Saturday 18 April 2009

Drogba aipeleka Chelsea Fainali FA CUP: Chelsea 2 Arsenal 1


Makosa makubwa yaliyofanywa na defensi ya Arsenal pale Silvestre, Toure na Kipa wao Fabianski walipojichanganya na kumpa mwanya Didier Drogba kuimiliki pasi ndefu iliyotoka nyuma, na kumpiga chenga Kipa Fabianski alietoka nje ya goli lake, kisha kuutumbukiza mpira kwenye nyavu tupu!!!
Hiyo ilikuwa dakika ya 84 ya mchezo.
Arsenal walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Theo Walcott baada ya kazi nzuri ya Adebayor. Bao hili lifungwa dakika ya 18.
Chelsea walisawazisha kupitia kwa Malouda dakika ya 33.
Hadi mapumziko mechi ilikuwa 1-1.
Sasa Chelsea ametinga Fainali itakayochezwa 30 Mei 2009 na mpinzani wake atapatikana kesho wakati Manchester United atakapokumbana na Everton.
Arsenal: Fabianski, Eboue, Toure, Silvestre, Gibbs, Walcott, Fabregas, Diaby, Denilson, Van Persie, Adebayor. Akiba: Mannone, Nasri, Vela, Ramsey, Song Billong, Arshavin, Bendtner. Chelsea: Cech, Ivanovic, Alex, Terry, Ashley Cole, Ballack, Lampard, Essien, Malouda, Anelka, Drogba. Akiba: Hilario, Carvalho, Di Santo, Mikel, Kalou, Belletti, Mancienne.
Refa: Martin Atkinson (W Yorkshire)

Wolverhamton yapanda daraja na kuingia LIGI KUU England msimu ujao!!

Wolverhampton leo imeifunga QPR bao 1-0 na kujihakikishia Ubingwa wa Daraja la Championship lililo chini tu ya LIGI KUU na pia kuwa Timu ya kwanza kutoka Daraja hilo kupanda kuingia LIGI KUU msimu ujao huku zimebaki mechi mbili ili msimu umalizike. Timu 3 toka Daraja hilo hupanda na tatu kutoka LIGI KUU huporomoka kila msimu. Mara ya mwisho Wolverhampton, au Wolves kama wanavyojulikana kwa kifupi, kuchezea LIGI KUU ilikuwa mwaka 2004.

MATOKEO LIGI KUU England leo:
Aston Villa 1-1 West Ham
Middlesbrough 0-0 Fulham
Portsmouth 1-0 Bolton
Stoke 1-0 Blackburn
Sunderland 1-0 Hull

Arsenal v Chelsea

Leo saa moja na robo saa za bongo, Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la FA itachezwa mjini London Uwanja wa Wembley kati ya Arsenal na Chelsea.
Nusu Fainali ya pili itachezwa kesho kati ya Manchester United na Everton pia Uwanjani Wembley.
Fainali ya Kombe hili la FA itafanyika Wembley tarehe 30 Mei 2009.
Timu zote zinakabiliwa na majeruhi kadhaa huku Arsenal wanaonekana wameathirika zaidi kwani watawakosa Kipa Almunia, Sagna, Clichy, Gibbs na Gallas.
Chelsea nao watamkosa Deco ingawa Nahodha wao John Terry anategemewa kuwepo Uwanjani baada ya kuikosa mechi ya juzi na Liverpool ambayo hakucheza kwa kuwa na Kadi. Mchezaji wao mlinzi wa pembeni, Jose Bosingwa, huenda akawepo baada ya kupona maumivu yaliyomkosesha mechi kadhaa.
Vikosi vinatumainiwa kutokana na:
Arsenal: Fabianski, Eboue, Toure, Silvestre, Gibbs, Arshavin, Song, Fabregas, Walcott, Adebayor, Van Persie, Mannone, Nasri, Diaby, Bendtner, Vela, Eduardo, Denilson, Ramsey.
Chelsea: Cech, Hilario, Belletti, Alex, Ivanovic, Carvalho, Terry, Mancienne, A Cole, Lampard, Ballack, Obi, Kalou, Essien, Malouda, Di Santo, Anelka, Quaresma, Stoch, Drogba
Refa atakuwa: Martin Atkinson

Ferguson amuunga mkono Allardyce kumshutumu Benitez!!!! Wamwita 'kiburi' na mwenye 'dharau' kubwa!!!!

