Saturday 25 July 2009

Mchezaji umri mdogo katika historia!!!!
Julio Cesar Baldiviesco, baba wa Kijana anaeaminika kuwa ndio Mchezaji wa Kulipwa wa Soka ambae ni mdogo kupita wote katika historia, amelazimika kujitoa kama Kocha wa Klabu ya Nchini Bolivia Aurora baada ya Menejimenti kumwambia asmchezesha mwanawe huyo aitwae Mauricio [pichani] aliecheza Jumapili iliyokwisha akiwa na umri wa miaka 12 na kuweka hiyo rekodi ya Dunia.
Baldiviesco alimwingiza Mwanawe kutoka benchi zikiwa zimebaki dakika 9 huku Aurora ikiwa nyuma bao 1-0 ikicheza na La Paz na uamuzi huo umezua mgogoro mkubwa huko Bolivia huku baadhi wakitaka kuwa na umri wa chini wa kuruhusu Wachezaji wa Kulipwa.
Baldiviesco, alieichezea Bolivia Kombe la Dunia mwaka 1994 huko Marekani, ametamka: ‘Inasikitisha kwa watu kutokukubali vipaji! Nchi hii na Dunia lazima ijue Bolivia kuna vipaji lakini Bolivia vipaji hukatwa miguu!’
Beckham apigwa faini!
David Beckham amepigwa faini ya Dola 1,000 na MLS [Major League Soccer], Chama cha Soka Marekani, baada ya kufarakana na Mshabiki mmoja wakati Timu yake LA Galaxy ilipokuwa ikicheza mechi ya kirafiki na AC Milan wiki iliyokwisha.
Katika mechi hiyo kuna kikundi cha Mashabiki kilichokuwa kikizomea na kumkashifu Beckham kwa vile aliiacha LA Galaxy na kwenda kucheza AC Milan kwa mkopo ili kujipa nafasi ya kuchukuliwa Timu ya Taifa ya England kitu ambacho alifanikiwa kukifanya na sasa ndie Mchezaji aliecheza mechi nyingi England kwa kucheza jumla ya mechi 112.
Sunderland yambeba Nahodha wa Marseille!
Klabu ya Sunderland imemnunua Kiungo na Nahodha wa Marseille ya Ufaransa, Lorik Cana, miaka 25, ambae ni raia wa Albania, kwa mkataba wa miaka minne.
Cana alijiunga Marseille akitokea Paris St Germain mwaka 2005 na ameshaichezea Timu ya Taifa ya Albania mara 31.
Bolton wachukua wawili kwa mpigo!!
Meneja wa Bolton, Gary Megson, amefanya usajili wake wa nne kwa msimu ujao baada ya kuwachukua Zat Knight kutoka Aston Villa na Sam Ricketts kutoka Hull City kwa madau ambayo hayakutajwa ila wote wawili wamepewa mkataba wa miaka mitatu kila mmoja.
Awali Megson aliwanunua Sean Davis kutoka Portsmouth na Paul Robinson kutoka West Bromwich Albion.
Gerrard akwepa Lupango!!!
Nahodha wa Liverpool na Kiungo wa England, Steven Gerrard, amepatikana kutokuwa na hatia katika kesi ya kushambulia na kumjeruhi Marcus McGee Desemba 29 mwaka jana huko Southport.
Ingawa Gerrard alikiri kumpiga ngumi McGee na kujitetea kuwa alifanya hivyo ili kujihami, Wazee wa Baraza Mahakamani wamekubali kauli yake na kumwona hana hatia.
Akiongea baada ya kesi kumalizika, Gerrard alisema: 'Nimefurahi na sasa haya yote yamepita!’
Adebayor adai ameuzwa kwani Arsenal hawana pesa!!
Emmanuel Adebayor amedai Arsenal ilimuuza kwa Manchester City kwa sababu walikuwa wanataka fedha.
Adebayor amenunuliwa na Man City kwa Pauni Milioni 25.
Adebayor ametamka: ‘Niliporudi toka likizo Wakala wangu akaniambia Klabu inataka kuzungumza na mimi. Ndipo Wenger akaniambia wamefikia makubaliano na Klabu nyingine kuhusu mimi. Nadhani walitaka pesa ila namshkuru Wenger kwa kunifikisha hapa!’
Matokeo mechi za kirafiki:
-Celtic 5 El Ahly 0
-Tottenham 1 Barcelona 1
-Chelsea 2 AC Milan 1
-FC Koln 0 Bayern Munich 2
-FC Seoul 2 Manchester United 3

Friday 24 July 2009

Kepteni wa Korea ndani ya Man U kwao Korea!
Park Ji-sung Ijumaa atakuwa nyumbani lakini si kwa Timu yake ya Taifa ya Korea ambayo yeye ni Kepteni bali ni Klabu yake Manchester United wakati Man U itakapocheza na FC Seoul kwenye mechi ya kirafiki.

Hii ni ziara ya pili kwa Man U Nchini Korea lakini itakuwa ni mechi ya kwanza kwa Park kucheza kwao akivaa Jezi ya Man U kwa sababu miaka miwili iliyopita Man U walipozuru huko Park alikuwa kaumia goti na hakucheza.

