Saturday 27 September 2008



KILIO ARSENAL SIKU WENGER ANAYOSHEHEREKEA MIAKA 12 KUWA HAPO!!

Arsenal 1 Hull City 2

Leo ni siku ya kuadhimisha miaka 12 tangu Arsene Wenger awe Meneja wa Arsenal lakini imekuwa siku ambayo atataka aisahau haraka baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 nyumbani kwake Emirates Stadium tena toka timu 'kibonde' Hull City iliyopanda Daraja msimu huu kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe.

Vilevile Hull City imekuwa timu ya pili kuwafunga Arsenal kwenye LIGI KUU hapo kwao Emirates Stadium tangu uwanja huo mpya uanze kuchezewa.

Timu ya kwanza kuifunga Arsenal kwenye mechi ya LIGI KUU hapo Emirates ni West Ham waliposhinda bao 1-0 lililofungwa na Mchezaji wao Bobby Zamora katika mechi iliyochezwa Aprili, 2007. Tangu siku hiyo mpaka kipigo cha leo Arsenal imecheza mechi 25 za LIGI KUU bila kupoteza mechi.

Hadi mapumziko mechi ilikuwa suluhu ya 0-0. Kipindi cha pili kuanza Arsenal walipata bao walilojifunga wenyewe Hull City. Mbrazil Giovanni alisawazishia Hull City kwa kiki kali ya kistadi sana na Mshambuliaji Cousin akawapatia Hull City bao la ushindi kwa kichwa baada ya kona.


MAN U 2 BOLTON 0


Ronaldo na Rooney waipa ushindi Mabingwa Man U baada ya kila mmoja kufunga goli katika kipindi cha pili. Ronaldo alichezewa rafu kwenye boksi na Refa akaamua ni penalti iliyofungwa na Ronaldo mwenyewe. Kisha Rooney akaingizwa uwanjani kuchukua nafasi ya Tevez na akapachika bao baada ya gonga safi za Man U.

STOKE O CHELSEA 2

Mabao ya Jose Bosingwa na Nicholas Anelka yamewapa ushindi wa ugenini Chelsea wa bao 2-0 zidi ya timu iliyopanda daraja Stoke City.

MATOKEO MECHI NYINGINE:

Aston Villa 2 Sunderland 1

Fulham 1 West Ham 2

Middlesbrough 0 West Brom 1

Newcastle 1 Blackburn 2

KINDUMBWENDUMBWE CHA MJI WA LIVERPOOL: Everton 0 Liverpool 2

Magoli mawili ya Fernando Torres ya kipindi cha pili yaliwapa ushindi Liverpool wakiwa ugenini Uwanja wa Goodison Park nyumbani kwa Everton kwenye kitimtim cha wenyeji wawili wa mji wa Liverpool ambao ni watani wa jadi.

Magoli hayo yalifungwa katika muda usiozidi dakika 4 kati yake na yaliwavunja nguvu Everton ambao mara tu baada ya mabao hayo mchezaji wao Tim Cahill alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya Kiungo wa Liverpool Xabi Alonso.

Everton pengine watalalamika sana kwa kunyimwa penalti ya wazi kipindi cha kwanza baada ya Mshambuliaji wao Yakubu kusukumwa kwa makusudi ndani ya boksi.

CARLING CUP: DRO YA RAUNDI YA 4 TAYARI!

Mechi za Raundi ya 4 kugombea CARLING CUP zimepangwa na Mabingwa watetezi wa Kombe hili Tottenham wamepangiwa kukutana na Liverpool. Tottenham watakuwa uwanja wao wa nyumbani.
Mechi nyingine zinazohusisha timu za LIGI KUU kukutana ni ile kati ya Sunderland na Blackburn na nyingine ni ya kati ya Arsenal na Wigan.
Mabingwa wa LIGI KUU Manchester United wamepangiwa kucheza uwanja wao wa nyumbani Old Trafford na watacheza na timu ya Daraja la Chini Queens Park Rangers [QPR].
Mechi hizi zitachezwa kwenye wiki ya kuanzia Novemba 10.

MECHI ZOTE NI:

Sunderland v Blackburn Rovers

Arsenal v Wigan Athletic

Chelsea v Burnley

Swansea City v Watford

Manchester United v Queens Park Rangers

Stoke City v Rotherham United

Mshindi kati ya Brighton na Derby v Leeds United

Tottenham Hotspur v Liverpool

RATIBA YA LEO: Jumamosi, 27 Septemba 2008 Saa ni za bongo]


Everton v Liverpool [saa 8 dak 45 mchana];


Aston Villa v Sunderland [saa 11 jioni];


Fulham v West Ham [saa 11 jioni];


Man U v Bolton [saa 11 jioni];


Middlesbrough v West Brom [saa 11 jioni];


Newcastle v Blackburn [saa 11 jioni];


Stoke City v Chelsea [saa 11 jioni];


Arsenal v Hull City [saa 1 na nusu usiku];
UEFA CUP KUITWA EUROPA LEAGUE MSIMU UJAO

Kuanzia mwakani, hasusan msimu ujao wa soka, UEFA CUP ambalo hushindaniwa na Klabu za Ulaya ambazo hazikufuzu kuingia UEFA CHAMPIONS LEAGUE na kujumuishwa na Klabu zilizoshika nafasi ya tatu kwenye Makundi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, litabadilishwa jina na kuitwa EUROPA LEAGUE.

Vilevile mtindo wa uchezaji utabadilishwa kutoka wa sasa wa mtoano na kuanzishwa mtindo wa ligi kama ilivyo kwa UEFA CHAMPIONS LEAGUE. Mfumo huu wa ligi utakuwa na jumla ya Klabu 48 zitakazogawanywa makundi 12 ya timu nne nne kila moja ambazo zitacheza kwa mtindo wa ligi wa mechi za nyumbani na ugenini.