Meneja wa Blackburn Rovers, Sam Allardyce, ametoa shutuma kali kuhusiana na vitendo vya Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, ambae alinaswa na kamera kwenya mechi kati ya Liverpool na Blackburn ya wiki iliyopita ambayo Liverpool walishinda 4-0 akitoa ishara za mikono kwenye dakika ya 33 mara baada ya Fernando Torres kufunga bao la pili kuashiria Blackburn 'wamekwisha'!!!

'Ni dharau kubwa kwangu na Timu yote ya Blackburn!' Sam Allardyce alidai. 'Inasikitisha na kukera! Ndio tulifungwa na Timu Bora Liverpool lakini kufanya kitendo kile ni dharau kubwa sana!
Allardyce alisema baada ya mechi hiyo iliyochezwa Anfield nyumbani kwa Liverpool alikwenda kwenye ukumbi wa Klabu hiyo ili apate mvinyo na Benitez kama ilivyo desturi kwenye LIGI KUU England kuwa Mameneja hukutana baada ya mechi lakini Benitez hakutokea na badala yake msaidizi wake Sammy Lee ndie alikuwepo.
Allardyce akazidi kusikitika: 'Hakutokea na hakujali hata kutuma ujumbe kwa nini hakuwepo wakati yeye ndio mwenyeji! Hii inadhihirisha yeye ni mtu wa aina gani!!'
Nae Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, ambae siku za hivi karibuni amekuwa akiandamwa na mashambulizi kutoka kwa Benitez, amemuunga mkono Sam Allardyce.
Ferguson alimponda Benitez kwa kusema: 'Huyu Benitez ameiita Everton ambayo tunacheza nayo Wembley Jumapili Nusu Fainali ya FA Cup 'klabu ndogo'!! Everton ni timu kubwa!!! Hiki ni kiburi!! Lakini huwezi kuisamehe dharau!! Walipowafunga Blackburn bao la pili zile ishara zake ni dharau kubwa!! Sidhani Sam Allardyce anastahili kufanyiwa vitendo hivyo!! Allardyce amefanya mambo makubwa kwenye LMA [League Managers Association: Chama cha Mameneja wa Ligi]'

Moyes wa Everton astuka uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha Nusu Fainali ya FA CUP dhidi ya Man U!!!

Meneja wa Everton, David Moyes, ambayo klabu yake inashuka Wembley Jumapili kupambana na Manchester United kwenye Nusu Fainali ya Kombe la FA, amehoji uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha pambano hilo.
Awali Refa Steve Bennet ndie alipangwa kuwa Mwamuzi laki ikabidi ajitoe kwa kuwa ni mgonjwa na uteuzi wa Mike Riley haukumfurahisha David Moyes ambae ashawahi kumlaumu Riley kwa kuipendelea Man U pale mwaka 2003 kwenye mechi ya mwisho kabisa ya LIGI KUU alipoipa Man U penalti iliyoiua Everton na kuwakosesha nafasi ya kucheza UEFA CUP msimu uliofuata.
Moyes anasema: 'Kuna Mwandishi alinihoji ikiwa mie nadhani Mike Riley ni shabiki wa Man U, nadhani ikiwa ni hivyo basi ni jukumu la FA kushughulikia hilo.'
FA, Chama cha Soka England, kimejibu hoja hizo kwa kutamka Marefa wao wote ni wakweli, hawapendelei na huchezesha kwa haki.
Walisema: 'Mike Riley ni mmoja wa Maarefa wetu wazoefu na wenye uwezo mkubwa. Tuna hakika Jumapili atafanya kazi nzuri'

KESI YA KUTEMA MATE: Fabregas atoa utetezi wake kwa FA

Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, amewasilisha utetezi wake kwa FA, Chama cha Soka cha England, kufuatia tuhuma kutoka Klabu ya Hull City kuwa alimtemea mate Meneja Msaidizi wa Hull, Brian Horton hapo Machi 17 mara baada ya mechi ya FA Cup kati ya Arsenal na Hull ambayo Arsenal walishinda 2-1. Siku hiyo Cesc Fabregas hakucheza kwa kuwa alikuwa majeruhi na ingawa alivaa kiraia alikuwepo kwenye benchi la Timu ya Arsenal.
Brian Horton na Kocha wa viungo wa Hull, Sean Rush, tayari washapeleka ushahidi wao.
FA imekiri kupokea makabrasha yote na wameahidi kutangaza nini kitafuatia hivi karibuni.

