Saturday 9 August 2008


PAZIA LA MSIMU 2008/9 KUFUNGULIWA KESHO!

MAN U vs PORTSMOUTH

kugombea NGAO YA HISANI

Uwanja wa Wembley mjini London, Uingereza kesho Jumapili saa 11 jioni saa za bongo utakuwa unafungua pazia la msimu wa Soka wa 2008/9 wa Uingereza kwa pambano kati ya Mabingwa wa LIGI KUU Manchester United na Mabingwa wa Kombe la FA Portsmouth watakapogombea NGAO YA HISANI.
Manchester United ndio Mabingwa watetezi wa Ngao hiyo baada ya kuwashinda Chelsea mwaka jana kwa penalti.
Portsmouth mara ya mwisho kulishika kombe la aina hii ni mwaka 1949 walipotoka suluhu na Wolverhampton na ikabidi wagawane kombe hilo kwa miezi sita sita.
Timu hizi mbili zilikutana mara ya mwisho mjini Abuja, Nigeria wiki mbili zilizokwisha katika mechi ya kirafiki ambayo Man U walishinda 2-1.
Timu zote zina majeruhi kadhaa na watakao kuwa nje kwa Man U ni Ronaldo, Rooney, Park, Hargreaves na Saha. Man U inategemewa itawachezeshaji chipukizi kutoka Brazil ambao wako timu yao ya akiba ambao ni ndugu mapacha Fabio na Rafael Da Silva pamoja na Possebon.
Portsmouth huenda ikakawakosa Kanu, Lauren na Nugent.
Refa katika mechi hii atakuwa Peter Walton ambae ameteuliwa dakika za mwisho tu baada ya Refa aliepangwa Mark Clattenburg kusimamishwa na FA na PGMO [Uongozi wa Marefa wa Kulipwa] kutokana na Kampuni zake kufilisika.
Wachezaji wanategemwa kuwa:
Manchester United : Van der Sar, Kuszczak, Neville, Brown, R Da Silva, Ferdinand, Vidic, O'Shea, Evans, Evra, Silvestre, F Da Silva, Nani, Carrick, Scholes, Fletcher, Gibson, Possebon, Giggs, Martin, Tevez, Campbell.
Portsmouth : James, Johnson, Campbell, Distin, Hreidarsson, Utaka, Diop, Pedro Mendes, Kranjcar, Crouch, Little, Sahar, Diarra, Defoe, Davis, Kanu, Wilson, Duffy, Lauren, Nugent, Mvuemba, Cranie, Ashdown.
Real Wang’aka: Robinho hauzwi!
Kibao chawageukia!!!
Real Madrid baada ya kumwandama na kujaribu kumrubuni Ronaldo kwa muda mrefu sasa kibao kimewageukia wenyewe baada ya kujikuta wakiandamwa na Chelsea waliotoa ofa rasmi na ya hadharani ya kutaka kumnunua Robinho.
Imebidi Rais wa Real Ramon Calderon ajitetee vikali na kudai Robinho haondoki klabuni hapo ingawa Robinho mwenyewe anataka kuhama.
Siku ya Alhamisi Chelsea walitoa ofa ya kumnunua Robinho kwa Pauni milioni 19.7 na mwenyewe Robinho anataka sana kuungana na Meneja Mbrazil wa Chelsea Felipe Scolari.
Ramon Calderon alisisitiza: ‘Hamna njia Robinho ataondoka! Ni mchezaji wetu bora!’

