Saturday 27 June 2009

FAINALI Jumapili 28 Juni 2009: USA v Brazil
UWANJA: ELLIS PARK, JOHANNESBURG SAA: 3.30 USIKU [Bongo Taimu]
USA itabidi wachezeshe Kiungo mwingine badala ya Michael Bradley ambae alipewa Kadi Nyekundu katika Nusu Fainali waliyoibwaga Spain 2-0.

Benny Felhaber anategemewa kuchukua nafasi yake.
Brazil, mbali ya Juan ambae ni majeruhi, hawana tatizo kwa Mchezaji mwingine yeyote.
Hii ni mara ya pili kwa Timu hizi kucheza kwenye Kombe hili huko Afrika Kusini kwani walikuwa Kundi moja na Brazil aliichapa USA 3-0 kwa magoli yaliyofungwa na Felipe Melo, Robinho na Maicon.
Mpaka sasa Brazil na USA zishacheza mara 15 na Brazil kushinda mara 14 na USA kushinda mara moja tu na hiyo ilikuwa mwaka 1998 walipoifunga Brazil 1-0 huko Los Angeles.
VIKOSI VINATEGEMEWA KUWA:
USA:
Howard; Spector, Onyewu, DeMerit, Bocanegra ,Dempsey, Felhaber, Clark, Donovan, Davies , Altidore
Brazil: Cesar; Maicon,Lucio, Luisao, Santos Melo, G Silva, Ramires, Kaka, Fabiano, Robinho.
Refa: M Hansson (Sweden).
Allardyce kumsaini Van Nistelrooy?
Meneja wa Blackburn Rovers Sam Allardyce anategemea kumchukua Ruud van Nistelrooy kutoka Real Madrid na amepinga wazo kuwa watamsaini Michael Owen kutoka Newcaslte.
Baada ya kumuuza Roque Santa Cruz kwa Manchester City na Matt Derbyshire alieenda Olympiakos ya Ugiriki wiki hii, Sam Allardyce yuko mbioni kuimarisha safu yake ya Mashambulizi.
"Nani alitegema nitampata Anelka nilipokuwa Bolton? Lakini nilimpata!" Allardyce anahoji. "Itakuwa vyema tukimpata Van Nistelrooy!’.
Kuhusu Owen, Allardyce amekataa kufikiria kumchukua na anatamka: ‘Ni tatizo la kuumia mara kwa mara! Nahitaji Straika atakaecheza mechi 30! Hilo halijatokea kwa Owen kwa miaka minne sasa!’
Ronaldo rasmi Real Julai 1!!!
Nyota wa Manchester United Cristiano Ronaldo atakamilisha taratibu za kuhamia Real Madrid hapo Julai 1 baada ya Manchester United na Real Madrid zote, kupitia tovuti zao, kuthibitisha wameshasaini mkataba kati yao.
Real Madrid imesema itamwanua Ronaldo rasmi hapo Julai 6.
Ronaldo ameshasaini mkataba wa miaka 6 na Real Madrid ambao utamfanya awe Mchezaji mwenye mshahara mkubwa sana Klabuni Real.
Uhamisho wake umeigharimu Real Madrid Pauni Milioni 80 ambayo ni rekodi ya dunia kwa uhamisho.
Glen Johnson rasmi Liverpool!!
Liverpool wamethibitisha kuwa Mlinzi wa England Glen Johnson amesaini mkataba wa miaka minne baada ya uhamisho wake kutoka Portsmouth wa Pauni Milioni 17.5 kukumilika.
Johnson alikuwa pia akiwindwa na Klabu yake ya zamani Chelsea na Manchester City lakini mwenyewe ameamua kwenda Liverpool.
Kutua kwa Johnson, ambae ni Beki wa pembeni kulia, kunamletea utata Beki mwingine kwenye nafasi hiyo, Alvaro Arbeloa, na inasemekana huenda akauzwa.
Tevez adai Berbatov ndio amemfanya akatae kubaki Man U!!!
Ingawa Carlos Tevez hajui ni wapi atacheza msimu ujao, amedai kuwa alitambua siku zake hapo Manchester United zilianza kuhesabika pale aliponunuliwa Dimitar Berbatov kutoka Tottenham. Mkataba wa Tevez na Manchester United unaisha rasmi Juni 30 baada ya kuwa hapo kwa miaka miwili kwa mkopo na Klabu za Manchester City na Chelsea ndizo zinamwania huku Klabu nyingine ya tatu ambayo haikutajwa ipo mawindoni pia.
Tevez anasema: ‘Ferguson aliniambia nisiwe na wasiwasi na Berbatov lakini sikufurahi nilipowekwa benchi!’
Ferdinand Bwana Harusi!!!
Nyota wa Manchester United Rio Ferdinand amekodisha ndege maalum ili kuwabeba Familia na Mrafiki zake zaidi ya 100 kuhudhuria harusi yake itakayofanyika huko Visiwa vya Caribbean.
Ferdinand, 30, anamuoa mpenzi wake wa siku nyingi Rebecca Ellison, 29, wikiendi hii.
Wageni waalikwa kwenye Harusi hii ni Wanafamilia tu na baadhi ya Marafiki zake wa zamani wakiwemo kama Mdogo wake Anton anaechezea Sunderland na Wachezaji wa zamani Michael Dubbery na Jody Morris aliekua akichezea Chelsea.
Rio na Rebecca wako pamoja kwa miaka 7 sasa na wanao watoto wa kiume wawili wanaoitwa Lorenz na Tate.
VIJANA CHINI MIAKA 21 ULAYA: England yaingia Fainali kwa Matuta!
England 3 Sweden 3
Baada ya kutoka suluhu 3-3, England iliwabwaga Wenyeji Sweden kwa mikwaju ya penalti 5-4 na kuingia Fainali watakapokutana na Germany walioifunga Italia 1-0.
Fainali hiyo itachezwa Jumatatu.
Mpaka mapumziko, England ilikuwa mbele kwa mabao 3-2 yaliyofungwa na Martin Cranie, Onuoha na la tatu Mattias Bjarsmyr wa Sweden alijifunga mwenyewe.
Kipindi cha pili Sweden wakarudisha bao zote 3 kupitia Ola Toivonen na Marcus Beg aliefunga 2.
Frazier Campbel, Kijana wa Manchester United, ataikosa Fainali baada ya kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu kufuatia Kadi 2 za Njano.
Kipa Joe Hart wa Manchester City nae ataikosa Fainali kwa kupewa Kadi ya Njano wakati wa kupigiana penalti kwa kosa la kuvuka mstari wa goli.

