Saturday 20 June 2009

KOMBE LA MABARA: Mechi za Mwisho KUNDI A!! Nani kuungana na Spain Nusu Fainali? Afrika Kusini au Iraq?
Spain v South Africa
UWANJA: FREE STATE, BLOEMFONTEIN SAA: 3 NA NUSU USIKU [bongo]
Spain imeshatinga Nusu Fainali hivyo itakuwa si ajabu ikiwa Mastaa watapumzishwa leo.
Wenyeji Afrika Kusini wanahitaji suluhu tu ili kuingia Nusu Fainali bila kujali matokeo ya mechi nyingine ya Kundi hili kati ya Iraq na New Zealand.
REFA: Pablo Pozo (Chile)
Iraq v New Zealand
UWANJA: Ellis Park, Jahannesburg SAA: 3 NA NUSU USIKU [Bongo]
New Zealand wameshatolewa mashindano haya na Iraq lazima washinde mechi hii na kuomba Afrika Kusini wafungwe ili kuingia Nusu Fainali.
Refa: Howard Webb (England
TEVEZ KUONDOKA MAN U!!!
Mabingwa wa England, Manchester United, wametoa taarifa kupitia tovuti yao kuwa Carlos Tevez hataendelea kuwepo hapo Klabuni baada ya Washauri wake kuwajulisha kuwa wamekataa ofa ya Man U ya mkataba wa miaka mitano, ada ya Pauni Milioni 25.5 na pia kumfanya awe mmoja wa Wachezaji wenye mshahara mnono sana hapo klabuni.
Taarifa ya Man U ilisema: ‘Kufuatia taarifa tulizopokea jana usiku kutoka kwa Washauri wa Carlos Tevez ikiwa ni mbele ya siku ya mwisho Klabu iliyoweka ili makubaliano yafikiwe, Manchester United inatangaza kuwa Carlos Tevez hatasaini mkataba mpya na Klabu yetu.’
‘Klabu ilikubali kulipa Pauni Milioni 25.5, kumpa mkataba wa miaka mitano na mshahara mkubwa wa kumfanya awe ni miongoni mwa Wachezaji wanaolipwa juu. Lakini, kwa masikitiko, Washauri wake wametujulisha, ingawa alipata mafanikio makubwa sana hapa Klabuni, hataki kuendelea kucheza hapa.
‘Klabu inapenda kumshukuru Carlos kwa utumishi wake kwa misimu miwili iliyopita na inamtakia kila la heri maisha yake ya baadae’
Tevez alichukuliwa na Man U kutoka West Ham kwa mkopo kutoka Kampuni inayommiliki kwa mkataba wa miaka miwili unaokwisha Juni 30.
Man City wamtwaa Santa Cruz
Manchester City wamefikia makubaliano na Blackburn Rovers ya kumnunua Straika kutoka Paraguay Roque Santa Cruz, 27, kwa ada ya Pauni Milioni 18.
Ununuzi wa Santa Cruz umekuwa wa taabu kwa vile kuna kipengele kwenye mkataba wake kwamba anaetaka kumnunua lazima ailipe Blackburn Pauni Milioni 18 juu ya ada ya uhamisho kwa vile mkataba wake unamalizika 2012.
Santa Cruz, alinunuliwa na Blackburn kutoka Bayern Munich mwaka 2007 kwa Pauni Milioni 3.8, ameichezea Blackburn mechi 70 na kufunga mabao 29. Msimu huu amekuwa akicheza kwa nadra sana kwa kusumbuliwa na goti.
Dili hii ya Santa Cruz ikikamilika huyu atakuwa Mchezaji wa pili kununuliwa na Man City baada ya kumnunua Gareth Barry kutoka Aston Villa.
Santa Cruz hapo Man City ataungana tena na Meneja Mark Hughes, mtu aliemnunua kutoka Bayern Munich alipokuwa Meneja wa Blackburn
Chelsea yakata rufaa UEFA kupinga adhabu za Drogba, Bosingwa!!!!!
Chelsea wamethibitisha kuwa wamekata rufaa UEFA kupinga ukali wa adhabu za Didier Drogba na Jose Bosingwa zilizotelewa na UEFA kufuatia kasheshe la kumkashifu Refa Tom Henning Ovrebo mara baada ya mechi ya NUSU FAINALI ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambayo Andres Iniesta aliisawazishia Barcelona dakika za majeruhi na kuwaingiza Barcelona Fainali kwa goli la ugenini.
Drogba amefungiwa mechi 6, mechi mbili zikisimamishwa kwa miaka miwili kuchunguza mwenedo wake, na Bosingwa, aliemwita Refa huyo kutoka Norway ‘mwizi’, amefungiwa mechi 4 huku moja ikiwekwa kiporo kuchunguza mwenendo wake.
Vilevile Chelsea imesema itakata rufaa kupinga Klabu kupigwa faini ya Pauni 85,000 kwa kushindwa kuwadhibiti Wachezaji pamoja na Mashabiki yake waliokuwa wakirusha ‘makombora’ uwanjani baada ya mechi kwisha.
Wigan wamsaini Gomez kutoka Espanyol
Meneja mpya wa Wigan Roberto Martinez amefanya usajili wake wa kwanza kwa kumchukua Kiungo Jordi Gomez kutoka Espanyol ya Spain kwa mkataba wa miaka mitatu na ada yake ya uhamisho imekadiriwa kuwa ni Pauni Milioni 1.7.
Meneja Martinez alikuwa na Mchezaji huyo huko Swansea msimu uliokwisha ambako Gomez alikuwa akicheza kwa mkopo na Martinez akiwa ndie Meneja wa Swansea.

Gomez, 24, aliifungia Swansea mabao 14.
KIPINDI CHA UHAMISHO LIGI KUU ENGLAND: Biashara yaanza kutokota!!!

