Saturday 4 July 2009

Ili kumchota Melo toka Fiorentina, Arsenal watoe ‘vijisenti’ pamoja na Eboue!!
Wakitaka kumchukua Kiungo Felipe Melo alieng’ara sana kwenye mechi za hivi karibuni za Timu ya Taifa ya Brazil za mchujo za Kombe la Dunia la Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini pamoja na Kombe la Mabara huko Afrika Kusini, Arsenal wameambiwa na Klabu ya Melo Fiorentina ya Serie A, Italia, ni lazima watoe dau nono na pia Emmanuel Eboue achukuliwe na Fiorentina.
Mbrazil, Felipe Melo, umri miaka 25, ameongeza mkataba kwa mwaka mmoja zaidi hapo Juni 30 ambao pia una kipengele cha Klabu yake Fiorentina kulipwa Pauni Milioni 21 ili ahame kabla mkataba kumalizika.
Melo alinunuliwa na Fiorentina kwa Pauni Milioni 7 kutoka Klabu ya Spain Almeria mwaka jana na baada ya kushirikiana na Kiungo wa zamani wa Arsenal, Gilbero Silva, kwenye Timu ya Brazil katika mechi za hivi karibuni na kung’ara, chati yake imepanda.
Melo, kwa sasa, ana mkataba na Fiorentina hadi mwaka 2013 na tangu acheze huko Italia amepata sifa ya kuwa Kiungo mpiga makwanja vizuri kitu kilichomsababisha apate Kadi za Njano 17 na Kadi Nyekundu 3 kwa msimu mmoja tu aliocheza Serie A huko Italia. Eboue, Mchezaji kutoka Ivory Coast, msimu uliokwisha alipata msukosuko mkubwa huko Uwanjani Emirates hasa baada ya kuzomewa Desemba 2008 hapo Emirates kwenye mechi dhidi ya Wigan baada ya kuingizwa kutoka benchi na kucheza Soka bovu.
Owen ashangazwa kuchukuliwa na Man U!!
Michael Owen amekiri kuwa hakutegemea kama Manchester United ingeweza kumtaka lakini anaamini kuwa anajiunga na Timu ya washindi.
Akiwa na umri wa miaka 29, Owen mwenyewe anajua siku zake bora zimepita lakini bado ana imani kuwa anaweza kuchangia ili Manchester United ipate mafanikio msimu ujao.
Owen amesema: ‘Ukizungumzia Manchester United siku zote unajua ni Washindi, Vikombe, Uwanja mkubwa na Mashabiki Mamilioni! Kuna Wachezaji bora hapa! Ndio maana wamepata mafanikio makubwa sana! Nadhani sitopata usingizi nikifikiria kuchukuliwa na Manchester United!’
Owen amekiri: ‘Katika miaka michache iliyopita niligundua Sir Alex alikuwa amenikubali kuwa nnao uwezo wa kucheza! Siku zote nilikuwa nikiomba aniombe nichezee Man U! Mie sio mjinga, najua kuna watu wanahisi sina tena uwezo lakini tungoje msimu uanze na nitazungumza nikiwa uwanjani!’
Possebon wa Man U aenda Ureno SC Braga kwa mkopo!!
Mchezaji Rodrigo Possebon, umri miaka 20, aliezaliwa Brazil, amechukuliwa kwa mkopo na Klabu ya Ureno SC Braga na ataisaidia Klabu hiyo itakayocheza Ligi mpya huko Ulaya inayoitwa UEFA Europa League msimu ujao.
Possebon, ambae ni Kiungo na ameshaichezea Timu ya Taifa ya Italia ya Vijana chini ya miaka 20, msimu uliokwisha alicheza Manchester United mechi chache na muda mwingi alikuwa akicheza Timu ya Akiba.
Wakati huohuo, Chipukizi wa miaka 16 kutoka Klabu ya Empoli ya Italia anaeitwa Alberto Massacci anaecheza kama Beki wa pembeni ametamka yuko njiani kujiunga na Manchester United baada ya kufanya mazungumzo na Sir Alex Ferguson.
Habari hizi hazijathibishwa na Manchester United na bila shaka zitazua zogo kubwa huko Italia kwani Chipukizi huyo anasemekana ni Mchezaji anaeonyesha matumaini makubwa ya kuwa bora huko usoni na Klabu za Italia zinashindwa kuwazuia kuondoka kwa vile sheria zinawabana kuwasaini Wachezaji chini ya miaka 18 na hali kama hii ni sawa kama ile ya Chipukizi nyota wa Manchester United, Federico Macheda, aliechukuliwa na Man U.
Ronaldo: ‘Ferguson yuko moyoni mwangu!’
Cristiano Ronaldo amekiri kuwa Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, yuko moyoni mwake na siku zote atamuenzi.
Ronaldo ametoa matamshi hayo huku Real Madrid wakijitayarisha kumtambulisha kama Mchezaji wao hapo Jumatatu kufuatia uhamisho ulioweka rekodi ya ada kubwa kupita zote ya Puni Milioni 80 kutoka Klabu ya Manchester United.
Sir Alex Ferguson alimnunua Ronaldo kutoka Klabu ya Ureno ya Sporting Lisbon kwa Pauni Milioni 12.2 mwaka 2003 na amemwezesha kuwa Mchezaji Bora Duniani.
Ronaldo ametamka: ‘Yeye ni Baba yangu kwenye michezo! Ni mtu muhimu sana kwenye maisha yangu! Inabidi nimshukuru kwa yote aliyonifundisha! Yeye ndio msingi wangu! Siku zote nitampenda na atakuwa moyoni mwangu! Vilevile nawashkuru Mkurugenzi Mkuu David Gill na Wakurugenzi wote!
Ronaldo pia amesema hivi karibuni atasafiri hadi Manchester ili kwenda kumshkuru Ferguson na pia alitoa shukrani zake za dhati kwa Mashabiki wa Man U kwa kusema: ‘Ni nyumbani kwangu! Nimecheza misimu 6 na siku zote walinipenda na kuniimba! Ni mashabiki spesho!’
Chelsea wamsaini Sturridge toka Man City
Chelsea wamemsaini Daniel Sturridge, umri miaka 19, kutoka Manchester City kwa mkataba wa miaka minne.
Sturridge alianza kuchezea Man City Februari 2007 na kufunga mabao manne katika mechi 26 alizocheza na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 24, akiwa ameukataa mkataba mpya hapo Man City, Klabu ya Chelsea itabidi iilipe fidia Man City kwa kumkuza Mchezaji huyo.
Sturridge ni mpwa wa Mchezaji wa zamani wa Derby Dean Sturridge.
Ince arudi tena MK Dons kama Bosi!!
Paul Ince amesaini mkataba wa miaka miwili na Klabu yake ya zamani Milton Keynes Dons kama Meneja na hii ni mara ya pili kwa Ince kuiongoza Klabu hiyo.
Ince anachukua nafasi ya Roberto Di Matteo aliehamia West Bromwich Albion.
Paul Ince anarudi tena MK Dons mwaka mmoja tu baada ya kuihama Klabu hiyo ili kujiunga na Blackburn Rovers ambako hakudumu na alifukuzwa Desemba mwaka jana.
Kwa sasa MK Dons inacheza ligi Daraja la Chini.
Dalglish arudi Liverpool
Kenny Dalglish, ambae alichukua Ubingwa wa England mara 8 katika miaka 14 aliyodumu Liverpool kama Mchezaji na Meneja, amerudi tena Klabuni hapo kama Afisa wa ngazi za Juu kwenye Chuo cha Soka na pia Balozi wa Klabu hiyo.
Akitangaza hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Liverpool, Christian Purslow, amesema: ‘Tunafuraha na hatua hii! ‘
Baada ya kuondoka Liverpool mwaka 1991, Kenny Dalglish akaenda kuwa Meneja huko Blackburn Rovers na kisha Newcastle United na baada ya hapo akawa Mkurugenzi wa Soka huko Celtic Nchini Scotland.
Gibbs aongeza mkataba Arsenal
Beki Chipukizi wa kushoto wa Arsenal, Kieran Gibbs, amesaini kile kinachoitwa ‘mkataba wa muda mrefu’ na Klabu hiyo.
Gibbs, miaka 19, ambae alichukua nafasi ya Beki wa kutumainiwa, Gael Clichy, alipoumia msimu uliopita na kusimama imara kabisa, hivi karibuni ameisaidia Timu ya Vijana ya England ya Chini ya Miaka 21 kuingia Fainali ya Kombe la Ulaya na kufungwa 4-0 na Ujerumani.
Refa Bennett ahamia Kriketi!!
Refa wa Ligi Kuu England Steve Bennett sasa amehamia kwenye mchezo wa Kriketi na atakuwa Mkurugenzi wa Chama cha Waamuzi wa Kriketi ndani ya Bodi ya Kriketi huko England na Wales.
Bennet, miaka 48, ni Refa wa muda mrefu katika Ligi Kuu England na alichezesha Fainali ya Kombe la FA mwaka 2007 na amekuwa Refa wa Ligi Kuu tangu mwaka 1999.
Muhammad Ali kuzuru Old Trafford, Wembley na Uwanja wa Klabu ya Stoke City!!!
Bingwa wa zamani Duniani na Bondia maarufu sana Duniani, Mkongwe Muhammad Ali, atatembelea England hivi karibuni ikiwa ni ziara maalum ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mfuko wa Kituo chake kiitwacho Kituo cha Muhammad Ali.
Akiwa England, Muhammad Ali ataitembelea Old Trafford, nyumbani kwa Mabingwa Manchester United, Uwanja wa Wembley na ule wa Klabu ya Stoke City uitwao Britannia.
Akizungumzia ziara hiyo, Muhammad Ali, amesema: ‘Uingereza iko moyoni mwangu. Nataka kufanya ziara hii si kwa sababu ya kuchangisha pesa tu bali pia kuiona Nchi hiyo nzuri na kuwaona Marafiki zangu na Mashabiki wangu!’

