabu hiyo isifilisiwe, hairuhusiwi kuomba leseni ya UEFA.
Msimamizi Maalum, Andrew Andronikou, ametamka kuwa wataka rufaa kupinga hatua hiyo ingawa alikiri wao walishindwa kuomba leseni kabla ya siku ya mwisho ya maombi, tarehe yake ilikuwa Machi 1, kwa sababu Klabu ilikuwa taabani kifedha.
Burnley yamfungia Mchezaji wake
Kiungo wa Burnley Joey Gudjonsson amefungiwa wiki mbili kwa matamshi yake kuhusu Meneja wa Klabu hiyo Brian Laws na ametakiwa asikanyage Klabuni hadi uchunguzi ukamilike.
Inadaiwa Mchezaji huyo alisema kuwa Brian Laws ameshindwa kuikontroli Timu na Wachezaji wote wamekosa imani kwake na ndio maana Timu inafungwa ovyo.
Kauli hiyo inadaiwa kutolewa kabla Burnley haijakung’utwa 6-1 na Manchester City kwenye Ligi Kuu.
Jumamosi, Burnley iliipiga Hull City bao 4-0.
Coyle amcheka Fergie kwa kusema Bolton ubwete kwa Chelsea
Owen Coyle amepuuza kauli ya Sir Alex Ferguson kwamba pambano la Chelsea na Bolton hapo kesho huko Stamford Bridge ni mechi rahisi kwa Chelsea.
Ikiwa Chelsea watashinda hiyo kesho watakuwa pointi 4 mbele ya Manchester United ambao jana walitoka 0-0 na Blackburn.
Owen Coyle, Meneja wa Bolton, amesema wao wana kila sababu ya kuitilia ngumu Chelsea hasa kwa vile wako pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho zilizo eneo la kushushwa Daraja.
Coyle amesema: “Ni uamuzi wake kusema lolote! Sisi tutakazania nini cha kufanya na si nini kimesemwa.”
Wakati huo huo, Nahodha wa Bolton, Kevin Davies, amesema anadhani Mastraika wa Chelsea, Didier Drogba na Nicolas Anelka, hawana uhusiano mzuri na hilo huenda litaathiri Timu hiyo.
Liverpool kupigwa bei
Wamarekani, Tom Hicks na George Gillett, wanaoimiliki Liverpool wanategemewa kuiingiza Klabu hiyo sokoni wiki hii kufuatia hatua yao ya kuiteua Benki ya Barclays kusimamia zoezi hilo na pia kumteau Martin Broughton, aliewahi kuwa Mwenyekiti wa British Airways, kuwa Mwenyekiti wa Liverpool mwenye jukumu la kusaka Wawekezaji.
Wakiwa wanakabiliwa na deni kubwa, Wamarekani hao wamekubaliana na Wadai wao kusogeza mbele ulipaji wa deni hilo ili waendelee kutafuta Wanunuzi au Wawekezaji.
Wamarekani hao, ambao wanapingwa vikali na Mashabiki wa Klabu hiyo, wanataka kitita cha Pauni Milioni 500 ili kuiuza Liverpool.
Ubingwa ni utata - Ferguson
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amekiri kuchukua Ubingwa ni mzigo mkubwa kwao kufuatia sare yao ya 0-0 na Blackburn Jumapili.
Man United walikosa nafasi kadhaa za kufunga katika mechi hiyo na Ferguson amekiri: “Ni pigo, hamna ubishi! Sasa ni ngumu sisi kuchukua Ubingwa! Ni matokeo mazuri kwa Chelsea!”
Chelsea bado ni vinara na wana pointi 74 na Man United ni wa pili wana pointi 73 lakini wamecheza mechi moja zaidi ya Chelsea.
Wakicheza bila ya Mfungaji wao mkuu, Wayne Rooney, Ferguson aliwachezesha Chipukizi Frederico Macheda na Dimitar Berbatov kama Mastraika lakini Macheda alipwaya na kutolewa dakika ya 65 na kuingizwa Ji-Sung Park.
Nae Berbatov, huku zikiwa zimebaki dakika 10 mechi kwisha, alikosa bao la wazi.