Sir Alex Ferguson akiwa na furaha kuhusu Park alieleza: 'Kijana wa nyumbani Ji-sung akiacha Nchi yake kuchezea Man U ni furaha lakini kufanikiwa na kuwa staa kama yeye bila shaka nyumbani atapokewa kwa shangwe! Pia yeye, kama Nahodha wa Timu ya Taifa, mapokezi yatakuwa bora! Korea ni Nchi ya soka, amerudi atapokewa vyema! Huyu ni mfano mwema!'

Thursday 23 July 2009

Wamiliki wa Man U Familia ya Glazer wadai 'vijisenti' vipo!!!
Wamiliki wa Manchester United, Familia ya kina Glazer, wamesisitiza kuwa Meneja wa Timu yao Sir Alex Ferguson analo bulungutu lililoshiba la kununua Mchezaji anaemtaka ila hawategemei kuwa atatumia ovyo pesa hizo.
Manchester United wamepata Pauni Milioni 80 kwa mauzo ya Cristiano Ronaldo kwa Real Madrid lakini wametumia pesa kidogo tu ambazo hazizidi Pauni Milioni 20 katika kununua wachezaji wapya.
Mpaka sasa Man U imemchukua Michael Owen bila gharama kwa vile alikuwa Mchezaji huru pamoja na Winga Luis Antonio Valencia, Kiungo Gabriel Obertan na Mshambuliaji Mame Biram Diouf.
Msemaji wa Wamiliki hao kina Glazer, Tehsin Neyani, ametamka: ‘Meneja anazo pesa za kununua Wachezaji. Tunazungumzia kiasi cha Pauni Milioni 60.”
Hata hivyo Sir Alex Ferguson mwenyewe ametangaza hasajili tena lakini Msemaji wa kina Glazer, Tehsin Neyani ameendelea kusema: ‘Meneja hajapata Wachezaji wanaofiti falsafa ya Man U. Hatununui Wachezaji mamluki!’
Gerrard amwomba Pilato msamaha!
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, leo akitoa ushahidi wake Mahakamani katika kesi inayomkabili ya kushambulia na kujeruhi, ameiomba Mahakama msamaha ingawa amedai alirusha ngumi kwa kujihami kwani alidhani Marcus McGee angemshambulia.
Gerrard alisema: ‘Ni kweli nimekosea kwani nilifikiri atanishambulia.”
Gerrard alidai alipewa ruhusa na Meneja wa Naitiklabu waliyokuwepo kuchagua muziki na alipokuwa akiangalia kadi ya muziki McGee akaja na kuipora mkononi kwake na wakaanza kubishana kisha yeye Gerrard akaondoka lakini akarudi tena dakika chache baadae.
Gerrard alisema aliwaambia Polisi kuwa alidhani McGee atamshambulia kwani alimsogolea lakini hakujua kusogea kwa McGee ni kwa sababu alikuwa amepigwa na wenzake Gerrard.
Kesi inaendelea.
Southgate anategemea Mido na Tuncay kuondoka Boro
Meneja wa Middlesbrough Gareth Southgate anategemea Wachezaji wake Mido na Tuncay Sanli kuondoka klabuni hapo katika wiki chache zijazo.
Southgate alisema: "Tunajua Mido na Tuncay hawataki kukaa Timu ya Daraja la chini na nina uhakika wanunuzi watakuja.’
Middlesbrough iliporomoka Daraja kutoka Ligi Kuu England msimu uliokwisha na msimu ujao watacheza Coca Cola Champions
hip.
Spurs yanyakua Vijana Naughton na Walker
Tottenham imewanunua Vijana wawili kutoka Sheffield United Timu inayocheza daraja la Chini ya Ligi kuu yaani Coca Cola Championship.
Vijana hao ambao wote ni Walinzi ni Kyle Naughton na Kyle Walker wamechukuliwa kwa jumla ya Pauni Milioni 10 ingawa hilo halikuthibitishwa.
Wakati Walker, miaka 19, atabaki Sheffield United kwa mkopo Naughton, miaka 20, atakuwepo Klabu yake mpya akigombea namba na kina Corluka na Hutton ambao wote huchezea nafasi moja.
Mikel ajikita Chelsea
Kiungo wa Chelsea anaetoka Nigeria, John Mikel Obi, miaka 22, amesaini mkataba mpya wa miaka mitano hapo Stamford Bridge.
Mikel alijiunga Chelsea akitokea Klabu ya Norway Lyn Oslo mwaka 2006 huku kukiwa na mvutano na Manchester United ambao ndio walimsaini kwanza na mzozo huo ulifika mpaka FIFA na ikabidi Chelsea wailipe Manchester United pauni Milioni 12.
Akizungumzia mkataba huu Mikel alitamka: ‘Ni rahisi kusaini kwani nina furaha hapa!’
Akiwa Chelsea, Mikel ashacheza chini ya Mameneja Jose Mourinho, Avram Grant, Luiz Felipe Scolari ,Guus Hiddink na sasa Carlo Ancelotti.
Gerrard alikiri kupiga ngumi 3!!
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, alikiri kumpiga Marcus McGee ngumi tatu lakini ni moja tu ndio ilitua usoni kufuatana stetimenti aliyoandika Polisi na kusomwa Mahakamani katika kesi dhidi yake na Wenzake 6 wanaotuhumiwa kumshambulia na kumjeruhi Marcus McGee Desemba 29 mwaka jana.
Gerrard mwenyewe anategemewa kutoa ushahidi wake leo.
Liverpool 1 Thailand 1
Mchezaji alietoka benchi na kuingizwa kipindi cha pili Sutee Suksomkit alifunga bao la kusawazisha kwa Thailand na kulazimisha sare ya 1-1 na Liverpool katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Bangkok, Thailand.
Bao la Liverpool, iliyosheheni Masupastaa, lilifungwa na Ryan Babel dakika ya 6.
Thailand inafundishwa na Mchezaji wa zamani wa England aliewahi pia kuwa Meneja wa Sunderland Peter Reid.
Hii ni suluhu ya pili mfululizo kwa Liverpool iliyo katika maandalizi ya msimu mpya.
Liverpool Jumapili inacheza na Timu ya Taifa ya Singapore
.