Friday 3 July 2009

Straika Veterani wa Liverpool Ian Rush akiri Owen atazaliwa upya Man U!!!
Ian Rush anaamini kabisa kwamba kwenda Michael Owen Manchester United kutamfanya azaliwe upya na kurudisha namba yake kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa ya England ambako amechezea mechi moja tu tangu kuanza kwa utawala wa Mtaliana Fabio Capello kama Meneja wa England.
Kwa wengi usajili wa Michael Owen Manchester United umekuja kwa mshangao mkubwa hasa ukichukulia historia ya Michael Owen ya miaka ya hivi karibuni ya kuumia mara kwa mara lakini Supastaa wa zamani na Mfungaji Veterani wa Liverpool Ian Rush yuko taofauti.
Ian Rush amesema: ‘Owen ni Mfungaji mzuri sana bila ubishi! Kwa Sir Alex Ferguson kumchukua si kucheza tombola na nina uhakika atawafungia mabao mengi sana! Angalia Ferguson alimchukua Larsson na ikawa ni mafanikio makubwa sana na Owen itakuwa hivyo hivyo!’
Ian Rush ameongeza kwa kusema Manchester United itamsaidia Owen kuitwa tena kuchezea England na hata kwenda Fainali Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini hasa kwa sababu Man U ina Wachezaji wazuri watakaomchezesha vizuri Owen na kumfanya ang’are.
Tovuti ya Manchester United imevamiwa na Washabiki wa Manchester United wakimpongeza Sir Alex Ferguson kwa kumchukua Michael Owen na wengi wameomba siku Man U ikicheza na Liverpool basi wangependa Michael Owen ndie afunge goli la ushindi dhidi ya maadui hao wakubwa wa Man U na Klabu ya zamani ya Owen.
Michael Owen asaini mkataba wa miaka miwili Man U!!!
Mshambuliaji wa England, Michael Owen, miaka 29, ambae mkataba wake Klabuni Newcastle ulimalizika Julai 1, leo amesaini mkataba wa miaka miwili na Mabingwa wa England, Manchester United.
Sir Alex Ferguson ametamka: ‘Owen ni Mchezaji wa kiwango cha juu sana duniani na ni mfungaji mahiri na hilo huwezi kulibishia! Ujio wake Manchester United na matumaini ambayo tunayo yatampa changamoto!’
Michael Owen mwenyewe amesema: ‘Nilikuwa nimeanza majadiliano na baadhi ya Klabu za Ligi Kuu lakini, bila kutegemea, Sir Alex akanipigia simu Jumatano mchana na kunialika kifungua kinywa siku ya pili ndipo siku hiyo akaniambia anataka nijiunge Manchester United! Sikusita hata sekunde moja! Nikakubali hapohapo!’ Hii ni nafasi bora sana kwangu na nimeipokea kwa mikono miwili!’
Owen akaongeza: ‘Nategemea kwa hamu kubwa sana kuanza mazoezi na Timu hii Wachezaji wakirudi likizo na nna bahati kubwa nawajua Wachezaji wengi hapa! Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Sir Alex Ferguson kwa imani yake kwangu na ninamhakikishia nitalipa fadhila yake kwa magoli na uchezaji wangu!’
Wadau wengi wanaamini kwa Sir Alex Ferguson kumsajili Michael Owen ni kucheza tombola kwa vile miaka ya hivi karibuni ameandamwa na kuumia mara kwa mara lakini pia inaweza ikawa ni karata ya trufu kama aliyoicheza wakati ule alipowasaini Henrik Larson na Teddy Sheringham, Wachezaji ambao wengi waliamini wamekwisha na ilikuwa makosa kwa Sir Alex Ferguson kuwachukua, lakini baadae, watu wote, baada ya Wachezaji hao kung’ara, wakakubali kuwa Ferguson ni mchawi na alifanya sahihi kuwasajili Larson na Sheringham.
REAL: BADO MTU MBILI!!!
Rais wa Real Madrid, Emmanuel Perez, amesema bado wanahitaji kusaini Wacheza wawili zaidi ili kukamilisha ujenzi wa Kikosi kipya huko Santiago Bernabeu.
Tayari Real Madrid, wakimwaga vijisenti kichizi, wameshawateka Cristiano Ronaldo, Kaka na Raul Albiol kwa jumla ya dau la ajabu la Pauni Milioni 148 na sasa wako njiani kumshika Karim Benzema kutoka Lyon ya Ufaransa.
Perez hakutaja ni Wachezaji gani watawabeba ingawa Kiungo wa Liverpool Xabi Alonso amehusishwa sana na pia Franck Ribery wa Bayern Munich ambae Klabu yake ya Bayern Munich haitaki aondoke.
Michael Owen huenda akajiunga na Man U!!!
Mshambuliaji Michael Owen leo alikwenda Uwanja wa Carrington ambako ndipo kambi ya mazoezi ya Klabu ya Manchester United kupimwa afya yake ikiwa ni hatua thabiti ya kumfanya ajiunge na Mabingwa hao.
Owen ameondoka Newcastle baada ya mkataba wake kumalizika na yeye mwenyewe kugoma kuuongeza kwa Klabu hiyo iliyoporomoka Daraja.
Owen, mwenye umri wa miaka 29, amekuwa pia akiwindwa na Klabu za Hull City na Stoke City lakini kwa sasa, akifaulu vipimo vya afya , atakuwa Mchezaji wa Manchester United.
Sir Alex Ferguson , baada ya kuondokewa na Ronaldo na Tevez, yuko mbioni kuimarisha Kikosi chake na tayari ameshamsaini Winga Luis Antonio Valencia kutoka Wigan na nia ya kumchukua Owen bila shaka imekuja baada ya kuvutiwa na uzoefu wa Owen katika ufungaji ingawa hivi miaka ya karibuni amekuwa akiandamwa na majeruhi ya mara kwa mara.
Bila shaka kujiunga kwa Owen Manchester United kutapokewa kwa maudhi makubwa na Washabiki wa Liverpool kwani Owen ndiko alikoanza kuchezea Soka tangu utoto na akadumu kwa miaka 8 na kisha kuhamia Real Madrid mwaka 2004 na huko alikaa mwaka mmoja na kununuliwa na Newcastle kwa mkataba wa miaka minne.
Owen pia ameichezea England mara 89.
Chelsea yagoma Nahodha wao Terry kwenda Man City!!
Klabu ya Chelsea, kwa mara ya pili sasa, imeikataa ofa ya Manchester City ya kutaka kumnunua Nahodha wao John Terry na habari hizi zimethibitishwa na Maafisa wa Stamford Bridge.
Msimu uliokwisha, Man City pia walitoa ofa ya kumnunua Terry lakini wakagomewa.
Wenger ana uhakika Adebayor haondoki!
Rais Laporta wa Barca adai Fabregas anaitaka Barcelona!!!
Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema ana uhakika Mshambuliaji wake Emmanuel Adebayor haondoki kwenda kujiunga na AC Milan lakini akitaka mwenyewe kuondoka hawezi kumzuia.
Kwa muda mrefu sasa, Mshambuliaji huyo kutoka Togo amehusishwa na Klabu hiyo ya San Siro na mwenyewe ameelezwa kuwa anapenda kwenda huko kwa sababu Arsenal haijapata mafanikio yeyote tangu 2005 walipochukua FA Cup.
Wenger ameongeza pia kuwa endapo Adebayor ataondoka basi angependa kumchukua mshambuliaji wa Bordeaux ya Ufaransa Marouane Chamakh kama mbadala wake na amedokeza kuwa Mchezaji huyo kutoka Morocco amekubali kuja Arsenal.
Wakati huohuo, Joan Laporta wa Brcelona ya Spain, amedai kuwa Kiungo na Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, ana nia ya kujiunga na Mabingwa hao wa Ulaya.
Cesc Fabregas, umri miaka 22, alikuwa Mchezaji wa Timu ya Vijana huko Barcelona na aliihama Klabu hiyo miaka 6 iliyopita na kujiunga na Arsenal na sasa, kufuatana na Lporta, anataka kurudi kwao Spain.
Lakini mpaka sasa hamna dalili yeyote kutoka kwa Fabregas mwenyewe kuwa ana nia hiyo kwani ni wiki iliyokwisha tu alitamka waziwazi nia yake kubakia Emirates Stadium.
Bayern Munich bado inamwinda Bosingwa!
Klabu Kongwe ya Ujerumani, Bayern Munich, bado ina nia ya kumnunua Mlinzi wa Ureno Jose Bosingwa kutoka Chelsea na nia hiyo imethibitishwa na Mwenyekiti wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
Rummenigge amesema Klabu yao ipo kwenye majadiliano kamambe na Chelsea na wana uhakika watamnasa Beki huyo ambae inategemewa ataziba pengo la Willy Sagnol aliestaafu.

