Saturday 18 July 2009

Gareth Barry amwambia Benitez anakosa heshima!
Kiungo mpya wa Manchester City, Gareth Barry, amemshambulia Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, na kumsema amekosa heshima kwa kutamka yeye ameichagua Man City badala ya Liverpool kwa uroho wa pesa tu.
Msimu uliokwisha Liverpool walitaka kumchukua Barry kutoka Aston Villa lakini Liverpool hawakuafiki dau walilolitaka Aston Villa.
Barry ambae pia huchezea Timu ya Taifa ya England amesema: ‘Ni dhahiri maneno ya Benitez ni kukosa heshima! Nadhani amechukizwa kwa kuwa sikwenda Liverpool! Liverpool walikuwa na kila uwezo kunichukua lakini wameona thamani yangu ndogo wakati Man City wamenithamini.’
Owen aipa ushindi Man U!!!
Michael Owen akianza mechi yake ya kwanza kwa Klabu yake mpya Manchester United amefunga bao lake la kwanza na la ushindi katika mechi ya kwanza katika ziara yao ya huko Asia kwa kuifunga Kombaini ya Malaysia kwenye Uwanja wa Bukit Jalil huko Kuala Lumpur kwa mabao 3-2.
Magoli mengine ya Man U yalifungwa na Rooney dakika ya 8 na Nani dakika ya 28.
Mpaka haftaimu Man U walikuwa mbele 2-1 lakini kosa kubwa la Kipa Ben Foster alieingia kipindi cha pili kushindwa kuzuia pasi aliyorudishiwa na mwenzake Gibson yaliwapa Malaysia bao la chee la kurudisha.
Ndipo Owen akafunga bao la 3 dakika ya 85 baada ya kazi nzuri ya Giggs.
Man U wanasafiri hadi Korea ya Kusini na Ijumaa ijayo watacheza na Klabu ya Korea FC Seoul.
Kikosi: Van der Sar; O'Shea, Ferdinand, Evans, Evra; Gibson, Scholes, Anderson, Nani; Rooney, Berbatov. Akiba: Foster, Neville, Brown, Owen, Giggs, Tosic, Fabio, Macheda
Fulham kucheza na FK Vetra au HJK Helsinki EUROPA LEAGUE
Klabu ya Ligi Kuu England, Fulham, itaanza Raundi ya Tatu ya Mtoano ya Kombe jipya huko Ulaya liitwalo EUROPA LEAGUE kwa kucheza na mshindi kati ya FK Vetra ya Lithuania au HJK Helsinki ya Finland.
Timu hizo zimeshacheza mechi ya kwanza na HJK Helsinki waliishinda FK Vetra ugenini bao 1-0 na watarudiana wiki ijayo na mshindi atapambana Fulham tarehe 30 Julai nyumbani na marudiano yatachezwa Craven Cottage nyumbani kwa Fulham tarehe 6 Agosti.
Fulham imeingizwa EUROPA LEAGUE baada ya kumaliza nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu England pamoja na Everton na Aston Villa zilizomaliza nafasi ya tano na ya sita lakini Everton na Aston Villa zitaanza kucheza Raundi inayofuata.
Man U wamyakua Kijana toka Senegal!!