Wednesday 22 July 2009

Mascherano ana nia kwenda Spain!!
Kiungo wa Liverpool anaetoka Argentina, Javier Mascherano, ana nia ya kweli kuhamia Spain kwa sababu amechoshwa na maisha ya Uingereza.
Inasadikiwa Mascherano angependa kuhamia Real Madrid au Barcelona na habari hizi zimethibitishwa na Wakala wa Mchezaji huyo, Walter Tamer, ambae amesema: ‘Barcelona ni rahisi kwake kwenda kwani angependa kuishi Spain. Amechoka na England. Hata mkewe hajapewa visa ya kudumu ya kuishi Uingereza. Liverpool hawataki kumuuza lakini wakipewa ofa nzuri wataongea tu!’
Hili ni pigo kwa Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, kwani Kiungo wake mwingine wa kutumainiwa, Xabi Alonso, nae pia anataka kutimkia Real Madrid.
Eriksson arudi tena England, yuko Notts County!!
Meneja wa zamani wa England, Sven Goran Eriksson, amateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Soka kwa mkataba wa miaka mitano na Klabu iliyo League Two, Notts County, na ameahidi kuipandisha hadi Ligi Kuu.
Eriksson baada ya kuondoka kama Meneja wa England aliifundisha Manchester City kwa msimu mmoja tu kisha akaondolewa na akapata kazi ya kuifundisha Timu ya Taifa ya Mexico ambako hakudumu nayo muda mrefu.
Mwenyewe Eriksson amesema hakwenda Notts County kutafuta pesa bali ni kwa sababu moja tu na nayo ni changamoto ya kuipandisha Ligi Kuu.
Wenger asema Nasri atakuwa nje wiki 6 tu!!
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ana matumaini Samir Nasri atarudi uwanjani baada ya wiki 6 na sio miezi mitatu iliyotangazwa mara baada ya kuvunjwa mguu huko kambini Austria hapo jana.
Wenger amesema: ‘Alimpora mtu mpira aliekuwa akitaka kuupiga na ndipo alipovunjwa mguu! Lakini ingawa amevunjika lakini si vibaya kama tulivyoogopa! Tunategemea atarudi baada ya wiki 6. Lakini tunae Rosicky ameshapona na Eduardo atarudi baada ya miezi miwili.”
Drogba asaini mkataba mpya Chelsea!
Mshambuliaji wa Chelsea Didier Drogba, umri miaka 31, anategemewa kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu kufuatana na kauli ya Meneja wake Carlo Ancelotti.
Drogba, ambae jana alifunga bao moja na Lampard la pili pale Chelsea walipowafunga Inter Milan kwenye mechi ya kirafiki, ameshaifungia Chelsea mabao 94 katika mechi 216.
Ancelotti ametamka: ‘Ni mtu muhimu kwetu. Tunataka aendelee kucheza hapa.”
Ndugu wa Riise atua Fulham
Mchezaji wa Kimataifa wa Norway ambae ni Kiungo, Bjorn Helge Riise, 26, amejiunga na Fulham kwa mkataba wa miaka mitatu na kwa dau ambalo halikutangazwa.
Bjorn Helge Riise, ambae Kaka yake John Arne Riise alicheza Liverpool kwa miaka mitano, anatokea Klabu ya Lillestrom na akiwa Fulham ataungana na Wachezaji wengine kutoka Norway, Brede Hangeland na Erik Nevland.
FIFA yaipiga Ivory Coast faini!
FIFA imekipiga Chama cha Soka cha Ivory Coast faini ya Dola Elfu 47 kufuatia uchunguzi kuhusu vifo vya Mashabiki 20 waliokufa mjini Abidjan kwenye Uwanja wa Felix Boigny mwezi Machi mwaka huu wakati Ivory Coast ilipokuwa ikicheza na Malawi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia na kushinda mabao 5-0.
FIFA pia imetoa Dola Elfu 96 ili kuzisaidia Familia za Wafiwa.
Vilevile FIFA imetaka hatua za kusalama zichukuliwe kabla ya mechi ijayo itakayochezwa hapo Abidjan kati ya Ivory Coast na Burkina Faso mwezi Septemba ikiwa pamoja na kutoruhusu Washabiki zaidi ya 20,000 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 34,000.
Hatua nyingine ni kuweka vizuizi mita 200 kuzunguka nje ya uwanja ili kuzuia watu wasio na tiketi kuvamia uwanja kwani hilo ndilo lilikuwa chanzo cha watu kufa.
Gerrard kumkabili Pilato pekee, Wenzake waungama na kusubiri hukumu!!!!
Nahodha wa Liverpool na Mchezaji wa Timu ya Taifa, Steven Gerrard, peke yake atasimama kizimbani ili kesi yake kuendelea kusikilizwa baada ya Washitakiwa wenzake wote 6 kukubali makosa na hivyo kungoja hukumu tu ya kosa la kumpiga na kumjeruhi Marcus McGee Desemba 29 mwaka jana kwenye Naitiklabu Lounge Inn huko Southport.
Gerrard amekana mashitaka hayo na hivyo kesi inaendelea kunguruma kwake tu na Mwendesha Mashtaka alisimama na kuelezea korti nini kilijiri huku mikanda ya video ya kamera za ulinzi ikionyeshwa.
Mwendesha Mashtaka huyo, David Turner, aliieleza Mahakama: ‘Ugomvi ulianza pale Gerrard alipotaka apewe kadi inayoongoza CD za muziki. McGee alipogoma kumpa, Gerrard akachukia.
Baada ya dakika 6 hivi, Gerrard, akamrudia McGee na kumtukana kisha Mshtakiwa mwenzake Gerrard akaja na kumsukuma McGee na kumpiga kipepsi na ndipo Gerrard akanza kuvurumisha masumbwi mithili ya Bondia!’
Turner akaongeza: ‘Swali zito hapa ni je Gerrard alikuwa akijihami? Gerrard ni Mchezaji Bora Duniani! Anayo heshima ya kuwa Nahodha wa Liverpool na kuichezea Timu ya Taifa ya England! Ni nyota yeye aliezaliwa Liverpool na hapa Liverpool Gerrard ni shujaa! Hatusemi Gerrard ni mtu mwenye kiburi! Hatusemi ni mbabe! Tunachosema hapa usiku ule Gerrard alipandwa hasira na kuanza kumshambulia mtu bila sababu! Amejiangusha yeye mwenyewe binafsi!’
Kesi inaendelea.