Washindi wawili wa juu wa kila Kundi watajumlishwa na timu 8 zilizoshika nafasi ya tatu kwenye Makundi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE kufanya jumla ya timu 32 zitakazocheza kwa mtoano hadi kufikia Fainali.

Friday 26 September 2008

Joe Kinnear ateuliwa Meneja wa muda NEWCASTLE

Tangu Kevin Keagan aachie ngazi Newcastle tarehe 4 Septemba 2008, Klabu hiyo imekuwa haina Meneja na timu ilikuwa chini ya uongozi wa aliekuwa kocha msaidizi Chris Hughton huku Menejimenti ikiyumba na kujikuta ikiwa na mzozo mkubwa na mashabiki wa timu hiyo waliochukua hatua ya kuandamana kupinga kuondoka Kevin Keagan.
Maandamano hayo yalimuudhi sana mmiliki wa Klabu Mike Ashley ambae akaamua kuiuza klabu hiyo. Hivi sasa yuko kwenye pilipilika za kuiuza huku kuna tetesi kwamba kuna Kampuni moja kubwa toka Nigeria imetoa ofa ya kuinunua ingawa habari nyingine zinasema mwenye klabu Mike Ashley anatafuta mnunuzi toka Arabuni.
Wakati mizozo na wasiwasi ukiendelea timu nayo imekuwa haifanyi vizuri uwanjani na imeshapata vipigo vitatu mfululizo tangu kuondoka Kevin Keagan hali iliyomfanya Kocha msaidizi Chris Hughton kutaka uongozi wa Klabu kutafuta Meneja wa kudumu.
Leo Menejimenti imemtaja Joe Kinnear, umri miaka 61, [pichani]kuwa Meneja wa muda mpaka mwishoni mwa Oktoba inapotegemewa klabu hiyo itakuwa ishauzwa.
Joe Kinnear, raia wa Ireland, mara ya mwisho alikuwa Meneja wa Nottingham Forrest kazi aliyojiuzulu Desemba 2004 na tangu wakati huo hajaongoza timu nyingine yeyote.
Kabla ya hapo alishakuwa Meneja wa Wimbledon na baadae Luton.
Nae Chris Hughton aliekuwa akiongoza timu ameukaribisha uteuzi huo kwa kutamka kuwa Joe Kinnear ni mzoefu sana na atasaidia klabu katika wakati huu mgumu.
BRAZIL WATAJA KIKOSI CHAO CHA MECHI ZA MTOANO KOMBE LA DUNIA

-KAKA, ROBINHO NDANI, RONALDINHO NJE!

Kocha wa Brazil ameteua kikosi cha Wachezaji 22 watakaocheza mechi za mtoano wa KUNDI LA NCHI ZA MAREKANI KUSINI kuwania kuingia FAINALI KOMBE LA DUNIA AFRIKA KUSINI 2010 ambapo watacheza mechi mbili mwezi ujao Oktoba.

Tarehe 12 Oktoba 08 Brazil inapambana na Venezuela na siku nne baadae inacheza na Colombia.

Dunga amemrudisha kikosini Kaka ambae hajachezea Timu ya Taifa tangu Novemba mwaka jana. Ronaldinho, ingawa aliiwakilisha Brazil kwenye Olympic huko Beijing akiwa Nahodha, ametupwa nje kwa kile Dunga alikiita kukosa nafasi ya kucheza mechi nyingi na Klabu yake mpya ya AC Milan.Wachezaji wapya wa Manchester City Jo na Robinho wamo kwenye kikosi hicho pamoja na Anderson wa Manchester United.

KIKOSI KAMILI [KLABU WANAZOTOKA]

MAKIPA: Julio Cesar (Inter Milan), Doni (AS Roma) WALINZI: Maicon (Inter Milan), Daniel Alves (Barcelona), Lucio (Bayern Munich), Juan (AS Roma), Thiago Silva (Fluminense), Alex (Chelsea), Kleber (Santos), Juan (Flamengo) VIUNGO: Gilberto Silva (Panathinaikos), Josue (Wolfsburg), Lucas (Liverpool), Anderson (Manchester United), Elano (Manchester City), Kaka (AC Milan), Mancini (Inter Milan/ITA), Julio Baptista (AS Roma/ITA) WASHAMBULIAJI: Luis Fabiano (Sevilla), Jo (Manchester City), Pato (AC Milan), Robinho (Manchester City)



KOMBE LA CARLING:
DRO YA MECHI ZA RAUNDI YA 4 KUFANYIKA KESHO JUMAMOSI 27 SEPTEMBA 2008
Dro ya kuamua timu zipi zinakutana kwenye RAUNDI YA 4 ya KOMBE LA CARLING itafanyika kesho Jumamosi tarehe 27 Septemba 2008.
Timu 16 zimeingia Raundi hii ya 4 zikiwa Timu 9 toka LIGI KUU na Timu 7 toka Daraja la Chini yake.
Timu za LIGI KUU ni Tottenham, Chelsea, Wigan, Blackburn, Liverpool, Sunderland, Stoke City, Man U na Arsenal.
Timu za Daraja la chini ni QPR, Brighton, Burnley, Leeds, Rotherham, Swansea na Watford.
Mechi za Raundi ya 4 zitachezwa wiki ya kuanzia Desemba 1, 2008.
Washindi wanane toka Raundi hiyo ya 4 watasonga kwenye Raundi ya 5 na washindi wa Raundi hii wanaingia Nusu Fainali itakayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Fainali ya CARLING CUP itafanyika tarehe 1 Machi 2009.
CARLTON COLE WA WEST HAM AKAMATWA AKIENDESHA GARI AKIWA NJWIII!

