Saturday 11 April 2009

Federico 'Kiko' Macheda awapa ushindi tena Man U!!!

Kijana wa miaka 17, Federico Macheda, aka Kiko, kwa mara ya pili mfululizo ameifungia Manchester United bao la ushindi baada ya kuingizwa kipindi cha pili dakika ya 74 kumbadilisha Berbatov na ilimchukua sekunde 46 tangu aingie kufunga bao la pili lililowapa Man U ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Sunderland.
Wiki iliyopita Macheda alifunga bao la 3 na la ushindi kwenye dakika za majeruhi Man U walipoifunga Aston Villa 3-2.
Man U wamerudi tena kileleni mwa LIGI KUU England baada ya uongozi kuchukuliwa na Liverpool kwa masaa kadhaa wakati Liverpool walipoishindilia Blackburn mabao 4-0 kwenye mechi iliyoaanza mapema leo.


MATOKEO MECHI ZINGINE ZA LEO NI:
Chelsea 4 Bolton 3
Middlesbrough 3 Hull 1
Portsmouth 2 West Brom 2
Tottenham 1 West Ham 0
Wigan 1 Arsenal 4
Liverpool 4 Blackburn 0

REFA ADAI KABLA YA MECHI CHELSEA WALIMTAKA ASIWAPE KADI WACHEZAJI WAO!!!

Refa kutoka Denmark, Claus Bo Larsena, aliechezesha pambano la Jumatano iliyopita huko Anfield kati ya Liverpool na Chelsea la Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambalo Chelsea ilishinda mabao 3-1, amedai kwenye Kikao cha kujadili usalama kabla ya mechi hiyo kilichohudhuriwa na Maofisa toka UEFA, Chelsea, Liverpool, Polisi na Waamuzi wa pambano hilo, alistushwa sana pale Afisa mmoja wa Chelsea kumwambia bila kificho 'hawakaribishi ' Wachezaji wao kupewa Kadi za Njano na hivyo kukosa mechi ya marudiano huko Stamford Bridge siku ya Jumanne. Hata hivyo kwenye mechi hiyo Refa Claus Bo Larsen alimtwanga Nahodha wa Chelsea, John Terry, Kadi ya Njano na hivyo ataikosa mechi ya Jumanne.
Wengine wa Chelsea waliokuwa hatarini kuikosa mechi hiyo ya Jumanne endapo wangepata Kadi ni Anelka na Ashley Cole lakini bahati nzuri waliepuka Kadi.
'Sijawahi kuona kitendo kama hicho!' Refa Claus Bo Larsen alisema 'Nimeshawahi kuhudhuria vikao vya aina hivyo zaidi ya 100, haijatokea! Lakini niliwaambia palepale Mchezaji akifanya kosa la Kadi ya Njano basi lazima nitampa Kadi!!'

Thursday 9 April 2009

MATOKEO: Duru la kwanza Robo Fainali UEFA CUP
Hamburg 3-1 Manchester City
PSG 0-0 Dynamo Kiev
Shakhtar Donetsk 2-0 Marseille
Werder Bremen 3-1 Udinese
Marudiano ni wiki ijayo tarehe 16 Aprili 2009.

Gallas kukosa mechi zilizobaki msimu huu!

Beki wa Arsenal, William Gallas, atazikosa mechi zote zilizobaki msimu huu baada ya kuumia goti kwenye mechi ya dro ya 1-1 na Villareal ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Habari hizi zimethibitishwa na Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal.

Gerrard kufanyiwa uchunguzi maumivu yake ya nyonga!

Nahodha na nguzo kubwa ya Liverpool, Steven Gerrard, atafanyiwa uchunguzi baada ya kuumia kwenye mechi waliyofungwa na Chelsea mabao 3-1 kwenye kinyang'anyiro cha UEFA CHAMPIONS LEAGUE na kuna wasiwasi mkubwa huenda akazikosa mechi muhimu zijazo.
Jumamosi, Liverpool wanapambana na Blackburn kwenye mechi muhimu ya LIGI KUU England na Jumanne ijayo wanarudiana na Chelsea kwenye mpambano wa UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

Vidic akiri: 'Tulijisahau!'