Friday 26 June 2009

UEFA U21: KOMBE LA VIJANA CHINI YA MIAKA 21: NUSU FAINALI LEO
  • SWEDEN v ENGLAND
  • GERMANY v ITALIA
Wenyeji Sweden leo wako Nusu Fainali ya Kombe la UEFA la Vijana wa Chini ya Miaka 21 na wanakutana na England mechi itakayoanza saa 1 usiku bongo taimu.
Italia watacheza na Germany saa 3 dakika 45 usiku.
Washindi watakutana Fainali Jumatatu tarehe 29 Juni 2009 kupata Bingwa wa Ulaya wa Timu za Taifa za Vijana wa chini ya miaka 21.

Thursday 25 June 2009

VUVUZELA LAZIMIKA KIUME!!
Ndani ya Ellis Park, Johannesburg, mbele ya Rais Jacob Zuma aliekaa pamoja na Sepp Blatter wa FIFA, VUVUZELA liligoma kunyamaza hadi dakika ya 88 pale Mchezaji wa Akiba, Dani Alvez, alieingizwa kuchukua nafasi ya Santos, kufunga bao kwa frikiki iliyopinda na kumzidi maarifa Kipa Khune na kuwapatia Brazil bao pekee na la ushindi.
Ingawa Brazil walitawala kidogo, Bafana Bafana walipigana kishujaa na kuyazima mashambulizi yote ya vijana wa Samba kwa mtindo wa kujihami Timu nzima na kushambulia Timu nzima.
Ingawa SAMBA imeibuka Ngoma Tamu, hakika VUVUZELA halikuiabisha Afrika.
Brazil itacheza Fainali na USA siku ya Jumapili.
Mechi ya utangulizi siku hiyo hiyo ni ya kutafuta Mshindi wa 3 kati ya Afrika Kusini na Spain.
VUVUZELA v SAMBA
Wengine wameshasingizia VUVUZELA kuwa ndilo limewakosesha ushindi, lakini, leo kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mabara, VUVUZELA linakutana na Ngoma Ngumu SAMBA!
Brazil, Vigogo wa Soka duniani na Mabingwa Watetezi wa Kombe hili la Mabara, waliwabamiza Mabingwa wa Dunia Italia 3-0 kwenye mechi yao ya mwisho ya Kundi lao.
Brazil wameshinda mechi zao zote za Kundi lao na kufunga jumla ya mabao 10 huku Luis Fabiano akiongoza kwa mabao matatu, Kaka mawili na Maicon, Robinho, Juan na Felipe Melo bao 1 kila mmoja.
Wenyeji Afrika Kusini walifungwa mechi yao ya mwisho ya Kundi lao mabao 2-0 na Spain lakini wametinga Nusu Fainali.
Katika Kundi lao wameshinda mechi moja, kufungwa moja na suluhu moja.
Wamefunga jumla ya mabao mawili na Mfungaji wao pekee wa mabao hayo ni Bernard Parker.
Afrika Kusini na Brazil wamekutana mara mbili tu na zote kashinda Brazil.
JE VUVUZELA na SAMBA NANI LEO ATABWAGA MANYANGA????
KIPIGO CHA MAREKANI: SPAIN WASINGIZIA VUVUZELA!!!!!!
Baada ya USA kuibamiza Misri mabao 3-0 siku ya Jumapili kwenye mechi yao ya mwisho ya Kundi lao iliyowafanya USA kutinga Nusu Fainali, Afisa mmoja wa Timu ya Misri alizilaumu taarifa za Vyombo vya Habari huko Afrika Kusini kwamba Timu yake ilikuwa ikizungukwa na MaCD kila wakati na hatimaye kuibiwa pesa ndizo zilizowaathiri na kusababisha wafungwe.
Kwa Xabi Alonso wa Spain, anaechezea Liverpool, VUVUZELA ndilo lililowatibua sana na, kwa yeye, ingekuwa bora kama lingepigwa marufuku uwanjani.
Katika mechi ya jana, kama desturi huko Bondeni, VUVUZELA lilitamba na kupulizwa dakika zote za mechi hiyo iliyowatoa ngebe Spain.

VUVUZELA ni tarumbeta la plastiki na ni kiburudisho mahsusi kwenye mechi huko Bondeni.
Lakini Kocha wa USA, Bob Bradley, amesema mafanikio ya USA yametokana na plani yao ya kuwasimamisha Spain.
Bradley anasema: ‘Spain ni Timu supa lakini tuliamini tutawafunga! Ilibidi tucheze kitimu, tujihami kwa pamoja na tuwe wakali tukishambulia. Kitu kikubwa ilikuwa tusiwape mwanya kwenye Kiungo, tuwakabe kila wakipata mpira na hasa Xavi. Tulihakikisha Xavi hapenyezi pasi zake mbele za kuikata defensi! Tulimlazimisha atoe pasi upande au arudishe nyuma!’
USA wanangoja mshindi wa leo kati ya Afrika Kusini na Brazil kucheza nae Fainali hapo Jumapili.
Fabregas apandwa mori na Bunduki bila risasi!!!!

Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, amezungumzia kuvunjika kwake moyo kwa Klabu yake kutoweza kunyakua Kombe lolote tangu mwaka 2005 na kudai hilo linamtia hasira sana.
Fabregas, anaevumishwa kuwa anataka kurudi kwao Spain kuchezea timu yake ya utotoni Barcelona, amesema: ‘Kukosa Mataji Arsenal ni kitu kinachontia hasira sana! Mwaka huu tulijitutumua kwa nguvu zote lakini hatukufikia kiwango kile kila mtu anachotegemea toka kwa Arsenal! Kama hushindi kitu kila mtu anakuwa na hasira. Miaka minne sasa, tunahitaji Taji turudishe imani!’
Tevez kwenda Man City?
Baada ya kuivua Jezi Nyekundu ya Man U sasa Tevez huenda akavaa Jezi ya Bluu ya Man City na hili limedokezwa na Mshauri wake Mkuu Kia Joorabchian ambae amedokeza kuwa kwa sasa wanatafakari ofa tatu kutoka kwa Man City, Chelsea na Klabu ya tatu ambayo hakuitaja.
Kia Joorabchian, akizungumza kwenye Radio moja huko Argentina, alisikika akisema: ‘Man City ndio wenye nafasi kubwa kwa sababu wanajenga Timu kubwa. Lakini mkataba wa Tevez na Man U unakwisha tarehe 30 Juni na tunauheshimu. Tutajua nini kitatokea baada ya siku 10.’
Wiki iliyokwisha Manchester United ilithibitisha kuwa Tevez anaondoka baada ya kukataa ofa yao.
NUSU FAINALI BONDENI: AFRIKA KUSINI v BRAZIL LEO!!!
Jana, Timu Bora Duniani, Spain, ilipata mkong’oto na USA bila kutarajiwa na kuaga Kombe la Mabara baada ya kipigo cha 2-0 kilichowaacha USA wakijikita Fainali kusubiri mshindi wa leo kati ya Wenyeji Afrika Kusini na Brazil mechi iitakayoanza saa 3 na nusu, saa za bongo, huko Johannesburg, Uwanja wa Ellis Park.
Timu zote, Afrika Kusini na Brazil, zitakosa Mchezaji mmoja kila upande huku Afrika Kusini kumkosa Kiungo Macbeth Sibaya ambae hachezi kwa kuwa na Kadi na Brazil watamkosa Mlinzi Juan ambae ni majeruhi.
Kwa Afrika Kusini, mbadala ni Lance Davids na Brazil ni Luisao.
Nchi hizi zimeshawahi kukutana mara mbili, mara zote zikiwa mechi za kirafiki na zote zilifanyika mjini Johannesburg na Brazil kushinda ya kwanza mabao 3-2 mwaka 1996 katika mechi ambayo Afrika Kusini waliongoza mabao 2-0 kwa magoli yaliyofungwa na Lucas Radebe na Doctor Khumalo lakini Brazil wakaibuka kidedea kwa mabao matatu yaliyofungwa na Rivaldo, Bebeto na Romario.
Mechi ya pili ilichezwa mwaka 1997, Nahodha wa Brazil kwenye mechi hiyo alikuwa Meneja wa sasa wa Brazil, Dunga, na Brazil walishinda 2-1.
Timu leo zitashuka uwanjani huku Brazil wakiwa na Jezi zao za kawaida za njano na Afrika Kusini itabidi wabadili na kuvaa za kijani.
Kocha wa Afrika Kusini, Joel Santana kutoka Brazil, anasema: ‘Tumestahili kuwa Nusu Fainali.’
Nae Dunga ametamka: ‘Afrika Kusini ni timu inayochipukia na tunajua mechi itakuwa ngumu. Wana nguvu, wepesi na mashabiki uwanja mzima ni wa kwao! Lakini tuko tayari, Brazil ni Kikosi imara na kila Mchezaji hapa anastahili kuwa timu ya kwanza!’

Wednesday 24 June 2009

NI USA FAINALI! SPAIN NJE!!!
Spain, Mabingwa wa Ulaya na Nambari Wani kwenye listi ya FIFA waliocheza mechi 35 bila kufungwa na kuifikia rekodi ya Brazil, leo kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mabara Uwanjani Free State, Blomfontein, Afrika Kusini, wametandikwa mabao 2-0 na USA, Timu ambayo wengi tuliidharau.
Mabao ya USA yalifungwa na Altidore dakika ya 27 na Mchezaji anaecheza Fulham, Clint Dempsey, alietunukiwa zawadi ya Mchezaji Bora wa mechi hii, alifunga la pili kwenye dakika ya 74.
USA imekita Fainali na wanasubiri Mshindi wa mechi ya kesho kati ya Brazil na Afrika Kusini.
Spain atacheza na atakaefungwa mechi hiyo ili kupata Mshindi wa 3.
VIKOSI:
Spain: Casillas, Pique, Puyol, David Villa, Xavi, Torres, Fabregas, Capdevila, Alonso,
Ramos, Riera
USA: Howard, Bocanegra, Onyewu, Dempsey, Davies, Donovan, Bradley, Clark, demerit, Altidore, Spector
REFA: Jorge Larrionda [Uruguay]
KUNRADHI WADAU WA SOKA!!!!!!!!!
Tuko mbioni kutengeneza TOVUTI rasmi kwa ajili ya SOKA tu na inaitwa www.sokainbongo.com

Mchango wako wa maoni, mawaidha au chochote kile ya jinsi ungependa TOVUTI hii itoke kivipi YANAKARIBISHWA!

TUMA HAPA AU BOFYA http://www.sokainbongo.com/ au tuma barua pepe: sokainbongo@sokainbongo.com ILI UTUME MAWAIDHA YAKO!

