Saturday 31 January 2009

Man U 1 Everton 0, sasa Mabingwa wako pointi 5 mbele!!
Kesho kimbembe: Liverpool v Chelsea!!!

Goli la penalti la dakika ya 43 la Cristiano Ronaldo baada ya Michael Carrick kuchezewa faulo na Mikel Arteta lawapa Mabingwa Manchester United ushindi wa bao 1-0 na hivyo sasa wanaongoza ligi wakiwa pointi 5 mbele ya Liverpool na Chelsea.
Kesho saa 1 usiku, bongo taimu, Liverpool na Chelsea wanakwaana Uwanja wa Anfield.
Timu zilikuwa:
Man Utd: Van der Sar, Neville, Ferdinand, Vidic, O'Shea, Ronaldo, Carrick, Fletcher, Park, Berbatov, Tevez.
Akiba: Kuszczak, Brown, Giggs, Welbeck, Fabio Da Silva, Gibson, Eckersley.
Everton: Howard, Hibbert, Jagielka, Lescott, Baines, Osman, Arteta, Neville, Pienaar, Fellaini, Cahill.
Akiba: Nash, Yobo, Castillo, Jacobsen, Rodwell, Anichebe, Gosling.
Arsenal butu, Villa wakabwa, Tottenham, Man City na Portsmouth chaliii!!!

Arsenal 0-0 West Ham

Aston Villa 0-0 Wigan

Bolton 3-2 Tottenham

Fulham 3-1 Portsmouth

Hull 2-2 West Brom

Middlesbrough 0-0 Blackburn

Stoke 1-0 Man City

Friday 30 January 2009

Vidic kuikosa mechi ya kwanza na Inter Milan!!

Beki mahiri wa Manchester United, Nemanja Vidic, amefungiwa mechi moja na FIFA baada ya kupewa Kadi Nyekundu kwenye Fainali ya Kombe la Dunia la Klabu kati ya Man U na LDU Quito mwezi Desemba ambayo Man U waliibuka Mabingwa wa Dunia kwa ushindi wa bao 1-0, bao alilofunga Wayne Rooney.
Adhabu hii, ambayo haiwezi kukatiwa rufaa, itasababisha Vidic kuikosa mechi dhidi ya Inter Milan itakayochezwa Februari 24 huko San Siro kwenye kinyang'nyiro cha UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Timu hizo zitarudiana Machi 11, huko Old Trafford nyumbani kwa Man U.
Vidic pia amepigwa faini ya Pauni 2,985.

NANI KASEMA???????

'Kipindi cha pili kilikuwa ni uchizi mtupu na gemu ikiwa ya kichizi huwezi kuidhibiti! Kwa nini ilikuwa ya kichizi? Kwa sababu ilikuwa ya kichizi!!!'
Rafa Benitez, Meneja wa Liverpool aliepata uchizi baada ya kutoka droo 1-1 na Wigan na kuwaacha Man U kileleni!.

'Hii ni Klabu ya Soka iliyojengwa na sijui na nani na na namna gani!! Ni mchanganyiko wa Wachezaji wa kushangaza sana!! Inatisha!!'
Harry Redknapp akiishangaa Timu yake mbovu ya Tottenham aliyoirithi kama Meneja mpya.

'Nadhani kuna watu wanahitaji kwenda Kanisani Jumapili kuungama!!'
Mshambuliaji wa Reading Stephen Hunt akiituhumu Klabu yake kwa kusema uongo kuwa hakuna Timu inayotaka kumnunua.

'Viva Da Silva, Viva Da Silva, wakiwa Uwanjani, humjui Nani ni Nani, Viva Da Silva!'
Mashabiki wa Manchester United wakiimba Old Trafford baada ya kumuona Pacha Mwenza wa Rafael Da Silva aitwae Fabio Da Silva, ambao wamefanana mno na huwezi kuwatofautisha, akicheza mechi yake ya kwanza kwa Timu hiyo dhidi ya Derby County kwenye Kombe la Carling.