Beki wa Mabingwa, Manchester United, Nemanja Vidic, amekiri mwendo mbovu wa Mabingwa hao katika mechi za hivi karibuni umetokana na wao wenyewe kulewa ushindi na kuzichukulia mechi zao kama kitu rahisi hasa watu walipoanza kuwasifu kuwa wana uwezo mkubwa wa kutwaa Mataji matano msimu baada ya tayari kuyatwaa yale ya Ubingwa wa Dunia na Kombe la Carling huku wakiwa kwenye nafasi nzuri kuutwaa Ubingwa wa LIGI KUU, kunyakua Kombe la FA na kuliteka tena Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Man U hivi karibuni walifungwa mechi mbili mfululizo kwenye LIGI KUU, walipigwa na Liverpool 4-1 na Fulham 2-1, kisha wakaokolewa na mtoto wa miaka 17 Federico Macheda alipowapa ushindi wa 3-2 dhidi ya Aston Villa.
Juzi walilazimishwa sare ya 2-2 na FC Porto kwao Old Trafford kwenye mpambano wa duru la kwanza la UEFA CHAMPIONS LEAGUE na sasa Mabingwa hao ama inabidi washinde huko Porto au watoke sare ya zaidi ya bao 2-2 ili waingie Nusu Fainali.

MECHI ZA WIKIENDI ZA LIGI KUU ENGLAND:
Jumamosi, Aprili 11
[saa 8:45 mchana]
Liverpool v Blackburn
[saa 11 jioni]
Chelsea v Bolton
Middlesbrough v Hull City
Portsmouth v West Brom
Sunderland v Man U
Tottenham v West Ham
Wigan v Arsenal
[saa 1:30 usiku]
Stoke City v Newcastle
Jumapili, Aprili 12
[saa 10 jioni]
Aston Villa v Everton
[saa 12;10 jioni]
Man City v Fulham
Liverpool yatolewa utumbo nyumbani Anfield: Liverpool 1 Chelsea 3

Wakiwa nyumbani Anfiled, Liverpool wamejikuta mguu mmoja nje ya kutolewa UEFA CHAMPIONS LEAGUE baada ya kupigwa bao 3-1 na Chelsea.
Marudiano ya timu hizi ni Jumanne ijayo Aprili 14 huko Stamford Bridge kwenye ngome ya Chelsea.
Fernando Torres aliwapa furaha Liverpool dakika ya 6 ya mechi alipofunga bao.
Lakini shujaa asiyetegemewa aliibuka kwa upande wa Chelsea pale Mlinzi Branislav Ivanovic aliposawazisha kwa kichwa dakika ya 39 na kupachika la pili dakika ya 62 kwa kichwa tena.
Kisha Didier Drogba akaweka msumari wa mwisho kwa kufunga bao la 3 dakika ya 67.
Chelsea walipata pigo kwenye mechi hii wakati Nahodha wao John Terry alipopewa Kadi ya Njano na hivyo kumaanisha hawezi kucheza mechi ya marudiano ya wiki ijayo.
Liverpool: Reina, Arbeloa, Carragher, Skrtel, Aurelio (Dossena 75), Kuyt, Lucas (Babel 79), Alonso, Riera (Benayoun 67), Gerrard, Torres.
Akiba hawakucheza: Cavalieri, Hyypia, Agger, Ngog.
Kadi: Aurelio.
Chelsea: Cech, Ivanovic, Terry, Alex, Ashley Cole, Kalou, Ballack, Essien, Lampard, Malouda, Drogba (Anelka 79).
Akiba hawakucheza: Hilario, Carvalho, Belletti, Mancienne, Mikel, Deco.
Kadi: Kalou, Terry.
Watazamaji: 42,543
Refa: Claus Bo Larsen (Denmark).