Mshambuliaji wa West Ham, Carlton Cole, umri miaka 24, alikamatwa na Polisi usiku wa manane wa Jumanne akiendesha gari katikati ya jiji la London huku akiwa amelewa chakari.
Alipokamatwa tu akapimwa hapohapo kwenye tukio kiwango cha pombe kilichopo mwilini kisha akapelekwa kituoni.
Baadae akaachiwa kwa dhamana.
Usiku wa Jumanne hiyo ya tukio timu yake ya West Ham ilifungwa na Watford bao 1-0 kwenye Mechi ya Kombe la Carling.
Wakati kesi yake ikiendelea kuchunguzwa itabidi arudi tena Polisi mwezi Novemba ili dhamana yake iendelee.

Thursday 25 September 2008

CROATIA WAPIGWA FAINI KWA KUWA WABAGUZI

FIFA kimewapiga faini Croatia kwa kosa la washabiki wao kuwa wabaguzi wa rangi katika mechi yao na Uingereza iliyochezwa mapema mwezi huu mji mkuu wao Zagreb ya kutafuta nchi zitakazoingia Fainali Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini mechi ambayo Croatia ilishindiliwa 4-1 na kupoteza rekodi yao ya kutofungwa nyumbani.
Ubaguzi huo ulifanywa na kikundi kidogo cha watazamaji kilichotoa sauti kama nyani kila Mshambuliaji wa Uingereza Emile Heskey [pichani] alipopata mpira.
Chama cha Mpira cha Uingereza kililalamika FIFA kwa kitendo hicho na sasa FIFA imeitwanga Croatia faini ya takriban Shilingi za bongo milioni 30.
Hii ni mara ya pili kwa Croatia kupatikana na hatia na kulimwa faini kwa kosa kama hili.
Katika mechi ya Robo Fainali ya EURO 2008 na Uturuki washabiki wa Croatia walileta ubaguzi na wakapigwa faini.
Sasa FIFA imewapa onyo la mwisho na endapo kosa hili litatokea tena basi watafungiwa.


Baada ya kitimtim cha Kombe la CARLING cha jana Jumatano na juzi Jumanne macho yote sasa yako kwenye LIGI KUU UINGEREZA itakayowaka moto Jumamosi na Jumapili kwa jumla ya mechi 10 ikimaanisha timu zote 20 za LIGI KUU zitakuwa zikicheza.
Mechi kubwa wikiendi hii bila shaka ni ile inayowakutanisha WATANI WA JADI wanaotoka mji mmoja mji wa Liverpool.
Kwa kuwa mechi hii ina ushindani mkubwa na hulifanya jiji lote la Liverpool lizizime na kupambwa kwa bendera za bluu kwa upande mmoja na nyekundu kwa upande mwingine inachezwa jua utosini saa sita dak 45 mchana kwa saa za huko kwa matakwa ya POLISI wa mji huo wa Liverpool. Bongo itakuwa saa 8 dak 45 mchana.
Mechi hii ni pambano kati ya Everton na Liverpool litakalochezwa Uwanja wa Goodison Park.


RATIBA KAMILI YA WIKIENDI:
Jumamosi, 27 Septemba 2008 Saa ni za bongo]

Everton v Liverpool [saa 8 dak 45 mchana];

Aston Villa v Sunderland [saa 11 jioni];

Fulham v West Ham [saa 11 jioni];

Man U v Bolton [saa 11 jioni];

Middlesbrough v West Brom [saa 11 jioni];

Newcastle v Blackburn [saa 11 jioni];

Stoke City v Chelsea [saa 11 jioni];

Arsenal v Hull City [saa 1 na nusu usiku];

Jumapili, 28 Septemba 2008

Portsmouth v Tottenham [saa 9 na nusu mchana];

Wigan v Man City [saa 12 jioni];


CHELSEA WAMSAINI KUNGO TOKA BRAZIL

Kiungo Mineiro raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 33 amesainiwa na Chelsea kama Mchezaji huru.
Mineiro alimaliza mkataba na Klabu yake ya mwisho Hertha Berlin ya Ujerumani mwishoni mwa msimu uliopita.
Ingawa kipindi cha uhamisho kimeisha rasmi tarehe 1 Septemba 2008 Wachezaji huru huruhusiwa kusaini kwenye klabu baada ya muda huo. Vilevile kumchukua Mchezaji kwa mkopo pia inaruhusiwa.
Meneja wa Chelsea Luis Felipe Scolari ambae ni raia wa Brazil amefurahia hatua hii kwani ana pengo kubwa la viungo kwenya timu yake baada ya Kiungo Michael Essien kufanyiwa upasuaji wa goti utakaomweka nje ya uwanja kwa miezi 6. Pia Deco aliumia kabla ya kuanza mechi na Man U na inasemekana atakuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja.
Mineiro ameshaichezea Timu ya Taifa ya Brazil mara 24 na alikuwa kwenye kikosi cha Brazil kilichocheza Kombe la Dunia mwaka 2006.
===============================================================

NAHODHA WA BORO AOMBA RADHI KWA KUMUUMIZA POSSEBON WA MAN U.