MAN U KUSAINI MSHAMBULIAJI KABLA YA WIKI IJAYO!!!!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson ana matumaini ya kumsaini mshambuliaji mmoja kabla msimu mpya wa ligi haujaanza wiki ijayo.
"Tunaangalia njia tatu au nne hivi na tunategemea kufanikiwa," alisema Ferguson.
Mshambuliaji wa Tottenham Dimitar Berbatov inasemekana yuko kwenye listi hiyo ya wachezaji watatu au wanne wanaowaniwa. Wengine wanaotajwa ni Mchezaji wa Valencia David Villa, Klaas-Jan Huntelaar wa Ajax, Mshambuliaji wa Lyon Karim Benzema na wa Blackburn Roque Santa Cruz.
Kwa sasa Man U inakabiliwa na upungufu wa washambuliaji hasa ikizingatiwa Wayne Rooney mgonjwa ingawa Ijumaa alianza mazoezi, Ronaldo yuko nje kwa wiki 6 akiuguza enka aliyofanyiwa operesheni na hali ya Luis Saha kama kawaida ni ya kutotegemewa.
Juu ya Saha, Ferguson alitamka: ‘Kwanini ukate tamaa kuhusu Saha ati kwa sababu ameumia kidogo? Akiwa fiti ni hatari sana na anaweza kufunga zaidi ya magoli 20 kwa msimu. Kwa sasa yupo chini ya programu maalum na akifanikiwa hiyo tutakuwa na mchezaji fiti na wa kutumainiwa.’

Friday 8 August 2008



FERGUSON: NI VIGUMU RONALDO KUHAMA

Baada ya kuhakikisha Cristiano Ronaldo anabakia kuwa mchezaji wa Man U, Sir Alex Ferguson anahisi Winga huyo wa Ureno ataona shida sana kuihama klabu hiyo kadri anavyozidi kukaa.
‘Tuna furaha.’ Bosi huyo alitamka leo. ‘Kama nilivyosema ishu hii imekufa. Yeye ni mchezaji wa Manchester na ana furaha kuwa hapa. Ni basi tu hawa Real walijaribu kumrubuni na kufanya maisha yake kuwa magumu.’
Ferguson aliongeza: ‘Kitu muhimu tumemaliza huu upuuzi wa Real. Kadri anavyokua ndio ataridhika kuwa hapa. Hii siku zote imetokea kwa wachezaji wanaokuwa hapa muda mrefu. Hawataki kuondoka!’
‘Mtizame Rio Ferdinand aliejiunga nasi akiwa mdogo tu kutoka Leeds United! Leo ni mchezaji wa kweli kweli wa Manchester United! Anaipenda klabu kwa moyo wote! Na Rio anatoka nchi nyingine…….anatoka London! Ni dunia nyingine kule! Hamna tofauti kati ya mtu anaehama London au Ureno na kuja Manchester. Unakuja hapa ni baridi sana, mvua nyingi! Lakini unakuja kwenye mji wa soka na miji mingi si hivi!’
Ferguson akamalizia: ‘Sasa Real wanatambua wanapambana na mnyama mwingine kabisaa!’

RONALDO: FERGUSON NI KAMA BABA YANGU WA PILI!
Nae Ronaldo alipohojiwa anahisi nini kuhusu imani ya Sir Alex Ferguson kuwa hahami Man U, alijibu: ‘Niamini kabisa, najisikia mwenye majivuno sana kujua Sir Alex ananithamini sana. Na yeye anajua namthamini sana. Yeye ni mtu muhimu sana katika maisha yangu. Si kwa sababu ya niliyojifunza kwake na ambayo ntaendelea kujifunza lakini vilevile ni kwa utu na ubinadamu wake. Ana hisia kubwa katika soka. Kama inawezekana basi maisha yote ningependa abaki na mimi na awe karibu yangu. Najua haiwezekani lakini yeye siku zote amekuwa kama baba yangu wa pili. Sitosahau aliponikabidhi jezi ya MAN U yenye namba 7 na kuniambia maana yake [Namba 7 Man U ilivaliwa na nyota George Best na Bryan Robson]. Daima itakuwa namba yangu. Sir Alex Ferguson amekuwa mtu muhimu katika maisha yangu ya soka. Kwa sababu hiyo, na kwa sababu tuna uhusiano wa karibu sana, najua anafahamu vizuri sana wakati gani awe na wasiwasi na nini kilicho bora kwa mwanawe.’
Jens Lehmann astaafu kuchezea Ujerumani
Kipa Jens Lehmann [umri miaka 38] ametangaza kustaafu kuchezea Timu ya Taifa ya Ujerumani.
Kipa huyo wa zamani wa Arsenal ametoa uamuzi huo mara baada ya mkutano na Meneja wa Ujerumani Joachim Low.
Lehmann ameichezea Ujerumani mara 61 katika kipindi cha miaka 10 na mara ya mwisho ilikuwa kwenye Fainali ya EURO 2008 walipofungwa na Spain ambayo ilitwaa ubingwa huo.
Lehmann alijiunga na Arsenal mwaka 2003 na juzi tu amehamia Klabu ya Stuttgart ya Ujerumani kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Wengi wanategemea atastaafu soka baada ya mkataba huu kumalizika.
WENGER AFURAHIA RONALDO KUBAKI MAN U!
REAL WASHUSHUKA, WAFUNGA MIDOMO!
Arsene Wenger amesema amefurahishwa na habari kwamba Cristiano Ronaldo atabaki Manchester United.
Amesema: ‘Nimefurahi kwa sababu anatuletea vitu spesho kwenye LIGI KUU. Tunataka iwe ligi bora duniani hivyo ni muhimu wachezaji bora wacheze hapa. Nimefurahi sakata hili limeisha kwa busara na watu wameheshimu mikataba. Ingesikitisha sana kumuona mmoja wa wachezaji bora duniani akidharau mkataba na kuondoka tu!’
Wakati huohuo, Rais wa Real Madrid, Ramon Calderon, amedai hajui kama Ronaldo amewashushua na akaongeza hataki kuongea lolote kuhusu mchezaji huyo!