Kipindi cha UHAMISHO Ligi Kuu England kitamalizika hapo tarehe 31 Agost 09 na ligi itaanza rasmi hapo Agosti 15, lakini Klabu za ligi hiyo zipo kwenye michuano mikali ya usajili wa Wachezaji.
Baadhi ya biashara zilizofanywa ni:
Arsenal
NDANI: Thomas Vermaelen (Ajax, £11m)
NJE:
Aston Villa
NDANI:
NJE: Martin Laursen (KASTAAFU),Gareth Barry (Manchester City, £12m)
Birmingham City
NDANI: Christian Benitez (Santos Laguna, £9m), Scott Dann (Coventry, £3.5m) NJE: Mehdi Nafti, Radhi Jaidi, Artur Krysiak (wameachwa), Stephen Kelly (Fulham, bure)
Blackburn Rovers
NDANI: Elrio Van Heerden (Bruges, bure)
NJE: Aaron Mokoena (Portsmouth, bure) Andre Ooijer (PSV Eindhoven), Tugay (astaafu), Johann Vogel (kaachwa)
Bolton Wanderers
HAMNA
Burnley
NDANI:
NJE: Steve Jones, Alan Mahon, Gabor Kiraly (wameachwa),
Chelsea
HAMNA
Everton
HAMNA
Fulham
NDANI: Stephen Kelly (Birmingham, bure)
NJE:
Hull City
NDANI:
NJE: Dean Windass, John Welsh, Michael Bridges (wameachwa), Wayne Brown (Leicester City, bure)
Liverpool
NDANI:
NJE: Jack Hobbs (Leicester,ada haikutajwa), Sami Hyypia (Bayer Leverkusen, bure), Ronald Huth, Godwin Antwi, Miki Roque, Gary MacKay-Steven (wameachwa)
Manchester City
NDANI: Gareth Barry (Aston Villa, £12m)
NJE:
Manchester United
NDANI:
NJE: Cristiano Ronaldo (Real Madrid, Usajili haujakamilika)
Portsmouth
NDANI: Aaron Mokoena (Blackburn, bure)
NJE:
Stoke City
NDANI:
NJE: Vincent Pericard (ameachwa)
Sunderland
NDANI:
NJE: Peter Hartley (Hartlepool, bure), Arnau Riera, Dwight Yorke, Nick Colgan, David Connolly (wameachwa), Darren Ward (kastaafu)
Tottenham Hotspur
NDANI:
NJE: Ricardo Rocha, Simon Dawkins, David Hutton (wameachwa)
West Ham United
NDANI: Peter Kurucz (Ujpest FC, ada haikutajwa),
NJE: Diego Tristan, Lee Bowyer, Walter Lopez, Kyel Reid, Tony Stokes, Jimmy Walker (wameachwa)
Wigan Athletic
NDANI: Jordi Gomez (Espanyol, £1.7m)
NJE:
Wolverhampton Wanderers
Ins: Nenad Milijas (Red Star Belgrade, ada haikutajwa), Marcus Hahnemann (Reading, bure)
RATIBA: KOMBE LA MABARA
JUMAMOSI 20 Juni 2009
Iraq v New Zealand
Spain v South Africa
JUMAPILI 21 Juni 2009
Egypt v USA
Italy v Brazil
RATIBA: KOMBE LA DUNIA 2010
JUMAMOSI 20 Juni 2009
ZAMBIA v ALGERIA
KENYA v MOZAMBIQUE
MOROCCO v TOGO
BURKINA FASO v IVORY COAST
TUNISIA v NIGERIA
SUDAN v GHANA
GUINEA v MALAWI
MALI v BENIN
Arsenal yathibitisha kumsaini Vermaelen
Arsenal wamethibitisha kukamilika kwa taratibu zote za kumsaini Mlinzi kutoka Ubelgiji anaechezea Klabu ya Ajax ya Uholanzi kwa ada ya Pauni Milioni 10
Thomas Vermaelen, 23, pia ni Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ubelgiji na alianza kucheza Ajax akiwa na miaka 18 na kucheza Klabuni hapo jumla ya mechi 143. Kwa sasa ndie Nahodha wa Ajax.

Thursday 18 June 2009

Mabingwa wa Dunia chali kwa Misri!!
Mabingwa wa Dunia Italia wamepigwa kimoja na Mabingwa wa Afrika Misri na sasa ni hekaheka nani ataingia Nusu Fainali kwenye KUNDI lao.
KUNDI B Brazil ndio vinara wana pointi 6, Italia pointi 3 na Misri pointi 3.
Mechi za mwisho ni Brazil v Italia,na huu ni moto kwa Italia kwani lazima washinde, Misri wanacheza na USA ambao, kwa hesabu za juu juu, washaaga Mashindano haya ingawa wana nafasi finyu ikiwa Brazil atashinda halafu wao wawatandike Misri kwa idadi bora ya magoli .
Huko Bondeni VUVUZELA laleta kasheshe!!!
FIFA kulijadili!!!!
Makampuni makubwa ya TV kutoka Ulaya yanayorusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Kombe la Mabara huko Afrika Kusini yamepeleka malamiko yao kwa FIFA wakikerwa na ‘VUVUZELA’.
VUVUZELA ni tarumbeta la plastiki ambalo hutumiwa na Mashabiki wa Bondeni kushangilia Timu zao zinapocheza na hupulizwa mfululizo kwenye mechi.
VUVUZELA ni desturi na ndio utamaduni wa Mashabiki wa Bondeni.
Lakini, Makampuni ya TV yamekerwa na sasa FIFA watafanya kikao kulijadili VUVUZELA.

Lakini, Mashabiki wa Bondeni wamesema VUVUZELA litadumu!!!
Brazil yanusa Nusu Fainali, waichapa USA 3-0!!!
Mabingwa wa Marekani ya Kusini, ambao pia ndio Watetezi wa Kombe la Mabara, Brazil, wanainusa Nusu Fainali ya Kombe la Mabara, baada ya kuifunga USA mabao 3-0 katika mechi ya KUNDI B iliyochezwa leo huko Tshwane, Pretoria Uwanja wa Loftus Versfeld.