Klabu za Manchester United na Molde F.K. ya Norway zimethibitisha kuwa zimekubaliana kuhusu uhamisho wa Mame Biram Diouf , miaka 21, raia wa Senegal, kwenda Man U kwa dau ambao halikutangazwa.
Mame atapimwa afya yake huko Manchester wiki ijayo lakini ataendela kuichezea Molde hadi Januari mwakani ili amalizie msimu wa Norway.
Akiongea na Waandishi wa Habari huko Kuala Lumpur, Malaysia ambako Manchester United wako ziarani, Sir Alex Ferguson alisema: ‘Tumekuwa tukimfuatalia kwa miaka miwili sasa! Tulikuwa hatuna nia ya kusajili mtu lakini kuhusu Mame imebidi tumchukue sasa kwa vile Klabu nyingi zimetoa ofa kwake!’
Mpaka leo, baada ya kucheza Klabu ya Molde, klabu ambayo Ole Gunnar Solskjaerpia alikuwa akiechezea, Mame ameshafunga mabao 38 katika mechi 73 na msimu huu katika mechi 21 ameshafunga mabao 17.
Mame anaichezea Timu ya Taifa ya Vijana ya Senegal.
Barca na Inter zabadilishana Washambuliaji!!
Barcelona na Inter Milan wamefikia makubaliano ya kubadilishana Zlatan Ibrahimovic atakaenda Barca na Samuel Eto'o atakaekwenda Inter.
Pia, katika mpango huo Barca itaongeza pesa na kumtoa Kiungo wa zamani wa Arsenal Alex Hleb achezee Inter Milan kwa mkopo.
Habari hizi zimethibitishwa na Rais wa Barcelona, Joan Laporta, aliesema: ‘Makubaliano hayo yanategemea kuridhika kwa upande wa Ibrahimovic na Eto’o.’
Mshambuliaji Manucho kuondoka Man Utd
Manchester United imemruhusu Mshambuliaji kutoka Angola Manucho [pichani akiwa na Ronaldo]kujiunga na Klabu ya Spain Real Valladolid kwa mkataba wa miaka mitano.
Manucho, miaka 26, amekuwa Man U kwa miezi 18 na alicheza mechi moja tu ya Ligi Kuu na kushindwa kupata namba na muda mwingi amekuwa akicheza Klabu nyingine kwa mkopo.
Alipojiunga tu na Man U akapelekwa Klabu ya Ugiriki Panathinaikos kwa mkopo na msimu uliokwisha alicheza Hull City pia kwa mkopo.
Hargreaves akaribia kurudi Uwanjani Man U
Mchezaji wa Manchester United Owen Hargreaves huenda akaanza kuonekana tena uwanjani kuanzia mwezi Septemba kufuatana na maelezo ya Bosi Sir Alex Ferguson.
Kiungo huyo hajaonekana uwanjani tangu mwanzoni mwa msimu uliokwisha kwa kusumbuliwa na matatizo ya magoti na kmfanya afanye opersheni kila goti huko Marekani.
Hargreaves, miaka 28, hayumo kwenye Kikosi cha Man U kilichopo ziarani Asia lakini huenda akajiunga na wenzake watakapokuwa Ujerumani kugombea Kombe la Audi wiki mbili zijazo.
Katika Kombe hilo Man U watacheza na Boca Juniors ya Argentina.
Mechi ya mwisho ya Hargreaves ilikuwa Septemba 21, 2008 Man U ilipocheza na Chelsea huko Stamford Bridge na kutoka suluhu 1-1 kwenye Ligi Kuu.