Lakini ni makosa ya Winga Valencia ya kipindi cha kwanza ndio Ferguson aliyazungumzia pale Valencia alipokosa bao la wazi akiwa uso kwa uso na Kipa Robinson na kumpelekea mpira moja kwa moja badala ya kupiga pembeni.
Mechi inayofuata kwa Man United ni ile dabi yao na Mahasimu wao Manchester City siku ya Jumamosi Uwanja wa City of Manchester.
Chelsea wao wanacheza Jumanne na Bolton na Jumamosi wana dabi ya Timu za London watakapocheza na Tottenham.

Sunday 11 April 2010

AS Roma yaishusha Inter kileleni
Kwa mara ya kwanza katika Miezi mitano, Inter Milan imepokonywa uongozi wa Serie A na AS Roma walioshinda 2-1 leo dhidi ya Atalanta.
Jana Timu ya Jose Mourinho, Inter Milan, ilitoka sare 2-2 na Fiorentina.
Mabao ya AS Roma, inayoongozwa na Meneja Claudio Ranieri, yalifungwa na Mirko Vucinic na Marko Cassetti.
AS Roma sasa wana pointi 68 na Inter wapo pointi moja nyuma huku zikiwa zimebaki mechi 5.
Nafasi ya 3 imeshikwa na AC Milan ambao walitoka sare na Catania ya bao 2-2 na sasa wako pointi 4 nyuma ya Inter.
POMPEY…..Jana wameshushwa Daraja, Leo watinga Fainali FA CUP!!!
Hii ndio hadithi ya Sinderela ama ile stori ya kulala Maskini, kuamka Tajiri!!!
Portsmouth imepita kwenye Msimu wa balaa kabisa na nusura Klabu ife pale iliponusurika kufilisiwa lakini haikunusurika kushuka Daraja hasa ilipokatwa pointi 9 na jana ushindi wa West Ham ndio ukawahakikishia kucheza Ligi ya Coca Cola Championship Msimu ujao.
Lakini leo, ikiwa Uwanjani Wembley kwenye Nusu Fainali ya FA Cup, ilimudu kuibwaga Tottenham kwa bao 2-0 na kutinga Fainali hapo Mei 15 itakapocheza na Chelsea ambao jana waliwatoa Aston Villa bao 3-0.
Hadi dakika 90 ngoma ilikuwa 0-0 na ndipo ikaja ile nusu saa ya nyongeza na ndipo nyota ya Pompey ikaanza kuchomoza katika mechi ambayo muda wote walikuwa ni Timu ya pili kwa ubora.
Kwenye dakika ya 99 Pompey walipata frikiki iliyodondoshwa ndani ya boksi lakini katika harakati za kuokoa Beki wa Tottenham Dawson akateleza na Straika wa Pompey Frederic Piquionne akawa mwepesi na kuwahi hiyo ‘luzi boli’ na kuipenyeza kumpita Kipa Gomes.
Hadi nusu ya kwanza ya dakika 30 za nyongeza kwisha, Pompey walikuwa mbele kwa bao 1-0 lakini Spurs walikuwa wakishambulia mfululizo.
Huku Spurs wakiendelea kushambulia na Pompey kulinda bao lao ikafika dakika ya 117 na shambulio la Spurs likaokolewa na Pompey na wakaanza kufanya ‘kaunta ataki’ ya haraka kupitia Aruna Dindane ambae aliwahadaa Mabeki waliodhani atatoa pasi lakini akachanja mbuga mwenyewe kuingia ndani ya boksi na akaangushwa na Wilson Palacios.
Refa Alan Wiley akaashiria penalti na Kevin-Prince Boateng akafunga penalti hiyo.
AMINI USIAMINI….POMPEY 2 SPURS 0….NA WAKO FAINALI!!!!!!!!
Vikosi vilivyoanza:
Tottenham: Gomes, Corluka, Dawson, Bassong, Bale, Bentley, Huddlestone, Palacios, Modric, Crouch, Defoe.
Akiba: Alnwick, Pavlyuchenko, Gudjohnsen, Kranjcar, Rose, Livermore, Assou-Ekotto.
Portsmouth: James, Finnan, Rocha, Mokoena, Mullins, Brown, Wilson, Yebda, Dindane, Piquionne, Boateng.
Akiba: Ashdown, Diop, Utaka, Smith, Hughes, Kanu, Basinas.