Ikiwa Misri watafungwa na Mabingwa wa Dunia Italia, Brazil watajihakikishia Nusu Fainali.
Mabao ya Brazil yalifungwa na Felipe Melo, dakika ya 7, Robinho, dakika ya 20, na Maicon, dakika ya 62.
Katika mechi ya kwanza Brazil waliwafunga Mabingwa wa Afrika, Misri, 4-3.
VIKOSI:
Brazil: Julio Cesar, Maicon, Lucio, Felipe Melo, Gilberto Silva, Luis Fabiano, Kaka, Robinho, Miranda, A. Santos, Ramires.
USA: Howard, Bornstein, Onyewu, Beasley, Dempsey, Donovan, Bradley, Demert, Kljestan, Altidore, Spector
REFA: Massimo Bussaca [Switzerland[
RATIBA: LEO SAA 3 NA NUSU USIKU [BONGO TAIMU] MISRI v ITALY
Bayern yamnyemelea Bosingwa!!!!
Bayern Munich imekubali kuwa inamtaka Beki kutoka Ureno wa Chelsea, Jose Bosingwa, ingawa mpaka sasa Klabu hizo mbili hazijafikia makubaliano.
Mwenyekiti wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummnigge amesema: ‘Tupo mazungumzoni, tunahitaji Chelsea wakubali.’
Bayern Munich wana pengo la Beki wa kulia baada ya Willy Sagnol kulazimika kustaafu na Massimo Oddo, alie Bayern kwa mkopo kutoka AC Milan,kuwa chini ya kiwango.
Sir Bobby Charlton asema ada ya Ronaldo ni ‘mbaya’ lakini sahihi!!!!
Mkongwe wa Manchester United ambae sasa ni mmoja wa Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Sir Bobby Charlton, amesema Manchester United walikuwa na kila haki kudai ada ambayo ni rekodi ya dunia kwa Mchezaji Bora Duniani.
Ingawa amekiri ada hiyo ni ‘uchafu’, amesema ni haki ya Klabu yake kuidai. Ronaldo ameuzwa kwa Real Madrid kwa Pauni Milioni 80 na ada hiyo imezua mijadala mingi na mirefu.
Charlton anasema: ‘Dili ni nzuri na ya haki! N pesa nyingi, ni wehu! Lakini kama Kampuni na kama Klabu tuna majukumu yetu. Ronaldo anatutoka kwa sababu ni ndoto yake kwenda Real Madrid. Tumembariki aondoke!’
Santa Cruz asikitishwa hakuna Klabu inayomtaka!!!

Mshambuliaji kutoka Paraguay, Roque Santa Cruz, ameanza kukata tamaa kuwa hakuna Klabu itakayoweza kumnunua kutoka Klabu yake ya sasa Blackburn Rovers kwa sababu mkataba wake una kipengele kigumu kinachotaka Klabu kuilipa Blackburn Pauni Milioni 20 juu ya ada ya kawaida ya uhamisho kwa sababu hajamaliza mkataba wake unaoisha 2012.
Manchester City walimuwania Januari lakini wakagonga mwamba kutokana na kipengele hicho.

Wednesday 17 June 2009

BONDENI 2 NEW ZEALAND 0
NEW ZEALAND NJE MABARA!!
Bao mbili zilizopigwa na Parker zimewang’oa New Zealand nje ya Kombe la Mabara na kuwapa matumaini Wenyeji Afrika Kusini kuingia Nusu Fainali ya Kombe hili.
Ili kujihakikishia kuingia Nusu Fainali Afrika Kusini wanahitaji suluhu na Spain ambao wameshatinga Nusu Fainali na matokeo hayo ni ya bila kujali mechi kati ya Iraq na New Zealand.
Endapo Iraq akifungwa au akitoka sare kwenye mechi hiyo, Afrika Kusini atatinga Nusu Fainali.
VIKOSI:
AFRIKA KUSINI: Khune, Gxa, Masilela, Mokoena, Sibaya, Pienaar, Modise, Dikgacoi, Booth, Prker
NEW ZEALAND: Moss, Locchead, Vicelich, Elliot, Brown, Smeltz, Killen, Bertos, Christie, Mulligan, Boyens
Korea Kaskazini ndani ya FAINALI KOMBE LA DUNIA 2010!!!
Kwa mara ya kwanza tangu 1966 walipoushangaza ulimwengu walipocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Uingereza na kutinga Robo Fainali na kuongoza 3-0 hadi mapumziko ingawa kwenye mechi hiyo walikung’utwa 5-3 na Ureno ya Eusebio wakati huo, leo Korea Kaskazini wametinga tena Fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini mwaka 2010 baada ya kutoka suluhu 0-0 na Saudi Arabia.
Mafanikio ya Korea Kaskazini pia yamesaidiwa na Iran kushindwa kuifunga Korea Kusini huko Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini.
Sasa Korea Kaskazini wanaungana na wenzao Korea Kusini, Japan na Australia kutoka KUNDI la Nchi za Asia, pamoja na Uholanzi kutoka Ulaya, kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010.
Saudi Arabia bado wana nafasi ya kuingia Fainali za Kombe la Dunia kwani Septemba watacheza mechi na jirani zao Bahrain na mshindi atakumbana na New Zealand ili kupata Nchi moja itakayoingia Fainali.
DROGBA AFUNGIWA MECHI 6, BOSINGWA 4 NA CHELSEA FAINI PAUNI ELFU 85!!!!
UEFA leo imemdunga Didier Drogba kifungo cha mechi 6 na mwenzie Jose Bosingwa mechi 4 kufuatia kasheshe waliyoileta baada ya mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE Uwanjani kwao Stamford Bridge Chelsea walipotolewa na Barcelona kwa goli la ugenini.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 6 na kuchezeshwa na Refa Tom Henning Ovrebo kutoka Norway na kumalizika 1-1 na Chelsea kuminywa si chini ya penalti 3 au 4 za wazi, Drogba alimvaa Refa mara baada ya filimbi ya mwisho na kumtukana huku Walinzi wakimzuia kwa nguvu asimkaribie Refa huyo.
Nae Jose Bosingwa alikaririwa baada ya mechi akimwita Refa ni ‘mwizi'.
Drogba atazikosa mechi 4 tu za Mashindano ya UEFA msimu ujao na mechi 2 zitasimamishwa kwa miaka miwili ili kuchunguza mwenendo wake.