Friday 17 July 2009

David Beckham: ‘Terry hahami Chelsea!’
Ingawa Nahodha wa Chelsea na England, John Terry, anatakiwa sana na Manchester City, Nahodha wa zamani wa England, David Beckham, anaamini
Terry hawezi kuhama.
Inaaminika Man City imetoa ofa ya Pauni Milioni 35 kumnunua Mchezaji huyo ambae binafsi ameelekea anataka kuondoka.
Beckaham amedai: ‘ Sidhani JT atang’oka! Yeye ni Chelsea damu!’
Wakati anazungumza hilo, Beckham amesema: ‘ Wakati ule sikupenda kuhama Man U! Nilipoondoka sikupenda kuitazama Man U! Roho iliniuma sana! Niliamua mie ni Mchezaji Man U milele! Kwa miaka miaka mitatu nilipokuwa Real nilishindwa kuitazama Man U kwenye TV roho iliuma!’

Man U wavunja safari ya Indonesia!
Safari ya Manchester United kwenda Jakarta, Indonesia imevunjwa baada ya Hoteli waliyotakiwa kufikia kulipuliwa na mabomu.
Viongozi wa Klabu wakishirikiana na Serikali wameamua kuahirisha safari na kuwataka radhi Mashabiki.

Thursday 16 July 2009

Ronaldo: 'Owen anastahili Jezi Namba 7 Man U!'
Cristiano Ronaldo anaamini Michael Owen ni mrithi bora wa Jezi Namba 7 aliyoivaa yeye alipokuwa Manchester United.
Jezi hiyo kihistoria imekuwa ikivaliwa na Wachezaji mahiri sana katika Klabu ya Manchester United na waliowahi kuivaa huko nyuma ni pamoja na Wachezaji walioacha historia kubwa kama George Best, Bryan Robson, Eric Cantona, David Beckham na wa mwisho ni yeye Ronaldo.
Ronaldo ametamka: 'Michael Owen ni Mchezaji mzoefu. Amecheza Klabu kubwa. Atashinda kila kitu akiwa Man U. Yupo kwenye Klabu murua sana na yeye ni Mchezaji Bora. Ni uamuzi mzuri kumpa Jezi Namba 7!'
Michael Owen amesainiwa hivi karibuni na Manchester United bila ya ada ya uhamisho kwa kuwa alikuwa Mchezaji huru baada ya mkataba wake na Newcastle kumalizika Juni 30.
Winga Downing aenda Villa kwa Pauni Milioni 12!
Winga wa Timu iliyoporomoka Daraja Middlesbrough, Stewart Downing, ambae pia yumo Kikosi cha England, amehamia Aston Villa kwa kitita cha Pauni Milioni 12.
Downing, umri miaka 24, ni Mchezaji wa kwanza kusainiwa na Meneja wa Aston Villa Martin O'Neill kwa ajili ya msimu ujao.
Downing aliwahi kuomba kuihama Middlesbrough mwezi Januari lakini akagomewa lakini baada ya Klabu hiyo kuporomoka Daraja Mwenyekiti wake Steve Gibson alitangaza hawezi kumzuia Mchezaji yeyote kuihama Klabu hiyo.
Adebayor aomba muda zaidi kutafakari uhamisho kwenda Man City!!!
Emmanuel Adebayor ameomba apewe muda zaidi kutafakari uhamisho wake kutoka Arsenal kwenda Manchester City kwa sababu anahofia lawama kubwa atakazopata nyumbani kwao Togo ambako Arsenal ni moja ya Klabu zinazopendwa sana.
Arsenal imeshakubali ofa ya Pauni Milioni 25 toka kwa Man City kumnunua Mshambuliaji huyo ambae tayari ameshapewa Kibali cha kubadili Mwajiri wa Kazi.
Hata hivyo inaaminika mapenzi ya Adebayor ni kuhamia AC Milan na huenda kusita kwake kuhamia Man City ni kupata muda zaidi ili mipango ya kwenda AC Milan isukike vizuri.
Man U huenda ikanunua Wachezaji zaidi!
Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, David Gill, amesema Klabu yake inaweza kununua Wachezaji kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa mwishoni mwa Agosti.
Kufuatia kuondoka kwa Ronaldo na Tevez, wengi walitegemea Man U itaingia sokoni kwa kishindo lakini hadi hii leo Mabingwa hao wamewanunua Luis Antonio Valencia, Michael Owen na Gabriel Obertan kwa dau lisilozidi Pauni Milioni 20 kwa Wachezaji wote.
Mwanzoni mwa wiki hii, Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, alisema hawana mpango wa kununua Mchezaji yeyote kwa vile soko limeota mbawa na thamani za Wachezaji zimebomoa paa.
Hata hivyo Bosi mkubwa David Gill, kabla ya Mabingwa hao kuanza ziara ya Asia, hakufunga milango na amekiri bado wanashughulikia ishu ya uhamisho. Gill amesema: ‘Nitaanza siku yangu kila siku kwa kufungua barua pepe na mawasiliano mengine na nina uhakika kutakuwa na masuala ya uhamisho wa Wachezaji!’
Fainali Copa Libertadores: Cruzeiro 1 v Estudiantes 2
Estudiantes ya Argentina imenyakua Ubingwa wa Klabu za Marekani ya Kusini ugenini baada ya kuifunga Cruzeiro ya Brazil 2-1 katika mechi ya marudiano ya Fainali ambayo ni ya 50 ya Mashindano hayo maarufu kwa jina la COPA LIBERTADORES baada ya Klabu hizo kutoka suluhu 0-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyokwisha.