Refa: Alan Wiley
Mechi zao ni 0-0, nini walisema………:
==Bosi wa Liverpool Rafael Benitez: "Nimesikitishwa. Nafasi ya 4 sasa iko mbali. Inategemea Timu nyingine, Timu 2 au 3 zitusaidie. Hilo ni kubwa mno. Torres hakucheza ameenda kuonana na Daktari Bingwa.”
==Meneja Msaidizi Man United Mike Phelan: "Sasa unaanza kuangalia matokeo ya Timu nyingine! Hatukubahatika leo lakini hata uteuzi wetu wa Timu haukuwa mzuri! Hatuwezi kumtegemea Rooney tu ingawa ni Mchezaji wetu mzuri! Hii ni Manchester United na Wachezaji wengine wanatakiwa waonyeshe kwa nini Klabu hii iliwanunua!”
==Bosi wa Blackburn Sam Allardyce: "Tulicheza jihadi na kupata pointi moja ni manufaa kwetu! Najua tunashindwa kufunga Msimu huu lakini defensi yetu ni nzuri!”
Man City yaishindilia Birmigham na kujichimbia nafasi ya 4
Wakiwa kwao City of Manchester Stadium, Manchester City leo wameitandika Birmingham mabao 5-1 na kutuma salam kwa Tottenham na Liverpool kuwa nafasi ya 4 kwenye Ligi Kuu ni yao.
Man City waliandika bao la kwanza kwa penalti iliyotolewa na Refa Phil Dowd dakika ya 35 pale Adebayor alipoingia ndani ya boksi na kuangushwa na Scott Dann.
Tevez akapiga penalti hiyo na kufunga bao la kwanza.
Dakika 5 baadae Man City wakawa bao 2 mbele kufuatia kona ya Adam Johnson kumkuta Nedum Onuoha aliefunga kwa kichwa.
Dakika 2 baadae Birmingham wakapata bao kupitia Cameron Jerome alieunganisha kwa kichwa krosi ya James McFadden.
Kabla ya mapumziko, Man City wakapachika bao la 3 baada ya mpira mrefu kukimbiliwa na Craig Bellamy alieuwahi kabla ya Kipa Maik Taylor na kumpasia Adebayor aliefunga kilaini.
Kipindi cha pili, Nedum Onuoha akafunga bao la 4 kwa Man City kwa mkaju toka nje ya boksi.
Katika dakika za lala salama, Adebayor akapachika bao la 5 na kuweza kuuchukua mpira uliochezewa mechi hii kuwa mali yake kwa vile amefunga bao 3 katika hii mechi.
Vikosi vilivyoanza:
Man City: Given, Onuoha, Kompany, Toure, Garrido, Adam Johnson, Vieira, Barry, Bellamy, Tevez, Adebayor.
Akiba: Nielsen, Wright-Phillips, Santa Cruz, De Jong, Boyata, Cunningham, Ibrahim.
Birmingham: Taylor, Carr, Johnson, Dann, Ridgewell, Gardner, Bowyer, Ferguson, Fahey, Jerome, McFadden.
Akiba: Doyle, Larsson, Phillips, Benitez, Michel, Parnaby, Vignal.
Refa: Phil Dowd
Liverpool nao.........................…kisikiiiiiii!
Liverpool wametoka sare ya 0-0 Uwanjani kwao Anfield walipocheza na Fulham kwenye mechi ya Ligi Kuu na inaelekea ile nafasi ya 4 kwao inaanza kuota mbawa kwani wapo nafasi ya 6 na wamebakisha mechi 4 na juu yao zipo Tottenham na Manchester City ambazo licha ya kuwa na pointi zaidi ya Liverpool pia wana mechi mkononi.
Liverpool wamecheza mechi 34 na wana pointi 56, Tottenham mechi 32 pointi 58 na Man City ndio wako nafasi ya 4 kwa mechi 32 na pointi 59.
Leo Liverpool ilicheza bila ya Staa Fernando Torres na pengo lake lilionekana kwani licha ya kutawala walishindwa kufunga.
Vikosi vilivyoanza:
Liverpool: Reina, Johnson, Kyrgiakos, Carragher, Agger, Aquilani, Mascherano, Maxi, Gerrard, Babel, Ngog.
Akiba: Cavalieri, Benayoun, Kuyt, Lucas, Degen, Ayala, Pacheco.