Tuesday 21 July 2009

Arsenal yakumbwa na balaa, Nasri avunjika mguu!!
Kiungo wa Arsenal, Samir Nasri amevunjika mguu katika mechi ya mazoezi huko Nchini Austria ambako Arsenal wameenda kupiga kambi ya mazoezi ya kujitayarisha na msimu mpya unaoanza Agosti 15.
Nasri, miaka 22, alikimbizwa hospitalini na Madaktari wamekadiria atakuwa nje ya uwanja kwa kati ya miezi miwili mpaka mitatu.
Klabu yake Arsenal imethibitisha habari hizo kupitia tovuti yake.
Portsmouth yanunuliwa na Tajiri toka Dubai!
Portsmouth imethibitisha kuwa Sulaiman Al Fahim ndie Mwenyekiti mpya wa Klabu hiyo baada ya kukubaliwa kuinunua na Wasimamizi wa Ligi Kuu England ambao siku hizi wameanzisha mfumo mpya wa kuhakikisha wanaozinunua Klabu za Ligi Kuu wana sifa wa kuzimiliki Klabu hizo.
Al Fahim, anaetoka Dubai, Falme ya Nchi za Kiarabu, ndie alieongoza ununuzi wa Manchester City alipowawakilisha Koo ya Kifalme ya Abu Dhabi katika ununuzi wake lakini safari hii ni yeye binafsi alieinunua Portsmouth.
Al Fahim ameinunua Portsmouth kutoka kwa Alexandre Gavdamak.
Real Madrid, Ronaldo akiwa ndani, waifunga Timu ndogo ya huko Ireland kwa mbinde!!!
Kwa mara ya kwanza Christiano Ronaldo amevaa Jezi nyeupe ya Real Madrid na kucheza dakika 45 za kwanza lakini alikuwa Mchezaji mpya mwenzake kutoka Ufaransa Karim Benzema aliefunga goli la ushindi dakika 3 kabla mpira kumalizika pale vigogo Real Mdrid walipoitungua Timu ndogo ya Ireland Shamrock Rovers bao 1-0.
VFL Wolfsburg 1 v Werder Bremen 2!
Bremen yatwaa Super Cup!!
Kombe liitwalo Super Cup huko Ujerumani jana lilikwenda kwa Mabingwa wa Kombe la Ujerumani Werder Bremen walipowafunga Mabingwa wa Ujerumani Vfl Wolfsburg mabao 2-1.
Bremen walitangulia kufunga dakika ya 20 kwa Per Mertesacker kufunga lakini Wolfsburg walisawazisha dakika ya 67 kupitia Mchezaji wao hatari kutoka Brazil Grafite dakika ya 67.
Lakini alikuwa Clemens Fritz kwenye dakika ya 81 alipowapa furaha Werder Bremen kwa kupachika bao la pili na la ushindi.