KOMBE LA MABARA HUKO BONDENI: Nusu Fainali kati ya Spain na USA!!!
Wengi hawakupinga kutinga kwa Spain Nusu Fainali lakini ni wachache mno ndio waliootea USA itatinga Nusu Fainali hasa baada ya kubamizwa katika mechi zao mbili za kwanza kwenye Kundi lao. Lakini wametinga Nusu Fainali baada ya kuwafunga Mabingwa wa Afrika, Misri, mabao 3-0 katika mechi yao ya mwisho Kundini huku Mabingwa wa Dunia, Italia, wakipigwa 3-0 na Brazil.
Mechi ya leo, inayoanza saa 3 na nusu usiku saa za bongo, inaikutanisha Spain, Mabingwa wa Ulaya na Nambari Wani Duniani katika listi ya FIFA, ambayo haijawahi kufungwa na USA.
Beki wa Spain, Gerard Pique wa Barcelona ambae pia aliichezea Manchester United, ametamka: ‘Ni ngumu kila mtu akikuona unastahili kushinda mechi na itabidi kufanya kazi ya ziada kuingia Fainali!’
Nae Kocha wa USA, Bob Bradley, anasema: ‘Tulicheza na Spain kabla ya EURO 2008 na tulicheza vizuri tu! Tumewatazama wanavyocheza na tunajua staili yao! Tunajua namna ya kuwasimamisha na tunajiamini!’

Refa wa mechi hii ni Jorge Larrionda kutoka Uruguay.
UEFA U21 CUP: Nusu Fainali ni England v Sweden na Italy v German siku ya Ijumaa
Wenyeji Sweden jana walidunda Nusu Fainali ya Kombe la UEFA la Vijana wa Chini ya Miaka 21 walipoifunga Serbia 3-1 mjini Malmo, Sweden na sasa watakutana na England siku ya Ijumaa.
Katika mechi nyingine ya Kundi A, Italia waliipiga Belarus 2-1 na pia kutinga Nusu Fainali watakayocheza na Germany pia siku ya Ijumaa.
Washindi watakutana Fainali Jumatatu tarehe 29 Juni 2009 kupata Bingwa wa Ulaya wa Timu za Taifa za Vijana wa chini ya miaka 21.
LIGI KUU……………….kwa ufupi:
Birmingham………………………..
Kipa Joe Hart wa Manchester City amepelekwa Birmingham kucheza kwa mkopo msimu ujao na mwenyewe ameonyesha masikitiko yake kwa uamuzi huo.
Joe Hart kwa sasa yuko na Kikosi cha England cha Vijana wa chini ya miaka 21 huko Sweden wakigombea Ubingwa wa Ulaya.
Hart amenena kwa masikitiko: ‘Si kitu nnachopenda, navumilia tu lakini si mwisho wa dunia!’
Klabu hiyo mpya ya Kipa Joe Hart, Birmingham iliyopanda Daraja kuingia Ligi Kuu, imemsaini Mchezaji wa Kimataifa wa Ecuador Giovanny Espinoza kutoka Klabu ya Barcelona Sporting Club ya Ecuador.
Beki huyo wa Kati, aliechezea mechi 80 kwenye Timu ya Taifa ya Ecuador na ambae ameshacheza Fainali za Kombe la Dunia mara 2, amesaini mkataba wa miaka wawili.
Kwa Meneja wa Birmingham, Alex McLeish, huyu ni Mchezaji wa 5 kumsaini kwa msimu ujao wengine wakiwa Christian Benitez, Scott Dann, Stephen Carr na Joe Hart.
Phil Brown wa Hull City atobolew mfuko………………!!!!!

Meneja wa Hull City, Phil Brown, amepigwa Faini ya Pauni 2500 na FA, Chama cha Soka England, baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Refa Mike Riley.
Sokomoko la Phil Brown lilitokea baada ya Hull City kufungwa 2-1 huko Emirates Stadium kwenye Robo Fainali ya Kombe la FA na Wenyeji Arsenal mwezi Machi na Brown kudai baada ya mechi hawakufungwa na Arsenal bali na Refa Mike Riley na Msaidizi wake walipokubali goli lililofungwa na William Gallas ambalo alidai ni ofsaidi.