Barcelona watamu!!!!!
Waichabanga Bayern Munich 4-0!!!!
Ndani ya Uwanja wao Nou Camp, Barcelona waliwapiga bila huruma Bayern Munich 4-0 huku wakicheza soka tamu sana.
Mabao ya Barcelona yalifungwa na Lionel Messi, mabao mawili, Samuel Eto'o na Thierry Henry.
Timu hizi zitarudiana Jumanne ijayo huko Ujerumani.
Vikosi vilikuwa:
Barcelona: Valdes, Dani Alves, Marquez, Pique, Puyol, Xavi, Toure Yaya (Busquets 81), Iniesta, Messi, Eto'o (Bojan 89), Henry (Keita 74).
Akiba hawakucheza: Pinto, Caceres, Gudjohnsen, Sylvinho.
Kadi: Messi, Marquez.
Magoli: Messi 9, Eto'o 12, Messi 38, Henry 43.
Bayern Munich: Butt, Oddo, Demichelis, Breno, Lell, Altintop (Ottl 46), Schweinsteiger, Van Bommel, Ze Roberto (Sosa 76), Ribery, Toni.
Akiba hawakucheza: Rensing, Podolski, Lahm, Borowski, Badstuber.
Kadi: Lell, Demichelis.
Watazamaji: 97,000
Refa: Howard Webb (England).

LEO ROBO FAINALI UEFA CUP: Hamburg v Man City

Timu pekee toka England iliyobaki kwenye UEFA CUP ni Man City na leo ipo ugenini huko Ujerumani ikipambana kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali na Timu ya Ujerumani Hamburg.
Marudio ya mechi hii yatafanyika wiki ijayo nyumbani kwa Man City, City of Manchester Stadium, tarehe 16 Aprili.
Mechi nyingine za duru la kwanza la Robo Fainali ni:
PSG v Dynamo Kiev
Shakhtar Donetsk v Marseille
Werder Bremen v Udinese

Wednesday 8 April 2009

Man U wabanwa kwao kwa sare ya 2-2, Arsenal wanufaika ugenini kwa sare ya 1-1!!!

Mabingwa watetezi wa Ulaya, Manchester United, wakicheza soka bovu kabisa nyumbani Ol Trafford wametoka suluhu 2-2 na FC Porto ya Ureno.
Man U sasa lazima washinde mechi ya marudiano huko Ureno wiki ijayo Jumatano tarehe 15 Aprili.
Na Arsenal waliokuwa ugenini huko Spain wakipambana na Villareal wametoka suluhu ya 1-1.
Matokeo haya si mabaya sana kwa Arsenal kwani wakiepuka kufungwa au suluhu ya zaidi ya 1-1 basi watasonga mbele.

Tuesday 7 April 2009

Badala ya Benitez kuzungumzia pambano lake na Chelsea kesho, amvaa Ferguson!!!!!
Gerrard, Drogba wako fiti kuvaana kesho!!!!

Katika hali ya kushangaza, Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, akihojiwa kuhusu pambano la kesho la UEFA CHAMPIONS LEAGUE la Robo Fainali kati ya Liverpool na Chelsea huko Anfield, alimvaa Sir Alex Ferguson na kumuita 'mwoga!'
Wiki iliyopita Sir Alex Ferguson alitamka kuwa Timu itakayobwagwa kati ya Liverpool na Chelsea itabaki ikielekeza macho yake kwenye LIGI KUU England tu na hivyo ndio itakuwa tishio kwa Manchester United.
Wakati huohuo, Steven Gerrard wa Liverpool na Didier Drogba wa Chelsea wametangazwa kuwa fiti kwa mechi hiyo ya kesho baada ya kuwa hatihati kuikosa mechi ya hiyo kwa kuwa majeruhi.
Hata hivyo Liverpool watamkosa Kiungo wao mahiri Javier Mascherano ambae haruhusiwi kucheza baada ya kulambwa Kadi kwenye pambano lao lililopita na Real Madrid.