Bosingwa atakosa mechi 3 huku ya 4 ikisimamishwa kwa miaka miwili ili kuchunguza mwenendo wake.
Mbali ya adhabu hiyo kwa Wachezaji hao wawili wa Chelsea, Klabu yenyewe imetwangwa faini ya Pauni Elfu 85 kwa kushindwa kuwadhibiti Wachezaji na Washabiki wao waliotupa vitu Uwanjani baada ya mechi
Drogba, Bosingwa na Klabu yao wamepewa siku 3 ili kukata rufaa..
David Villa aiingiza Spain NUSU FAINALI!!
Bao la David Villa la kipindi cha pili dakika ya 55 limeivusha Spain kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mabara walipowashinda Iraq 1-0 kwenye mechi ya KUNDI A iliyochezwa Mangaung, Bloemfontein Uwanja wa Free State.
Ingawa Spain walitawala mechi hii Iraq walipigana kiume na kuwabana vizuri Spain ambayo ni Timu Nambari Wani duniani.
VIKOSI:
SPAIN: Casillas, Pique, Marchena, David Villa, Xavi, Torres, Capdevila, Alonso, ramos, Cazorla, Mata
IRAQ: Mohammed K., Mohammed Ali, Basem, Fareed, Nashad, Hawar, Salam, Ali Hussein, Alaa , Sameer, Muayad.
REFA: Matthew Breeze [Australia]
Mabingwa Man U kuanza LIGI KUU na Birmingham
Manchester United wataanza utetezi wa Taji lao la LIGI KUU England nyumbani kwake Old Trafford kwa kuchuana na Birmingham, Timu iliyopanda Daraja,wakati mechi za ufunguzi zitakapochezwa hapo tarehe 15 Agosti.
Washindi wa pili wa LIGI KUU, Liverpool wanaanza ligi wakiwa ugenini kwa kupambana na Tottenham, Chelsea wataanzia nyumbani Stamford Bridge kwa kucheza na Hull City na Arsenal watakuwa ugenini mjini Liverpool watakapocheza Uwanja wa Goodison Park nyumbani kwa Everton.
Timu zilizopanda Daraja za Wolves na Burnley zitaanza kwa Wolves kuwa kwake Molineux na kucheza na West Ham na Burnley atakuwa mgeni wa Stoke City.
Timu ya Matajiri Manchester City watasafiri kwenda kucheza na Blackburn Rovers.
BIGI MECHI ZA BIGI 4:
-29 Agosti Old Trafford, Manchester United v Arsenal na marudiano ni Januari 30.
-3 Oktoba, Stamford Bridge, Chelsea v Liverpool marudio 1 Mei 2010.
-24 Oktoba Anfield, Liverpool v Manchester United na marudio 20 Machi 2010.
-7 Novemba, Stamford Bridge, Chelsea v Manchester United marudio 3 Aprili 2010.
-28 Novemba Emirates, Arsenal v Chelsea marudio Februari 6
-12 Desemba Anfield, Liverpool v Arsenal marudio Februari 9
RATIBA KAMILI YA SIKU YA UFUNGUZI 15 Agosti 2009:
Aston Villa v Wigan
Blackburn v Man City
Bolton v Sunderland
Chelsea v Hull City
Everton v Arsenal
Man Utd v Birmingham
Portsmouth v Fulham
Stoke v Burnley
Tottenham v Liverpool
Wolverhampton v West Ham

Tuesday 16 June 2009

FIFA yatupilia mbali malalamiko ya Misri!!!
Jioni hii FIFA imewaandikia Chama cha Soka cha Misri kuhusu malalamiko yao juu ya mechi ya jana kati ya Brazil na Misri hasa uamuzi wa Refa Howard Webb wa Uingereza wa kuwapa penalti Brazil baada ya kuashiria ni kona.
FIFA walipokea barua ya malalamiko toka kwa Misri mara baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Free State huko Mangaung, Bloemfontein.
Misri hawakupinga uamuzi wa Refa Howard Webb kutoa penalti kwa Brazil na kumpa Kadi Nyekundu Mlinzi wao Ahmed El-Mohamadi, walichokipinga kilikuwa ni jinsi Refa huyo alivyofikia uamuzi huo baada ya kwanza kuamua ipigwe kona.
FIFA imeelezea kwenye barua yao kuwa baada ya kuchunguza ushahidi wote ukiwa pamoja na Ripoti ya Mechi ya Refa Howard Webb na maelezo ya ziada kutoka kwa Refa huyo, imeridhika kuwa uamuzi wa kutoa penalti na Kadi Nyekundu ulifikiwa baada ya Refa Howard Webb kushirikiana vyema na Mike Mullarkey aliekuwa Mshika Kibendera, au tumwite Msaidizi wa Refa kama ipasavyo siku hizi, ambaye pia alithibitisha kila kitu kilichosemwa na Refa Howard Webb.
Tukio hilo la utata lilitokea dakika za majeruhi huku mechi ikiwa 3-3 na katika kizaazaa golini mwa Misri Beki El-Mohamadi akaokoa mpira akiwa kwenye mstari wa goli kwa mkono na kisha kujidondosha chini, akishika kichwa na kuvunga kaumia. Refa Howard Webb alionekana waziwazi akitoa kona na Wachezaji wa Brazil wakamzonga wakilalamika na kutoa ishara mpira umeshikwa kwa mkono.
Wakati huo El-Mohamadi alikuwa kajigalagaza chini na, pengine, hapo ndipo Refa Howard alipoambiwa yule Beki wa Misri aliushika mpira.
MISRI WAKATA RUFAA FIFA KUHUSU MAAMUZI YA REFA WEBB!!
FIFA imepokea malamiko rasmi kutoka Misri ambayo jana katika mechi ya kwanza ya KUNDI B kugombea Kombe la Mabara huko Afrika Kusini ilipigwa bao 4-3 na Brazil huku bao la ushindi la Brazil likifungwa kwa penalti dakika za majeruhi.
Refa aliechezesha pambano hilo ni Mwingereza Howard Webb na alionekana akiashiria kuwa ipigwe kona lakini akabadili uamuzi na kumtoa Mlinzi wa Misri Ahmed El Mohamady kwa Kadi Nyekundu na kuwapa Brazil penalti iliyofungwa na Kaka.
Misri hawapingi uamuzi wa Refa Howard Webb kutoa Kadi Nyekundu na penalti ila wanachopinga ni jinsi Refa huyo alivyoutoa uamuzi huo.
Misri pia hawapingi kuwa Mchezaji wao aliushika mpira bali wanachodai ni kuwa Refa aliamua ipigwe kona kwa sababu yeye na Mshika Kibendera hawakuliona tukio lakini, wakati Mchezaji alietenda madhambi akivunga kaumia, ndipo akajulishwa na Mwamuzi wa Akiba kwa redio baada ya kuona marudio ya tukio hilo kwenye video.
Kocha Msaidizi wa Misri, Gharib Chawki, anadai: ‘Tunavyojua sheria haziruhusu matumizi ya video kwa Marefa.’
Hata Mchezaji wa Brazil, Luis Fabiano, amekiri kuwa Refa na Msaidizi wake hawakuliona tukio ila walijulishwa kwa redio na Mwamuzi wa Akiba, Matthew Breeze, kutoka Australia.
Utata huu unaikumbusha dunia lile tukio lililotokea kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 pale Zinedine Zidane alipotolewa kwa Kadi Nyekundu kwa kumtwanga kichwa Materazzi wa Italy katika tukio ambalo Waamuzi hawakuliona bali walijulishwa na Mwamuzi wa Akiba ambae pia hakuliona ila marudio yake kwenye video ndio aliyoyaona na kumtonya Refa kwa redio.
Hata hivyo FIFA siku zote imekuwa ikiyakataa madai hayo.