Tuesday 23 June 2009

Malouda asaini upya Chelsea!!
Winga wa Chelsea Florent Malouda amesaini mkataba mpya wa miaka minne na Klabu yake huku kukiwa kumesalia miaka miwili kwenye mkataba wa sasa.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 29 alikuwa amezungukwa na minong’ono mikubwa kwamba atauzwa hasa baada ya kuonekana anapwaya enzi za Kocha Luis Felipe Scolari.
Lakini tangu alipotua Meneja mpya wa ‘mpito’ Mdachi Guus Hiddink kuchukua nafasi ya Scolari, Malouda alizaliwa upya na kuonyesha cheche zilizomfanya acheze jumla ya mechi 31 na kufunga mabao 9 na kuiwezesha Chelsea kufika Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na kutwaa Kombe la FA.
Malouda alitua Stamford Bridge mwaka 2007 akitokea Klabu ya Lyon ya Ufaransa.
FIFA yaridhishwa na uandaaji wa Kombe la Mabara huko Bondeni
FIFA imetamka imeridhika na maandalizi na uendeshwaji wa Kombe la Mabara huko Afrika Kusini lakini imekiri bado kuna matatizo yanayobidi yamalizwe kabla ya Fainali ya Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini.
Huku kukiwa na mahudhurio mabovu ya Watazamaji, matatizo ya usafiri na uhaba wa Vyumba Mahotelini, FIFA imekiri Kombe la Mabara si Fainali za Kombe la Dunia lakini wamepata fununu kubwa nini wategemee ngoma ikilia.
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valckle, amesema: ‘Kwa sasa tumeridhika. Dunia sasa inajua Afrika Kusini wanaweza kuandaa mashindano makubwa.’
Kitu kikubwa kilichokuwa kikihofiwa ni usalama wa Mashabiki na hili lilijichomoza hasa baada ya Timu za Misri na Brazil kuibiwa vitu na pesa kwa baadhi ya Wachezaji wao toka kwenye vyumba vya Hoteli zao.
Lakini FIFA imesema imeridhishwa kwa ujumla kuhusu usalama na ushirikiano walioupata toka kwa wahusika wote.
MAN U YATHIBITISHA JEZI MPYA!!!
Jezi za kuchezea nyumbani za msimu wa 2009/10 zitazinduliwa rasmi wiki ijayo tarehe 1 Julai baada ya Manchester United kuthibitisha taarifa zilizozagaa leo mitandaoni kuzianika Jezi hizo hasa kwa wale Mawakala Wauzaji kupitia tovuti mbalimbali.
Kwa sababu Jezi hizi hazijazinduliwa rasmi zimetangazwa leo huku zikiwa kwenye kivuli ili kuzizuia zisionekane waziwazi.
Klabu ya Man U imesema Jezi hizo ni kuadhimisha miaka 100 ya Old Trafford na mfumo wake ni kama ule uliovaliwa Karne moja iliyopita.
Jezi hizi zitaanza kuonekana rasmi kwenye Timu pale itakapozuru Mashariki ya Mbali kucheza mechi Nchini Malaysia, Indonesia, Korea na China.
Man U wataruka tarehe 16 Julai kuanza ziara hiyo na siku hiyo ndio Jezi zitaanza kuuzwa kwa Washabiki.
Rio Ferdinand amesema: ‘Kudumisha utamaduni wa Klabu ni muhimu. Msimu uliokwisha tulikuwa na Jezi za Bluu ikiwa kumbukumbu ya kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwaka 1968 na hizi za sasa ni za miaka 100 ya Klabu! Klabu hii siku zote inajivunia historia yake na sisi Wachezaji tunaskia fahari!’
FIFA KUMUENZI MARC-VIVIEN FOE FAINALI YA KOMBE LA MABARA
FIFA imetangaza kuwa siku ya Jumapili kabla ya Fainali ya Kombe la Mabara kuanza kutafanyika kumbukumbu maalum ya Kiungo wa Cameroun Marc-Vivien Foe alieanguka na kupoteza fahamu kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mabara huko Ufaransa mwaka 2003 na baadae kufariki mara tu alipofikishwa hospitali.
Foe, umri miaka 28, aligundulika kuwa alikuwa na ugonjwa wa moyo.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, amesema: ‘Lilikuwa tukio la kusikitisha na baya sana. Kabla ya Fainali kuanza, timu zote zitasimama katikati ya Uwanja na tutakuwa na ujumbe kwa dunia nzima kuhusu nini kilitokea.’
Siku aliyokufa Foe alikuwa akiichezea Cameroun mechi yake ya 64.
Foe alizichezea Klabu za Manchester City na Racing Lens ya Ufaransa.

Man City imeistaafisha Jezi Namba 23 aliyokuwa akivaa na kwenye Uwanja wao City of Manchester kuna bustani ndogo ya ukumbusho wake.
Klabu ya Racing Lens iliuita mtaa mmoja jirani na Uwanja wao wa Felix Bollaert jina la Foe kama kumuenzi.
Huko kwao Cameroun alipewa mazishi ya kitaifa.
UZI MPYA WA MAN U WAANULIWA!!!
Jezi mpya zinazosemekana zitatumiwa na Mabingwa Manchester United kwa mechi za nyumbani leo zimezagaa kwenye vyombo vya habari na barua pepe za kibiashara.
Jezi hizo [pichani] nyekundu zina ‘V’ nyeusi kifuani na ukosi mweusi na zinafanana na Jezi zilizovaliwa na Manchester United mwaka 1908-9 walipofika Fainali ya Kombe la FA.
Nike, waliotengeneza Jezi hizo, wametangaza kuwa ni za kusherehekea miaka 100 ya Klabu hiyo.
Jezi hizo zinaambatana na bukta nyeupe yenye mstari mwekundu pembeni na stokingi nyeusi zenye ‘V’ nyekundu nyuma.
England chini ya miaka 21 waikwaa Nusu Fainali UEFA!!
Timu ya Taifa ya England ya Vijana chini ya miaka 21, U21, [Under 21] imeingia Nusu Fainali ya Kombe la UEFA la Vijana baada ya kutoka suluhu 1-1 na Timu ya Vijana ya Ujerumani U21 hapo jana katika mechi ya Kundi B.
England wamemaliza Kundi hilo kwa kuwa vinara wakiwa na pointi 7 na Ujerumani, wa pili wakiwa na pointi 5, na wote wanasonga mbele kuingia Nusu Fainali.
Wapinzani wa England kwenye Nusu Fainali watajulikana leo baada ya mechi za Kundi B kumalizika.
Hadi sasa Kundi B linaongozwa na Italia wenye pointi 4, Sweden pointi 3, Serbia pointi 2 na Belarus pointi 1.
Mechi za mwisho za leo za Kundi hilo ni kati ya Serbia v Sweden na Belarus v Italia.
Katika Kundi lake, England ilizifunga Finland 2-1 na Spain 2-0.
Kikosi cha England kilichopo Fainali hizi ni:
Makipa: Joe Hart, Joe Lewis, Scott Loach.
Walinzi: Martin Cranie, Andrew Taylor, Richard Stearman, Nedum Onuoha, Jack Rodwell, James Tomkins, Micah Richards, Michael Mancienne, Kieran Gibbs.
Viungo: Lee Cattermole, James Milner, Craig Gardner, Mark Noble, Adam Johnson, Fabrice Muamba, Andrew Driver, Danny Rose.
Washambuliaji: Gabriel Agbonlahor, Theo Walcott, Frazier Campbell.
NUSU FAINALI zitachezwa tarehe 26 Juni na FAINALI 29 Juni.