'Kaka, popote ulipo,
Umeisikia Man City?
Usiende huko,
Utalia machozi,
Hawajachukua Kikombe Miaka 33'
Mashabiki wa Wigan wakiwaimbia na kuwatambia Manchester City timu zao zilipokutana huku wakimuonya Kaka wa AC Milan na Brazil.
MACHO YAKO KWA Liverpool v Chelsea Jumapili, Mtaalam anena atakaefungwa : 'USIKU MWEMA KWA UBINGWA!!!'

Timu zote za LIGI KUU England zitacheza Jumamosi na Jumapili za Wikiendi hii, lakini ukweli ni kwamba macho ya Washabiki siku ya Jumamosi yatakuwa kwa Mabingwa Manchester United wakiwakaribisha Everton Old Trafford na wengi wanaamini Man U watashinda na kuwa pointi 5 mbele ya Liverpool na Chelsea wanaopambana wenyewe Jumapili huko Anfield, mjini Liverpool.
Mtaalam mmoja anaekubalika vizuri huko England amesema:
'Yeyote kati ya Liverpool au Chelsea akifungwa tu hiyo Jumapili basi atakuwa ametamka 'Usiku Mwema' kwa Ubingwa wa LIGI KUU! Nategemea Man U itaifunga Everton siku ya Jumamosi na hivyo kuwa pointi 5 mbele ya Chelsea na Liverpool. Ni muhimu mmoja ashinde ili awe anaifukuza na kuweka presha kwa Man U lakini atakaefungwa ana kazi kubwa sana ya kupigana na Aston Villa anaekuja kama mbogo kugombea nafasi ya 3! Aahh, Arsenal, naamini wataibuka tu!!'
FAINALI YA UEFA CHAMPIONS LEAGUE 2011 KUFANYIKA WEMBLEY

UEFA imeteua Uwanja wa Wembley, uliopo London huko England, kuchezewa Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya maarufu kama UEFA CHAMPIONS LEAGUE ya mwaka 2011.
Mara ya mwisho kwa Wembley kuchezewa Fainali kama hiyo ilikuwa mwaka 1992 Barcelona ilipoifunga Sampdoria.
Na mara ya mwisho kwa UEFA CHAMPIONS LEAGUE kuchezewa England ilikuwa 2003 wakati Fainali ilipochezwa Old Trafford nyumbani kwa Manchester United.
Uteuzi wa Wembley unafuatia mchuano mkali na Viwanja vingine viwili vilivyokuwa vinataka fursa hiyo na navyo ni kile cha Munich kiitwacho Allianz Arena na kile cha Berlin kiitwacho Olympiastadion.
Hii itakuwa ni mara ya 6 kwa Wembley kuwa mwenyeji wa Fainali za Klabu Bingwa Ulaya nyingine zikiwa ni kama ifuatavyo pamoja na Timu zilizocheza Fainali hizo:
-1992 Barcelona v Sampdoria 1-0
-1978 Liverpool v Club Brugge 1-0
-1971 Ajax v Panathinaikos 2-0
-1968 Man U v Benfica 4-1
-1963 AC Milan v Benfica 2-1
Fainali ya mwaka huu itachezwa mjini Rome kwenye Uwanja uitwao Stadio Olimpico ambao kwa pamoja hutumiwa na Klabu za Serie A huko Italia za AS Roma na Lazio.
Fainali ya mwakani 2010 itchezewa nyumbani kwa Real Madrid Uwanja wa Santiago Bernabeau huko Madrid, Spain.

LIGI KUU: Uhamisho

Zikiwa zimebaki siku mbili ili dirisha la Uhamisho lifungwe hapo tarehe 1 Februari 2009, harakati za kupata Wachezaji dakika za mwisho zimepamba moto huku tetesi zikizagaa kila kona.
Zilizoshika hatamu ni:

Nahodha wa Bolton Nolan kwenda Newcastle

Kevin Nolan [26] ambae ni Nahodha wa Bolton yuko mbioni kukaguliwa afya ili asaini mkataba kuichezea Newcastle.
Habari hizi zimethibitishwa na Garry Megson Meneja wa Bolton.
Nolan amechezea mechi 323 Bolton tangu alipoanza mwaka 1999.

Diouf kutua Blackburn!