Thursday 2 July 2009

NI YALE YALE: Ribery ni Real tu!!!!
Franck Ribéry, aliehusishwa kwenda Chelsea au Manchester United, ametoka bayana na kusema anataka kwenda Real Madrid na si kwingineko.
Hii inafuatia uthibitisho kuwa Mchezaji mwenzake wa Ufaransa, Karim Benzema, yuko safarini kuelekea Real.
Pia, kauli ya Ribery inatoa ushahidi mkubwa kuwa huwezi kumchukua Mchezaji yeyote wa Ufaransa endapo Real Madrid inamtaka kwa sababu tu upo mkono mkubwa wa Zinedine Zidane anae warubuni Wachezaji hao kwa sababu ni Balozi wa Real Madrid.
Hata hivyo, Klabu ya Franck Ribery, Bayern Munich ya Ujerumani ambayo Ribery alijiunga 2007 akitokea Marseille ya Ufaransa, imetoa msimamo wao kupitia Meneja Mkuu Uli Hoeness ambae ameshangaa: ‘Ni kweli Franck anataka kwenda Real? Kwa sisi, hiyo haibadilishi kitu! Maisha siku zote si ndoto tamu! Real hawajaongea chochote na sisi hatuhitaji pesa zao!’
Benzema aenda Real Madrid!!!!
Karim Benzema, umri miaka 21, ametangazwa na Klabu yake ya Lyon ya Ufaransa kuwa atanunuliwa na Real Madrid kwa Pauni Milioni 30 na dau hilo linaweza kupanda hadi Milioni 35 kutegemea na mafanikio yake huko Real Madrid.
Karim Benzema ni Mrafansa alieanza kucheza Lyon tangu akiwa na miaka 9 kwenye Timu ya Watoto na alianza kucheza Kikosi cha kwanza cha Timu hiyo akiwa na miaka 17.
Msimu wa mwaka 2007/8 Benzema alifunga mabao 31 katika mechi 51 na kuwapa Ubingwa wa Ufaransa Lyon lakini msimu uliokwisha amefunga jumla ya mabao 23 tu katika mechi zote alizocheza na Lyon ikaukosa Ubingwa wa Ufaransa kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka minane.
Ingawa ilivumishwa Karim Benzema atanunuliwa na Sir Alex Ferguson kwenda Manchester United lakini hilo halikuwezekana kwa sababu tu Real Madrid huwa wanamtumia Mfaransa Zinedine Zidane aliekuwa Mchezaji wa Real na ambae sasa wamemfanya Balozi wao ili kuwarubuni Wafaransa wenzake.
Mkono wa Zidane pia umewazuia Manchester United na Klabu nyingine yeyote kumchukua Franck Ribery kutoka Bayern Munich kwa sababu tu mpaka sasa Real Madrid wanaonyesha nia ya kumtaka Ribery.
Mpaka sasa Real Madrid imeshawanunua pia Cristiano Ronaldo, Kaka na Mlinzi Raul Albiol kwa kitita kikubwa sana cha Pauni Milioni 148.
Nani atafuata? Ribery? Alonso? Fabregas?
NANI ANAJUA?