Hamna Sheria ya Soka inayotamka Refa atasaidiwa na matumizi ya video.
RATIBA KOMBE LA MABARA [saa za Bongo]
-Jumatano 17 Juni 2009-06-05
KUNDI A
Spain v Iraq [saa 11 jioni]
Afrika Kusini v New Zealand [saa 3 na nusu]
-Alhamisi 18 Juni 2009
KUNDI B
USA v Brazil [saa 11 jioni]
Egypt v Italia [saa 3 na nusu usiku]
WIGAN WAMCHUKUA MARTINEZ KUWA MENEJA!!!!
Wigan Athletic wamethibitisha kuwa Roberto Martinez [35] , kutoka Spain, ndie Meneja wao mpya atakaerithi nafasi iliyoachwa wazi na Steve Bruce aliekwenda Sunderland.
Roberto Matinez ametokea Klabu ya Daraja la Chini Swansea na amesaini mkataba wa miaka mitatu.
Wakati akiwa Mchezaji, Martinez alizichezea Klabu za Wigan na Swansea na mwaka 2007 akapewa nafasi ya Umeneja huko Swansea na akamudu kuipandisha Swansea kuingia Ligi Wani katika msimu wake wa kwanza tu.
LIVERPOOL WAMNYAKUA GLEN JOHNSON!!!
Klabu ya Liverpool imefanikiwa kumchukua Beki wa Portsmouth, Glen Johnson [24] kwa dau la Pauni milioni 17.
Klabu za Chelsea na Manchester City pia zilikuwa zikimuwania Beki huyo wa zamani wa Chelsea iliyomuuza kwenda Portsmouth mwaka 2006 kwa Pauni Milioni 4 tu lakini mwenyewe akaichagua Liverpool.
Sasa inaelekea Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, atamuuza Beki Andrea Dossena ili kupata dau la kununua Wachezaji.
DRO YA RAUNDI YA KWANZA CARLING CUP YAFANYWA!!
Ratiba ya Raundi ya kwanza ya Kombe la Carling imetolewa na kama kawaida Klabu za LIGI KUU England huwa hazishirikishwi duru hili.
Mechi za Raundi hii zitafanyika kuanzia Agosti 10.
Klabu pekee iliyoporomoka Daraja kutoka LIGI KUU na kupangwa kwenye Raundi hii ya kwanza ni West Bromwich Albion watakaokumbana na Bury.
RATIBA KAMILI NI:
Accrington Stanley v Walsall
Huddersfield v Stockport
Rotherham v Derby
Tranmere v Grimsby
Sheffield Wednesday v Rochdale
Bury v West Brom
Notts County v Doncaster
Lincoln v Barnsley
Scunthorpe v Chesterfield
Coventry v Hartlepool
Darlington v Leeds
Preston v Morecambe
Crewe v Blackpool
Carlisle v Oldham
Nottingham Forest v Bradford
Macclesfield v Leicester
Sheffield United v Port Vale
Cardiff v Dagenham & Redbridge
Wycombe v Peterborough
Southampton v Northampton
Barnet v Watford
Hereford v Charlton
Bristol Rovers v Aldershot
Millwall v Bournemouth
Gillingham v Plymouth
Colchester v Leyton Orient
Reading v Burton Albion
Exeter v Queens Park Rangers
Cheltenham Town v Southend
Brentford v Bristol City
Yeovil v Norwich City
Crystal Palace v Torquay
MK Dons v Swindon
Swansea v Brighton & Hove Albion
Shrewsbury v Ipswich
REAL MADRID KUWATEMA LUNDO LA WACHEZAJI!!!
Baada ya kutobokewa mifuko kwa kuwanunua Ronaldo na Kaka kwa bei mbaya sana, Real Madrid sasa inawabidi kuuza lundo la Wachezaji na Maafisa wake sasa wanahaha Ulaya nzima na hasa England kutafuta soko kwa Wachezaji hao.
Wachezaji ambao Real Madrid inataka kuwauza ni Arjen Robben, Van Nistelrooy, Klaas-Jan Huntelaar, Wesley Sneijder, Rafael van der Vaart, Royston Drenthe, Gabriel Heinze, Mahamadou Diarra na Javier Saviola.
Inasemekana Huntelaar na Van Nistelrooy huenda wakaenda Tottenham.
Mwenyekiti Bayern Munich asema Man U, Chelsea na Barca wametoa ofa kwa Ribery!!!
Mwenyekiti wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge, ametoboa kuwa Vilabu vya Manchester United, Chelsea na Barcelona vimetoa ofa rasmi kumnunua Kiungo wao kutoka Ufaransa Franck Ribery.
Rumenigge amesema: ‘Hatuna mchecheto! Tumewakatalia Real Madrid kumnunua Ribery! Na pia Man U, Chelsea na Barca wametoa ofa! Lakini sisi ndio wenye nguvu na hatumuuzi!’
Wadau wengi wanaamini kauli na msimamo huo wa Bayern Munich ni ule ule kama walivyowafanyia Manchester United walipotaka kumnunua Owen Hargreaves na hatimaye wakamuuza kwa bei ambayo ilikuwa juu mno.
.