Mchezaji machachari wa Senegal, El-Hadji Diouf [28], yuko mbioni kujumuika tena na aliekuwa Meneja wake wa zamani pale walipokuwa wote Bolton, Sam Allardyce, safari hii wakiwa Klabu ya Blackburn, baada ya kufuzu ukaguzi wa afya.
Diouf kwa sasa ni Mchezaji wa Sunderland.

Blackburn wagomea dau la Pauni Milioni 18.5 la Man City kumnunua Santa Cruz!!

Meneja wa Man City, Mark Hughes, amethibitisha kuwa Blackburn wamegoma kumuuza Mshambuliaji wao nyota toka Paraguay Roque Santa Cruz kwa ofa waliyotoa ya Pauni Milioni 18.5 kwa kuwa Blackburn wanataka Pauni Milioni 20.

Kipa Shay Given wa Newcastle aomba rasmi ahamie Man City

Golikipa wa siku nyingi Newcastle, Shay Givens [32], amewasilisha rasmi klabuni kwake ombi la kutaka kuhama ili kuharakisha uhamisho wake kwenda Manchester City ambao umekwama kufuatia mvutano wa dau la uhamisho.
Newcastle wanataka walipwe Pauni Milioni 8 wakati Man City wako tayari kulipa Pauni Milioni 5 kwa Kipa huyo namba moja wa Newcastle kwa miaka 12 sasa.

Thursday 29 January 2009

Liverpool wakwaa kisiki, Chelsea achupa juu yake, Arsenal mwendo mdebwedo lakini Man U bado juu, pointi 2 mbele, mechi moja mkononi!!!!!

Mabingwa Manchester United sasa wako juu ya Wapinzani wao Chelsea na Liverpool kwa pointi 2 na bado wana mechi moja mkononi kufuatia matokeo ya mechi za juzi na jana.
Juzi, Man U waliwachabanga West Brom Albion 5-0 na jana Liverpool walikwaa kigingi pale walipotoka sare 1-1 na Wigan huku Chelsea akiifunga Middlesbrough 2-0.
Liverpool walifunga bao lao kupitia Yossi Benayoun lakini Mmisri Mido, akicheza mechi yake ya kwanza kwa Wigan tangu ahamie hapo kwa mkopo toka Middlesbrough, alisawazisha kwa penalti dakika ya 84.
Nae Salomon Kolou aliifungia Chelsea mabao 2 na kuwapa ushindi wa 2-0 dhidi ya Middlesbrough na kuwafanya Chelsea kuipita Liverpool katika msimamo wa Ligi na kuwa wa pili nyuma ya Man U na sasa wako pointi 48 sawa na Liverpool lakini Chelsea yuko mbele kwa kuwa na tofauti ya magoli bora wote wakiwa wamecheza mechi 23.
Man U yuko kileleni akiwa na pointi 50 kwa mechi 22.
Aston Villa walijikita nafasi ya 4 kwa ushindi wa bao 1-0 walipoifunga Portsmouth nyumbani kwake juzi na sasa wana pointi 47 kwa mechi 23 wakiwa mbele ya Arsenal kwa pointi 5.
Nao Arsenal sasa inaelekea wanaaga rasmi kuwania Ubingwa kwani jana nusura wafungwe pale walipochomoa kigoli dakika za majeruhi dhidi ya Everton.
Everton walipachika bao lao kupitia Tim Cahill dakika ya 61 aliefunga kwa kichwa kama kawaida yake lakini Robin van Persie aliisawazishia Arsenal kwa shuti kali kwenye dakika ya 91.
Sasa Arsenal wamecheza mechi 23 na wana pointi 42 huku Everton wako nyuma ya Arsenal wakiwa na pointi 37 kwa mechi 23 pia.

MECHI ZIFUATAZO:


Jumamosi, 31 Januari 2009

[saa 9 dak 45 mchana]

Stoke v Man City

[saa 12 jioni]

Arsenal v West Ham
Aston Villa v Wigan
Bolton v Tottenham
Fulham v Portsmouth
Hull v West Brom
Middlesbrough v Blackburn

[saa 2 na nusu usiku]

Man U v Everton

Jumapili, 1 Februari 2009
[saa 10 na nusu jioni]

Newcastle v Sunderland

[saa 1 usiku]

Liverpool v Chelsea

Wednesday 28 January 2009

ROBINHO MBARONI KWA TUHUMA ZA KUBAKA!!