Fainali hii ilichezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Cruzeiro walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Henrique dakika ya 52 lakini Estudiantes walisawazisha dakika ya 58 kupitia Gasto Nicolas Fernandes na Mauro Boselli akawapa Ubingwa kwa bao la dakika ya 73.
Man U waanza ziara bila Vidic!!
Nemanja Vidic hayumo kwenye Kikosi cha Manchester United kilichopanda ndege leo kuelekea Malaysia, Korea na China.
Mwezi uliokwisha Vidic alijitoa kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa ya Serbia kilichopambana na Visiwa vya Faroe kwenye mechi ya Makundi kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia enka na inasadikiwa kuachwa kwake kusafiri ni kumpa muda zaidi wa kuuguza hiyo enka.
Mchezaji mwingine ambae hakuwemo kwenye msafara huo ni Chipukizi Rafael Da Silva.
Lakini, majeruhi wa muda mrefu, Wes Brown na Gary Neville, walikuwemo pamoja na Wachezaji wapya Michael Owen, Antonio Valencia na Gabriel Obertan.
Man U wanacheza na Kombaini ya Malaysia Jumamosi, siku mbili baadae watacheza na FC Seoul huko Korea na tarehe 26 Julai watacheza China na Hangzhou Greentown.
Kikosi kamili kilichosafiri ni: Edwin van der Sar, Tomasz Kuszczak, Ben Foster, Jonny Evans, Patrice Evra, Rio Ferdinand, Gary Neville, Wes Brown, John O’Shea, Fabio da Silva, Nani, Zoran Tosic, Darren Fletcher, Anderson, Darron Gibson, Paul Scholes, Michael Carrick, Ryan Giggs, Michael Owen, Dimitar Berbatov, Federico Macheda, Wayne Rooney.
Benitez aota kubeba Ubingwa LIGI KUU England!!
Bosi wa Liverpool, Rafa Benitez, amekiri ili Timu yake ichukue Ubingwa wa Ligi Kuu England inabidi wasifanye kosa lolote na kupoteza mechi yeyote.
Liverpool msimu uliokwisha walimaliza Ligi wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Mabingwa Manchester United na kuambua jumla ya pointi 86 huku Manchester United wakichota pointi 90.
Liverpool wanahaha kuumaliza ukame wa miaka 20 wa kutotwaa Ubingwa ingawa Benitez anaamini ana Kikosi imara kupita vyote vya nyuma lakini bado ana wasiwasi wanahitaji kuboreka zaidi.
Benitez amesema: ‘Inabidi ufanye kila kitu sahihi huwezi kukubali kufungwa mechi nyingi! Chelsea, Man U na Arsenal ni Timu ngumu na msimu huu Tottenham, Aston Villa na Man City zitatoa upinzani! Ni Ligi ngumu!’
Moyes: ‘Lescott hauzwi!’
Meneja wa Everton, David Moyes, amesisitiza Mlinzi wake anaechezea England, Joleon Lescott hauzwi baada ya kuandamwa mfululizo na Klabu tajiri Manchester City.
Akiongea kwenye mkutano na Wadau wa Klabu hiyo, Moyes amesema: ‘Nilishasema hakuna Mchezaji atakaeuzwa hapa Everton na sina haja kurudia hilo!’
Msimamo huo wa David Moyes umeungwa mkono na Mwenyekiti wa Everton, Bill Kenwright, aliesema David Moyes ndie mwenye kauli
ya mwisho kuhusu Wachezaji.