Monday 20 July 2009

Sir Alex Ferguson: ‘Kuondoka Ronaldo ni pigo kwetu! Yeye ni bora kupita Kaka na Messi!’
-Man City sio tishio kwetu!

-Tishio bado Chelsea, Liverpool, Arsenal!
Meneja wa Manchester United Alex Ferguson ametamka kuondoka kwa Cristiano Ronaldo ni pigo kubwa kwa Mabingwa hao.
Ferguson amesisitiza: ‘Ni pigo kubwa! Sina cha kusema ila kumsifia kijana Yule! Kwa vyovyote vile yeye ni Mchezaji Bora Duniani! Ni bora kuliko Kaka na Messi! Yuko mbali sana kupita hao!’
Akiwageukia Mahasimu wao wa jadi, Manchester City, Klabu ambayo ni jirani zao mjini Manchester, Sir Alex Ferguson amekiri yeye pamoja na dunia nzima ya soka inashangazwa na jinsi wanavyonunua Wachezaji kwa bei mbaya.
Manchester City juzi tu wamemnunua Mshambuliaji wa Arsenal Emmanuel Adebayor kwa dau linalokadiriwa kuwa Pauni Milioni 25 na atajumuika na Wachezaji wengine wapya Gareth Barry, Roque Santa Cruz na Carlos Tevez.
Akiongea akiwa Kuala Lumpur, Malaysia ambako Man U wako ziarani Asia, Ferguson amenena: ‘Uhamisho wao wote waliofanya hawawezi kutupa ushindani labda kwenye kurasa za nyuma za Magazeti! Wao watashinda kwenye magazeti kwani kila siku zipo hadithi za ununuzi wao! Washindani wetu wakubwa bado ni Chelsea, Liverpool na Arsenal!’
Ferguson amesema itakuwa vigumu sana kwa Manchester City kushinda chochote licha ya kununua Wachezaji kwa sababu wamenunua Wachezaji wenye majina na tena sasa wana Washambuliaji 10 na amekiri hao ni wengi mno.
Ferguson ameongeza kwa kusema ameongea na baadhi ya Mameneja wenzake wa Ligi Kuu na wamejiuliza Man City watampanga nani na kumwacha nani, na yupi utamwambia hachezi.
Ferguson, akitafakari, alitamka: ‘Siwezi kusema kati ya Chelsea na Liverpool ipi ni timu ngumu zaidi kwani kila timu ni wazoefu! Arsenal wana kazi kubwa kuendeleza timu hasa baada ya kumuuza Adebayor. Pia hawana pesa kama za Chelsea na Liverpool. Jinsi Wenger atakavyoendeleza timu yake ndio mtihani wao mkubwa!’
‘Lakini…’ Ferguson akaongeza. ‘…..kitu kimoja tunachojua kuhusu Arsenal ni kuwa watakuja na soka bora kabisa! Watapata nafasi na ni rahisi kujijenga upya na kuleta ushindani!’
Ferguson akamalizia kwa kuigusa historia: ‘Tumekuwa Mabingwa mara 3 mfululizo na katika historia ya England hakuna Timu iliyokuwa Bingwa mara 4 mfululizo! Lyon huko Ufaransa wamechukua mara 7 mfululizo, Dynamo Kiev mara 9 na pia Celtic na Rangers! Dinamo Berlin ya ile Ujerumani Mashariki zamani walichukua mara 11! England huwezi kupata hilo!’
Sir Alex Ferguson akahitimisha: ‘Naongoza Klabu yenye falsafa sahihi. Nimepata wakati murua hapa. Kila mechi ya nyumbani Old Trafford kuna Mashabiki 76,000 wanatizama mechi laivu uwanjani hivyo siwezi kuijali Timu nyingine jirani hata wakifanya chochote!’
Liverpool wafungwa huko Austria!
Huku wakiandamwa na kashfa ya Nahodha wao, Steven Gerrard, kutinga Mahakamani na shinikizo la Xabi Alonso kuhusishwa na Real Madrid, Liverpool jana walipigwa kimoja na Rapid Vienna ya Austria kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Austria ambako Liverpool wako ziarani.
Hii ni mechi ya pili ya kirafiki kwa Liverpool wanaojitayarisha kwa mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu England baada ya kutoka suluhu 0-0 na Club St Gallen ya Switzerland Jumatano wiki iliyopita.
Bao la Rapid Vienna lilifungwa na Nahodha wao Steffen Hofmann dakika ya 58 kwa frikiki bomba.
Jumatano Liverpool watakuwa huko Asia Nchini Thailand kucheza na Timu ya Taifa ya Thailand.
Gerrard apanda kizimbani leo!