Wednesday 1 July 2009

Brazil yaing’oa Spain, sasa ni NAMBARI WANI Duniani!!!
Bongo tuko Topu Mia!!!
Baada ya kunyakua Kombe la Mabara huko Afrika Kusini Jumapili iliyopita, Brazil wamechukua Nambari Wani kwenye Listi ya FIFA ya Nchi Bora Kisoka Duniani na kuidondosha Spain hadi nafasi ya pili.
Kwa mara ya mwisho Brazil kuwa kileleni ni Agosti mwaka 2007.
Timu ya 3 ni Uholanzi, 4 ni Italia na Ujerumani ni nafasi ya 5.

Nafasi ya 6 ni Urusi, England ni wa 7 na Argentina wa 8.
Timu ya juu kabisa toka Afrika ni Ivory Coast walio nafasi ya 18 wakifuatiwa na Cameroun nafasi ya 29, Gabon ya 30, Nigeria ya 34, Ghana 35 na Misri ya 38.
Timu yetu, Bongo, tuko nafasi ya 97 tukiwa tumezipita Gambia ambao wako nafasi ya 99, Congo DR nafasi ya 102, Angola 103, Kenya 105, Malawi 110, Rwanda 113, Namibia 115, Zimbabwe 116.
Timu ya mwisho kabisa kwenye listi hiyo ya FIFA ni Papua New Guinea walio nafasi ya 203.
Watano watimuliwa Portsmouth!
Portsmouth imeanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya kwa kuwaondoa Wachezaji watano toka kwenye Kikosi chao.
Wachezaji Noe Pamarot, Lauren, Glen Little, Djimi Traore na Jerome Thomas wamearifiwa kuwa mikataba yao haitaongezwa na wako huru kutimka.
Kati ya hao Beki Djimi Traore ameshapata Klabu Ufaransa kwa kusaini mkataba na AS Monaco huku Mnigeria Kanu bado anatafakari ofa ya nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja aliopewa na Sol Campbell, ambae mkataba wake umekwisha, bado anajadiliana na Portsmouth kuhusu nyogeza.
Beki wa zamani wa Arsenal, Lauren, miaka 32, pamoja na Traore hawakucheza hata mechi moja msimu uliopita na Pamarot alicheza mechi 22.
Mbali ya hao watano waliomwagwa, Glen Johnson, Jermaine Pennant na Armand Traore wameshahamia Klabu nyingine.
Ramsey apewa ofa mpya Arsenal!
Chipukizi Aaron Ramsey, miaka 18, amesaini mkataba mpya na wa muda mrefu Klabuni kwake Arsenal.
Kiungo huyo kutoka Wales aliechukuliwa kutoka Cardiff City kwa Pauni Milioni 5 msimu uliokwisha alichezea mechi 22 Arsenal msimu uliopita.
Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema: ‘Alitoa mchango bora. Alionyesha ni Mchezaji mwerevu. Bado ana miaka 18 lakini ataendelea kukua na sisi.’
Wakati huohuo, Arsenal imemtema Kiungo kutoka Ureno, Amaury Bischoff, miaka 22, mwaka mmoja tu tangu atue hapo kutoka Timu ya Ujerumani Werder Bremen.
Bischoff alicheza mechi 4 tu msimu uliopita.
STEVE BRUCE: ‘Kwa Luis Antonio Valencia, Fergie amevua lulu!!’
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Steve Bruce, ambae kwa sasa ni Meneja wa Sunderland na kabla ya hapo alikuwa Klabu ya Wigan, amesema Sir Alex Ferguson amevua lulu kwa kumsaini Luis Antonio Valencia, umri miaka 23, kutoka Wigan.
Valencia amehamia Manchester United jana kwa dau la Pauni Milioni 16 kutoka Wigan ambako Steve Bruce alikuwa Meneja wao kabla ya kuhamia Sunderland msimu uliokwisha ulipomalizika.
Steve Bruce amenena: ‘Antonio ni lulu! Ni Mchezaji mahiri, mchapa kazi kiwanjani na nje ya uwanja ni mwungwana! Ni Winga mwenye nguvu, kasi, akili na ni Mchezaji kitimu! Si haki kumfananisha na Ronaldo lakini yeye ni mpiganaji kupita Ronaldo!’
Steve Bruce amehitimisha kwa kunena ana uhakika Sir Alex Ferguson atafaidika na mchango wa Valencia na kuwa endapo Valencia atajiboresha katika ufungaji basi ni lazima atakuwa Staa mkubwa hapo Old Trafford.
Wakati huohuo, Luis Antonio Valencia ametoa shukrani zake za dhati kwa Klabu ya Wigan kwa kumpa nafasi ya kujiendeleza Ligi Kuu England wakati akiwa bado ni kinda tu. Valencia alianza kucheza Wigan kwa mkopo miaka mitatu iliyopita akitokea Villareal ya Spain.
Valencia amesema: ‘Ni kitu chepesi! Bila ya Wigan nisingekuwa hapa Man U! Wigan ndio imenifikisha hapa! Natoa shukrani zangu kubwa na za dhati kwa Paul Jewell [Meneja aliekuwa Wigan aliposajiliwa], Chris Hutchings na Steve Bruce! Shukran zangu kubwa sana zinaenda kwa Mmiliki na Mwenyekiti wa Wigan, Dave Whelan!’
Real waikabidhi Pauni Milioni 80 Man U!!
Fergie amsifia Ronaldo!!!
Cristiano Ronaldo leo rasmi amekuwa Mchezaji wa Real Madrid baada ya Klabu hiyo kuilipa Manchester United kitita chote cha Pauni Milioni 80.
Sir Alex Ferguson, ambae jana aliripoti ofisini baada ya kuwa likizo, ametamka: ‘Kila mtu anamtakia kila la kheri! Cristiano alikuwa Mchezaji bora kwa Manchester United! Miaka yake 6 hapa Old Trafford ilimfanya awe Mchezaji Bora Duniani! Mchango wake ulichangia mafanikio makubwa ya Klabu hii alipokuwepo na kipaji, uwezo wa kufurahisha Washabiki pamoja na utu wake umemfanya apendwe na Washabiki dunia nzima!’
Vidic atoboa: ‘Mke wangu haipendi Manchester, mie ni Man U damu!!’
Nemanja Vidic amepasua kuwa alipata ofa za kwenda kucheza Klabu za AC Milan, Real Madrid na Barcelona lakini amezikataa kwa sababu ya mapenzi yake kwa Manchester United ingawa Mke wake hapendi kuishi Jiji la Manchester.
Vidic, anaesifiwa kuwa ni mmoja wa Mabeki wa Kati wazuri duniani tangu ahamie Manchester United, amesema: ‘Mke wangu Ana hana furaha na mtindo wa maisha ya Manchester lakini siwezi kubadilisha mawazo kwa sababu nina furaha kuchezea Man U! Nilipata ofa kutoka AC Milan, Real Madrid na Barcelona lakini nimezikataa na nikawa mkweli nikaenda kumwambia Bosi wangu Sir Alex Ferguson!’ Vidic anaongeza: ‘Walitaka kulipa ada ya Pauni Milioni 30 kwa uhamisho wangu! Sir Alex Ferguson akaniongezea malupulupu na sasa, ingawa silipwi kama Rooney au Rio, nalipwa kama Berbatov au Carrick! Ntabaki Man U mpaka 2012!’