Robinho, ambae wiki iliyokwisha alitoroka kwenye kambi ya Timu yake Manchester City iliyokuwa imepigwa huko Spain na kutimka kwao Brazil na kusababisha Klabu yake kumpiga faini na kumpa onyo kali, sasa yuko mikononi mwa Polisi wanaouchunguza uhalifu wa shambulio la ngono lilotokea Januari 14 kwenye naiti klabu.
Msemaji wa Polisi wa West Yorkshire amethibitisha kukamatwa kwa mtu mmoja anaesadikiwa ni Robinho ingawa amesema mtu huyo amekanusha tuhuma hizo na ametoa ushirikiano na yuko nje kwa dhamana.


ENGLAND YAOMBA RASMI KUANDAA FAINALI KOMBE LA DUNIA 2018

FA ya England imewasilisha ombi rasmi kwa FIFA la kuomba kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2018.
Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ya kuwa mwenyeji wa Kombe hilo ni tarehe 2 Februari.
England walikuwa wenyeji wa Fainali hizo mwaka 1966 na ndio safari pekee waliyotwaa Kombe hilo.
Mpaka sasa ni Spain na Portugal, kwa pamoja, na, Holland na Belgium, pia kwa pamoja ndio waliowasilisha maombi ya kuwa wenyeji.
Nchi binafsi zilizoomba ni Urusi, Australia na Qatar huku China, Japan na USA zinasadikiwa zitaomba.
Sharti kubwa la kuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia ni kuwa na Viwanja si chini ya 12 vyenye uwezo wa kuchukua Watazamaji 40,000 kila kimoja n Fainali ichezwe kwenye Uwanja wa Watazamaji 80,000.
Fainali za Kombe la Dunia za 2010 zitafanyika Afrika Kusini na za 2014 zitakuwa Brazil.
FIFA itatangaza Wenyeji wa Fainali za 2018 na 2022 mwezi Desemba 2010.

HATMA YA VIDIC KUPEWA KADI NYEKUNDU FAINALI YA KLABU BINGWA YA DUNIA NI IJUMAA!!!

Beki wa Manchester United, Nemanja Vidic, atajua siku ya Ijumaa nini kitamkuta kama adhabu ya nyongeza baada ya kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu kwenye Fainali ya Kombe la Dunia la Klabu mwezi Desemba huko Japan katika pambano la Man U na LDU Quito wakati alipompiga kiwiko Claudio Bieler.

FIFA imelipeleka suala hilo kwa UEFA kwani Manchester United walikuwa wanaiwakilisha UEFA kwenye mashindano hayo na UEFA imetamka itasikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi siku ya Ijumaa.

Man U watakuwa wanaomba UEFA ichukue uamuzi kama walioufanya miaka miwili iliyopita pale walipoamua kutochukua hatua yeyote ya ziada kwa Mchezaji wa AC Milan Kakha Kaladze aliepewa Kadi Nyekundu kwenye Fainali za Klabu Bingwa ya Dunia na FIFA wakaisukumia UEFA kutoa adhabu zaidi lakini Mchezaji huyo hakupewa adhabu nyingine yeyote na UEFA.

Tuesday 27 January 2009

West Brom 0 Man United 5!!!
Kipa Van Der Sar avunja rekodi ya kutofungwa goli kwa zaidi ya dakika 1,025!!