LEO NI:
Jumamosi, 18 Aprili 2009 [saa za kibongo]
LIGI KUU ENGLAND
[saa 11 jioni]
Aston Villa v West Ham
Middlesbrough v Fulham
Portsmouth v Bolton
Stoke v Blackburn
Sunderland v Hull City
FA CUP NUSU FAINALI
[saa 1 na robo usiku]
Arsenal v Chelsea

Klabu ya Macedonia FK Pobeda yafungiwa miaka 8 na UEFA kwa kupanga matokeo!!! Rais wake na Mchezaji mmoja wala kifungo cha maisha!!!!

UEFA imeifungia Klabu ya Macedonia, FK Pobeda, kwa miaka minane kutoshiriki mashindano yeyote ya UEFA kwa kupatikana na hatia ya kupanga matokeo kwenye mechi zilizochezwa Julai 13 na 21 mwaka 2004 dhidi ya FC Pyunit za UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

UEFA vilevile imemfungia Rais wa Klabu hiyo na Mchezaji wake mmoja maisha. Pia UEFA imeiomba FIFA ihalalishe adhabu zote hizi kuwa za dunia nzima.

Friday 17 April 2009

MECHI ZIJAZO: [saa ni za bongo]

Jumamosi, 18 Aprili 2009

LIGI KUU ENGLAND
[saa 11 jioni]
Aston Villa v West Ham
Middlesbrough v Fulham
Portsmouth v Bolton
Stoke v Blackburn
Sunderland v Hull City
FA CUP NUSU FAINALI
[saa 1 na robo usiku]
Arsenal v Chelsea

Jumapili, 19 Aprili 2009

LIGI KUU ENGLAND
[saa 9 na nusu mchana]
Tottenham v Newcastle
[saa 11 jioni]
Man City v West Brom
FA CUP NUSU FAINALI
[saa 12 jioni]
Man U v Everton

Jumanne, 21 Aprili 2009

LIGI KUU ENGLAND
[saa 4 usiku]
Liverpool v Arsenal

Jumatano, 22 Aprili 2009

LIGI KUU ENGLAND
[saa 4 usiku]
Chelsea v Everton
Man U v Portsmouth

Man City watupwa nje UEFA CUP!!!!!

Manchester City, mbali ya kuwafunga Hamburg ya Ujerummani kwa bao 2-1 hapo jana, walijikuta wakitolewa nje ya Kombe la UEFA kwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa huko Ujerumani wiki iliyopita walifungwa mabao 3-1. Hivyo Man City wameyaaga mashindano hayo kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3. Sasa Hamburg wanaingia Nusu Fainali na watakumbana na Wajerumani wenzao Werder Bremen.

MATOKEO MECHI NYINGINE ZA ROBO FAINALI ZA JANA:

Dynamo Kiev 3 PSG 0 [Kiev anasonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0]

Udinese 3 Werder Bremen 3 [Werder Bremen mshindi kwa jumla ya mabao 6-4]


Marseille 1 Shakhtar Donetsk 2 [Shakhtar Donetsk mshindi kwa bao 4-1]


NUSU FAINALI:

30 Aprili 2009
Dynamo Kiev v Shakhtar Donetsk
Hamburg v Werder Bremen


MARUDIO NI TAREHE 7 MEI 2009


FAINALI TAREHE 20 MEI 2009

Wednesday 15 April 2009

Cristiano Ronaldo awaua Wareno wenzake!!!

Goli linalostahili kufungwa na Mchezaji Bora Duniani lilifungwa na Mchezaji Bora Duniani pale Cristiano Ronaldo alipopiga shuti la umbali wa kama mita 30 kwenye dakika ya 5 na kuipa Timu yake Manchester United ushindi ugenini.
Haijatokea hata siku moja Timu yeyote ya Uingereza kushinda Ureno.
Manchester United, wakiwa na Mchezaji Bora Duniani Ronaldo, walihitaji ushindi ili waingie Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na waliupata ushindi na kutawala mechi yote.