Nahodha wa Liverpool na Kiungo wa England, Steven Gerrard, leo ametinga Mahakamani ili kusikilizwa kesi yake anayotuhumiwa yeye na wenzake 6 ya kumshambulia na kumjeruhi Marcus McGee kwenye Naitiklabu usiku wa Desemba 29 mwaka jana huko Liverpool.
Kufuatana malumbano ya kisheria na pia kutoteuliwa Wazee wa Mahakamani, kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Jumanne na inategemewa kesi hiyo itadumu wiki 2 au 3 mpaka kumalizika.
Gerrard, miaka 29, amekanusha mashtaka hayo ambayo ameunganishwa na Kipa wa Klabu ndogo iitwayo Accrington Stanley anaeitwa Ian Dunbavin, 28, na pia Kiungo wa Timu hiyo Robert Grant, 18. Wengine ni John Doran, 29, Ian Smith, 19, John McGrattan, 33, na Paul McGrattan, 31.
Inaaminika genge hilo la Gerrard lilikuwa linasheherekea ushindi wa Liverpool wa siku hiyo walipoibamiza Newcastle bao 5-1.
Owen afunga tena!!
Michael Owen akicheza mechi yake ya pili leo akiwa na Jezi Namba 7 ya Manchester United amefunga bao kwa mara nyingine tena kwenye mechi Man U waliyowafunga wenyeji wao Malasyia mjini Kuala Lumpur bao 2-0.
Bao la kwanza la Manchester United lilifungwa na Chipukizi Macheda dakika ya 11 na la pili alipachika Owen dakika ya 13.
Katika mechi hiyo ya kirafiki kila Timu ilifanya mabadiliko ya Wachezaji wengi mno huku Man U ikiwaingiza katika kipindi cha pili Kipa Kuszczak, Rio Ferdinand, Nani, Berbatov, Scholes, Anderson, Gibson, O’Shea, Evra na Rooney.
Sasa Man U wanaelekea Korea ya Kusini kucheza na Klabu ya FC Seoul siku ya Ijumaa.
Kikosi cha Man U kilichoanza ni: Foster; Neville, Brown, Evans, Fabio; Fletcher, Carrick, Giggs, Tosic; Owen, Macheda.
Alonso akiri Real kunapendeza!!!
Kiungo wa Liverpool, Xabi Alonso ambae ashabatukiwa na Meneja wake Rafa Benitez kuwa akitaka uhamisho kwenda Real Madrid basi lazima aandike barua rasmi kuomba, amekiri kuwa anavutiwa na kujiunga na Real.
Alonso amesema: ‘Mchezaji hujisikia vizuri ukitakiwa na Real hasa ukizingatia wakati huu nilio. Lakini hili ni suala la pande tatu nikiwemo mimi.’
Alonso ameongeza kuwa akiwa Nchini Austria ambako Liverpool wamepiga kambi ya mazoezi na kuwa ziarani huko ataongea na Benitez kuhusu uhamisho.
Mido aendelea kutwangwa faini kadri anavyochelewa kurudi Boro!!
Mchezaji wa Misri, Mido, ambae mpaka sasa wiki mbili zimepita na bado hajaripoti kwenye Timu yake Middlesbrough ambayo imeshuka Daraja kutoka Ligi Kuu England msimu uliokwisha, ameendelea kukung’utwa faini zaidi na Klabu hiyo.
Meneja wa Boro, Gareth Southgate, amesema: ‘Mido lazima arudi na kufanya mazoezi na sisi. Klabu haiwezi kumlipa mtu yeyote kama hayupo na sisi!’
Mpaka sasa Mido, ambae alimaliza msimu uliokwisha akichezea Wigan kwa mkopo, ameshapigwa faini ya mshahara wa wiki mbili.
Mido alisainiwa na Boro mwaka 2007 kutoka Tottenham Hotspurs kwa Pauni Milioni 6.
Guardiola hamtaki Eto'o!!
Kocha wa Barcelona Pep Guardiola, ambae msimu uliokwisha alimweka Samuel Eto'o kwenye listi ya uhamisho, amesema lazima Eto’o aondoke.
Barcelona na Inter Milan zipo kwenye mazungumzo ili zifikie makubaliano ya kubadilishana Et’oo na Zlatan Ibrahimovic.
Guardiola amesema: ‘Nina imani kitu bora kwa Barca ni kuondoka kwa Eto’o. Siko hapa kumbadili mtu tabia ila niko hapa kufanya uamuzi. Umefika wakati kubadilika kwa ajili ya msimu ujao.’
LEO UJERUMANI NI SUPER CUP: VFL Wolfsburg v Werder Bremen!
Mabingwa wa Ujerumani, Vfl Wolfsburg, leo wanafungua msimu wa Ujerumani kwa kupambana na Mabingwa wa Kombe la Ujerumani, Werder Bremen, kugombea Kombe liitwalo Germany Super Cup.
Mechi hii itaanza saa 3 dakika 20 saa za kibongo.