Nahodha wa Middlesbrough Emmanuel Pogatetz ameomba radhi kwa kumuumiza kiungo chipukizi wa Man U Rodrigo Possebon juzi huko Old Trafford kwenye mechi ya CARLING CUP ambayo Man U waliikung’uta Boro mabao 3-1.
Pogatetz alicheza rafu hiyo mbaya dakika ya 66 ya mchezo na kupewa kadi nyekundu kwa tukio hilo.
Possebon alipewa huduma ya kwanza hapo uwanjani iliyochukua dakika 6 na kisha kukimbizwa hospitali alikolazwa hadi asubuhi kwa uchunguzi ndipo ilipothibitika hakuvunjika wala hakuathirika goti na akaruhusiwa kutoka..
Pogatetz amekiri alikosea kwani alijitosa akidhani atauwahi mpira na mara baada ya kitendo hicho alibisha na kudai amecheza mpira tu lakini baada ya kuangalia video amekubali alicheza rafu mbaya na anaomba msamaha.
Pogatetz alisema: ‘Nitampigia simu Possebon na kumwomba anisamehe kwa kumuumiza. Naomba vilevile apone haraka.’

MATOKEO CARLING CUP: MECHI ZA JUMATANO 24 SEPTEMBA 2008

Timu za LIGI KUU Aston Villa na Manchester City zimeaga CARLING CUP baada ya kubwagwa na timu za Daraja la Chini za QPR na Brighton.
Aston Villa ikiwa nyumbani kwake ilipigwa bao 1-0 na QPR.
Manchester City wakicheza ugenini nyumbani kwa Brighton walikwenda sare ya 2-2 katika dakika 90 na muda wa nyongeza wa nusu saa haukupata mshindi ndipo tombola ya penalti ikawapa ushindi Brighton wa mabao 5-3.
Nayo timu isiyokuwa na Meneja, Newcastle, ilipata pigo jingine baada ya kupigwa nyumbani mabao 2-1 na Tottenham.
Chelsea walionyesha ubabe pale walipowabamiza Portsmouth waliokuwa wakicheza nyumbani kwa mabao 4-0.
Katika mechi nyingine Wigan wanaocheza LIGI KUU waliibwaga Ipswich inayocheza Daraja la Chini mabao 4-1 licha ya Ipswich kuwa uwanja wa nyumbani.

Blackburn wakiwa nyumbani Ewood Park waliwatoa wenzao kwenye LIGI KUU Everton kwa bao 1-0.


Wednesday 24 September 2008

CARLING CUP: mechi za leo

Leo tena vumbi litatimka viwanja mbalimbli huko Uingereza kwenye michuano ya mtoano kuwania KOMBE LA CARLING.

Mechi zinazongojewa kwa hamu ni zile zinazokutanisha vilabu vya LIGI KUU UINGEREZA kati ya Portsmouth ambae ni Bingwa wa Kombe la FA na Chelsea ambae ni mshindi wa pili LIGI KUU. Nyingine ni ile ya Newcastle na Tottenham timu ambazo zimezorota kwenye LIGI KUU msimu huu.

JUMATANO, 24 Septemba 2008:


[saa 3 dak 45 usiku bongo taimu]


Aston Villa v QPR;

Blackburn v Everton;

Brighton v Man City;

Ipswich v Wigan;

Newcastle v Tottenham;

Portsmouth v Chelsea.


FERGUSON AFOKA KUHUSU KUUMIZWA CHIPUKIZI WAKE

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amekuja juu kuhusu kuumizwa kwa Kiungo chipukizi wake Rodrigo Possebon kutoka Brazil mwenye umri wa miaka 19 katika mechi ya jana ya KOMBE LA CARLING ambayo Man U waliifunga Middlesbrough 3-1.
Possebon aliumizwa kwenye dakika ya 66 na Nahodha wa Middlesbrough Emmanuel Pogatetz ambae alipewa kadi nyekundu kwa kosa hilo.
Mechi ilisimama kwa dakika 6 kumtibu Possebon uwanjani na kisha akakimbizwa hospitali alikolazwa usiku mzima na kuruhusiwa asubuhi ilipothibitika hakuvunjika na hakuna madhara makubwa kwenye goti.
Ferguson alifoka: 'Ni rafu mbaya sana na kinachosikitisha ni kuona mchezaji aliefanya faulo analalamika kwamba sio kosa na benchi lake likiunga mkono kuwa sio kadi nyekundu! Afadhali kidogo Meneja wa Middlesbrough Derek Southgate amekubali ni faulo mbaya!'
Possebon ndio kwanza alikuwa anaanza mechi yake ya kwanza kwa Man U.
Nae Nahodha huyo wa Middlebrough Emmanuel Pogatetz sasa atafungiwa kucheza mechi 3 zijazo.
CARLING CUP: Matokeo kamili ya mechi za jana=


BURNLEY 1 FULHAM 0;


LIVERPOOL 2 CREWE 1;


LEEDS 3 HARTLEPOOL 2;


ROTHERHAM 3 SOUTHAMPTON 1;


SUNDERLAND 2 NORTHAMPTON 2 [SUNDERLAND ASHINDA KWA PENALTI 4-3];


STOKE CITY 2 READING 2 [STOKE ASHINDA KWA PENALTI 4-3];


SWANSEA 1 CARDIFF 0;


WATFORD 1 WEST HAM 0;


MAN U 3 MIDDLESBROUGH 1;


ARSENAL 6 SHEFFIELD UNITED 0

CARLING CUP: MATOKEO YA MECHI ZA JUMANNE 23 Septemba 2008


Timu za LIGI KUU Fulham na West Ham jana zilipigwa vikumbo na timu za Daraja la chini na kutolewa nje ya CARLING CUP.
Fulham ilifungwa 1-0 na Burnley wakati Watford iliipa West Ham kipigo hichohicho cha bao 1-0.
Vigogo Man U, Arsenal na Liverpool wote walishinda. Chelsea anacheza leo usiku.
Timu nyingine za LIGI KUU zilizonusurika kutolewa ni Sunderland na Stoke City ambazo zilijitutumua hadi muda wa nyongeza na kisha kushinda timu za Darala chini kwa mikwaju ya penalti.
Sunderland ilikuwa magoli mawili nyuma zidi ya Northamton Town lakini iksawazisha na kwenda muda wa nyongeza ambao haukutoa mshindi. Hivyo mikwaju ya penalti ikawapa ushindi Sunderland wa 4-3.
Nao Stoke City pia walitoka dro 2-2 na Reading mpaka wa muda wa nyongeza kwisha na wakashinda kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Arsenal 6 Sheffield United 0