Nae Meneja wa Real Bernd Schuster amesema: ’Inasikitisha kwani ni mchezaji ambae angetuinua sana! Lakini hatujali! Tuna kundi la wachezaji wazuri hapa.’
FERGUSON APINGA VIKWAZO KWA WACHEZAJI WASIO RAIA WA UINGEREZA LIGI KUU
Sir Alex Ferguson amewasihi viongozi wa Soka wa Uingereza wasiburuzwe katika kuweka vikwazo kwa wachezaji kutoka nje ya Uingereza kuchezea LIGI KUU UINGEREZA.
Meneja huyu wa Manchester United akiandika utangulizi wa gazeti rasmi la ufunguzi wa msimu wa 2008/9 wa LIGI KUU UINGEREZA alihoji: ‘Kwa nini uhangaike kutengeneza kitu wakati hakijaharibika?’
"Kumekuwa na lawama kwenye vyombo vya habari na wito wa kuweka idadi maalum ya Wachezaji wasio Waingereza kucheza mechi ili kuhakikisha Waingereza wanapata namba.’ Aliandika Ferguson. ‘Mimi sikuchezesha Wachezaji 6 Waingereza kwenye Fainali ya LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA kwa sababu tu za kisiasa mie niliwachagua wale kwa sababu tu walikuwa na uwezo wa kunyakua Kombe hilo.’
Alikuwa akimaanisha Wachezaji Waingereza 6 wa MAN U walioanza Fainali ya LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA walipowafunga Chelsea. Wachezaji hao ni Wes Brown, Rio Ferdinand, Owen Hargreaves, Michael Carrick, Paul Scholes na Wayne Rooney.
FIFA imeshika bango ikitaka Wachezaji wasio raia wawekewe vikwazo kwenye LIGI KUU UINGEREZA hali ambayo inaelekea kuungwa mkono na UEFA na FA, Chama Soka Uingereza.
Lakini Ferguson anapinga hilo na kudai wageni hawazuii Waingereza kujitokeza na kuonyesha umahiri wao na anaonya hatua hiyo ya FIFA, UEFA na FA huenda ikaibomoa LIGI KUU UINGEREZA kutoka ligi bora, ngumu na yenye sifa duniani kitu kilichodhirishwa na kuwa na Timu 4 kwenye Nusu Fainali ya LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA msimu uliopita na hatimaye Kombe kuchukuliwa na Timu ya Uingereza-Manchester United.
......................KUHUSU RONALDO FERGUSON ASEMA:
'Kadri anavyokua ndio atajua na kukubali na kuridhika kwamba Man U ndio klabu anayostahili kuwepo. Mtizame Rio Ferdinand. Sasa humbandui hapa. Lakini nimefurahi sana upumbavu huu wa Real Madrid umekwisha. Sasa wanajua vizuri wanapambana na watu gani!'