RATIBA: MECHI ZA KIRAFIKI LEO!
[saa za bongo]
-saa 9 dak 45 mchana MALAYSIA XI v MAN U [mjini Kuala Lumpur]
-saa 3 dak 20 usiku LINCOLN CITY v ARSENAL [mjini London]
-saa 4 usiku SHAMROCK ROVERS v REAL MADRID [mjini Dublin, Ireland]
Sakata la John Terry laendelea, Lampard aongeza mkanganyo!!!
Kiungo wa Chelsea, Frank Lampard, ameongeza mkanganyiko kuhusu hatima ya Nahodha wao John Terry pale alipokiri hajui kama Terry anabaki au anaondoka huku Meneja wa Manchester City Mark Hughes, Klabu inayodaiwa ndio inamzuzua Terry, kudai kuwa wao bado wana imani kubwa Terry atakwenda Manchester.
Ingawa Chelsea yenyewe, ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Peter Kenyon na Kocha mpya Carlo Ancelotti, wameng’ang’ania Nahodha wao atabaki hakuna lolote Terry mwenyewe amesema kuhusu utata huu.
Lampard ametamka: ‘Sijui mwenyewe anataka nini. Kila mtu klabuni anataka abaki. Lakini watu wasimlaumu. Watu lazima waheshimu uamuzi wake kuchagua.'
Wakati huo huo, Meneja wa Manchester City, Mark Hughes, amekiri kuwa bado ana matumaini ya kumnasa John Terry ingawa Chelsea wameshaigomea ofa moja rasmi ya Man City.
Hughes anasema: ‘Ni Mchezaji wa hali ya juu. Bado hatujafikia pale tunaweza kukata tamaa hatumpati.”
Rooney: ‘Mzigo wa magoli ni kwangu, Berbatov na Owen!’
Wayne Rooney, akiwa ziarani na Timu yake Manchester United huko Asia, mbali ya kukubali kuna kazi kubwa ya kuziba pengo la Ronaldo na Tevez waliohama ambao kwa pamoja waliifungia Man U jumla ya mabao 41 msimu uliopita, anaamini pengo hilo haliwasumbui yeye, Berbatov na Owen.
Rooney vilevile amesema hawamlaumu Ronaldo kwa kuondoka kwani alikuwa mtumishi bora kwa Klabu hiyo kwa miaka 6 aliyodumu na amekiri kuwa yeye na Ronaldo wanaelewana sana.
Rooney anasema: ‘Kuondoka kwa Ronaldo kunafanya tuliobaki kufunga magoli mengi zaidi. Hatumlaumu Ronaldo kwa kuondoka.’
Kuhusu Tevez, Rooney ametamka: ‘ Ni rafiki yangu! Alikuwa akinifundisha maneno mengi ya matusi ya Kihispania! Ni bahati mbaya tulishindwa kurekebisha mkataba wake. Nadhani watu wengi watazungumza mengi kuhusu kuhamia kwake Man City lakini mimi sisemi chochote.’
Rooney mwenyewe amekiri kuwa endapo atachezeshwa kama Sentafowadi badala ya kupangwa pambeni au nyuma ya Sentafowadi atamudu kufunga mabao mengi sana.