Wednesday 15 July 2009

Fainali Copa Libertadores: Leo marudio Cruzeiro v Estudiantes!
Mechi ya pili ya Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa za Nchi za Marekani ya Kusini, ambayo ni Fainali ya 50 ya Mashindano hayo maarufu kwa jina la COPA LIBERTADORES, leo itachezwa nchini Brazil baina ya Timu za Nchi Mahasimu Kisoka Argentina na Brazil , baada ya Klabu hizo za Estudiantes ya Argentina na Cruzeiro ya Brazil kutoka suluhu 0-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyokwisha.
Fainali hii inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Wachezaji wa Nigeria kupimwa kutambua umri!!
Wachezaji wa Nigeria watakaocheza Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 itabidi wapimwe mifupa ili kuthibitisha umri wao katika Fainali hizo ambazo Nigeria ndio Wenyeji wa mashindano hayo yatakayochezwa kati ya Oktoba 24 na Novemba 15 mwaka huu.
Kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya Nigeria katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kwamba Nigeria huchezesha Wachezaji waliozidi umri.
Nigeria wameshatwaa Kombe hilo la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 mara 3 katika miaka ya 1985, 1993 na 2007.
Melo ajiunga Juve!!
Kiungo kutoka Brazil alieng'ara sana kwenye michuano ya hivi karibuni ya Kombe la Mabara huko Afrika Kusini na kuiwezsha Brazil kutwaa Kombe hilo, Felipe Melo, amehamia Juventus kutoka Fiorentina kwa ada ya Euro Milioni 25.
Melo alikuwa akihusishwa sana na Klabu ya Arsenal na hasa baada ya kupigiwa debe na Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Gilberto Silva, ambao wote ndio Viungo wa sasa wa Brazil.
Adebayor akaribia kutua Man City
Mshambuliaji toka Togo na Arsenal, Emmanuel Adebayor, anaelekea kukaribia kuwa Mchezaji mpya wa Manchester City baada ya kufaulu vipimo vya afya na pia kupata Kibali cha Kazi.
Man City katika wiki hii moja imemnasa Carlos Tevez na Nahodha wa Chelsea, John Terry, yupo mbioni kujiunga ingawa mpaka sasa Chelsea wanang’ang’ana hauzwi.
Klabu ya Arsenal haijatoa tamko lolote kuhusu uhamisho wa Adebayor.
UEFA yapunguza adhabu za Drogba na Bosingwa
Chama cha Soka Ulaya, UEFA, kimewapunguzia adhabu Didier Drogba na Jose Bosingwa walizopewa baada ya utovu wa nidhamu dhidi ya Refa Tom Henning Ovrebo kutoka Norway baada ya mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa Stamford Bridge kati ya Chelsea na Barcelona ambayo Barca waliibuka washindi kwa goli la ugenini.
Drogba alifungiwa mechi 4 na sasa imepunguzwa hadi mechi 3 na Bosingwa amepunguziwa kutoka mechi 3 hadi 2.
Kupunguziwa adhabu hizi kunafuatia rufaa ya Wachezaji hao iliyofanywa leo na kuhudhuriwa na Wachezaji hao.
Wakati huo huo, Klabu ya Chelsea imetangaza imeongeza mkataba wao na Wafadhili wao Samsung hadi mwaka 2013.
Kampuni hiyo ya Elektroniki ilianza kuwa mfadhili wa Chelsea tangu mwaka 2005.