Arsenal Waingia Nusu Fainali kwa kishindo!

Arsenal, wakiwa kwao Emirates Stadium, wamepata ushindi wa kishindo wa bao 3-0 dhidi ya Villareal na sasa watakutana na Mabingwa Watetezi wa Ulaya Manchester United kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

Nusu Fainali nyingine itawakutanisha Chelsea na Barcelona.

RATIBA NI:

28 APRILI 2009

Barcelona v Chelsea

29 APRILI 2009

Man U v Arsenal

5 MEI 2009

Arsenal v Man U

6 MEI 2009

Chelsea v Barcelona
Ferguson: 'Leo Wachezaji lazma waukumbuke ule moto wa 1999!!!'

Wenger: 'Hatuchezi tupate sare leo, tutacheza kutafuta ushindi tu!!!'


Sir Alex Ferguson amewataka Wachezaji wa Manchester United waikumbuke ari na moyo wa ile Timu yake ya mwaka 1999 [pichani] wakati leo wanapoingia Uwanja wa FC Porto uitwao Estadio do Dragao ambao hakuna hata Timu moja toka England iliyowahi kucheza hapo, zikiwamo Arsenal, Liverpool, Chelsea na Man U wenyewe, na kutoka na ushindi. Man U, baada ya kutoka sare 2-2 na FC Porto huko Old Trafford wiki iliyopita, wanahitaji ushindi au sare ya zaidi ya 2-2 ili wasonge mbele na kuingia Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mwaka 1999, Man U ilitoka sare na Juventus Uwanjani kwake Old Trafford na katika mechi ya marudiano huko Turin, Italia ikajikuta iko nyuma kwa bao 2-0 lakini wakiongozwa na Nahodha wao Roy Keane waliibuka kwenye mechi hiyo washindi kwa bao 3-2 na wakaendelea mpaka Fainali ambayo walikuwa nyuma ya Bayern Munich kwa bao 1-0 lakini wakashinda kwenye dakika za majeruhi kwa bao 2-1 na kuwa Mabingwa wa Ulaya [pichani wakiwa na Kombe].
Ferguson anasema: 'Naiamini Timu yangu na naamini tunaweza kucheza kwa juhudi na moyo kama ule wa mwaka 1999!'
FC Porto ambao ndio wenyeji leo watacheza mechi hii huku wakiwa na dosari kubwa baada ya UEFA kuthibitisha kuwa Meneja wa FC Porto, Jesualdo Ferreira, kufungiwa mechi moja na hivyo haruhusiwi kukaa benchi la akiba.
Ferreira amefungiwa baada ya kupatikana na hatia ya kumkashifu Refa kwenye mechi ya nyuma ya mashindano haya wakati Porto ikicheza na Atletico Madrid hapo Februari 24.
Arsenal ambao walitoka suluhu ya 1-1 huko Spain walipocheza na Villareal, leo Uwanjani kwao Emirates wanahitaji sare ya 0-0 ili wasonge mbele lakini Meneja wao, Arsene Wenger, amesema wao siku zote wanacheza kushinda tu na ukitafuta suluhu basi unakaribisha maafa!!
Ingawa Arsenal wana majeruhi wengi wakiwemo Kipa Almunia, Gallas, Clichy na Djourou, Wenger bado anaamini Chipukizi wake watashinda tu.
Wenger anadai: 'Vijana wangu ni washindi!! Hatukati tama! Hata kwenye ligi ingawa tuko nyuma sana lakini bado tuna imani!!'


Wachezaji wa Man U wamejaa kwenye listi ya Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka anaechaguliwa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa [PFA]!!!!


Katika Listi ya mwisho ya Wachezaji watakaopigiwa kura na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa huko England [PFA yaani Professional Footballers Association] kuteua Mchezaji Bora wa mwaka wapo Wachezaji Watano kutoka kwa Mabingwa Manchester United. Wachezaji hao ni Rio Ferdinand, Ryan Giggs, Cristiano Ronaldo, Edwin van der Sar na Nemanja Vidic.
Mchezaji pekee ambae yumo kwenye listi hiyo na hatoki Man U ni Steven Gerrard wa Liverpool.
Uteuzi na Tuzo yenyewe hiyo zitatolewa Aprili 26.
Wale waliomo kwenye listi ya mwisho kugombea Tuzo ya Mchezaji Chipukizi wa mwaka ni Gabriel Agbonlahor [Aston Villa], Rafael Da Silva [Man U], Jonny Evans [Man U], Stephen Ireland [Man City], Aaron Lennon [Tottenham] na Ashley Young [Aston Villa].