RATIBA SOKA:
OLYMPIC BEIJING 2008


JUMAPILI 10 Agosti 2008
Saa 7 mchana
Argentina v Australia
Nigeria v Japan,
New Zealand v Brazil
Cameroon v Honduras
Saa 9 dak 45 mchana
Serbia v Ivory Coast
USA v Netherlands
Belgium v China
Italy v South Korea


JUMATANO 13 Agosti 2008
Saa 7 mchana
Nigeria v USA
South Korea v Honduras
Cameroon v Italy
Netherlands v Japan
Saa 9 dak 45
Argentina v Serbia
New Zealand v Belgium
Ivory Coast v Australia
China v Brazil

MATOKEO YA SOKA OLYMPIC BEIJING 2008:
Alhamisi 7 Agosti 2008

KUNDI A:

Australia 1-1 Serbia

Ivory Coast 1-2 Argentina

KUNDI B:

Japan 0-1 USA

Netherlands 0-0 Nigeria

KUNDI C:

Brazil 1-0 Belgium

China 1-1 New Zealand

KUNDI D:

Honduras 0-3 Italy

South Korea 1-1 Cameroon
CHELSEA WATOA KITITA KUMNUNUA ROBINHO!!!
Chelsea wametangaza wametoa ofa ya Pauni milioni 19 kwa Real Madrid ili kumnunua Winga wa Brazil Robinho.

Inasemekana Robinho hana furaha Real na ukweli ni kwamba tangu ahamie hapo hana namba ya kudumu.
Endapo Chelsea watafanikiwa kumchukua Robinho basi huyu atakuwa Mbrazil wa pili kutua hapo tangu Meneja Mbrazil Scolari aanze kazi Chelsea.

Wa kwanza ni Mchezaji wa Ureno aliezaliwa Brazil Deco aliesainiwa kwa dau la Pauni milioni 8 kutoka Barcelona.

Thursday 7 August 2008

Refa wa LIGI KUU UINGEREZA Mark Clattenburg asimamishwa!!
-ALIKUWA ACHEZESHE MECHI YA NGAO YA HISANI YA MAN U vs PORTSMOUH JUMAPILI!!!!
Chama cha Soka Uingereza [FA] na Bodi ya Marefa wa Kulipwa [PGMO] vimetangaza kumsimamisha Refa anaechezesha LIGI KUU UINGEREZA Mark Clattenburg kutokana na Kampuni zinazohusiana na yeye kupigwa mufilisi kisheria.


FA na PGMO vimesema imekuwa ni busara Refa huyo asimamishwe ili uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu madeni na kufilisika kwa kampuni zake ili hadhi ya Soka Uingereza isitiwe dosari.
Mark Clattenburg alipangwa kuchezesha mechi ya Jumapili tarehe 10 Agosti 2008 ya ufunguzi rasmi wa msimu wa 2008/9 wa Soka Uingereza kugombea NGAO YA HISANI kati ya Mabingwa wa LIGI KUU MAN U na Mabingwa wa Kombe la FA PORTSMOUTH itakayochezwa Uwanja wa Wembley.