Tuesday 14 July 2009

Benitez: 'Alonso aombe rasmi kama anaenda Real'
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, amesema kuwa Kiungo wake Xabi Alonso anapaswa kuomba kwa maandishi ikiwa anataka kuhamia Real Madrid ili kila mtu ajue kwamba kweli anayo nia hiyo.
Inasemekana Alonso alimpigia simu Meneja huyo na kumwambia anataka kuhamia Real Madrid na Benitez akamtaka aandike barua.
Hata hivyo, Benitez amesisitiza ikiwa kweli Real wanamtaka Alonso basi lazima wailipe Liverpool Pauni Milioni 35 ingawa Real wametamka thamani ya Alonso haizidi Pauni Milioni 25.
Kocha mpya wa Real Madrid anaetoka Argentina, Manuel Pellegrini, ametamka: 'Si siri, tunamtaka Alonso lakini kumpata ni ishu nyingine!'
Fergie atunukiwa Digrii!!
Meneja wa Mabingwa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametunukiwa Digrii ya Heshima na Chuo Kikuu cha Mjini Manchester kwa mchango wake kwa Jiji la Manchester.
Sir Alex Ferguson, aliezaliwa Desemba 31, mwaka 1941, alijiunga na Klabu ya Manchester United mwaka 1986 na kuiwezesha kutwaa Vikombe vingi kupita Meneja yeyote katika historia ya soka huko Uingereza.
Mwaka 1999, Malkia wa Uingereza alimtunuku heshima ya kuitwa 'Sir' kwa kuiwezesha Manchester United kutwaa Vikombe vitatu kwa mpigo, yaani, FA Cup, Ligi Kuu na Kombe la Klabu Bingwa Ulaya.
Vilevile, Sir Alex Ferguson anayo heshima ya kupewa Tuzo ya Uhuru wa Mji wa Aberdeen huko Scotland baada ya kuiwezesha Klabu ya Aberdeen ya huko Scotland katika miaka ya 1980 kuvunja himaya ya Klabu Vigogo za huko, Celtic na Rangers, na kutwaa Vikombe kadhaa likiwemo Kombe la Washindi la Ulaya walipowafunga Real Madrid mabao 2-1 katika Fainali iliyochezwa Mei 11, mwaka 1983.
Baada ya kumnasa Tevez, Man City wapo mezani kuhusu Adebayor
Manchester City wako kwenye majadiliano mazito ili kumnasa Mshambuliaji kutoka Togo anaecheza Arsenal Emmanuel Adebayor mara tu baada ya Carlos Tevez kumwaga wino kwa Mahasimu hao wa Manchester United.
Inaaminika Adebayor, miaka 25, anaweza akachukuliwa na Man City kwa Pauni Milioni 25 baada ya kuichezea Arsenal kwa miaka mitatu na nusu akitokea Monaco ya Ufaransa.
Adebayor msimu uliokwisha aliifungia Arsenal mabao 16 na kujiunga kwake na Man City kutaimarisha Kikosi hicho ambacho tayari kishawabeba Washambuliaji Carlos Tevez, Roque Santa Cruz na Kiungo Gareth Barry.
Vilevile, Kikosi hicho cha Meneja Mark Hughes kinaweza kuimarika zaidi kwani pia kuna habari nzito Nahodha wa Chelsea na England, John Terry, anaishinikiza Klabu yake imruhusu afanye mazungumzo na Man City ili kuona uwezekano wa kuhama ingawa mpaka sasa hakuna kilichotamkwa.
Kwa kumsaini, Emmanual Adebayor, Mchezaji aliehamia Arsenal kutoka Monaco kwa Pauni Milioni 7 tu, Mark Hughes ana uhakika wa kupata huduma bora ya ufungaji magoli kwani Adebayor katika mechi 142 alizochezea Arsenal amepachika mabao 62.
Msimu wa mwaka 2007/8, Adebayor aliifungia Arsenal mabao 30 lakini msimu uliokwisha majeruhi ya mara kwa mara yamemfanya afunge goli 16 tu kitu kilichowafanya Mashabiki wa Arsenal wahoji moyo wake kwa Klabu.
Kuhama kwa Adebayor hakumstui sana Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ambae tayari ameshamweka sawa Mshambuliaji kutoka Morocco, Marouane Chamakh, anaecheza Bordeaux ya Ufaransa, kuziba pengo hilo.

Monday 13 July 2009

Tevez yuko Man City!!
Kuna taarifa zimeibuka na kuthibitishwa kuwa Carlos Tevez amejiunga na Wapinzani wa Manchester United, Manchester City.
Meneja wa Manchester City, Mark Hughes, amethibitisha habari hizo na kushangilia usajili huo kwa kumsifia Tevez kuwa ni Mchezaji wa Kimataifa wa kiwango cha juu.
Tevez anategemewa kupimwa afya kabla ya kukamilisha taratibu za usajili.
Tevez alichukuliwa na Manchester United kwa mkopo toka Kampuni inayommiliki baada ya kucheza West Ham na alikaa Man U kwa miaka miwili.
Man U walikuwa tayari kulipa pesa za kumnunua Tevez na pia walishampa ofa ya mkataba wa miaka mitano na mshahara mkubwa tu ambao ungemfanya Tevez awe mmoja wa Wachezaji wa Man U wanaolipwa donge nono sana, lakini Tevez aligoma kwa madai kuwa msimu uliokwisha alidharauliwa kwa kutopangwa mara kwa mara.
Mkataba wa Tevez na Manchester United ulimalizika Juni 30.
Sir Alex: 'Hatununui mtu! Hizi mtu 3 tosha!' Owen apewa Jezi Namba 7!!

Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametangaza kuwa hanunui Mchezaji yeyote tena kwa sababu Wachezaji Nyota wote Ulaya bei zao zimefumuka bila kukidhi thamani sahihi.

Sir Alex Ferguson amesema pia ingawa alishazoea kununua Wachezaji kwa bei mbaya kwa vile tu Klabu zinazouza Wachezaji hao zinajua fika wanawauzia Man U lakini 'sama' hii bei 'zimebomoa paa'!