Piga, nikupige ya Chelsea na Liverpool yaishia Liverpool chaliiiiiii!!!!!!

Ndani ya ngome yao, uwanjani Stamford Bridge huku wakicheza bila Nahodha wao John Terry aliekuwa na Kadi, Chelsea waliweza kuulinda ushindi wao wa 3-1 walioupata nyumbani kwa Liverpool, Anfield wiki iliyopita, kwa kuweza kutoka suluhu ya mabao 4-4 na hivyo kusonga mbele kuingia Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE kwa jumla ya mabao 7-5 na sasa watapambana na timu ngumu Barcelona ambao jana walitoka dro ya 1-1 na Bayern Munich na hivyo pia kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya kuishinda Bayern Munich 4-0 kwenye mechi ya kwanza. Liverpool, wakicheza bila ya Nahodha wao Steven Gerrard ambae ni majeruhi, waliongoza 2-0 kwa mabao yaliyofungwa na Aurelio dakika ya 19 na lile la penalti ya Alonso dakika ya 28.
Kipindi cha pili mabao ya Drogba dakika ya 52 na Alex dakika ya 57 yaliwafanya Chelsea wasawazishe na dakika ya 76 Lampard akawapa uongozi wa mabao 3-2.
Liverpool wakaibuka na kusawazisha kupitia Lucas [81] na dakika moja baadae Kuyt akawafungia bao la 4 na kuwafanya Liverpool wahitaji bao moja tu ili waingie Nusu Fainali huku mechi ikiwa imebakiza dakika 8 kwisha.
Lakini Frank Lampard akawagalagaza aliposawazisha dakika ya 89 na mechi ya piga nikupige ikaisha kwa mabao 4-4 huku Chelsea wakitoka kidedea kwa kuingia Nusu Fainali.

Leo ni zamu ya Man U huko Ureno na Arsenal nyumbani Emirates Stadium.


Leo usiku Man U, Mabingwa watetezi wa Kombe hili la UEFA CHAMPIONS LEAGUE wanashuka Estadio do Dragao kutafuta ushindi au angalau suluhu ya 3-3 ili waingie Nusu Fainali wataporudiana na wenyeji wao FC Porto ya Ureno.
Katika mechi ya kwanza huko Old Trafford, Timu hizi zilitoka suluhu 2-2.
Man U wameongezewa nguvu baada ya kutangazwa Mlinzi wao mahiri Rio Ferdinand ambae hajacheza mechi kadhaa kwa kuwa alikuwa majeruhi sasa yuko fiti na leo ataingia dimbani.
Nao Arsenal, wakiwa nyumbani Emirates Stadium, wana nafasi nzuri ya kusonga mbele hasa baada ya kutoka suluhu ugenini ya bao 1-1 na Villareal huko Spain wiki iliyopita.
Arsenal, ingawa watawakosa Johan Djourou, Gael Clichy na William Gallas walioumia, watanufaika sana kwani Villareal wataikosa injini yao ya kwenye kiungo Marcos Senna ambae ameumia na ambae ndie alikuwa Mfungaji wa bao la Villareal timu hizi zilipocheza wiki iliyopita
.

Tuesday 14 April 2009

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Marudiano leo ni Chelsea v Liverpool na Bayern Munich v Barcelona!!!!

Leo usiku, saa 3 dakika 45 saa za bongo, Chelsea, akiwa nyumbani Stamford Bridge, atawakaribisha Liverpool huku akiulinda ushindi wake wa ugenini alioupata huko Anfield wa bao 3-1. Ili Liverpool asonge mbele Nusu Fainali itayochezwa Aprili 28 ni lazima ashinde mabao si chini ya 3-0.
Mechi nyingine ya marudiano leo ni ile itakayochezwa Ujerumani kati ya Bercelona na Bayern Munich. Kwenye mechi ya kwanza Barcelona alishinda mabao 4-0.
Washindi wa mechi za leo watapambana Nusu Fainali hapo tarehe 28 Aprili 2009 kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Kesho usiku ni marudio kati ya FC Porto na Manchester United huko Ureno na Arsenal v Villareal mjini London, Emirates Stadium, nyumbani kwa Arsenal.