Monday 15 June 2009

Italy 3 Marekani 1
Mechi ya pili ya KUNDI B imewakutanisha Mabingwa wa Dunia Italy na USA ndani ya Uwanja wa Loftus Versfeld, uliopo Tshwane, Pretoria.
Kipindi cha kwanza USA walipata pigo kubwa pale Clark alipoivaa Kadi Nyekundu kwenye dakika ya 33 baada ya Refa kutoka Chile, Pablo Pozo, kuamua amecheza rafu mbaya dhidi ya Gattuso.
Hata hivyo, Marekani hawakukata tamaa na waliendelea kuwabana Italy na hatimaye ilipofika dakika ya 40 Refa Pozo akawapa penalti baada ya Chiellini kucheza faulo kwa Altidore na Nahodha Landon Donovan akamhadaa vizuri Kipa Buffon wa Italy na kupachika bao kwa USA.
Mapumziko: USA 1 Italy 0
Kipindi cha pili, kwenye dakika ya 57, Kocha Marcello Lippi akafanya mabadiliko na kuwaingiza Giuseppe Rossi, bwana mdogo wa zamani Man U badala ya Mkongwe Gattuso, na Montolivi badala ya Camoranes.
Dakika moja baadae Giuseppe Rossi akapiga mkwaju wa mbali uliomshinda Tim Howard, Kipa wa USA ambae zamani walikuwa nae Man U, na mechi kuwa 1-1.
Dakika ya 72, Tim Howard tena alizidiwa na shuti la mbali liliopigwa na Daniele De Rossi ingawa ana kila sababu ya kuwalaumu Mabeki wake kwa kumchuuza.
Lakini goli la 3 la Giuseeppe Rossi, kama la kwanza, Tim Howard hawezi kulaumu mtu au kulaumiwa, ni kigongo kisichozuilika.
USA: HOWARD, BORNSTEIN, ONYEWU, DEMPSEY, DONOVAN, BRADLEY, CLARK, DEMERIT, ALTIDORE, SPECTOR, FEILHABER
ITALY: BUFFON, GROSSO, CHIELLINI, LEGROTTAGLIE, GATTUSO, DE ROSSI, GILARDINO, IAQUINTO, CAMORANES,ZAMBROTTA, PIRLO
REFA: Pablo Pozo [Chile]
Brazil 4 Misri 3
Mabingwa wa Afrika, Misri, licha ya kufungwa imeonyesha waziwazi sasa Afrika si mdebwedo baada ya kuwabana na kutishia kuwabwaga Vigogo wa Soka Brazil na mpaka ikabidi Brazil wapate goli la ushindi kwa njia ya penalti dakika ya 90 baada ya Beki A. Elmohamadi kudaka mpira akiwa mstari wa golini na Refa Mwingereza anaechezesha Ligi Kuu, Howard Webb, akamzawadia Kadi Nyekundu na kuamuru ipigwe penalti iliyofungwa na Mchezaji mpya wa Real Madrid, Kaka.
Brazil ndio waliotangulia kupata bao kupitia Kaka dakika ya 5, lakini Mchezaji machachari wa Misri Zidan akasawazisha dakika ya 9.
Brazil wakapachika mabao mawili dakika ya 12 kupitia Luis Fabiano na Mlinzi Juan akafunga kwa kichwa dakika ya 32.
Hadi mapumziko Brazil 3 Misri 2.
Kipindi cha pili, Misri wakaweza kurudisha mabao yote ndani ya dakika moja tu pale Shawky, anaechezea Middlesbrough, kufunga bao la pili dakika ya 54 na Zidan kurudisha la 3 dakika moja baadae.
Huku wengi wakiamini ngoma droo ndipo kizaazaa kwenye goli la Misri kufuatia kona kikamfanya Beki Elmohamadi kuuzuia mpira uliokuwa unatinga wavuni kwa mkono na Refa Howard Webb wa England hakubabaika na akamtwanga Kadi Nyekundu na kuamuru ipigwe penalti aliyofunga Kaka bao la 4.
VIKOSI:
Brazil: Julio Cesar, Lucio, Juan, Felipe Melo, Kleber, Elano, Gilberto Silva, Luis Fabiano, Kaka, Robinho, Dani Alves.
AKIBA: Maicon, Victor, Luisao, Miranda, A. Santos, Ramires, Julio Baptista, Kleberson, Pato, Nilmar, Gomes, Josue.
Egypt: El Hadary, A. Said, Hani, A. Fathi, Hosni, Zidan, M. Shawky, A. Hassan, Wail gomaa, Abo Terika.
AKIBA: M. Fathalla, A. Elmohamadi, A. Khairy, A. Eid, M. Homas, A. Tawfik, A. Farag, Wahid, A. Abdelghani, Abo Grusha, A. Raouf, M. Sobhi
REFA: Howard Webb [England]

SAA 3 NA NUSU USIKU [BONGO TAIMU] NI USA v ITALY
LIGI KUU England kuanza Agosti 15, Ratiba kutoka Jumatano!!!!
Ule uhondo, utamu, mashamushamu, mijadala, ngonjera, mabishano na hata masumbwi yanayoletwa na starehe kubwa ya LIGI KUU ENGLAND kwa Wadau wengi yataanza kuonekana kwenye kila kijiwe kuanzia tarehe 15 Agosti 2009 pale msimu mpya wa mwaka 2009/10 utakapoanza.
Msimu huu utamalizika tarehe 9 Mei 2010.
Na kama kawaida Msimu mpya hutanguliwa na ile mechi ya Fungua Pazia ambayo huchezwa wiki moja kabla msimu kuanza kwa kugombea NGAO YA HISANI kati ya Bingwa wa LIGI KUU na Bingwa wa Kombe la FA.
Kwa hivyo, Manchester United, kama Bingwa wa LIGI KUU, atachuana na Chelsea, anaeshikilia Kombe la FA tarehe 9 Agosti 2009 Uwanjani Wembley mjini London.
Ratiba ya msimu huu mpya wa 2009/10 itatolewa rasmi Jumatano tarehe 17 Juni 2009.
Uandaaji wa ratiba hii, huku ukisaidiwa na teknolojia ya kisasa kabisa ya kutumia kompyuta , umechukua karibu mwezi mzima na ulianza tu mara baada ya kujulikana ni Timu zipi zimepanda Daraja kuingia Ligi Kuu hasa ukizingatia mbali ya Timu 2 zilizopanda Daraja moja kwa moja kwa kumaliza nafasi za kwanza na za pili, Timu hizo zikiwa ni Wolverhampton Wanderers na Birmingham, Timu ya 3 kupanda Daraja ilikuwa kwenye kinyanga’nyiro maalum kilichoshirikisha Timu zilizoshika nafasi ya 3, 4, 5 na 6 ili kupata Timu moja na Burnley ikaibuka kidedea.
Baada ya hapo, Wasimamizi wa Ligi Kuu na wale wa Ligi za Chini ikabidi wakutane ili wapambanue Timu zinazotoka maeneo mamoja, hata kama wako Madaraja tofauti, wote hawachezi nyumbani siku moja.