Mara nyingi kwenye Kikosi cha Manchester United, Rooney hucheza kama mtu wa kumsapoti Mshambuliaji mkuu akiwa ama nyuma yake au pembeni yake kitu kilichokuwa kikimfanya awe mlishaji na si msifungaji.
Lakini Rooney amekiri suala hilo hawajaongea na Bosi wake Sir Alex Ferguson.

Rooney anasema: ‘Kila mtu anajua nipo hatari nikicheza Sentafowadi! Unafanya kazi kidogo, huzunguki mno uwanjani na unapata nafasi nyingi za kufunga!’

Sunday 19 July 2009

Man City yafungwa Bondeni!!
Manchester City wakiwa kwenye ziara ya mechi 3 huko Afrika Kusini wameanza ziara hiyo kwa kufungwa mechi ya kwanza na Orlando Pirates bao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa Polokwane.
Mabao ya Orlando Pirates yalifungwa na Lucas Thwala kwa penalti na la pili na Phenyo Mongala.
Siku ya Jumanne Man City watacheza na Kaizer Chiefs mjini Durban na kumaliza ziara hiyo kwa kucheza Jumamosi mjini Pretoria.
Oliveira anunuliwa Abu Dhabi na kuweka rekodi!!!
Mchezaji wa Kimataifa wa Brazil Ricardo Oliveira, miaka 29, [pichani] aliekuwa akicheza Spain kwenye Klabu ya Real Betis amenunuliwa na Klabu ya Abu Dhabi Al-Jazira kwa dau la Pauni Milioni 19 ambayo ni rekodi kwa ununuzi wa Mchezaji huko Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.
Klabu ya AL-Jazira inamilikiwa na Sheikh Mansur Ben Zayed al-Nahyan, mmoja wa Wanafamilia kutoka Koo ya Kifalme ya huko Abu Dhabi, ambae pia ni Mmiliki wa Manchester City.
Oliveira mwenyewe, ambae amechezea Timu ya Taifa ya Brazil mara 11, ameungama kuwa anajua Ligi ya Falme za Nchi za Kiarabu, iliyoanzishwa rasmi mwaka jana, kiwango chake ni duni ukilinganisha na Spain, lakini ofa aliyopewa imemfanya yeye na Familia yake washindwe kuikataa.
Bayern Munich watishia kuishitaki Real Madrid!!
Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge ametishia kuchukuwa hatua dhidi ya Real Madrid kama wataendelea kumrubuni Mchezaji wao Franck Ribery.
Kiungo huyo kutoka Ufaransa ameshaambiwa na Mabosi wa Bayern kuwa hauzwi msimu huu lakini Vigogo hao wa Spain wameendelea kumfuata na kusababisha hasira za Bayern Munich.
Rummenigge amekaripia: ‘Real wamekuwa wakivunja kanuni za FIFA wiki nenda rudi kwa sababu hawajapata kibali chetu kuongea na Ribery au Wakala wake. Nitawasiliana na Perez [Rais wa Real] kumtaka aache upuuzi huu au tutawaripoti FIFA.’
Carlo Ancelotti: ‘Terry ni alama ya Chelsea!!’
Meneja mpya wa Chelsea Carlo Ancelotti amesema Nahodha wa Timu hiyo John Terry ni ‘alama’ ya Klabu hiyo na ana uhakika wa zaidi ya aslimia mia moja kuwa Terry atabaki Stamford Bridge.
Manchester City, ikitumia miguvu ya mipesa toka kwa Wamiliki wake Matajiri toka Koo ya Kifalme kutoka huko Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu, imekuwa ikimsaka Terry kwa udi na uvumba.
Akiongea baada ya Chelsea, wakiwa ziarani Marekani, kuwafunga Seattle Sounders mabao 2-0 mjini Seattle, Kocha huyo Mtaliano alisema: ‘Terry ni mwungwana. Hawezi kuhama Timu ambayo yeye ni nguzo!’
Owen: ‘Nitamudu shinikizo la kuwa Man U!!’
Baada ya kufungua kitabu chake cha magoli kwa Timu yake mpya katika mechi yake ya kwanza tu alipofunga bao la 3 na la ushindi wakati Manchester United walipowapiga wenyeji wao Malaysia kwa bao 3-2 mjini Kuala Lumpur, Michael Owen ametamka hana wasiwasi na atamudu kuziba pengo la Ronaldo akishirikiana na wenzaki kina Giggs na Rooney.
Owen ametamka: ‘Ni nafasi kubwa kwangu kuonyesha uwezo na pia kuwa naweza kumudu shinikizo. Kupewa Jezi Namba 7 iliyovaliwa na Wachezaji bora ni shinikizo kubwa kwangu lakini nitaitumikia ipasavyo! Sir Alex Ferguson alinitaka nivae Jezi hiyo na alitaka Mchezaji anaeweza kuimudu Jezi hiyo yenye historia kubwa kwa Man U! Nikamjibu naweza!’
Hatimaye Adebayor yupo Man City!!
Klabu ya Manchester City imekamilisha uhamisho wa Mchezaji kutoka Togo Emmanuel Adebayor, miaka 25, kwa Pauni Milioni 25 baada ya kuichezea Arsenal kwa miaka mitatu na nusu akitokea Monaco ya Ufaransa.

Adebayor msimu uliokwisha aliifungia Arsenal mabao 16 na kujiunga kwake na Man City kutaimarisha Kikosi hicho ambacho tayari kishawabeba Washambuliaji Carlos Tevez na Roque Santa Cruz na Kiungo Gareth Barry.
Baada ya kukamilika taratibu hizo za uhamisho, Adebayor alitamka: ‘Nimezaliwa kucheza mpira na hilo ndilo nataka kufanya. Nawashkuru Man City kwa mapokezi mazuri!’
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amethibisha uhamisho huo wa Adebayor upo na amedai kupona kwa Mafowadi Thomas Rosicky na Eduardo kutaziba pengo la kuondoka kwa Adebayor.
Wenger amesema: ‘Tutamkosa Adebayor lakini ni bora tu tuangalie Wachezaji tuliokuwa nao. Namtakia kila la kheri na kumshukuru kwa mchango wake Arsenal.’
MECHI ZA KIRAFIKI:
-Seattle Sounders 0 Chelsea 2
Mchezaji mpya wa Chelsea Daniel Sturridge alifunga bao lake la kwanza kwa Klabu yake mpya na kumtengenezea Frank Lampard kufunga la pili na kuwafanya Chelsea washinde mechi yao ya kwanza huko ziarani Marekani mjini Seattle kwa kuifunga Timu ya Seattle Sounders mabao 2-0.
-Barnet 2 Arsenal 2
Arsenal, wakicheza mechi yao ya kwanza ya kirafiki ikiwa ni matayarisho ya msimu mpya, wametoka suluhu na Timu ya Daraja la chini Barnet kwa mabao 2-2 huko mjini London.
Mabao ya Barnet yalifungwa na Yakubu dakika ya 45 na la pili dakika ya 83 na Charles.
Wafungaji wa Arsenal ni Arshavin dakika ya 44 na Barazite dakika ya 49.
-Man U wakubali kurudiana na Malaysia
Manchester United, wakiwa ziarani huko Asia, wamekubali kurudiana na Malaysia mjini Kuala Lumpur siku ya Jumatatu baada ya kuifunga Nchi hiyo mabao 3-2 siku ya Jumamosi.
Jumatatu Manchester United walitakiwa kucheza Jakarta, Indonesia lakini ziara ya huko imefutwa kufuatia kulipuliwa kwa Hoteli ambayo Man U walipangiwa kufikia.
Baada ya mechi hiyo Nchini Malaysia, Man U wataruka hadi Korea ya Kusini kucheza na Klabu ya FC Seoul mjini Seoul, Korea hapo Ijumaa.

Powered By Blogger