Sunday 12 April 2009

LIGI KUU England yaingia patamu!!!

Man U aongoza kwa pointi 1 mechi 7 mkononi, Liverpool, Chelsea wamfukuza wakiwa na mechi 6 bado!!!

Arsenal ndio mwenye 'Trufu' ya nani Bingwa!!!!!

Vita ya msituni kati ya Ferguson na Benitez yapamba moto!!!!

Mabingwa Watetezi, Manchester United, dhahiri wakionyesha kuyumba ambako kumestaajabisha wadau wengi hasa walipopigwa mechi mbili mfululizo ile na Liverpool na ile na Fulham na kupata ushindi mwembamba mechi mbili zilizofuata baada ya kifaa chao kipya Chipukizi Macheda aka Kiko kuwapa ushindi katika mechi hizo dhidi ya Aston Villa na Sunderland, bado wanang'ng'ania uongozi kwa pointi moja tu ingawa wamecheza mechi moja pungufu.
Nyuma ya Man U wako Liverpool wakifuatiwa karibu na Chelsea huku Arsenal hawako mbali sana.
Zikiwa zimesalia mechi 7 kwa Man U wenye pointi 71, mechi 6 kwa Liverpool wenye pointi 70, mechi 6 kwa Chelsea wakiwa na pointi 67 na Arsenal wana pointi 67 huku nao wamebakiza mechi 6, hakika LIGI KUU England baada ya kutupa uhondo, mashamsham, furaha, karaha, matumaini na kutuumiza mioyo pia, sasa polepole ndio inaelekea ukingoni na rasmi pazia litafungwa Jumapili Mei 24 kwa mechi za mwisho kuchezwa siku hiyo.
Je nani, siku hiyo Mei 24 au kabla ya hapo, atakuwa Bingwa wa msimu 2008/9?
Ni Mwenyezi Mungu tu anajua jibu lake ingawa kuna 'Watabiri' wa kila aina na wana majibu ya kila aina!!
Tunachojua, hili linasapotiwa na Wadau Wataalam, ukiaacha matokeo yasiyo tarajiwa, Arsenal ndio mwenye 'Turufu' ya nani Bingwa.
Katika mechi zake 6 alizobakisha, Arsenal atapambana na Liverpool huko Anfield tarehe 21 Aprili, Arsenal, akiwa nyumbani Emirates, atakwaana na Chelsea hapo Mei 10 na mechi moja kabla ya mechi yao ya mwisho, huko Old Trafford, Arsenal atavaana na Manchester United.
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, anaamini sana wao ndio 'watamtengeneza Bingwa'.
Arsene Wenger anasema: 'Ndio sisi pengine tutaamua nani Bingwa! Lakini kwetu hilo si muhimu, muhimu ni kumkimbia Aston Villa anaetufuata na kisha kuwakaribia Chelsea na Liverpool, halafu tutajua nini kinaendelea! Lakini naamini Man U wana nafasi kubwa kutwaa Ubingwa kwani mechi yao ya mkononi [dhidi ya Portsmouth]wanachezea Old Trafford'
Wakati Arsene Wenger akitoa msimamo wake, 'vita ya msituni' iliyoaanzishwa na Rafa Benitez, Meneja wa Liverpool, huku akielekeza 'mashambulizi; yake kwa Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, ilikuwa ikizidi kupamba moto.
Vita hii ilianza rasmi Januari pale Benitez alipotoa tuhuma kuwa Timu ya Ferguson inapendelewa na Ferguson akajibu kwa ufupi kwa kusema kuna kitu kinamtia hasira Benitez.
Wakati huo, Benitez alikuwa mgonjwa na alifanyiwa operesheni kadhaa kutoa vijiwe kwenye figo zake.
Wiki iliyopita, siku moja kabla Liverpool haijacheza na Chelsea kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Benitez akihojiwa na Waandishi wa Habari kuhusu pambano hilo ambalo hata hivyo Liverpool aliambua kipigo cha 3-1 nyumbani Anfield, aliwashangaza wengi pale alipomrukia Sir Alex Ferguson na kudai Ferguson anaiogopa Liverpool badala ya kuongelea pambano lao na Chelsea.
Baadae, Sir Alex Ferguson akihojiwa, alijibu ni jambo la kushangaza kusikia akizungumziwa yeye badala ya mechi ngumu inayoikabili timu na akaongeza: 'Ukiniuliza swali kuhusu timu nyingine, ntakupa maoni yangu! Hilo si kosa mbona Wenger wiki chache zilizopita alizungumzia Man U na akatoa jibu zuri tu bila kutukandya? Kitu cha ajabu, Rafa Benitez ana mechi ngumu na Chelsea na anahojiwa kuhusu mechi hiyo, yeye anamzungumzia Alex Ferguson! Sikujua kama mimi ni mtu muhimu sana!!'
Baada ya kujibu hivyo, hapo hapo Ferguson akaulizwa kama huwa anamkera, kumchemsha na kumuudhi Benitez kwa makusudi, Ferguson akacheka 'kifisadi' na kujibu: 'Sina jibu.'
Lakini Ferguson akaongeza: 'Nadhani Chelsea ule ushindi mkubwa kwa Liverpool umewapa morali kubwa na wao ndio watakuwa tishio kwetu na si Liverpool. Kwa sasa tumebakisha mechi 7 kwenye ligi. Muhimu ni pointi tu na kumaliza mechi moja baada ya nyingine. Hatuifikirii hiyo mechi moja mkononi.'