Wakati Lazio yalalama, Baba wa Nyota Mpya Macheda atetea uamuzi wao wa kuhamia Manchester United

Pasquale Macheda [34], Baba Mzazi wa Kijana wa miaka 17 Federico Macheda alieibuka kuwa Nyota Mpya baada ya kuwapa Manchester United ushindi kwenye mechi yao ya LIGI KUU na Aston Villa ikiwa ni mechi yake ya kwanza kabisa kuichezea, ametetea uamuzi wao wa kifamilia kuhamia Manchester ili kumpa nafasi mtoto wao kuichezea Manchester United.
Baada ya Macheda kuibuka kuwa lulu siku ya Jumapili, Klabu ya Lazio ilinung'unika kwa kumpoteza Macheda aliekuwa Mchezaji wao kwenye Timu yao ya Vijana.
Rais wa Lazio, Claudio Lotito, aliitaka Italia ibadilishe sheria zake inayozuia Vijana wa chini ya miaka 18 kusaini mkataba na Klabu.
Manchester United ilimnyakua Macheda kutoka Lazio Septemba 2007 wakati akiwa na miaka 16 na kumsainisha mkataba wa kuwa Mchezaji mwanafunzi kwenye Chuo chao cha Soka.
Macheda alisaini mkataba kamili Mwaka jana, mwezi Agosti, alipotimiza miaka 17, wa kuwa Mchezaji wa Kulipwa wa Man U na akaingizwa kwenye Timu ya Akiba.
Baba huyo wa Nyota Macheda anasema: 'Tunaishkuru Lazio kwa kumfunza vyema. Ilikuwa ngumu kuikataa ofa ya Manchester United.'
Baba huyo alihangaika sana wakati akiwa Italia ili kumpa nafasi mwanawe Federico Macheda nafasi ya kuendeleza ndoto yake ya kuwa Staa wa Soka.
Ilibidi afanye kazi zaidi ya mbili kwa siku, sokoni na nyingine usiku kucha, ili kugharamia ndoto ya mwanawe, na kuendesha gari kwa saa zaidi ya moja ili kumfikisha mwanawe Uwanja wa Lazio kwa mazoezi na baadae kwenda kumchukua baada ya mazoezi.
Macheda aliposaini na Manchester United mwaka 2007, familia yake ikahamia Manchester na kupewa nyumba jirani na Uwanja wa Carrington ambako Man U hufanyia mazoezi.
Siku ya mechi ya juzi na Aston Villa, Pasquale Macheda, mkewe Loredana na Simone, mtoto wao wa kiume, mdogo wa Federico, walikuwepo Old Trafford wakishuhudia historia ikiwekwa.
Baada ya kufunga bao hilo la ushindi, Federico alikimbia hadi walipoketi familia yake na kumkumbatia Baba yake aliyekuwa akilia kwa furaha.
Kitendo hicho cha kutoka nje ya uwanja kilimafanya Macheda apewe Kadi ya Njano na Refa Mike Riley.
Ingawa Lazio wanalalamika kupokonywa Macheda, mtu pekee aliyekuwa na furaha kwa mafanikio ya Kijana huyo ni Kocha wake wa zamani wa Timu ya Vijana hapo Lazio, Stefano Avincola, aliesema: 'Nimefurahi sana kwa ajili yake! Tulijaribu kuwashawishi abaki Lazio lakini tunaelewa nini kimewapeleka Man U. Familia ya Macheda ni waungwana kwani walikuja kutushkuru kwa kumlea vizuri Federico.'

Monday 6 April 2009

ULAYA kuwaka moto kesho na Jumatano!!

UEFA CHAMPIONS LEAGUE inaingia hatua ya Robo Fainali hapo kesho usiku na Jumatano.