Tuesday 30 June 2009

NI RASMI, VALENCIA YUKO OLD TRAFFORD!!
Manchester United, kupitia tovuti yake, imethibitisha imefanya usajili wake wa kwanza kwa ajili ya msimu ujao baada ya kumnunua Winga kutoka Ecuador, Antonio Valencia, aliekuwa akichezea Timu ya Wigan kwa mkataba wa miaka minne na dau ambalo halikutajwa.
Valencia, umri miaka 23, ameshaichezea Nchi yake mara 34 na kufunga mabao manne.
Sir Alex Ferguson ametamka mbele ya Valencia waliposaini mkataba: ‘Antonio ni Mchezaji tuliekuwa tukimhusudu kwa muda sasa na baada ya kuwa Ligi Kuu kwa miaka miwili sasa nina uhakika kasi yake na kipaji chake itasaidia sana Kikosi chetu.’
Valencia nae alizungumza: ‘Kujiunga Manchester United ni ndoto iliyotimia kwangu! Nilifurahi nilipokuwa Wigan lakini sasa nna nafasi ya kupata mafanikio makubwa hapa! Kucheza mbele ya Washabiki 76,000 na kucheza pamoja na kina Rooney, Ferdinand na Giggs ni kitu cha kustaajabisha kwangu! Siwezi kujizuia kwa hamu yangu!’
Blackburn yamnasa Chipukizi toka Ufaransa N’Zonzi!!
Blackburn Rovers, chini ya Meneja Sam Allardyce, leo wamefanya usajili wao wa nne kwa msimu ujao baada ya kumnasa Kiungo wa miaka 20 kutoka Ufaransa aitwae Steven N’Zonzi aliekuwa akichezea Klabu ya Amiens ambayo imeshushwa Daraja huko Ufaransa.
Blackburn pia imewasaini Walinzi Gael Givet na Lars Jacobsen na Kiungo kutoka Bondeni Elrio van Heerden.
Bosi Sam Allardyce ameonyesha nia yake kumsaini Mchezaji wa tano ambae ni Mkongwe wa Real Madrid Ruud van Nistelrooy.
Maldini agoma kufundisha Chelsea!!
Meneja wa Chelsea, Mtaliana Carlo Ancelotti, amekiri kuwa ofa yake kwa Paolo Maldini ajiunge nae Stamford Bridge ili kuwa mmoja wa Makocha imetupwa chini na Maldini ambae alistaafu kucheza soka AC Milan msimu ulioisha mwezi Mei ambako walikuwa pamoja na Ancelotti.
Ancelotti anasema: ‘Nilimpa ofa lakini amekataa kwani anataka mapumziko toka kwenye Soka.’
Tangu itangazwe Carlo Ancelotti kuwa Meneja mpya hapo Chelsea Klabu hiyo haijasaini Mchezaji yeyote mpya kwa msimu ujao na Ancelotti anasema: ‘Soko la Uhamisho limekuwa gumu! Baada ya Ronaldo kuhamia Real, kila kitu kimepata wazimu!’
Mmisri Zaki anataka kurudi Wigan
Amr Zaki anataka kurudi Klabu ya Wigan Athletic na ana matumaini Meneja mpya wa Klabu hiyo Roberto Martinez atampa mkataba wa kudumu.
Zaki alikuwa Wigan msimu uliokwisha kwa mkopo kutoka Zamalek ya Misri lakini akajiingiza matatani na aliekuwa Meneja wa Wigan Steve Bruce baada ya kuwa na tabia ya uchelewaji kurudi Klabuni kila anapoenda kwao MIsri kuichezea Nchi yake kwenye mechi za Kimataifa hali iliyomfanya Steve Bruce agome kumchukua kwa mkataba wa kudumu ingawa aling’ara Wigan.
Baada kuhama Steve Bruce kwenda Sunderland na ujio wa Meneja mpya Roberto Martinez kumpa matumaini mapya kurudi Wigan, Zaki anasema: ‘Nataka kubaki Wigan. Nasikia Martinez ni Kocha mwenye kipaji na bado Kijana na hivyo yuko karibu na Wachezaji.’
Tevez amlaumu Fergie!!!!
Carlos Tevez hakucheza Fainali ya Roma kati ya Barcelona na Manchester United, mechi ambayo Man U walifungwa 2-0 na badala yake Sir Alex Ferguson akaanza na Kikosi chenye Washambuliaji Ronaldo,Park Ji-sung na Wayne Rooney, na sasa Tevez anadai kuwekwa kwake benchi ni makosa na ndio kumesababisha Man U kufungwa.
Tevez, ambae ameikataa ofa ya Man U na sasa yuko mbioni kwenda Klabu nyingine baada ya mkataba wake wa kuwa hapo Old Trafford kumalizika leo, amelalama: ‘Huwezi kumbishia Alex Ferguson! Yeye ni kama Rais wa England! Siku zote huwezi kumshinda kwani utashindwa tu! Lakini alifanya kosa kuniweka benchi! Hiyo ndio fainali pekee Man U wameipoteza tangu niwe hapo!’
Wakala wa Eto’o adai hang’oki Barca ng’oo!!
Josep Maria Mesalles, Wakala wa Mshambuliaji kutoka Cameroun Samuel Eto’o anaechezea Barcelona, aliitisha mkutano wa Waandishi Habari ili kuvunja utata kuhusu Mteja wake ambae mkataba wake na Barcelona unamalizika mwishoni mwa msimu ujao na kutamka kuwa Eto’o ameongezewa miaka miwili na Barca kwa vipengele vilevile vilivyomo kwenye mkataba wa sasa.
Wakala huyo amelazimika kusimama kidete huku kukiwa kumezagaa taarifa kuwa Manchester City imetoa ofa ya Pauni Milioni 25 kumnunua Eto’o na kumpa mkataba ambao masilahi yake ni makubwa mno kiasi ambacho Rais wa Barca Joan Laporta kuuita ni mkataba wa ‘hali ya juu mno!’
Hata hivyo Wakala Josep Maria Mesalles hakufunga milango na ametamka: ‘Eto’o anarudi mazoezini Julai 20 kutoka mapumziko. Kama kuna ofa kutoka Man City yenye uzito na Barca wameiafiki basi na sisi hatuoni ugumu kufikia makubaliano.’
Vijana Ujerumani Mabingwa wa Ulaya!! Waikung'uta England 4-0!!!
Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 21 ya Ujerumani jana huko Malmo, Sweden iliibamiza England kwa mabao 4-0 na kutwaa Ubingwa wa Ulaya wa Vijana.
Mpaka mapumziko Ujerumani walikuwa mbele bao 1-0 kwa bao la alilofunga Gonzalo Castro dakika ya 23.
Kipindi cha pili, Ujerumani waliongeza bao 3 zilizofungwa na Ozil dakika ya 48 na mawili kupitia wagner dakika za 79 na 84.
VIKOSI:
Germany: Neuer, Beck, Howedes, Boateng, Boenisch, Hummels, Johnson, Castro, Khedira, Ozil, Wagner.
Akiba: Fromlowitz, Aogo, Ebert, Marin, Schwaab, Grote, Adlung, Ben-Hatira, Schmelzer, Ede, Sippel.
England: Loach, Cranie, Richards, Onuoha, Gibbs, Cattermole, Muamba, Noble, Milner, Walcott, Johnson.
Akiba: Lewis, Taylor, Stearman, Gardner, Rodwell, Tomkins, Mancienne, Driver, Rose.
Refa: Bjorn Kuipers (Holland).