Timu ya Arsenal uwanjani kwao Emirates na kikosi cha chipukizi waliibamiza timu ya Daraja la chini ya LIGI KUU Sheffield United mabao 6-0 kwenye mtoano wa CARLING CUP.
Hivyo Arsenal wanasonga mbele kuingia raundi ya nne.
Arsenal: Fabianski, Hoyte, Djourou, Song Billong (Lansbury 70), Gibbs, Randall, Ramsey, Merida (Coquelin 71), Wilshere, Bendtner (Simpson 71), Vela.
AKIBA: Mannone, Emmanuel-Thomas, Ogogo, Frimpong.
MAGOLI: Bendtner 31, 42, Vela 44, 50, Wilshere 57, Vela 87.
Sheff Utd: Kenny, Halford, Morgan, Kilgallon, Naysmith, Cotterill (Naughton 46), Speed (Hendrie 73), Quinn, Montgomery, Beattie (Robertson 76), Webber.
AKIBA: Bennett, Sharp, Geary, Ehiogu.
KADI: Halford.
REFA: Phil Dowd (Staffordshire).
WATAZAMAJI: 56,632

Man United 3 Middlesbrough 1

Mabingwa wa LIGI KUU na Ulaya Manchester United jana waliifunga Middlesbrough 3-1 katika Uwanja wa Old Trafford na kuwatoa kwenye CARLING CUP.
Man U wakiwa na kikosi mchanganyiko wa chipukizi na maveterani waliutawala mchezo kabisa licha ya timu ya LIGI KUU Middlesbrough kushusha kikosi chao cha kwanza..
Mechi hii iliingia dosari kwenye kipindi cha pili dakika ya 66 pale Pogatetz wa Middlesbrough alipocheza rafu mbaya na kumuumiza vibaya kijana mdogo wa Brazil Kiungo wa Man U Rodrigo Possebon. Refa alimpa kadi nyekundu Pogatetz na Possebon alikimbizwa hospitali baada ya kuchanika mguu na kuna wasiwasi amevunjika pia.
Man Utd: Amos, Rafael Da Silva, Vidic, Brown, O'Shea, Nani, Possebon (Gibson 72), Anderson, Giggs (Manucho 84), Welbeck, Ronaldo (Tevez 61). AKIBA: Zieler, Cleverley, Gray, Eckersley.


MAGOLI: Ronaldo 25, Giggs 79, Nani 90.

Middlesbrough: Jones, Hoyte, Wheater, Pogatetz, Taylor, Downing, Digard (Riggott 72), O'Neil, Shawky (Adam Johnson 46), Aliadiere, Alves (Emnes 85). AKIBA: Turnbull, Arca, Walker, Craddock.
KADI NYEKUNDU: Pogatetz (66).
KADI YA NJANO: Adam Johnson.

GOLI: Adam Johnson 56.

WATAZAMAJI: 53,729

REFA: Andre Marriner (W Midlands).


Tuesday 23 September 2008

CARLING CUP: vumbi kutimka leo.

Arsenal v Sheffield United

Arsenal leo wakiwa nyumbani Emirates Stadium wana nafasi nzuri kujaribu chipukizi wao kama kawaida wanavyofanya kwenye michuano hii ya Kombe la Carling kwa kuchezesha kikosi cha vijana.
Leo Arsenal wanakutana na timu ya daraja la chini Sheffield United na Meneja Arsene Wenger atawatumia vijana kama Aaron Ramsey, Jack Wilshere, Gavin Hoyte, Kieran Gibbs na Emmanuel Frimpong wakiimarishwa na wenye uzoefu kama kina Alex Song, Johan Djourou and Lukasz Fabianski.
Sheffield United wanategemewa kumtumia mkongwe wao James Beattie ambae zamani aliwahi kucheza kwenye LIGI KUU.

Liverpool v Crewe

Liverpool nao wako nyumbani kuwakaribisha Crewe timu ya daraja la chini na wanategemewa kumchezesha kwa mara ya kwanza Kipa kutoka Brazil Diego Cavalieri aliesajiliwa mwezi wa Agosti.
Inategemewa mastaa Fernando Torres na Steven Gerrard watapumzishwa.

Manchester United v Middlesbrough

Hili ni pambano linalizikutanisha timu za LIGI KUU na Manchester United watakuwa nyumbani.
Wengi wanategemea Manucho, Mshambuliaji hatari toka Angola, atachezea Man U kwa mara ya kwanza ingawa Meneja wake Sir Alex Ferguson amedokeza pengine asiwemo kwenye kikosi kwani hajapona sawasawa mguu uliovunjika mfupa wa kidole.
Wachezaji kama Anderson, Nani, Gary Neville, Cristiano Ronaldo na Owen Hargreaves wana nafasi kubwa kuwepo kwani Ferguson amesema wanahitaji michezo mingi kuwa fiti zaidi baada ya kukosa mechi nyingi kwa kuwa majeruhi.
Nao Middlesbrough huenda ikawakosa Mido, Tuncay, Jeremie Aliadiere na Adam Johnson kwa kuwa na maumivu.