Kesho Jumanne, saa 3 dakika 45 usiku, Villareal ya Spain watakuwa wenyeji wa Arsenal ambayo itakuwa na pengo kubwa la kumkosa Mshambuliaji wao wa kutegemewa Robin van Persie ambae ni majeruhi.
Nao Mabingwa Watetezi wa Kombe hili, Manchester United, watakuwa nyumbani Old Trafford wakiikaribisha Klabu ya Ureno FC Porto na watawakosa Rio Ferdinand na Dimitar Berbatov walioumia lakini Wachezaji wengine ambao hawakucheza mechi ya jana ya ushindi dhidi ya Aston Villa kina Wayne Rooney, Nemanja Vidic, Paul Scholes na Park wote wamo kwenye Kikosi.
Jumatano usiku, pia saa 3 dakika 45, bongo taimu, kutakuwa na mechi zinazotegemewa kuwa na patashika kubwa pale Barcelona watakapoikaribisha Bayern Munich na nyingine ni ile vita ya Timu za England wakati Liverpool, wakiwa nyumbani Anfield, watakapomenyana na Chelsea ambayo itakuwa na muuaji wao hatari Didier Drogba alieikosa mechi ya LIGI KUU Jumamosi dhidi ya Manchester City kwa kuwa na maumivu.
Mechi hizi zitarudiwa wiki ijayo.
Dunia nzima inajiuliza Federico Macheda, kijana mdogo shujaa mpya wa Man U , ni nani?
Mwenyewe asema: 'Ni ndoto!!'

Kijana wa miaka 17 mzaliwa wa Rome, Italia, Federico Macheda, ambae huchezea Timu ya Akiba ya Man U na jana ikiwa ni mara ya kwanza kabisa kuchezea Kikosi cha kwanza, alijiandikia historia kwa kuifungia Man U bao la ushindi dhidi ya Aston Villa katika dakika za majeruhi na kuwarusha Mabingwa hao hadi kileleni mwa LIGI KUU England.
Leo dunia nzima ya soka inajiuliza: Macheda ni nani na katokea wapi?
Mwenyewe Federico Macheda anaelezea: 'Nilikuwa nikiiota siku kama hii!! Niligeuka na kupiga shuti kisha nikashangilia na kuikimbilia familia yangu!!'
Macheda alienda kwa Watazamaji kumkumbatia Baba yake Mzazi aliekuwa akibubujikwa na machozi ya furaha.
Kitendo hicho kilifanya Macheda apewe Kadi ya Njano na Refa Mike Riley.
Meneja wake, Sir Alex Ferguson, alisema: 'Nilimpa hongera! Nikamwambia asivimbe kichwa ila aongeze juhudi. Kuchezesha kikosi kile na chipukizi wale ni kucheza bahati nasibu! Ni hatari lakini ni lazima ujaribu bahati wakati mwingine! Hatukujihami vizuri lakini siku zote tunajiamini tuna uwezo wa kufunga magoli!'
Baada ya mechi hiyo na Aston Villa ambayo mbali ya kuwa shujaa wa Man U, Wadhamini rasmi wa LIGI KUU England, Kampuni ya Barclays, walimteua kuwa ndie MCHEZAJI BORA WA MECHI.
Je ni nani Macheda?
Huko Old Trafford huitwa 'Kiko' ikiwa ndio a.k.a yake.
Macheda alizaliwa Rome mwaka 1991 na kuanza soka lake akiwa na Timu ya Watoto ya Klabu ya Lazio ya Italia na angeendelea kubaki hapo lakini sheria za Italia haziruhusu kumsaini mtu aliye chini ya miaka 18 kuwa Mchezaji wa Kulipwa na ndipo Man U wakamnyakua toka Lazio mwaka 2007 akiwa na miaka 16 na kumsainisha mkataba wa kuwa mwanafunzi kwenye Chuo chao cha Soka.
Aliposaini mkataba huo Familia yake , yaani Baba, Mama na mdogo wake, wote wakahamia Manchester.
Mwaka jana, mwezi Agosti, alipotimiza miaka 17, akasaini mkataba wa kuwa Mchezaji wa Kulipwa wa Man U.
Macheda akiwa kwenye Kikosi cha Timu ya Akiba kilicho chini ya usimamizi wa Nyota wa zamani Ole Gunnar Solskjaer ameshafunga goli nane kwenye mechi nane alizocheza yakiwemo magoli matatu kwenye mechi dhidi ya Timu ya Akiba ya Newcastle mwezi uliopita.
Kijana huyo kwa sasa yuko kwenye Kikosi rasmi cha Wachezaji 25 kilichosajiliwa UEFA kwa mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Macheda pia yumo kwenye Timu ya Taifa ya Italia ya Vijana wa chini ya umri wa miaka 18.