Monday 29 June 2009

KOMBE LA MABARA: Nini Tathmini ya FIFA kwa Afrika Kusini kuandaa KOMBE LA DUNIA mwakani?
Kombe la Mabara lilishindaniwa na Timu 8 tu, Brazil ikaibuka kidedea, mechi kuchezwa kwenye Miji minne tu na wengi wa Watazamaji kuwa ni Raia wa Afrika Kusini.
Mwakani, kwenye Fainali za Kombe la Dunia, hali itakuwa tofauti kabisa kwani Washabiki Wageni zaidi ya 500,000 watatua Afrika Kusini kuziona Timu 32 zikicheza mechi kwenye Viwanja 10 kila kona ya Afrika Kusini.
Hata hivyo kuandaa na kuendesha Kombe la Mabara kumewapa Afrika Kusini nafasi nzuri kujifunza nini wategemee mwakani na vilevile kuwapa fursa FIFA kutoa tathmini na pia kuangalia wapi pana mapungufu.
FIFA, wakilinganisha mahudhurio ya mechi za Kombe la Mabara yaliyopita, wameridhishwa kuwa mahudhurio yalikuwa bora kwani, kulingana na Danny Jordaan, Mwandalizi wa Fainali za Kombe la Dunia 2010, wastani wa Washabiki 38,000 walitizama mechi wakati huko Ujerumani mwaka 2005 lilipochezwa Kombe la Mabara ni wastani wa Washabiki 37,000 tu walihudhuria.
Huko Ufaransa mwaka 1997 ni watu 30,000 tu waliona mechi uwanjani.
Hata hivyo, mapengo mengi yalionekana Uwanjani wakati wa mechi na hata zile za Nusu Fainali kati ya Bafana Bafana na Brazil na pia Fainali ya jana mechi zote zikiwa Uwanja wa Ellis Park, Johannesburg.
Tathmini inasema hiyo imetokana na sababu kadhaa zikiwemo Tiketi kuuzwa mara 3 zaidi ya bei ya zile mechi za Ligi Kuu ya Bondeni na pia mechi kama ile kati ya Iraq na New Zealand kutokuwa na mvuto kwa Mashabiki.
Sababu nyingine ni kuwa wakati huu ni msimu wa baridi huko Afrika Kusini na Mashabiki wamezoea mechi zao kuchezwa majira ya joto.
Lakini, FIFA imesema kuna maombi ya tiketi zaidi ya 500,000 kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia na Asilimia 80 ni ya Raia wa Kigeni.
Kitu kingine kilichozua mjadala ni VUVUZELA.
Katika kila mechi sauti kubwa za tarumbeta za plastiki, mithili ya kundi kubwa la Tembo wakivamia, zilitawala.
Blatter, pamoja na Timu nyingi za Kigeni, walionyeshwa kukerwa na kelele hizo lakini Danny Jordaan anasema: ‘Ni kweli Vuvuzela lina mikelele lakini kwenye Kombe la Dunia kwenye mechi za Brazil au England kutakuwa na Vuvuzela chache kwani Mashabiki wa Nchi hizo watajazana!’
Kombe la Mabara lilichezwa kwenye Viwanja vinne-Ellis Park, Johannesburg, Free State, Bloemfontein, Royal Bafokeng, Rustenburg na Loftus Versfeld, Pretoria-vyote vikiwa pia ndivyo vitakavyochezewa Fainali za Kombe la Dunia pamoja na Viwanja vingine 6 vipya vinavyojengwa kikiwemo kile kikubwa kupita vyote ambazo mechi za ufunguzi na Fainali zitafanyika, Kiwanja chenye uwezo wa kuchukua Washabiki 94,000 kiitwacho Soccer City huko Soweto, Johannesburg.
Soccer City kitakamilika Desemba na kukabidhiwa kwa FIFA Machi mwakani.
Soccer City kimejengwa kwenye saiti iliyokuwa Uwanja wa FNB, uwanja ambao Nelson Mandela alitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kutoka jela mwaka 1990.
Tatizo kubwa lililojitokeza wakati wa Mashindano ya Kombe la Mabara na FIFA kuliona ni uhaba wa maeneo ya kupaki magari kwenye Viwanja vingi ukiondoa kile cha Soccer City chenye eneo la kuegesha magari 15,000.
Usafiri wa kwenda na kutoka Viwanjani kwa kutumia Mabasi umekuwa hamna na Mashabiki imebidi watembee kwa miguu, waendeshe gari zao au wakodi teksi.
Lakini Mji wa Johannesburg, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, unaanzisha Usafiri maalum wa Mabasi yaendayo Kasi, mradi ambao umepingwa vikali na wenye teksi.
Juu ya yote, tatizo kubwa kwa wengi ni hali ya usalama na uhalifu uliokithiri huko Bondeni.
Kwenye Kombe la Mabara hili liliibuka vibaya pale Timu za Misri na Brazil kuibiwa Hotelini mwao.
Hata hivyo Danny Jordaan amesisitiza Serikali ya Afrika Kusini inalipa kipau mbele tatizo hilo sugu na imewekeza zaidi Rand Bilioni 1.3 kulikabili.
Mbali ya mikakati ya maandalizi ya Kombe la Dunia mwakani, kwa wengi na hasa Danny Jordaan, mchezo wa kuridhisha wa Bafana Bafana umewatia moyo washabiki wengi hasa mechi dhidi ya Brazil na ile ya kutafuta Mshindi wa 3 na Spain.
Danny Jordaan anasema: ‘Tuna Mashabiki zaidi ya Milioni 2 hapa Nchini ambao ni Wazungu na hushabikia Manchester United, Liverpool na Chelsea lakini kwenye Kombe hili la Mabara wote walikuwa Bafana Bafana!’
Jordaan anakiri kuwa ili Kombe la Dunia liende vizuri ni lazima nayo Bafana Bafana ifanye vizuri.
Juu ya yote, Jordaan anakubali tatizo la Ulinzi na Usafiri ndilo kubwa kupita yote ingawa kwa ujumla anakubali Kombe la Mabara lilifanikiwa.
LEO FAINALI ULAYA YA VIJANA CHINI YA MIAKA 21: England v Germany
UWANJA: NEW STADIUM, Malmo, Sweden SAA: 3.45 usiku [bongo]
Timu ya Taifa ya England ya Vijana Chini ya Miaka 21 leo inakutana Fainali na wenzao wa Ujerumani huko Malmo, Sweden kugombea Ubingwa wa Ulaya.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Timu hizi kukutana kwenye Fainali za Kombe hili huko Sweden kwani walikuwa Kundi moja mechi za awali na kutoka suluhu 1-1.
Kwenye Nusu Fainali, England iliwabwaga Wenyeji Sweden kwa matuta baada ya dakika 120 kwisha kwa Timu kuwa sare bao 3-3.