RATIBA KAMILI YA LEO NI:

JUMANNE, 23 Septemba 2008

[saa 3 dak 45 bongo taimu

Arsenal v Sheffield United

Burnley v Fulham

Leeds v Hartlepool

Rotherham v Southampton

Stoke City v Reading

Sunderland v Northampton

Swansea v Cardiff

Watford v West Ham

[saa 4 usiku bongo taimu]

Liverpool v Crewe

Man U v Middlesbrough

Sir Alex Ferguson: Sasa subirini muone tukipaa!!!


Mashetani Wekundu Manchester United huenda wakawa wameuanza msimu polepole lakini Meneja wao Sir Alex Ferguson anasisitiza vimbwanga vyao vitaanza kuonekana wakati wowote kuanzia sasa.
Suluhu ya 1-1 na Chelsea siku ya Jumapili huko Stamford Bridge imewafanya wawe na pointi 5 kwa mechi 4 walizocheza lakini Ferguson ana uhakika hamna haja ya kuingiwa hofu.
'Tulikuwa na mwanzo mgumu,' Ferguson alitamka. 'Ilibidi tucheze ugenini Anfield na tulipoteza mchezo ule na Liverpool kwa kuwapa zawadi ya magoli mawil! Sasa ikabidi twende tena ugenini Stamford Bridge! Lakini tumecheza ugenini Portsmouth na kushinda
na naamini hapo Portsmouth timu nyingi zitakwama kwani ni wagumu sana kwao!'
Akaongeza: 'Ni vigumu kusema hii dro ya 1-1 na Chelsea itatufikisha wapi lakini ikifika Oktoba watu wataona Man U iko wapi- ni juu inapostahili!'
Mechi za Man U za LIGI KUU zinazofuata ni na Bolton Jumamosi hii hapo Old Trafford kisha na Blackburn, ikifuatiwa na West Brom, halafu na Everton na ya mwisho kwa mwezi Oktoba ni ya West Ham.
Ferguson aliendelea kufafanua: 'Wachezaji wengi waliokuwa majeruhi watapata mazoezi zaidi na kuwa fiti zaidi. Ronaldo na Berbatov ambao hawajacheza mechi nyingi msimu huu watakuwa wameshajijenga vizuri.'
Sir Alex Ferguson pia aliponda magazeti mengi yaliyoandika kwamba endapo Man U watafungwa na Chelsea basi watakuwa pointi 9 nyuma.
Alidai hawa wapuuzi wanasahau Man U wamecheza mechi moja pungufu.
Leo usiku saa 4 [bongo taimu] Manchester United wanaingia kwao Old Trafford kupambana na Middlesbrough kwenye mpambano wa kuwania Kombe la Carling. Ferguson ameahidi kushusha kikosi mchanganyiko wa chipukizi na mastaa ambao hawajacheza mechi nyingi msimu huu.
Amewataja Owen Hargreaves, Ji-sung Park, Nani, Anderson na Cristiano Ronaldo wote watakuwa kwenye kikosi kwa kuwa wanahitaji mechi ila kuwa fiti zaidi. Chipukizi wanaoweza kuwemo pia ni Jonny Evans, Darron Gibson, Danny Welbeck na Rafael.
Alisikitika kwamba Muangola Manucho hawezi kucheza kwani hajapona sawasawa mfupa wa kidole alichovunjika mazoezini.

'ZAKUMI': chui ambae ndie katuni rasmi wa KOMBE LA DUNIA AFRIKA KUSINI 2010!


Chui mwenye nywele 'AFRO' za rangi ya kijani ametambulishwa rasmi kama ndie atakuwa 'KATUNI' rasmi wa mashindano ya FAINALI za KOMBE la DUNIA AFRIKA KUSINI 2010 na amepewa maalum jina na tarehe yake ya kuzaliwa.


Katuni huyu ataitwa 'ZAKUMI' na tarehe yake ya kuzaliwa ni 16 Juni 1994.
Maana ya jina lake ni: Herufi mbili za kwanza 'ZA' ni kifupi cha jina la nchi yaani SOUTH AFRICA kwa lugha ya Afrikaans ambayo ni moja ya lugha 11 rasmi za nchi ya Afrika Kusini na 'KUMI' maana yake ni 10 kwa lugha nyingi za Kiafrika huko kusini na inamaanisha mwaka 2010 ambao ni mwaka wa FAINALI hizo.


Tarehe rasmi ya kuzaliwa ZAKUMI, 16 Juni 1994, ndio siku ambayo UBAGUZI WA RANGI huko Afrika Kusini ulitokomezwa rasmi.


Tarehe hii kwa sasa husheherekewa kila mwaka kama SIKU YA VIJANA ikiashiria machafuko ya Soweto ya mwaka 1976 wakati waandamanaji vijana walipoleta pigo kubwa kwa utawala dhalimu wa kibaguzi wa Weupe wachache huko Afrika Kusini.


Msemaji wa Kamati ya Maandalizi ya fainali hizo Tim Modise, wakati wa utambulisho rasmi ambako mtu alievaa guo linalofanana na ZAKUMI alicheza danadana na Mark Fish mchezaji wa zamani wa Afrika Kusini aliewasaidia kunyakua Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1996, alitamka: 'ZAKUMI hapa Afrika Kusini kwa lugha nyingi zetu za wenyeji ina maana 'NJOO HAPA''.


Nae mbunifu wa ZAKUMI, Andries Odendaal wa Cape Town, Afrika Kusini amesema nwele za kijani za chui huyu zinamaanisha nyasi za uwanja wa mpira.
FIFA walibuni mtindo wa kuwa na KATUNI mahsusi wa kila FAINALI za KOMBE la DUNIA mwaka 1966 wakati fainali zikifanyika Uingereza kwa kuwa na simba alievaa bendera ya Uingereza alieitwa Willie.