Mabingwa Manchester United wakicheza ugenini Uwanja wa Hawthorns waliwashindilia wenyeji wao West Bromwich Albion mabao 5-0 na kuwafanya wazidi kuongoza LIGI KUU England sasa wakiwa pointi 3 mbele ya Liverpool.
Kwa kutofungwa hata goli moja kwenye mechi hii, Man U wameweka rekodi mpya ya LIGI KUU kwa kucheza mechi 11 bila ya nyavu zao kutikisika rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Chelsea tangu msimu wa 2004/5.
Na ilipofika dakika ya 84 ya mchezo Kipa wa Man U Edwin van der Sar alivunja rekodi ya Kipa wa Chelsea ya kucheza dakika 1,025 bila kufungwa hata goli moja kwenye LIGI KUU England, dakika ya 84 ya mechi hii ilikuwa van der Sar anaingia dakika yake ya 1,026 bila kufungwa!!!
Sasa anashikilia rekodi kwa kucheza dakika 1,032 bila kufungwa goli kwenye LIGI KUU!!
Mechi hii ilichelewa kuanza kwa dakika 30 kwa sababu Watazamaji wengi walichelewa uwanjani kutokana na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara zote zilizokuwa zinaelekea hapo Hawthorns.
Iliwachukua dakika 22 kwa Man U kuanza kufunga kwa goli la Berbatov.
Na kazi ya Man U ilirahisishwa pale Nahodha wa West Brom Paul Robinson alipopewa Kadi Ny ekundu baada ya kumchezea Ji-Sung Park rafu mbaya.
Katika dakika ya 43 Kipa Scott Carson aliutema mpira kufuatia frikiki ya Ryan Giggs na Tevez akauwahi na kuushindilia wavuni. Vidic akapachika la 3 dakika ya 60 na Ronaldo akafunga mawili dakika ya 65 na 73.
West Brom: Carson, Hoefkens, Pele, Donk, Robinson, Zuiverloon (Morrison 64), Borja Valero, Koren, Brunt, Simpson (Bednar 64), Fortune (Cech 46).
Akiba hawakucheza: Kiely, Kim, Dorrans, Filipe Teixeira.
Kadi Nyekundu: Robinson (40).
Kadi Njano: Koren, Bednar, Carson, Donk, Morrison.
Man Utd: Van der Sar, Neville (Eckersley 71), Ferdinand (Brown 70), Vidic, O'Shea, Park, Carrick, Giggs, Ronaldo, Berbatov (Tosic 77), Tevez.
Akiba hawakucheza: Kuszczak, Scholes, Fletcher, Gibson.
Kadi Njano: Park, Carrick.
Magoli: Berbatov 22, Tevez 44, Vidic 60, Ronaldo 65, 73.
Watazamaji: 26,105
Refa: Rob Styles

MATOKEO MECHI NYINGI ZA LEO ZALIGI KUU ENGLAND:
Portsmouth 0-1 Aston Villa

Sunderland 1-0 Fulham

Tottenham 3-1 Stoke

MECHI ZA Jumatano, 28 Januari 2009

[saa 4 dak 45 usiku]
Chelsea v Middlesbrough
Man City v Newcastle
Wigan v Liverpool

[saa 5 usiku]
Blackburn v Bolton
Everton v Arsenal
West Ham v Hull

Meneja wa Newcastle apigwa faini na FA kwa kumwita Refa Katuni 'Mickey Mouse!!!'

Joe Kinnear, Meneja wa Newcastle, amepigwa faini ya Pauni 500 baada ya kumwita Refa Martin Atkinson Katuni 'Mickey Mouse' aliechezesha mechi Newcastle waliyofungwa 2-1 na Fulham Novemba 9 mwaka jana.
Kinnear alikasirishwa na Refa huyo kwa kukataa kuwapa frikiki na badala yake akaruhusu mpira uendelee na hapo hapo akawapa Fulham penalti waliyofunga bao la pili na la ushindi.
Kinnear hakuadhibiwa katika kesi yake ya pili iliokuwa ikimkabili ya kumkashifu Mwamuzi katika mechi waliyocheza na Stoke City baada ya kuonekana hana hatia.
Sasa Kinnear bado ana kesi moja hapo FA pamoja na Meneja wa Hull City Phil Brown ambayo wote wawili walitolewa nje na kuamriwa kukaa kwa Watazamaji na Refa baada ya kuonekana wanazozana vikali pembeni ya uwanja huku mechi inaendelea wakati timu zao Newcastle na Hull City zilipokutana Januari 14.

Staa wa Chelsea John Mikel Obi abambwa na Polisi akiendesha gari huku akiwa njwiiiiii!!!