Katika mechi hiyo, England walikuwa wakiongoza 3-0 hadi mapumziko lakini Sweden walisawazisha kipindi cha pili.
Ujerumani wametinga Fainali baada ya kuifunga Italia bao 1-0.
England inaongozwa na Meneja Stuart Pearce ambae ni Mchezaji wa zamani England aliewahi kuwa Meneja wa Manchester City na itabidi leo afanye mabadiliko kwa kuwakosa Kipa wake wa kwanza Joe Hart, Washambuliaji Frazier Campbel na Gabriel Agbonlahor ambao wote wanaikosa Fainali kwa kuwa na Kadi.
Leo England itawategemea sana Nyota Chipukizi wa Arsenal, Theo Walcott, Viungo Fabrice Muamba, Mark Noble na Lee Cattermole huku Ngome ikisimamiwa na Nedum Onuoha na Micah Richards wa Manchester City pamoja na Beki wa kushoto wa Arsenal, Kieran Gibbs.
Nao Wajerumani chini ya Meneja Horst Hrubesch wana imani wataimudu England huku Meneja huyo akitamka: ‘Ile mechi ya Makundi, England walituzidi kidogo lakini safari hii hilo halipo.’
Ujerumani walitoka suluhu 0-0 na Spain, kuwafunga Finland 2-0, sare na England 1-1 kwenye mechi za awali za Kundi lao na Nusu Fainali kuibwaga Italia 1-0.
Mchezaji wa Ujerumani Ashkan Dejagah haruhusiwi kucheza Fainali kwa kuwa na Kadi na nafasi yake itachukuliwa na Sandro Wagner.
Rooney: ‘Nitabeba mzigo wote!’
Wayne Rooney amewahakikishia Mashabiki wa Mabingwa Manchester United kwamba anaweza kuchukua nafasi na kuziba mapengo ya Ronaldo na Tevez.
Manchester United imewapoteza Cristiano Ronaldo anaehamia Real Madrid na Carlos Tevez ambae nae pia anaondoka baada ya kuikataa ofa ya Man U lakini Rooney, licha ya kuamini kuwa Meneja wake Sir Alex Ferguson atanunua Wachezaji na kuimarisha Kikosi, amedai kuwa ana uwezo wa kufunga magoli kama walivyokuwa wakifanya Ronaldo na Tevez.
Rooney amesema: ‘Cristiano na Tevez walitufungia magoli mengi sana msimu uliokwisha na ule uliopita nyuma yake lakini nina uwezo wa kuziba pengo hilo. Nilishasema kabla kwamba nikipangwa nafasi nzuri nina uwezo wa kufunga! Wengi wanajua nikicheza kama Sentafowadi nakuwa bora!’
Msimu uliokwisha, mara nyingi Rooney alikuwa akipangwa pembeni na mara nyingine nyuma ya Mshambuliaji mkuu.
USA 2-3 Brazil !!
Brazil abeba Kombe la Mabara!
Nini Makocha wamesema baada ya mechi?
USA waliongoza 2-0 hadi kipindi cha kwanza kumalizika lakini Brazil walipachika bao 3 kipindi cha pili na kutwaa Kombe la Mabara.
Kocha wa USA Bob Bradley amesema: ‘Kufungwa kunatuumiza sana! Nasikia fahari juu ya Wachezaji wangu lakini tunajisikia vibaya kuacha ushindi ukituponyoka! Nadhani dunia nzima sasa watagundua tuna Timu nzuri na Wachezaji wazuri!’
Kocha wa Brazil Dunga anatamba: ‘Hata baada ya kuwa 2-0 nyuma, Timu ilikuwa na uhakika! Hafutaimu tuliwaambia wacheze kwa kutumia Wingi na wawe wavulimivu! Tulifanya hivyo, tuko pamoja siku 29 sasa na tulilitaka sana Kombe hili!’
Kaka atwaa Mpira wa Dhahabu!! Mpira wa Fedha na Kiatu cha Dhahabu chabebwa na Luis Fabiano!!!
Wakati Timu yao imenyakua Kombe la Mabara, Wachezaji wawili wa Brazil wamepata Tuzo za juu za Mashindano haya na nao ni Kaka aliyetunukiwa Mpira wa Dhahabu wa Adidas na Luis Fabiano aliyeshinda Tuzo mbili, moja ikiwa ni Mpira wa Fedha na Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora wa Kombe la Mabara kwa kufunga bao 5.
Mpira wa Shaba ulichukuliwa na Clint Dempsey wa USA, Kiatu cha Fedha kimebebwa na Fernando Torres wa Spain kwa kufunga bao 3 na Kiatu cha Shaba kapewa David Villa wa Spain.
Kipa Bora wa Mashindano hayo ameteuliwa kuwa Tim Howard wa USA na amezawadiwa Glovu za Dhahabu.
Timu Bora ni Brazil na imetunukiwa Tuzo ya Uchezaji wa Haki na FIFA.