Wengine walikuwa Naranjito wa Spain mwaka 1982 aliekuwa na umbo la chungwa, mwaka 1990 huko Italia alikuwepo katuni mwenye shepu ya vijiti alievaa bendera ya Italia iliyokuwa na alama ya 'kwaheri' na Footix alikuwa jogoo wa Kifaransa mwenye rangi za bendera ya Ufaransa kwa fainali zilizochezwa nchi hiyo mwaka 1998.

Monday 22 September 2008


CARLING CUP

Kesho na Jumatano baadhi ya timu za LIGI KUU UINGEREZA wakiwemo vogogo Man U, Arsenal, Chelsea na Liverpool, watashuka dimbani ili kuchuana na timu nyingine kwenye mitoano ya kuwania CARLING CUP. Michuano hii hushirikisha timu zote bila kujali daraja wanalotoka na huchezwa kwa mtindo wa kutoana.
Msimu uliokwisha, Tottenham ndio walionyakua kombe hilo baada ya kuwafunga mabao 2-1 timu ya Chelsea kwenye Fainali iliyochezwa Uwanja wa Wembley mjini London.
Mabingwa hao watetezi wa Kombe hili la CARLING Tottenham wanaanza utetezi wao kwa kucheza ugenini na timu ya Newcastle.

JUMANNE, 23 Septemba 2008

[saa 3 dak 45 bongo taimu]

Arsenal v Sheffield United

Burnley v Fulham

Leeds v Hartlepool
Rotherham v Southampton

Stoke City v Reading

Sunderland v Northampton

Swansea v Cardiff

Watford v West Ham

[saa 4 usiku bongo taimu]

Liverpool v Crewe

Man U v Middlesbrough

JUMATANO, 24 Septemba 2008

[saa 3 dak 45 usiku bongo taimu]

Aston Villa v QPR

Blackburn v Everton

Brighton v Man City

Ipswich v Wigan

Newcastle v Tottenham

Portsmouth v Chelsea

VITA DARAJANI:
CHELSEA 1 MAN U 1


=Scolari afurahia dro!

=Ferguson ajutia nafasi za magoli ya wazi!

Rekodi ya Chelsea ya kutofungwa nyumbani kwao Stamford Bridge imeendelea kubaki baada ya Mchezaji wao Kalou kuingizwa kutoka benchi na kusawazisha
katika dakika ya 80.
Man U ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza kwenye dakika ya 18 baada ya gonga safi sana kati ya Rooney, Berbatov na Evra na kisha mpira ukadondoka kwa Ji-sung Park aliemalizia.
Mabingwa wa LIGI KUU Man U walikuwa na uwezo wa kuongeza bao la pili lakini walipoteza nafasi za wazi kadhaa.
Baaada ya mechi, Meneja wa Chelsea Scolari alisema ameridhishwa na pointi hiyo moja waliopata hasa baada ya kupata pigo kwa kuumia Mchezaji wao wa kutuimaniwa Deco wakati akipasha joto kabla ya mechi kuanza.
Nae Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson amesema hii ilikuwa nafasi murua ya kuwafunga Chelsea ila kosa lao la kupoteza nafasi za wazi za magoli ndilo liliwaua.
Chelsea: Cech, Bosingwa, Carvalho (Alex 12), Terry, Ashley Cole, Obi, Joe Cole, Ballack (Kalou 74), Lampard, Malouda (Drogba 46), Anelka.AKIBA: Cudicini, Bridge, Belletti, Ferreira.
KADI: Obi.
GOLI: Kalou 80.
Man Utd: Van der Sar (Kuszczak 32), Neville, Ferdinand, Evans, Evra, Fletcher, Hargreaves, Scholes (Ronaldo 55), Park (O'Shea 75), Berbatov, Rooney.Subs Not Used: Brown, Giggs, Nani, Tevez.
KADI: Scholes, Ferdinand, Neville, Berbatov, Rooney, Evra, Ronaldo.
GOLI: Park 18.
WATAZAMAJI: 41,760
REFA: Mike Riley (Yorkshire).

Sunday 21 September 2008


MAN CITY WAWABAMIZA PORTSMOUTH!


Wakati BIG MECHI kati ya CHELSEA v MAN U imeisha 1-1, leo MAN CITY wakiwa nyumbani waliwashindilia Portsmouth 6-0 na huu ni ushindi mkubwa wa kwanza tangu LIGI KUU ianze msimu huu.
Wafungaji wa Man City ni Jo, Richard Dunne, Robinho, Shaun Wright-Phillips na Ched Evans.

Katika mechi nyingine, Everton wakiwa ugenini wakicheza nyumbani kwa Hull City, walikuwa nyuma kwa bao 2-0, waliibuka na kurudisha na ngoma ikawa 2-2.
Magoli ya Hull City yalifungwa na Michael Turner kufuatia kona na la pili lilimbabatiza Nahodha wa Everton Phillip Neville na Kipa Tim Howard na kuingia.
Kipindi cha pili Everton walimwingiza Luis Saha kuchezea mechi yake ya kwanza tangu ahamie Everton kutoka Man U lakini walikuwa Tim Cahill aliepata bao la kwanza kwa Everton na kazi nzuri ya Luis Saha ilimfanya Leon Osman asawazishe.

Nao Tottenham Hotspurs wameendelea kusuasua baada ya kutoka dro ya 0-0 nyumbani walipocheza na Wigan.
Baada ya mechi 5 Tottenham wamepiga nanga kama timu ya mwisho kwenye msimamo wa LIGI KUU.
BIG MECHI: CHELSEA 1 MAN U 1

Mechi kubwa ya leo CHELSEA v MAN U imemalizika kwa suluhu ya 1-1.
Ji Sung Park alifunga goli kwa Man U baada ya muvu kali ya Man U dakika ya 18 lakini Chelesea walisawazisha dakika za mwisho.

Taarifa kamili baadae.