Mpaka sasa Manchester United imenunua Wachezaji watatu tu ambao ni Michael Owen, Luis Antonio Valencia na Gabriel Obertan [pichani wakiwa na Ferguson].

Veterani Michael Owen amepewa Jezi Namba 7 ambayo kihistoria Manchester United waliivaa Wachezaji waliotukuka kama George Best, Bryan Robson, Eric Cantona na David Beckham.

Mchezaji wa mwisho kuivaa ni Ronaldo aliehamia Real Madrid.

Ferguson amenukuliwa akisema: 'Ni mwisho wa biashara yetu! Hadithi nyingine zote-sahau! Kila kona England na Ulaya, thamani ya Wachezaji imepasua paa! Hamna uhamisho wenye thamani ya kweli!'

Ferguson, akiwapoza Washabiki, akasisitiza: 'Tuna Kikosi imara. Kuondoka Mchezaji mmoja watu wasianze kuhamanika! Tumemruhusu aondoke na sisi tuna Kikosi kizuri! Nimeleta Chipukizi na Mkongwe Owen na mtaona akifunga magoli! Siku zote nilikuwa nikiwaambia Madifenda wangu tukicheza nae, msijiache mmesimama tu, atawaponyoka na kufunga, ni hatari huyu!'

Adebayor kwenda Man City???
Kuna uvumi mkubwa kuwa Mshambuliaji wa Arsenal, Emmanuel Adebayor kutoka Togo, yuko mbioni kujiunga na Manchester City iliyokosa kumsaini Mshambuliaji wa Cameroun Samuel Eto'o.

Inaelekea Manchester City wamewapiku AC Milan waliokuwa wakimwania kwa muda mrefu na hata Mchezaji mwenyewe kukiri, wakati fulani, kuwa AC Milan ni Timu nzuri.

Inategemewa Adebayor akihama, Meneja Arsene Wenger atamchukua Mshambuliaji toka Morocco Marouane Chamakh anaecheza Klabu ya Ufaransa Bordeaux ambae mwenyewe yuko tayari kutua Uwanjani Emirates.

Sunday 12 July 2009

John Terry amwomba kibali Abramovich ili aongee na Man City
Kuna taarifa nzito kuwa jana usiku Nahodha wa Chelsea John Terry na Mwenye Klabu hiyo Roman Abramovich walikuwa kwenye mazungumzo mazito ili kuamua hatima ya Terry baada ya Mchezaji huyo kuomba apewe kibali ili azungumze na Manchester City ambao wanamtaka Sentahafu huyo kwa udi na uvumba.
Manchester City, Klabu inayomilikiwa na Matajiri waliokubuhu kutoka Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu wanaotoka Koo za Kifalme za huko, inasadikiwa wako tayari kutoa dau la Pauni Milioni 50 kumnunua Terry na pia kumpa mshahara wa Pauni Laki 2 na nusu kila wiki kitita ambacho kitamfanya awe Mchezaji mwenye mshahara mkubwa Uingereza yote.
Terry, mwenye miaka 28, ambae amekuwa Chelsea tangu utotoni, anaichukulia nafasi hii kama karata yake ya mwisho na hategemei kuipata tena.
Mpaka sasa haijajulikana nini kiliamuliwa katika mazungumzo hayo kati ya Tajiri na Mchezaji wake.
Ibrahimovic adai Chelsea inamtaka!!
Mshambuliaji kutoka Sweden anaecheza Inter Milan, Zlatan Ibrahimovic, amedai kuwa Klabu ya Chelsea inataka asaini huko ingawa Klabu yake inagoma kuwa Mchezaji huyo haendi kokote.
Mwenyewe Ibrahimovic hakusema moja kwa moja kama yuko tayari kuhamia Chelsea ingawa amekubali kuwa ikifika hatua ya uamuzi basi yuko tayari kutafakari kwa undani kama Ligi Kuu England inamfaa na Klabu ipi ni bora kwake.
Mbali ya Chelsea, Ibrahimovic pia amevumishwa kuwa Manchester United wanamuwinda ingawa si yeye wala Manchester United waliothibitisha habari hizo.
Powered By Blogger