Nafasi ya Refa huyu kuchezesha mechi hiyo itachukuliwa na Peter Walton.
UHAMISHO LIGI KUU UINGEREZA
Fulham wamemchukua Mshambuliaji Andy Johnson kutoka Everton kwa dau la Pauni milioni 10 na nusu.
Andy Jonhson ilikuwa asaini mkataba tangu mwezi uliokwisha lakini kukawa na mzozo baada ya matokeo ya kupimwa afya kuonyesha goti lake sio timamu na kuwatia kiwewe Fulham na ikabidi wawalazimishe Everton wapunguze ada waliyoitaka ya Pauni milioni 12.
Jonhson sasa amesaini mkataba wa miaka minne.
=============================================
Aston Villa wamekubaliana na Middlesbrough ili wamnunue Mlinzi Luke Young ambae msimu uliopita alinunuliwa na Middlesbrough kutoka Charlton kwa ada ya Pauni milioni 2 na nusu.
Aston Villa watalipa Pauni milioni 5 kumchukua mchezaji huyo.
=============================================
Klabu Klabu ya Deportivo La Coruna ya Spain imetangaza mchezaji wake Fabricio Coloccini anahamia Newcastle.
Coloccini [26] ni Mlinzi kutoka Argentina na alitishia kuishitaki Deportivo La Coruna kama klabu hiyo haimruhusu kuhama.
=============================================
West Ham imemwachia huru Kiungo Freddie Ljungberg [31] baada ya makubaliano kufikiwa kukatisha mkataba wake.
Mchezaji huyu wa zamani wa Kimataifa wa Sweden na Arsenal huenda akastaafu soka kwa sababu ya kuumia.
Alijiunga na West Ham kutoka Arsenal Julai 2007 kwa ada ya Pauni milioni 3 na kwa mkataba wa miaka minne.
Msimu aliopita alicheza mechi 22 kati ya mechi 38 za LIGI KUU kwani aliandamwa na kuumia mara kwa mara. Mara ya mwisho alivunjika mbavu.
Alicheza EURO 2008 akiwa Nahodha wa Sweden na alitangaza kujiuzulu kucheza mechi za Kimataifa mara tu baada ya Sweden kutolewa mashindano hayo.
=============================================
Bolton wamesaini mkataba wa kumnunua Mnigeria mlinzi Danny Shittu [27] kutoka Klabu ya daraja la chini Watford kwa dau ambalo halikutangazwa.
Mnigeria huyu amechezea Timu ya Taifa ya Nigeria mechi moja na awali alishachezea klabu za QPR na Charlton zote za Uingereza.
=============================================
Blackburn imemsaini mdogo wake Mshambuliaji wao hatari kutoka Paraguay Roque Santa Cruz.
Julio Santa Cruz [18] ametoka Klabu ya Paraguay iitwayo Cerro Porteno na atajiunga na Blackburn Rovers mara tu baada ya kupata kibali cha uhamisho cha kimataifa.

RONALDO ATAMKA: ‘NABAKI MAN U!’
Baada ya miezi kadhaa ya utata Cristiano Ronaldo jana usiku alithibitisha kwamba atabaki Manchester United.
Alisema: ‘Nathibitisha ntachezea Man U msimu ujao. Ntacheza kwa roho na moyo wangu wote na ntapigana na kulinda heshima ya jezi ya Man U nnayovaa kama nilivyokuwa nafanya siku zote. Kocha wangu Sir Alex Ferguson alifanya wema sana kuja kuniona mjini Lisbon siku chache zilizopita. Tulikuwa na mazungumzo ya wazi na ukweli kati ya watu wawili wanaopendana, wanaoheshimiana na wenye urafiki mkubwa. Sir Alex alinisikiliza na mimi nikamsikiliza na tukaona ni bora kwa pande zote nibaki Old Trafford. Kwa hilo sijitoi muhanga ila ni heshima kubwa. Kuna vitu muhimu vya kushinda nchini Uingereza. Nataka kutetea taji letu la Ulaya na kuisaidia Man U kuwa Mabingwa wa Dunia bila kusahau LIGI KUU na mashindano mengine. ’
Ronaldo akaongeza: ‘Sikutaka kuondoka Man U bila ridhaa yao na nitasema kitu ambacho sijamwambia mtu yeyote- laiti tusingechukua Ubingwa wa Ulaya nisingefikiria kuhama Man U. Lakini tulipochukua ubingwa huo, nilihisi miaka mitano nlokaa Man U nimesaidia kushinda kila kitu. Tulichukua LIGI KUU mara mbili na binafsi nimeshinda tuzo kadhaa ikiwa pamoja na Mfungaji Bora LIGI KUU na LIGI ya KLABU BINGWA ULAYA. Nilihisi nahitaji chalenji nyingine. Nilijua Real Madrid wananitaka na kwa muda nilitaka Man U wakubali ofa yao. Nilitaka kucheza Spain ili kuwa karibu na familia yangu. Lakini nataka hili liishe.’
Kwa unyenyekevu, Ronaldo akaongeza: ‘Nafahamu Klabu hii imenifanyia mengi. Daima ntashkuru. Walipokataa ofa ya Real ilionyesha dhahiri jinsi wanavyonithamini. Wakati ule sikuelewa hili vizuri lakini sasa nashkuru sana hilo lilitokea.’
Jana usiku Sir Alex Ferguson alizungumza: ‘Mashabiki lazima wafahamu ni vigumu sana kwa kijana mdogo kuvumilia wakati akirubuniwa na mihela kibao. Hasa kwa kijana alietoka Madeira [sehemu fukara huko Ureno nyumbani kwa Ronaldo]. Baba yake alikufa akiwa mdogo na jukumu la kuwatunza mama yake, dada na kaka yake liko kwake. Ronaldo siku zote ana furaha hapa. Haya yote sasa yamekwisha.’