WEST BROM 1 ASTON VILLA 2

West Bromwich Albion wamepigwa mabao 2-1 nyumbani kwake na jirani zao Aston Villa.
Magoli mawili ya Aston Villa yalifungwa ndani ya dakika moja kupitia John Carew kwa kichwa maridadi na la pili lilipigwa dakika moja baadae na Gabriel Agbonlahor.
Goli la West Brom lilifungwa na James Morrison baada ya Kipa wa Aston Villa kuutema mkwaju wa Robert Koren.
Sasa macho ya wote yako kwenye mechi ya Chelsea na Mabingwa Manchester United inayoaanza sasa.
Matokeo kamili baadae.
FERGUSON v SCOLARI: mara ya pili timu timu zinazoongozwa na wao kukwaana!!


Leo saa kumi jioni saa za bongo Chelsea wanawakaribisha uwanjani kwao Stamford Bridge mjini London Mabingwa wa LIGI KUU Manchester United katika pambano linalongojwa kwa hamu dunia nzima.
Wengi wanahisi pambano hili ni kati ya timu zinazotegemewa kunyakua ubingwa wa LIGI KUU ingawa vilevile Liverpool na Arsenal pia zimo kundi hilo.
Pambano hili la leo linakutanisha Mameneja wazoefu sana kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya LIGI KUU.
Pengine wengi hawajui kuwa hii ni mara ya pili kwa timu zinazoongozwa na Sir Alex Ferguson na Luiz Felipe Scolari kupambana uso kwa uso.
Mara ya kwanza ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1999 wakati Sir Alex Ferguson alipoingoza Manchester United wakati huo ikiwa ni Bingwa wa Klabu za Ulaya kupambana na Klabu ya Brazil Palmeiras ambayo ilikuwa Klabu Bingwa ya Nchi za Marekani Kusini ikiongozwa na Meneja Luiz Felipe Scolari katika pambano la kugombea Kombe la Mabara huko Tokyo, Japan.
Bao la Nahodha Roy Keane kufuatia krosi ya Ryan Giggs liliwapa Kombe hilo Manchester United.
Alipoulizwa Scolari kama anakumbuka hilo alijibu: 'Nakumbuka wakati Ferguson akipanda jukwaani kupokea kombe mie nilikuwa tayari nimeyayuka!'

BOSI WA LIVERPOOL ALILIA GOLI!!!

Bosi wa Liverpool Rafael Benitez amelalamika vikali kuhusu kukataliwa goli lao katika mechi ya LIGI KUU jana ambayo Liverpool walitoka dro ya 0-0 na Stoke City hapo kwao Anfield.
Nahodha Steven Gerrard alipiga frikiki kwenye sekunde ya 76 tu tangu pambano lianze lakini Refa Andre Marriner akalikataa bao hilo.
Hata Meneja wa Stoke City Tony Pulis amekiri kwamba walibahatika sana kwa goli hilo kukataliwa.

MECHI YA LIGI KUU:
CHELSEA v MAN UNITED
==utambi wazidi kupulizwa!!


Sir Alex Ferguson amezidi kuchochea moto unaofukuta kwa mechi ya kesho baada ya kutoa kauli ya mzaha kuhusu Manchester United kurudi tena kucheza Uwanja wa Chelsea Stamford Bridge wakati alipokumbusha jinsi Wachezaji wake hasa Patrice Evra alivyokashifiwa, kutukanwa na kushambuliwa na Wasimamizi wa kukata nyasi za uwanja huo walipokwenda kucheza mechi msimu uliokwisha.
Ugomvi huo uliibuka mara baada ya mechi kwisha wakati Wachezaji wa Man U ambao hawakucheza mechi hiyo walitakiwa wakapashe joto uwanjani.
Wachezaji hao walikuwa ni Patrice Evra, Scholes, Tevez na Park.
Lakini walipoanza mazoezi yao wakisimamiwa na Mkufunzi wa Mazoezi wa Man U wakatokea wakata majani wa uwanja huo wa Chelsea na kuwatukana huku wakimpakia matusi ya ubaguzi Evra kwa sababu ni mweusi.

Mara ya mwisho kuja kucheza Stamford Bridge ilikuwa msimu uliokwisha ambao Man U walikuwa wanaongoza ligi na wakateremsha kikosi wengi wanadhani ni 'hafifu' ingawa bao la penalti la ya utata ndio liliwapa ushindi Chelsea ambao hata hivyo ushindi huo haukuwasaidia wao Chelsea kunyakua ubingwa.
Man U ndie alieibuka bingwa.

Kwa sasa kuna kesi FA inayowahusu Wasimamizi wa uwanja wa Chelsea na Patrice Evra.

Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson akakejeli:'Mara ya mwisho wakata nyasi walitushambulia, sasa hatujui Jumapili wameweka nini! Labda tutakuta katapila la kuvunia!'

Ferguson hakuishia hapo bali aliongeza:'Kama utatazama na kukumbuka miaka 12 au 13 ya LIGI KUU, nani ulimuona? Arsenal v Manchester United, Manchester United v Arsenal! Ndio, kwa sasa tuna Chelsea lakini historia ya Arsenal na Manchester United unazungumzia historia za klabu hizo ambazo ni historia za kweli! Sasa hao Chelsea ndio kwanzaaa wanaanza historia sisi na Arsenal tushatengeneza!!'

Ferguson akazidi kupiga msumari: 'Hawana tofauti na msimu uliokwisha! Tofauti ni kwamba hawana tena kwenye kiungo ile miguvu ya Makelele au Essien, wana Deco mchezaji mdogo, mjanja, mchezaji mzuri na hilo limesababisha tofauti ndogo ya uchezaji wao!'
Powered By Blogger