Mikel Obi alikamatwa na Polisi alfajiri ya Jumamosi iliyokwisha akiendesha gari mjini London huku akiwa amelewa chakari.
Mchezaji huyo atafikishwa Mahakamani tarehe 3 Aprili kujibu shtaka hilo.


Brazil yamwita tena Ronaldinho kundini!!!!

Kocha wa Brazil, Dunga, amemwita tena Ronaldinho kwenye Timu ya Taifa ya Brazil itakayocheza mechi ya kirafiki na Italia mwezi ujao mjini London Uwanja wa Emirates Februari 10.
Ronaldinho hajaitwa Timu ya Brazil tangu mwaka jana na alicheza mechi yake ya mwisho mwezi Septemba Brazil walipotoka 0-0 na Bolivia kwenye mechi ya Mtoano wa Kombe la Dunia.

Mechi zilizofuata za Brazil dhidi ya Venezuela na Colombia za Kombe la Dunia, Ronaldinho aliachwa pamoja na mechi ya kirafiki na Portugal iliyochezwa Novemba mwaka jana.
Brazil na Italia walicheza mara ya mwisho mwaka 1997 na kutoka sare 3-3 huko Ufaransa.

Kabla ya hapo walikutana kwenye Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1994 mechi iliyoisha 0-0 na Brazil wakashinda kwa penalti na kuwa Mabingwa wa Dunia.
Kikosi kamili [klabu wanazochezea kwenye mabano]:
Makipa: Doni (AS Roma), Julio Cesar (Inter Milan)
Walinzi: Daniel Alves (Barcelona), Adriano Correia (Sevilla), Maicon (Inter Milan), Marcelo (Real Madrid), Lucio (Bayern Munich), Luis¿o (Benfica), Juan (AS Roma), Thiago Silva (AC Milan)
Viungo: Anderson (Manchester United), Gilberto Silva (Panathinaikos), Felipe Melo (Fiorentina), Josue (VfL Wolfsburg), Elano (Manchester City), Julio Baptista (AS Roma), Kaka (AC Milan), Ronaldinho (AC Milan)
Washambuliaji: Alexandre Pato (AC Milan), Adriano (Inter Milan), Lus Fabiano (Sevilla), Robinho
UHAMISHO: Klabu za LIGI KUU England:

Dirisha la Uhamisho wa Wachezaji linafungwa tarehe 1 Februari 2009 na Klabu mbalimbali zipo kwenye harakati za kuuza na kununua Wachezaji.
Baadhi ya makubaliano yaliyofanyika ni kama ifuatavyo:

Chimbonda arudi tena Tottenham!!

Pascal Chimbonda, Beki mwenye umri wa miaka 29, amerudi tena Tottenham kutoka Sunderland ambako alicheza mechi 16 tangu aende huko kutoka Tottenham mwezi Agosti mwaka jana.
Chimbonda, ambae pia ameshachezea Timu ya Taifa ya Ufaransa, alikwenda England kuchezea Wigan akitokea Klabu ya Bastia ya Ufaransa na mwezi Agosti, 2006 alijiunga na Tottenham.

Tottenham wamsaini Kipa Cudicini toka Chelsea!

Kipa Carlo Cudicini, miaka 35, amehamia Tottenham kutoka Chelsea kwa uhamisho wa bure baada ya mkataba wake kukaribia kuisha.
Cudicini alijiunga Chelsea mwaka 1999 akitokea Castel de Sangro ya Italia na ameshaidakia Chelsea mechi 208 lakini tangu Kipa Petr Cech aingie Chelsea 2004, Cudicini amekuwa hana namba.
Hata huko Tottenham atapata ushinda mkubwa kwani kuna Makipa Heurelho Gomes, anaesifika sana kwa kutoa maboko na chipukizi Ben Alnwick.

West Ham wamchukua Nsereko aliezaliwa Uganda!!

Savio Nsereko, kijana wa miaka 19 mzaliwa wa Uganda ingawa sasa ni raia wa Ujerumani, amejiunga na West Ham akitokea Klabu ya Italia ya Serie B Brescia kwa dau la Pauni Milioni 7 na nusu.
Nsereko huchezea Timu ya Taifa ya Ujerumani ya Vijana wa chini ya miaka 19.