Hii ni kwa sababu ya kiusalama na kuzuia misongamano.
Hivyo, Timu kama vile Aston Villa na Wolverhampton walio Ligi Kuu wanaweza kupangiwa kucheza nyumbani na wenzao wa eneo moja Birmingham City na West Brom Albion, iliyo Daraja la Chini, lazima wacheze ugenini.
Sababu nyingine zinazozingatiwa katika upangaji ratiba ni kama:
-Klabu hazipangiwi, bila sababu maalum, mechi zaidi ya mbili mfululizo za nyumbani tupu au ugenini tupu.
-Mwanzoni mwa ligi na mwishoni mwa ligi ni lazima Klabu zicheze kwa mpangilio wa mechi moja nyumbani na inayofuata ugenini ili kuleta usawa na ushindani bora.
-Klabu inayocheza ugenini siku ya Krismasi lazima iwe nyumbani siku ya Mwaka mpya au kinyume chake. Katika siku hizo za Sikukuu mechi za Wapinzani wa Jadi, kama vile Man U v Liverpool, Liverpool v Everton, Man U v Man City nk., hazipangwi.
Mbali ya vitu vya msingi kama hivyo Polisi na Viongozi wa Miji ya kila Klabu hushirikishwa ili kutoa michango yao na maoni na kitu kikubwa, mara nyingi, kwa sababu ya kiusalama, Bigi Mechi, kama vile Man U v Liverpool, huchezwa mchana kweupe jua likiwa ‘utosini’ kwa sababu za kiusalama.

Klabu za Spain kuendelea 'kupora' England???
  • Alonso, Mascherano kuhama?

  • Fabregas kurudi 'nyumbani' Barca?
Wakati Cristiano Ronaldo yuko njiani kutimiza ‘ndoto yake’ ya kucheza Spain Klabuni Real Madrid, Klabu nyingine za Ligi Kuu England zimetangaza vita ya kujihami ili wasiporwe Mastaa wao na Klabu za Spain hasa Real Madrid na Barcelona.
Liverpool imebidi itangaze waziwazi Xabi Alonso na Javier Mascherano hawauzwi kwa bei yeyote ile baada ya kuibuka habari nzito kutoka Spain kuwa na wao wako njiani kuhama Anfield kwenda Spain.
Mchezaji wa Kimataifa wa Argentina, Mascherano, inasemekana anapata shinikizo kubwa kutoka kwa Mkewe wahamie Spain na hasa Barcelona wakati Alonso anaunganishwa na Real Madrid huku Rais wa Real Florentino Perez akionyesha kila dalili Alonso yuko kwenye listi yake ya ‘manunuzi’.
Taarifa hizo za kuhama kwa Alonso na Mascherano zimezagaa mno kiasi Klabu ya Liverpool imebidi itoe taarifa rasmi kwenye tovuti yake inayosema: ‘Ingawa kuna taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kuhusu uhamisho wa Xabi Alonso na Javier Mascherano, Liverpool haijapokea ombi lolote rasmi au ofa yeyote kutoka Klabu yeyote kuhusu Wachezaji hao. Hata hivyo wote hawauzwi na Liverpool pia haina nia ya kuchukua Mchezaji yeyote kutoka Spain.’
Nae Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, amedokeza kuwa endapo Pep Guardiola, Meneja wa Barcelona, atamtafuta yeye basi atachukulia hilo kama kitu ‘spesho!’
Hata hivyo, Fabregas pia amedokeza kuwa kwa sababu yeye ni Nahodha wa Arsenal ni jukumu lake kuhakikisha Klabu yake inatwaa Vikombe.
Kauli hizi za utata zinaendelea kuwachanganya Wadau na kuzipa uzito taarifa kuwa Fabregas nae yuko njiani kurudi Barcelona Klabu aliyoanzia tangu kiwa kijana mdogo sana.
Spain 5 New Zealand 0
Mabao matatu ya Straika wa Liverpool, Fernando Torres, yaliyofungwa ndani ya dakika 20 yamewawezesha Mabingwa wa Ulaya Spain kuirarua New Zealand kwa mabao 5-0.
Cesc Fabregas wa Arsenal akafunga bao la 4 na David Villa akapachika bao la 5.
VIKOSI:
New Zealand:
Moss, Lochhead, Vicelich, Mulligan, Boyens, Elliott, Brown, Bertos, Smeltz, Killen, Brockie. Akiba: Paston, Bannatyne, Scott, Oughton, Sigmund, Barron, Christie, James, Old, Wood, Bright, Smith.
Spain: Casillas, Sergio Ramos, Puyol, Albiol, Capdevila, Xavi, Fabregas, Riera, Alonso, Villa, Torres. Akiba: Reina, Diego Lopez, Pique, Marchena, Pablo, Busquets, Llorente, Guiza, Arbeloa, Santi Cazorla, Silva, Mata.
Refa: Bonaventure Codija (Benin)
MECHI ZA LEO:
-Jumatatu 15 Juni 2009-06-05
KUNDI B
Brazil v Egypt [saa 11 jioni]
USA v Italy [saa 3 na nusu usiku]