Wednesday 6 August 2008

SAKATA LA RONALDO LAISHA!!!!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson ametamka jana kuwa sakata la Cristiano Ronaldo kuhama sasa limekwisha na winga huyo atabaki OLD TRAFFORD.
Tangu kuisha Fainali ya LIGI ya KLABU BINGWA ULAYA mwezi Mei ambayo Man U walitawazwa kuwa Mabingwa wa Ulaya, uvumi ambao hasa ulichochewa na Real Madrid ulizagaa kwamba Ronaldo atanunuliwa na klabu hiyo ya Spain.
Ronaldo jana alirudi Manchester baada ya mapumziko na vilevile kujiuguza baada ya operesheni ya enka aliyofanyiwa Amsterdam, Uholanzi mwezi uliopita.
Habari hizi za Ronaldo kubaki Man U zinathibitika kwa kauli ya Rais wa Real Madrid Ramon Calderon aliyoitoa jana hiyo aliposema: ‘Rafael van der Vaart ni mchezaji pekee tutakae msaini msimu huu’.
Jana hiyohiyo Real ilimtambulisha rasmi mchezaji huyo wa Kiholanzi Rafael van der Vaart iliemnunua kutoka Hamburg ya Ujerumani.
Sir Alex Ferguson alimaliza sakata hili lililodumu tangu Mei kwa msisitizo: ‘Jambo hili limekwisha. Yeye ni mchezaji wa Manchester United-mwisho! Atacheza hapa msimu ujao.’
Cristiano Ronaldo ana mkataba unaoisha mwaka 2012 na alisaini mkataba huu wa sasa mwaka jana tu.
.....NA ROONEY MGONJWA!!
Mshambuliaji Wayne Rooney huenda akaikosa mechi ya ufunguzi ya LIGI KUU UINGEREZA ya tarehe 17 Agosti wakati Man U itakapocheza na Newcastle kwa sababu ni mgonjwa.
Sir Alex Ferguson alisema jana: ’Sidhani kama Rooney atakuwa fiti. Aliugua tulipokuwa Nigeria na hajafanya mazoezi tangu wakati huo.’
Kuugua kwa Rooney ni tatizo kubwa kwa Man U kwani Ronaldo hatakuwepo uwanjani kwa takriban miezi miwili baada ya operesheni, Nani amefungiwa mechi mbili kwa kupewa kadi nyekundu msimu uliokwisha, Anderson yuko na Timu ya Brazil huko Beijing kwenye Olympic na Saha ni majeruhi.
Hivyo, Man U imebakiwa na fowadi mmoja tu- Carlos Tevez.
Inategemewa chipukizi Frazier Campbell [20] ataingizwa
kikosi cha kwanza kuleta sapoti.

Tuesday 5 August 2008

Van Nistelrooy astaafu kuchezea UHOLANZI!!!
Mshambuliaji mahiri Mholanzi anaechezea Real Madrid, Ruud van Nistelrooy [32], ametangaza kustaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Uholanzi aliyoanza kuichezea mwaka 1998 na kuifungia magoli 33 na kumfanya kuwa Mfungaji Bora wa 3 katika historia ya timu hiyo.
Hakucheza EURO 2000 kutokana na kuwa majeruhi lakini alicheza na kufunga kwenye EURO 2004, EURO 2008 na Kombe la Dunia mwaka 2006.
Ruud van Nistelrooy alijijengea jina alipokuwa Klabu ya PSV Eindhoven ingawa aliumia vibaya goti lakini hilo halikumzuia Sir Alex Ferguson kumchukua kwenda MAN U mwaka 2001 kwa Pauni milioni 19 na kuweka rekodi ya Uingereza ya kununua mchezaji kwa bei ghali kwa wakati huo.
Alikaa MAN U kwa miaka mitano iliyojaa mafanikio makubwa na mwaka 2006 akahamia Real Madrid kwa dau la Pauni milioni 10.
SOKA: OLYMPIC BEIJING 2008
Mechi za soka katika mashindano ya OLYMPIC BEIJING 2008 zitaanza Alhamisi tarehe 7 Agosti 2008 huku timu zikiwa zimegawanywa katika makundi manne ya timu 4 kila kundi na zitacheza kwa mtindo wa ligi.
Timu mbili za juu zitaingia raundi inayofuata.