Monday 22 June 2009

MATOKEO: KOMBE LA DUNIA 2010 Makundi ya Afrika


JUMAMOSI 20 Juni 2009
ZAMBIA 0 v ALGERIA 2
KENYA 2 v MOZAMBIQUE 1
MOROCCO 0 v TOGO 0
BURKINA FASO 2 v IVORY COAST 3
TUNISIA 0 v NIGERIA 0
SUDAN 0 v GHANA 2
JUMAPILI 21 Juni 2009
GUINEA 2 v MALAWI 1
MALI 3 v BENIN 1
KOMBE LA MABARA: Nusu Fainali Jumatano na Alhamisi
Nusu Fainali za Kombe la Mabara zitachezwa siku ya Jumatano Juni 24 Spain itakapochuana na USA Uwanjani Free State huko Mangaung, Bloemfontein na Alhamisi ni Brazil na Wenyeji Afrika Kusini Uwanjani Ellis Park, Johannesburg, uwanja ambao ndio wa nyumbani wa Klabu maarufu huko Bondeni, Orlando Pirates.

Mechi hizi zote zitaanza saa 3 na nusu usiku saa za kibongo.
Lippi hajuti, Dunga kicheko, Wachezaji Brazil walizwa Hotelini!!!!
Kocha wa Italia, Marcello Lippi, ametamka hana nia ya kubadilisha Kikosi cha Italia kwa ajili ya Utetezi wao wa Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini baada ya kipigo cha jana cha mabao 3-0 walichobebeshwa na Brazil na kubwagwa nje ya Kombe la Mabara huko Afrika Kusini.
Lippi amesema Kikosi ni kizuri ingawa Waandishi waliomhoji walidai Wachezaji ni Wakongwe.
Lippi alijibu: ‘Vijana gani uwalete? Huwezi ukachezesha Wachezaji wadogo wapya 6 au 7 wakati mmoja!’
Miongoni mwa Wakongwe waliocheza ni Nahodha Fabio Cannavaro, mwenye miaka 35, ambae jana alifikisha rekodi ya Paolo Maldini ya kuichezea Italia mechi 126. Lippi aliongeza: ‘Sijuti. Kama kusikitika basi ni kuwa mechi haikuonyesha dunia ile Italia tunayoijua!’
Nae Kocha wa Brazil Dunga amesema: ‘Tumefurahi! Kadri tunavyozidi kukaa pamoja ndio tunaimarika!’
Nusu Fainali ya Kombe la Mabara, Brazil wanapambana na Wenyeji Afrika Kusini inayofundishwa na Kocha kutoka Brazil, Joel Santana. Dunga anasema: ‘Santana ni Kocha anaeheshimika sana Brazil! Lakini hatuchezi na Santana, tunacheza na Afrika Kusini! Ni Timu ngumu na kama Wenyeji, itakuwa ngumu kuwafunga lakini nina imani na Wachezaji wangu!’
Wakati huo huo, Polisi huko Afrika Kusini wanachunguza wizi wa pesa za Mkufunzi wa Viungo wa Brazil na Mchezaji wao Kleber uliofanyika hotelini kwao.
Owen kutimka Newcastle!
Michael Owen amethibitisha atahama Timu iliyoporomoka Daraja Newcastle mkataba wake utakapoisha mwishoni mwa mwezi huu.
Owen, 29, alikataa kuongeza mkataba na Newcastle mwanzoni mwa mwaka na ametangaza nia yake kuendelea kucheza Ligi Kuu England badala ya Daraja la chini la Coca Cola ambako ndiko iliko Newcastle sasa.
Owen amesema: 'Sisaini mkataba. Nataka niwe Ligi Kuu au kokote kule kwenye Daraja la juu.’
Owen, anaepata mshahara wa Pauni Laki 1 kwa wiki alihamia Newcastle kutoka Real Madrid mwaka 2005 kwa ada ya Pauni Milioni 16 na kwa sasa atakuwa Mchezaji huru.
Tangu ahamie Newcastle, Owen amekuwa akikumbwa na majeruhi ya mara kwa mara na amecheza mechi 79 na kufunga mabao 30.
Ruud van Nistelrooy ahimiza Wadachi wenzake kutimka Real Madrid!!!
Ruud van Nistelrooy ametamka ni manufaa kwa Timu ya Taifa ya Uholanzi ikiwa wadachi wote waliokuwa Real Madrid watahama hapo.
Kuna taarifa nzito kuwa Real Madrid inataka kuwamwaga wadachi wote hapo Real na inahaha kutafuta Klabu za kuwauza. Wapo wadachi 6 hapo nao ni Van Nistelrooy, Arjen Robben, ­Wesley ­Sneijder, Royston Drenthe, Rafael van der Vaart na Klaas-Jan Huntelaar.
Pamoja na Wadachi hao Wachezaji wengine walio kwenye ‘listi ya mauzo’ ni Javier Saviola, Mahamadou Diarra and Beki wa zamani wa Manchester United Gabriel Heinze.
Ruud van Nistelrooy ametamka: ‘Wachezaji wa Udachi wana malengo makubwa mbele yao, moja likiwa ni kucheza Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini 2010! Wakipata ofa Klabu nyingine ni lazima wakubali! Hapa hamna maana kwao!’
Kuhusu hatma yake binafsi, van Nistelrooy, 32, ambae alifanyiwa operesheni ya goti baada ya kuumia vibaya, anasema: ‘Mimi ni tofauti kwani ndio kwanza nimepona goti! Sijui nani atanitaka!’