Wigan wamnunua Straika toka Colombia!

Mshambuliaji mwenye umri wa miaka 23 aitwae Hugo Rodallega amejiunga na Wigan kutoka Klabu ya Mexico Necaxa kwa ada ya Puni Milioni 4 na nusu na mkataba wa miaka mitatu na nusu.
Rodallega pia yumo Timu ya Taifa ya Colombia ambayo ameichezea mechi 21.
Kujiunga kwa Rodallega Wigan kuna nia ya kujiimarisha baada ya Mshambuliaji wao staa Emile Heskey kuhamia Aston Villa wiki iliyokwisha.
Safu hiyo ya mashambulizi pia imeongezwa nguvu baada ya Wigan kumchukua Mmisri Mido kwa mkopo kutoka Middlesbrough.

LIGI KUU kuendelea leo usiku!!!

Baada ya mshikemshike wa FA CUP, LIGI KUU England inarudi tena ulingoni leo usiku kwa ratiba ifuatayo:

Jumanne, 27 Januari 2009
[saa 4 dak 45 usiku]

Sunderland v Fulham

West Brom v Man U

[saa 5 usiku]
Portsmouth v Aston Villa
Tottenham v Stoke

Jumatano, 28 Januari 2009
[saa 4 dak 45 usiku]
Chelsea v Middlesbrough
Man City v Newcastle
Wigan v Liverpool
[saa 5 usiku]
Blackburn v Bolton
Everton v Arsenal
West Ham v Hull

Jumamosi, 31 Januari 2009
[saa 9 dak 45 mchana]
Stoke v Man City
[saa 12 jioni]
Arsenal v West Ham
Aston Villa v Wigan
Bolton v Tottenham
Fulham v Portsmouth
Hull v West Brom
Middlesbrough v Blackburn
[saa 2 na nusu usiku]
Man U v Everton

Jumapili, 1 Februari 2009
[saa 10 na nusu jioni]
Newcastle v Sunderland
[saa 1 usiku]
Liverpool v Chelsea

Sunday 25 January 2009

FA CUP: DRO YA RAUNDI YA 5 YAFANYIKA: mechi kuchezwa Februari 13, 14 au 15!!

[TIMU INAYOTAJWA KWANZA ITAKUWA NYUMBANI]

Sheffield United v Hull

Watford v Chelsea

West Ham v Middlesbrough

Sunderland au Blackburn v Coventry

Derby au Nottingham Forest v Manchester United

Swansea v Fulham

Liverpool au Everton v Doncaster au Aston Villa

Cardiff au Arsenal v West Brom au Burnley
KOMBE LA FA: Bila shaka Everton watalia: OOOHHH REFA!!!!
Liverpool 1 Everton 1

Wakicheza ugenini, nyumbani kwa Watani wao wa Jadi Liverpool Uwanjani Anfield, Everton walionekana dhahiri kukandamizwa na Waamuzi wa mechi hiyo wakiongozwa na Refa Steve Bennet.
Dakika ya 5 tu ya mchezo walinyimwa penalti ya wazi pale Kiungo wa Liverpool Xabi Alonso alipomkwatua Steven Pienaar.
Lakini Mwamuzi alishindwa kulikataa goli safi na la wazi la Mlinzi wa Everton Joleon Lescott aliefunga kwa kichwa kufuatia kona ya Steven Pienaar dakika 27 na kumkuta Tim Cahill aliepiga kichwa kilichokuwa kinaenda wavuni lakini Lescott akamalizia na kujihesabu yeye ndie mfungaji.
Mpaka mapumziko Liverpool 0 Everton 1.
Kipindi cha pili Liverpool huku wakibebwa na Waamuzi walijitutumua na kusawazisha dakika ya 54 kupitia mkombozi na Nahodha wao Steven Gerrard.
Hii ni mara ya pili kwa Liverpool kushindwa kumfunga Mtani wake hapo kwake Anfield ndani ya wiki moja baada ya kutoka droo ya 1-1 kwenye mechi ya LIGI KUU Jumatatu iliyokwisha.
Sasa timu hizi zitarudiana huko Goodison Park nyumbani kwa Everton wiki ijayo tarehe 4 Februari 2009 ili kuamua ni nani kati yao ataingia Raundi ya 5 ya Kombe la FA.
KOMBE LA FA:

Cardiff 0 Arsenal 0


Cardiff City, Timu ya Daraja la chini ya LIGI KUU England, ikicheza Uwanja wa nyumbani Ninian Park iligangamala na kulazimisha suluhu ya 0-0 na Arsenal katika mechi ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA.
Sasa timu hizi itabidi zirudiane nyumbani kwa Arsenal Emirates Stadium tarehe 3 Februari 2009 ili kupata timu itakayosonga Raundi ya 5.
VIKOSI VILIKUWA:

Cardiff: Enckelman, McNaughton, Gyepes, Roger Johnson, Kennedy, Rae, Parry, Ledley, Burke, Bothroyd, McCormack.
Akiba: Heaton, Capaldi, Purse, Eddie Johnson, McPhail, Comminges, Blake.
Arsenal: Fabianski, Sagna, Toure, Djourou, Gibbs, Nasri, Ramsey, Song Billong, Eboue, Van Persie, Bendtner.
Akiba: Almunia, Diaby, Gallas, Vela, Denilson, Wilshere, Adebayor.
Refa: Martin Atkinson
Mechi ya jana ya FA CUP kati ya Hull City na Millwall yatawaliwa na fujo za mashabiki wa Millwall!!! Kikosi cha Polisi wa Kuzuia Fujo chaingilia na kuwakamata Washabiki 12!!!

Katika mechi ya jana kati ya Hull City na Millwall ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA ambayo Hull aliibuka na ushindi wa mabao 2-0, vurugu na fujo kubwa ziliibuka kabla ya mechi kuanza na hata wakati mechi ikiendelea hasa kwenye jukwaa walilokaa Washabiki wa Millwall ambao ndio walikuwa uwanja wa ugenini.
Kizaazaa hicho hakijawahi kuonekana kwenye mechi za Soka England kwa miaka sasa.
Ilibidi Kikosi Maalum cha Polisi wa Kuzuia Fujo waliovalia rasmi kwa mapambano kuitwa na waliangusha mkong'oto mkubwa na kuwakamata Mashabiki 12 wa Millwall na uchunguzi wa video unaendelea ili kuwakamata wahusika wengine.
Klabu ya Hull City iko mbioni kudai fidai kwa kuharibiwa uwanja wao ambao viti viling'olewa, vyoo kuvunjwa na mali zao nyingi kuharibiwa.
Mechi ilihudhuriwa na Watazamaji zaidi ya 18,000.
DRO YA RAUNDI YA 5 YA KOMBE LA FA KUFANYIKA LEO USIKU.

Dro ya kuamua Timu zipi zinakutana kwenye Raundi ya 5 ya FA Cup ambayo itajumuisha Timu 16 itafanyika leo usiku baada ya mechi ya Raundi ya 4 ya Kombe hili kati ya Liverpool na Everton itakayoanza saa 1 usiku [bongo taimu].
Mechi nyingine ya Raundi ya 4 inayochezwa leo ni kati ya Cardiff na Arsenal inayoanza saa 10 na nusu jioni [bongo taimu].
Mechi nyingine za Raundi ya 4 inazobidi zirudiwe baada ya kutoka suluhu hapo jana ni kama ifuatavyo:

Jumanne, 3 Februari 2009
Burnley v West Brom
Jumatano, 4 Februari 2009
Aston Villa v Doncaster
Blackburn v Sunderland
Nottingham Forest v Derby

Washindi wa mechi hizo za marudiano, pamoja na Washindi wa mechi 2 za leo, watajumuika na Timu zilizofuzu kuingia Raundi ya 5 zifuatazo: Manchester United, Hull City, West Ham, Sheffield United, Swansea City, Chelsea, Coventry City, Fulham, Watford na Middlesbrough.
Mechi hizi za Raundi ya 5 zitachezwa tarehe 14 Februari 2009.
Powered By Blogger