Sunday 14 June 2009

Afrika Kusini 0 Iraq 0
Katika mechi ya ufunguzi ya Mashindano ya kugombea Kombe la Mabara la FIFA, Wenyeji Afrika Kusini leo wametoka sare ya 0-0 na Mabingwa wa Asia Iraq katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Ellis Park, mjini Johannesburg.
Timu hizi zipo KUNDI A pamoja na Spain na New Zealand ambao watacheza baadae leo kuanzia saa 3 na nusu usiku, saa za bongo, kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng huko Rustenburg.
VIKOSI:
AFRIKA KUSINI: KHUNE, GAXA, MASILELA, MOKOENA, MHLONGO, SIBAYA, MODISE, DIKGACOI, BOOTH, PARKER, FANTENI.
IRAQ: MOHAMMED K., MOHAMMED ALI, BASIM, FAREED, NASHAT, IMAD, YOUNUS, KARRAR, SALAM, ALI HUSSEIN, MAHDI
VIDIC ASEMA SING’OKI MAN U NG’O!!!!
Beki wa Manchester United Nemanja Vidic ametupilia mbali uvumi kwamba anaelekea Spain kujiunga na Real Madrid au Barcelona kwa kutamka wazi wazi kuwa hana nia ya kuhama kwenda kokote.
Vidic ametamka: ‘Nina furaha hapa na msimu ujao tunaanza upya! Sina nia ya kwenda kokote!’
Vidic amesistiza kuwa msimu ujao Manchester United inataka kuweka historia mpya kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya 4 mfululizo.
REFA WA LIGI KUU ASTAAFU!!!
Rob Styles, mmoja wa Marefa wa Ligi Kuu England ambae siku zote utata humwandama kila anapochezesha mechi, amestaafu kuwa Refa na habari hizi zimethibitishwa na Bodi ya Marefa wa Kulipwa.
Rob Styles, mwenye umri wa miaka 45, amekuwa akiandamwa na malalamiko mengi kutoka Klabu za Ligi Kuu kutokana na maamuzi yake yenye utata.
Msimu uliokwisha Mameneja kadhaa walilalamika na Gary Megson wa Bolton Wanderers alipiga kelele mno pale Rob Styles alipoipa Manchester United penalti baada ya Jlloyd Samuel wa Bolton kuucheza mpira kihalali kabisa na Styles akaamua alimchezea faulo Ronaldo wakati hakumgusa.
Katika mechi nyingine inadaiwa aliipa Chelsea penalti yenye utata walipocheza na Liverpool mwanzoni mwa msimu wa 2007/8.
Inadaiwa lawama hizo za mara kwa mara pamoja na kutopewa mechi kubwa kuchezesha kumemfanya akate tamaa na kuamua kustaafu. Mechi yake pekee kubwa aliyochezesha ni Fainali ya Kombe la FA mwaka 2005.
LEO NI MABARA BONDENI!!
South Africa v Iraq
KUNDI A, KIWANJA: Ellis Park, Johannesburg SAA: 11 JIONI [BONGO]
Wenyeji, Afrika Kusini, wakiongozwa na Nahodha Aaron Mokoena aliyekuwa Blackburn Rovers lakini msimu ujao atachezea Portsmouth watafungua dimba na Mabingwa wa Asia Iraq.
Kikosi cha Afrika Kusini kina Wachezaji Wachezaji wengine wanaochezea Ligi Kuu England ambao wanategemewa kuanza hivi leo nao ni Steven Piennaar wa Everton na Mchezaji mpya wa Blackburn Rovers Elrio van Heerden.
Kikosi cha Iraq inasemekana kipo kamili bila majeruhi na ni pamoja Kiungo Nashat Akram ambae amenunuliwa na FC Twente ya Uholanzi na ataonekana rasmi msimu ujao.
Mchezaji wao mwingine ambae ameshawahi kucheza Ulaya ni Hawar Mulla Mohammed.
Kwa Afrika Kusini hii ni nafasi nzuri sana kujizoeza na mikimiki ya Kombe la Dunia ambalo mwakani wao ni Wenyeji. Meneja wa Afrika Kusini ni Mbrazil Joel Santana.
Pamoja na Iraq, Afrika Kusini wako Kundi moja na Spain na New Zealand.
Iraq wameingia Mashindano haya kwa sababu ni Mabingwa wa Asia lakini kwa mwaka mmoja Timu imekuwa ikisuasua na hawajashinda mechi yeyote kwa mwaka mzima sasa na ni hivi karibuni tu ndio wameteua Kocha kutoka Serbia, Bora Milutinovic, ambae amewahi kusimamia Nchi 5 tofauti kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Afrika Kusini na Iraq hawajahi kukutana hata mara moja. Kwa Afrika Kusini hii ni mara ya pili kushiriki Kombe la Mabara mara ya kwanza ikiwa mwaka 1997 walipotolewa hatua ya Makundi baada ya kutoka suluhu mechi moja na kufungwa 2.
Refa: Hany Abu Rida (Egypt)
Wasaidizi: Karoly Torok (Hungary), Vincent Monnier (Switzerland)
Spain v New Zealand
KUNDI A, KIWANJA: Royal Bafokeng Stadium, Rustenburg SAA 3 NA NUSU USIKU [BONGO]
Mabingwa wa Ulaya, Spain, ambayo ndio Timu nambari Wani kwa ubora kwenye listi ya FIFA wanaingia uwanjani kupambana na Mabingwa wa Nchi za Baharini [Oceania] New Zealand huku Spain wakiwakosa nyota Andres Iniesta na Marcos Senna ambao ni majeruhi.
Lakini Mastaa wao wengine waliokuwa hatihati kutoonekana kwa maumivu sasa wamepona na wanategemewa kucheza. Nao ni kama Carles Puyol, Sergio Ramos, David Silva, Santi Carzola, Gerard Pique na Sergi Busquets.
New Zealand watamkosa Nahodha wao Ryan Nelsen, anaechezea Blackburn Rovers, aliechanika musuli ya mguu. Hata hivyo Mchezaji wa zamani wa Fulham, Simon Elliott na yule wa Celtic, Chris Killen, watakuwepo.
Spain wako Afrika Kusini chini ya Meneja wa zamani wa Real Madrid, Vicente del Bosque, alieichukua Timu baada ya EURO 2008 na tangu wachukue EURO 2008 hawajafungwa katika mechi 10 sasa.
Hii ni mara kwanza kwa Spain kushiriki Kombe la Mabara.
New Zealand, walio chini ya Meneja Ricki Herbert, ni mara yao ya 3 kucheza Kombe la Mabara lakini hawajahi kuambua hata pointi moja mara zote za nyuma.
Kabla ya kutua Afrika Kusini, Ne Zealand walicheza mechi ya moja ya kirafiki mjini Dar es Salaam, Tanzania na kufungwa 2-1 na Tanzania, kisha wakatoka suluhu na Botswana na wakafungwa na Mabingwa wa Dunia, Italy, 4-3 siku ya Jumatano huko Afrika Kusini.
Spain na New Zealand hawajahi kukutana uso kwa uso ingawa katika Fainali za Kombe la Dunia la Vijana wa chini ya miaka 17, Spain waliikung’uta New Zealand mabao 13-0.
Refa: Coffi Codjia (Benin)
Wasaidizi: Komi Konyoh (Togo), Alexis Fassinou (Benin)
Powered By Blogger