Sunday 21 June 2009

NUSU FAINALI ni Spain v USA na Brazil v Afrika Kusini!!!!!!
BRAZIL 3 ITALIA 0
Mabao ya kipindi cha kwanza ya Luis Fabiano mabao mawili, dakika ya 37 na 43, na lile la kujifunga mwenyewe Dossena, dakika ya 45, limewapa ushindi Brazil na kutinga Nusu Fainali na sasa watakutana na Wenyeji Afrika Kusini.
VIKOSI:
Italia:
Buffon, Chiellini, Cannavaro, Toni, De Rossi, Iaquinta, Camoranesi, Zambrotta, Montolivo, Pirlo, Dossena
Brazil: Julio Cesar, Maicon, Lucio, Juan, Felipe Melo, Gilberto Silva, Luis Fabiano, Kaka, Robinho, A. Santos, Ramires
REFA: Benito Archundia [Mexico]
MISRI 0 USA 3
Huku Italia ikipigwa mweleka na Vigogo Brazil wengi walitegemea Misri anaweza kupata suluhu na kujipenyeza Nusu Fainali lakini USA waliopigwa mechi zao zote mbili za kwanza wamewabamiza Misri bao 3-0 na kuingia Nusu Fainali kukutana na Spain.
Mashujaa wa USA ni Davies, aliefunga dakika ya 21, Bradley dakika ya 63 na Dempsey dakika ya 71.
VIKOSI:
Misri: El Hadary, A. El Mohamadi, Hani, Fathi, Hosni, Eid, Shawky, Farag, Abdelghani, Gomaa, Abo Terika
USA: Guzan, Bornstein, onyewu, Dempsey, Davies, Donovan, Bradley, Clark, Demerit, Altidore, Spector
REFA: Michael Hester [New Zealand]
BIGI 4: Ratiba ya Mechi za Kirafiki kabla msimu kuanza na mechi za mwanzo za Ligi Kuu!!!
Msimu wa LIGI KUU England utaanza rasmi Agosti 15 na Agosti 9 ni ile mechi ya ‘Fungua Pazia’ kati ya Bingwa wa LIGI KUU, Manchester United, na Bingwa wa Kombe la FA, Chelsea, itakayochezwa Uwanja wa Wembley, London.
Kawaida kabla msimu haujaanza Timu huanza maandalizi ya msimu mpya kwa mazoezi makali ambayo huambatana na safari za nje kutembelea kona mbalimbali za dunia.
Arsenal wanategemewa kuzuru Ujerumani na kisha kurudi nyumbani Emirates Stadium watakapokuwa na Mashindano maalum kugombea Emirates Cup itakayoshirikisha Klabu za Atletico Madrid ya Spain na Rangers ya Scotland.
Chelsea watakuwa Marekani na watacheza mechi na Inter Milan huko Los Angeles na Club America huko Dallas.
Liverpool wanategemewa kuwa Switzerland, Austria, Thailand na Singapore.
Manchester United watazuru huko Mashariki ya Mbali kwa kucheza mechi Nchini Malaysia, Indonesia, Korea na China. Baada ya hapo wataenda Ujerumani kushiriki Kombe la AUDI watakapocheza na Boca Juniors ya Argentina tarehe 29 Julai na Mshindi atapambana na Mshindi kati ya Bayern Munich na AC Milan.
Ifuatayo ni RATIBA ya kila Klabu ya Mechi za Kirafiki na zile za mwanzo za LIGI KUU England:
ARSENAL
Mechi za Kirafiki
18 Julai 2009
Barnet v Arsenal,
20 Julai 2009
Lincoln City v Arsenal,
1 August 2009
Arsenal v Atletico Madrid,
2 Agosti 2009
Arsenal v Rangers,
LIGI KUU
15 Agosti 2009
Everton v Arsenal,
18 Agosti 2009
Arsenal v Bolton, [IMEAHIRISHWA ILI Arsenal wacheze mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE hatua za awali za mtoano]
22 Agosti 2009
Arsenal v Portsmouth,
CHELSEA
Mechi za Kirafiki
18 Julai 2009
Chelsea v Seattle,
22 Julai 2009
Chelsea v Inter Milan,
25 Julai 2009
AC Milan v Chelsea,
27 Julai 2009
Chelsea v Club America
NGAO YA HISANI
9 August 2009
Man U v Chelsea,
LIGI KUU
15 August 2009
Chelsea v Hull,
18 Agosti 2009
Sunderland v Chelsea,
22 August 2009
Fulham v Chelsea,
LIVERPOOL
Mechi za Kirafiki
15 Julai 2009
St Gallen v Liverpool,
19 Julai 2009
Rapid Vienna v Liverpool,
22 Julai 2009
Thailand v Liverpool,
26 Julai 2009
Singapore v Liverpool,
5 Agosti 2009
Lyn v Liverpool,
8 August 2009
Liverpool v Atletico Madrid,
LIGI KUU
15 Agosti 2009
Tottenham v Liverpool,
MAN U
Mechi za Kirafiki
18 Julai 2009
Malaysia v Man U
20 Julai 2009
Indonesia All Stars v Man Utd,
24 Julai 2009
FC Seoul v Man U
26 Julai 2009
Hangzhou Greentown v Man U
KOMBE LA AUDI
29 Julai 2009
Man U v Boca Juniors,
5 August 2009
Man U v Valencia,
NGAO YA HISANI
9 August 2009
Man U v Chelsea,
LIGI KUU
15 Agosti 2009
Man Utd v Birmingham,
18 Agosti 2009
Burnley v Man Utd,
22 Agosti 2009
Wigan v Man U
29 Agosti 2009
Man Utd v Arsenal,
12 Septemba 2009
Tottenham v Man Utd,
19 Septemba 2009
Man U v Man City,
Mmoja wa Wamiliki wa Liverpool kuuza mali zake kuikwamua Liverpool!!!!!!
George Gillet, mmoja wa Wamarekani wawili wanaomiliki Liverpool, yuko mbioni kuuza baadhi ya rasilimali zake ili kupunguza makali yanayoikabili Klabu ya Liverpool hasa likiwa deni la Pauni Milioni 350 ambalo linatakiwa lilipwe ifikapo Julai 24. Liverpool inamilikiwa na Wamarekani wawili mmoja akiwa huyo George Gillet na mwingine ni Tom Hicks na waliinunua Liverpool Februari 2007 na kuweka ahadi kibao kubwa ikiwa ni kujenga Uwanja mpya utakaokuwa na ujazo mkubwa lakini hadi leo ahadi hizo zote hakuna hata moja iliyotimizika na badala yake Klabu imeingia kwenye lindi la madeni.
Mbali ya deni hilo la Pauni Milioni 350 linalotakiwa kulipwa Julai 24, Wakaguzi wa Mahesabu walitangaza kuwa kwa mwaka ulioishia Agosti 2008, Klabu ilipata hasara ya Pauni Milioni 42.6 na hasara kubwa ni riba ya deni hilo kubwa.
Ili kuinusuru Klabu, George Gillet ameamua kuuza hisa zake kwenye Timu kubwa ya Mpira wa Magongo wa Barafu, Montreal Canadiens, iliyoko Canada na inategemewa atapata zaidi ya Pauni Milioni 300 kutokana na mauzo ya Uwanja wa Timu hiyo na Kampuni yake tanzu ambayo yeye anaimiliki kwa asilimia 80.
Ronaldo ajutia kuwa chanzo cha mfarakano kati ya Man U na Real!!!
Asema Ferguson ni Baba yake!!!
Anena ni heshima iliyotukuka kuvaa Jezi Namba 7 Man U!!!
Cristiano Ronaldo, ambae yuko mbioni kukamilisha uhamisho kutoka Manchester United kwenda Real Madrid utakaogharimu Pauni Milioni 80 ikiwa ni rekodi ya dunia, amesema anajuta kuwa chanzo cha mgogoro kati ya Klabu hizo mbili na wa kulaumiwa ni yeye na si Klabu hizo.
Ronaldo amesema: ‘Kulikuwa hamna makubaliano kati ya Klabu hizo. Ni mimi niliefungua mdomo na kukaribisha kila aina ya matatizo!’
Ronaldo akasisitiza juu ya heshima yake kwa Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, na kusisitiza: ‘Nimesema mara nyingi tu, yeye ni kama Baba yangu! Amenifundisha mengi sana na sijawahi kukutana na mtu mwenye moyo na munkari na soka kama yeye! Yeye ndio amenipa moto wote na kunifanya niwe mshindi! Amenifundisha ukiwa nambari mbili huna maana!’
Ronaldo anaendelea: ‘Nimepata vitu vingi toka kwake vinavyonifanya niwe mtu bora! Watu hawaelewi jinsi anavyowajali na kuwatunza Wachezaji wake hata nje ya Uwanja! Anamjali kila mmoja wa Wachezaji wake!’
Akizungumzia alivyojiunga Manchester United na kupewa Jezi Namba 7 ambayo kihistoria Klabuni hapo imevaliwa na Wachezaji mahiri kama vile George Best, Bryan Robson, Eric Cantona na David Beckham, Ronaldo ametamka: ‘Sir Alex alionyesha imani kubwa kwangu tangu nikiwa mdogo! Nilipotua Man U alinikabidhi Jezi Namba 7 na nikasita kuichukua. Akaniweka chini na kuniambia historia ya Jezi hiyo namba 7 na akaniuliza: Unaelewa nnachotaka kukuambia? Akaongeza kuwa wewe unastahili kuvaa Jezi hii!!’
Ronaldo, huku akionekana kusononeka, akatamka: ‘Nikifikiria Wachezaji Bora wa Man U waliovaa Jezi ile Namba 7, sasa naelewa jinsi alivyoniamini na kunipenda! Naomba na mimi nionekane kama wale Wachezaji Bora waliopita waliovaa Jezi ile Namba 7!!!
Spain 2 Afrika Kusini 0