Fulham: Schwarzer, Baird, Hangeland, Hughes, Konchesky, Greening, Murphy, Etuhu, Duff, Nevland, Zamora.
Akiba: Zuberbuhler, Kelly, Shorey, Okaka, Riise, Smalling, Dikgacoi.
Refa: Andre Marriner
Man United wakwaa kisiki, Chelsea wachekelea!!
Wakiwa ugenini Ewood Park, Manchester United leo wamewapa nafuu kubwa Wapinzani wao wakubwa katika kinyang’anyiro cha kutwaa Ubingwa Msimu huu, Chelsea, walipotoka sare ya 0-0 na Blackburn Rovers.
Kwa matokeo hayo, Chelsea bado wapo kileleni wakiwa na pointi 74 na Man United ni wa pili wakiwa na pointi 73 lakini sasa wamecheza mechi moja zaidi ya Chelsea.
Mechi inayofuata kwa Chelsea ni Jumanne watakapokuwa kwao Stamford Bridge kucheza na Bolton Wanderers.
Vikosi vilivyoanza:
Blackburn: Robinson, Salgado, Samba, Jones, Givet, Nzonzi, Grella, Emerton, Pedersen, Olsson, Kalinic.
Akiba: Brown, Nelsen, Dunn, Roberts, Andrews, Diouf, Di Santo.
Man Utd: Van der Sar, Neville, Ferdinand, Vidic, O'Shea, Valencia, Scholes, Giggs, Nani, Berbatov, Macheda.
Akiba: Kuszczak, Evra, Park, Jonathan Evans, Fletcher, Obertan, Gibson.
Refa: Peter Walton
LIGI KUU: Wolves 0 Stoke 0
Hii ndio mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kuchezwa leo Jumapili na ilimalizika kwa sare ya 0-0 huku Watazamaji wakipiga kelele kuikejeli mechi yenyewe kwa kupiga mbiu: “Imepooza! Imepooza!”.
Lakini hilo si ajabu kwani Stoke tayari wako salama kushushwa Daraja na Wolves leo wamejihakikishia kuwa pointi 6 juu ya zile Timu 3 zilizo mkiani ambazo ndizo ziko hatarini kushushwa Daraja huku zimebaki mechi 4 tu.
O’Neill amponda Refa Webb
Msimu huu, kila baada ya mechi imekuwa kawaida kwa Mabosi wa Timu kulalamikia uamuzi na Nusu Fainali ya FA Cup ya jana ambayo Chelsea walitandika Aston Villa bao 3-0, haikuwa tofauti.
Bosi wa Aston Vlla, Martin O’Neill amelia na Refa Howard Webb, ambae ni mmoja wa Marefa watakaochezesha Kombe la Dunia huko Afrika Kusini kuanzia Juni 11, kuhusu matukio mawili ya mechi hiyo jana.
O’Neill amefoka: “Sijui kama uliiona ile rafu ya Terry kwa Milner! Ni mbaya! Milner ana bahati kubwa hakuvunjwa! Ile ni Kadi Nyekundu! Na Refa alikuwa hapo hapo!”
Tukio la pili ni pale Mikel John Obi alipomchezea rafu Gabriel Agbonlahor ndani ya boksi na Refa Webb kupeta.
EL CLASICO: Real 0 Barca 2
FC Barcelona jana waliifunga Real Madrid bao 2-0 katika BIGI MECHI ya huko Spainiliyofanyika nyumbani kwa Real Uwanja wa Santiago Bernabeau na kushuhudiwa na Mamilioni kila kona ya Dunia.
Barcelona sasa wamekamilisha vipigo viwili kwa Real kwenye La Liga baada ya kushinda mechi ya kwanza kati yao bao 1-0 mwezi Novemba na ushindi wa jana umewapa uongozo wa Ligi wakiwa pointi 3 juu ya Real huku zimebaki mechi 7.
Ni yule Mchawi Duniani Lionel Messi alieipatia Barca bao la kwanza ya dakika ya 33 baada ya kumtoka Beki Raul Albiol na kumhadaa Kipa Iker Casillas.
Pedro aliipatia Barca bao la pili dakika ya 56 kufuatia bonge la pande kutoka kwa Xavi.
Powered By Blogger