Mechi zilizobaki: [Timu inayotajwa kwanza iko nyumbani]:


ARSENAL

21 Aprili: Liverpool v Arsenal

26 Aprili: Arsenal v Middlesbrough

2 Mei: Portsmouth v Arsenal

10 Mei: Arsenal v Chelsea

16 Mei: Man U V Arsenal

24 Mei: Arsenal v Stoke

CHELSEA

22 Aprili: Chelsea v Everton

25 Aprili: West Ham v Chelsea

2 Mei: Chelsea v Fulham

10 Mei: Arsenal v Chelsea

17 Mei: Chelsea v Blackburn

24 Mei: Sunderland v Chelsea

LIVERPOOL

21 Aprili: Liverpool v Arsenal

25 Aprili: Hull v Liverpool

3 Mei: Liverpool v Newcastle

9 Mei: West Ham v Liverpool

17 Mei: West Brom v Liverpool

24 Mei: Liverpool v Tottenham

MAN U

22 Aprili: Man U v Portsmouth

25 Aprili: Man U v Tottenham

3 Mei: Middlesbrough v Man U

10 Mei: Man U v Man City

13 Mei: Wigan v Man U

16 Mei: Man U v Arsenal

24 Mei: Hull v Man U

LIGI KUU LEO Jumapili Aprili 12:

[saa 10 jioni kibongo]

Aston Villa v Everton

[saa 12 dakika 10 kibongo]


Man City v Fulham


Ferguson amsifu Bwana Mudogo Federico Macheda aka Kiko!!!!!

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amemsifu chipukizi wao wa miaka 17 mzawa wa Italia, Federico Macheda, maarufu kama 'Kiko', baada ya mara ya pili mfululizo, ndani ya siku sita tu, akitoka benchi na kuingia uwanjani na kuipa ushindi Man U.

Jana aliingizwa kumbadilisha Berbatov katika dakika ya 74 huku mechi ikiwa Sunderland 1 Man U 1 na baada ya sekunde 46 tu ukiwa ndio mpira wake wa kwanza kuugusa akaipatia Man U bao la pili na la ushindi.
Wiki iliyopita aliingizwa kipindi cha pili na katika dakika za majeruhi huku mechi ikiwa Man U 2 Aston Villa 2, akapachika bao la 3 na la ushindi.
Katika mechi zote hizo mbili, kama matokeo yangebaki suluhu, basi Liverpool angenyakua uongozi wa LIGI KUU England lakini ushujaa wa Macheda aka Kiko umehakikisha Man U anaendelea kuongoza ligi.
Sir Alex Ferguson amesema: 'Huyu kijana ana kitu spesho!! Nilipomwingiza sikumpa maelekezo yeyote maalum! Nilimwambia tu ingia na cheza!!'
Powered By Blogger