Sunday 5 April 2009

Man U warudi kileleni, Kijana wa miaka 17 awapa ushindi!!!!

Wakichezesha kikosi hafifu bila Wachezaji wao vigogo kama vile Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Paul Scholes, Wayne Rooney na Dimitar Berbatov waliokosekana kwa ama kuwa na Kadi au kuwa majeruhi, Mabingwa Man U walijikuta wakichungulia kipigo kutoka kwa Aston Villa uwanjani kwao Old Trafford huku zikiwa zimesalia dakika 10 tu wakati walipokuwa nyuma kwa mabao 2-1.
Lakini Mchezaji Bora Duniani, Ronaldo, akawasawazishia na katika dakika za majeruhi, dakika ya 92, Mchezaji wa Timu ya Akiba ambae hajawahi kucheza Kikosi cha kwanza hata mara moja, kijana chipukizi wa miaka 17 Federico Macheda, aliibuka ndie shujaa mpya wa Manchester United pale alipofunga bao tamu sana baada ya kupata pasi murua toka kwa Giggs na kumhadaa beki kisha akapiga shuti lililopinda na kumuacha Kipa wa zamani wa Liverpool Brad Friedel akidaka hewa na kugalagala chini.
Kijana Federico Macheda alishangilia bao hili kwa kukimbia walipokaa familia yake na kumkumbatia Baba yake Mzazi aliekuwa akitokwa machozi kwa furaha.
Refa Mike Riley alimpa Macheda Kadi ya Njano kwa kwenda kwa mashabiki kushangilia.
Kwa ushindi wa leo, Man U wamerudi kileleni wakiwa na pointi 68 kwa mechi 30, Liverpool wa pili pointi 67 mechi 31, wa tatu ni Chelsea mechi 31 na pointi 64 na Arsenal waliocheza mechi 31 pia ni wa nne wakiwa na pointi 58.
Vikosi vilikuwa:
Man Utd: Van der Sar, Neville, O'Shea, Evans, Evra, Nani (Macheda 61), Carrick, Fletcher, Ronaldo, Giggs, Tevez (Welbeck 87).
Akiba hawakucheza: Foster, Park, Gibson, Martin, Eckersley.
Kadi: Macheda.
Goli: Ronaldo 14, 80, Macheda 90.
Aston Villa: Friedel, Luke Young, Cuellar, Davies, Shorey, Milner (Reo-Coker 76), Petrov, Barry, Ashley Young, Carew, Agbonlahor.
Akiba hawakucheza: Guzan, Delfouneso, Knight, Salifou, Gardner, Albrighton.
Kadi: Milner, Ashley Young.
Goli: Carew 30, Agbonlahor 58.
Watazamaji:75,409
Refa: Mike Riley (Yorkshire).
Everton 4 Wigan 0
Everton leo wameikung'uta Wigan mabao 4-0 Uwanjani kwao Goodison Park.
Mabao ya Everton yalifungwa na Jo [ba0 2], Fellaini na Osman.
Powered By Blogger