Afrika Kusini watinga Nusu Fainali licha ya kufungwa!!!

Wenyeji Afrika Kusini wamepigwa 2-0 na Spain lakini wametinga Nusu Fainali baada ya Iraq, katika mechi nyingine ya KUNDI A, kushindwa kuifunga New Zealand na hivyo kujikosesha nafasi ya kwenda Nusu Fainali.
Ingawa Afrika Kusini walifungwa mechi hii, walipata nafasi kadhaa walizozikosa.
Hata Kipa wao, Itumeleng Khune, alikuwa shujaa alipookoa penalti dakika ya 51 iliyopigwa na David Villa lakini, dakika moja baadae, alishindwa kuzuia mkwaju wa Villa uliotinga wavuni na kuandika bao la kwanza.
Mchezaji alieingizwa kutoka benchi, Llorente, alifunga bao la pili kwa Spain dakika ya 72.
Spain atacheza na Mshindi wa Pili KUNDI B ambao wanamaliza mechi zao leo usiku.
Iraq 0 New Zealand 0
Iraq wameikosa nafasi murua ya kusonga kuingia Nusu Fainali pale waliposhindwa kuifunga New Zealand.
Kwa Spain kuifunga Afrika Kusini, Iraq alihitaji ushindi wa aina yeyote ile ili kusonga mbele lakini walishindwa kuupata katika mechi ambayo Timu yeyote katika hizo mbili ilikuwa na uwezo wa kushinda kwa jinsi mechi ilivyokuwa wazi.
KUNDI B: Nani kutinga Nusu Fainali?
Leo Saa 3 na nusu usiku ni mechi za mwisho KUNDI B wakati Brazil, anaeongoza Kundi hili kwa pointi 6 baada ya kushinda mechi zote mbili, anapambana na Italia mwenye pointi 3.
Misri, mwenye pointi 3 pia, anacheza na USA aliekwisha kuaga mashindano haya kwa kufungwa mechi zake zote mbili.
Kimahesabu, Brazil, Italia na Misri zote zina nafasi ya kusonga Nusu Fainali ingawa ukweli ni kwamba ni Brazil tu ndie mwenye nafasi kubwa zaidi.
Italia hana ujanja ni lazima ashinde na kuomba Misri asipate ushindi mkubwa au akwamishwe na USA.
Kwa Misri nao hali ni hiyo hiyo, lazima ashinde na aombee Italia akwame.

Powered By Blogger