Sunday 28 June 2009

Brazil Mabingwa Kombe la Mabara!!
USA 2 BRAZIL 3
Wakiwa nyuma hafutaimu kwa mabao 2-0 baada ya Clint Dempsey wa USA kufunga dakika ya 10 na Donovan kuweka la pili dakika ya 27, Brazil walizinduka kipindi cha pili na kufunga bao 3 kupitia kwa Luis Fabiano aliepachika 2, dakika ya 46 na 74, na Lucio kuleta ushindi kwa kichwa dakika ya 84 kufuatia kona iliyochongwa na Elano.
VIKOSI:
USA: Howard, Spector, DeMerit, Onyewu, Bocanegra, Dempsey, Clark, Feilhaber, Donovan, Davies, Altidore.Akiba: Guzan, Bornstein, Califf, Wynne, Pearce, Beasley, Kljestan, Adu, Torres, Bradley, Casey, Robles.Brazil: Julio Cesar, Maicon, Lucio, Luisao, Andre Santos, Ramires, Felipe Melo, Silva, Kaka, Luis Fabiano, Robinho.Akiba: Victor, Juan, Kleber, Dani Alves, Miranda, Josue, Julio Baptista, Elano, Kleberson, Alexandre Pato, Nilmar, Gomes.Refa: Martin Hansson (Sweden)
KOMBE LA MABARA: Mchezaji gani leo kunyakua MPIRA wa DHAHABU wa ADIDAS?
FIFA, kupitia Kundi lake la Kitaalam, limeteua wachezaji 10 walioshiriki Kombe la Mabara huko Afrika Kusini wakitoka Timu za USA, Brazil, Spain na Afrika Kusini, ili kugombea Tuzo ya Adidas ya Mpira wa Dhahabu ili kuashiria ndie Mchezaji Bora wa Mashindano hayo.
Watakaowapigia kura Wachezaji hao 10 ni Waandishi wa Habari walioruhusiwa kuripoti Mashindano hayo huko Afrika Kusini na kila Mwandishi atatakiwa ateua Wachezaji wake Bora wa tatu na kuwapa wa kwanza pointi 5, wa pili pointi 3 na wa tatu pointi moja.
Mara tu baada ya mechi ya Fainali kumalizika, FIFA itajumlisha pointi hizo kutoka kwa hao Waandishi wa Habari na kumtangaza nani alienyakua Tuzo ya Mpira wa Dhahabu wa Adidas, wa pili atapewa Mpira wa Fedha na yule wa 3 atapata Mpira wa Shaba.
Wachezaji 10 watakaopigiwa kura ni:
DEMPSEY, Clint (USA)
DONOVAN, Landon (USA)
KAKA (Brazil)
LUIS FABIANO (Brazil)
PARKER, Bernard (South Africa)
PIENAAR, Steven (South Africa)
ROBINHO (Brazi)
TORRES, Fernando (Spain)
VILLA, David (Spain)
XAVI (Spain)
Washindi waliopita wa Tuzo ya Mpira wa Dhahabu wa Adidas wa Kombe la Mabara la FIFA na mwaka waliochukua ni:
1997 - Denilson (Brazil)
1999 - Ronaldinho (Brazil)
2001 - Robert Pires (Ufaransa)
2003 - Thierry Henry (Ufaransa)
2005 - Adriano (Brazil)
Scolari awalaumu Drogba, Cech na Ballack!!!
Luiz Felipe Scolari amedai kuwa baadhi ya Wachezaji wa Chelsea walikuwa hawamheshimu yeye wala jinsi alivyokuwa akifundisha alipokuwa Meneja wa Chelsea kwa kipindi cha miezi minane.
Scolari, umri miaka 60, sasa ndie Kocha wa Klabu ya Uzbekistan iitwayo Bunyodkor, amewataja Didier Drogba kutoka Ivory Coast, Mjerumani Michael Ballack na Kipa kutoka Czech, Petr Cech, kuwa ndio waliokuwa na tabia hiyo isiyokubalika.
Scolari, alieanza kuifundisha Chelsea mwaka jana mwezi Julai na kutimuliwa Februari mwaka huu, amesema: ‘Kwa sasa Wamiliki wa Soka ni Wachezaji. Kocha, kwa Vilabu vingi Ulaya, hana ubavu wa kuwapinga!’
Scolari akaongeza: ‘Watu wanaofukuzwa siku zote ni Makocha! Wachezaji wakubwa wanajua hilo! Hilo ndio lilikuwa tatizo langu huko Chelsea!’
Scolari vilevile akaongelea juu ya uhamisho wa Ronaldo kwenda Real Madrid na kusema Kaka na Ronaldo watapatana na kuwa na uhusiano mzuri.
Scolari ni Mbrazil hivyo anamjua vizuri Kaka na alishawahi kuwa Kocha wa Ronaldo kwenye Timu ya Taifa ya Ureno.
Scolari ametamka: ‘Kaka ni mtu bora kiwanjani na nje! Ingawa amepata sifa kubwa na ni tajiri, Kaka siku zote anajituma uwanjani! Wataelewana ila tatizo ni Raul! Huyo ni veterani na ndio Bosi kwenye Vyumba vya Kubadilishia Jezi! Huenda kukatokea mfarakano kama hampendi mtu!’
KOMBE LA MABARA: Mechi ya Mshindi wa 3: Afrika Kusini 2 Spain 3!!!
SPAIN WATWAA USHINDI WA 3!!!!
Katika mechi iliyokwisha dakika chache zilizopita, Wenyeji Afrika Kusini, wakiwa Uwanjani Royal Bafokeng huko Rustenrburg, walitangulia kupata bao dakika ya 77 kupitia Mphela lakini ndani ya dakika moja Spain waliweza kusawazisha na kupachika la pili, mabao yaliyofungwa na Guiza dakika ya 88 na 89.
Hata hivyo Afrika Kusini waliweza kusawazisha kwenye dakika za majeruhi pale Mphela tena alipofunga kwa frikiki na kuifanya gemu iwe 2-2 na kuingizwa kwenye dakika 30 za nyongeza.
Robo saa ya Kipindi cha kwanza cha nyongeza kilikwisha huku mechi ikibaki 2-2.
Dakika 2 tu baada ya Kipindi cha Pili cha Nyongeza kuanza, Spain wakapachika la 3 kupitia Alonso aliefunga kwa frikiki na hivyo kuwafanya Spain kuwa Washindi wa 3 wa Kombe la Mabara.

Fainali itakayoanza baadae leo kati ya USA na Brazil itatoa Bingwa na Mshindi wa pili.
VIKOSI:
SPAIN: CASILLAS, ALBIOL, VILLA, TORRES, CAPDEVILA, SERGIO, ALONSO, RIERA, ARBELOA, CAZORLA.
AFRIKA KUSINI: KHUNE, GAXA, MASILELA, MOKOENA, SIBAYA, TSHABALALA, PIENAAR, MODISE, DIKGACOI, BOOTH, PARKER
REFA: MATTHEW BREEZE [AUSTRALIA]
Barcelona yatoboa Man City imetoa ofa kubwa kumnunua Eto’o!!!
Rais wa Barcelona Joan Laporta amepasua kuwa Manchester City wametoa ofa ya dau ‘kubwa sana’ kumnunua Samuel Eto’o.
Eto’o, Mchezaji wa Kimataifa toka Cameroun mwenye umri wa miaka 28, amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake na Barcelona na inasadikiwa atahama.
Ingawa Eto’o hataki kuhama Barcelona lakini inaaminika dau na malupulupu atakayopewa na Man City yatamfanya ashindwe kukataa ofa hiyo.
Laporta anasema: ‘Eto’o hataki kuondoka lakini ofa kama hii huwezi kuikataa!’
AC Milan yathibitisha kumtaka Adebayor!!!
Makamu wa Rais wa AC Milan Adriano Galliani amethibitisha kuwa Klabu yake ambao ni Vigogo wa Serie A huko Italia wana nia ya kumnunua Emmanuel Adebayor kutoka Arsenal.
Baada ya kumuuza Kaka kwenda Real Madrid, AC Milan wana kitita cha kumnunua Adebayor ingawa inaaminika nia yao hasa ni kumchukua Edin Dzeko kutoka Wolfsburg ya Ujerumani.
Dzeko ni raia wa Bosnia.
Galliani amethibitisha ameshazungumza na Meneja wa Arsenal Arsene Wenger kuhusu Adebayor.

LEO FAINALI KOMBE LA MABARA: USA v BRAZIL huko Bondeni!!!
Kocha wa Brazil, Dunga, haamini kuwa kile kipigo cha 3-0 walichowapa USA huko Bondeni wiki iliyopita kwenye mechi za Makundi kwenye Kombe hili la Mabara kina maana yeyote kwenye Fainali ya leo ambayo Brazil wanakutana tena na Marekani Uwanja wa Ellis Park huko Johannesburg, Afrika Kusini katika mechi ya Fainali itakayoanza saa 3 na nusu, bongo taimu.
Hata alipoambiwa kuwa katika mechi 15 Brazil walizocheza na USA, ni mara moja tu USA walishinda na Brazil kushinda mara 14, Dunga alitamka: ‘Soka si historia, haihusu yaliyopita au mapya yatakayokuja!’
Falsafa ya Dunga inamwonyesha ni mtu wa aina gani, yaani mtu makini mwenye mpangilio wa nini muhimu!
Kwa yeye kitu muhimu ni Fainali ya leo na wala si ule ushindi wa bao 3-0 walipowapiga USA huko Tshwane, Pretoria siku 10 zilizopita.
Dunga anasema: ‘Ushindi ule umepita! Lazima uiheshimu Timu ambayo baada ya kufungwa mechi 2 wakaibuka na kuwafunga Misri na Spain! Wana nidhamu kwenye mbinu zao na wakakamavu dakika zote 90!’
Dunga akiongelea Timu yake amesema: ‘Hii ni gemu ambayo lazima tuwe na uwiano kati ya defensi na mashambulizi. Nimejifunza miaka mingi kuwa kama timu haina uwiano huo, haifiki mbali! Ni lazima tuwe na Wachezaji wapiganaji pale kati wanaosaidia defensi, kunyang’anya mipira na kulisha fowadi. Kule Brazil huwa tunawaita hawa Wapiga Piano. Ndio maana kwenye mtindo wetu Gilberto Silva na Felipe Melo ni muhimu sana! Wao wanahenya ili kuwapa mwanya wataalam wetu, Wachezaji wenye vipaji wawe huru kucheza soka lao!’
Powered By Blogger