Makundi ni:

KUNDI A: IVORY COAST, ARGENTINA, AUSTRALIA, SERBIA

KUNDI B: UHOLANZI, NIGERIA, JAPAN, USA

KUNDI C: CHINA, NEW ZEALAND, BRAZIL, UBELGIJI

KUNDI D: KOREA, CAMEROUN, HONDURAS, ITALY

Kufuatana na taratibu za FIFA, wachezaji wanaoruhusiwa kucheza michuano hii ni lazima wawe chini ya umri wa miaka 23 ingawa kila timu inaruhusiwa kuwa na wachezaji watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 23.

RATIBA YA MECHI ZA KWANZA:
ALHAMISI 7 AGOSTI 2008

KUNDI A: AUSTRALIA VS SERBIA [SHANGHAI STADIUM]
KUNDI A: IVORY COAST VS ARGENTINA [SHANGHAI STADIUM]

KUNDI B: JAPAN VS USA [TIANJIN OLYMPIC SPORTS CENTER]
KUNDI B: HOLLAND VS NIGERIA [TIANJIN SPORTS CENTER]

KUNDI C: BRAZIL VS BELGIUM [SHENYANG CENTER]
KUNDI C: CHINA VS NEW ZEALAND [SHENYANG CENTER]

KUNDI D: HONDURAS VS CAMEROUN [QINHUANGDAO CENTER]
KUNDI D: KOREA VS CAMEROUN [QINHUANDAO CENTER]
Ronaldo arudi Manchester!!
Mwezi mmoja baada ya kufanyiwa opresheni ya enka ya mguu wa kulia huko Amsterdam, Uholanzi, Cristiano Ronaldo leo anarudi mjini Manchester kwa uchunguzi zaidi ambao ndio utabaini ni lini anaweza kurudi tena uwanjani.
Wakati Ronaldo anatua Manchester vyombo vingi yva habari hasa vya Spain vinachukulia kurudi kwake ni kwa sababu moja tu na ambayo ni kwenda kumuona Meneja wa MAN U Sir Alex Ferguson na kudai uhamisho ili aende Real Madrid wakisahau kwamba Ronaldo ni mchezaji halali wa MAN U mwenye mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo!!!!
Ingawa MAN U wameshakataa katakata kwamba Ronaldo hauzwi Real Madrid na vigazeti vya Spain vimeendelea kumrubuni Ronaldo ahamie huko.
Kampeni hii sasa imeanza kuwaudhi hata wachezaji wa Real ambao wengi wameanza kutamka hadharani kuwa sasa wao kama mastaa wanadharauliwa na anapewa kipau mbele Ronaldo ambae si mchezaji wa Real.
Juzi Ruud van Nistelrooy alithibitisha kero hii ya wachezaji wa Real na akaongeza kwa kusema kwa jinsi anavyomjua Ferguson basi akishasema mchezaji hahami basi ujue
hahami.
Blackburn wamchukua kinda wa Man Utd Simpson
Beki chipukizi wa Man U Danny Simpson ameenda Blackburn Rovers kwa mkopo.
Simpson [21] alicheza Man U mechi 8 msimu uliopita na ameshawahi kuchezea kwa mkopo timu za Sunderland, Ipswich na klabu ya Ubelgiji Royal Antwerp.
Mpaka sasa, Blackburn ishawasaini wachezaji watatu kwa msimu ujao na wengine ni aliekuwa Kipa wa Uingereza Paul Robinson na Carlos Villanueva.
Drogba ATAKOSA MWANZO WA LIGI
Didier Drogba[30] atakosa kucheza mwanzo wa msimu kutokana na kuuguza goti alilofanyiwa operesheni. Taarifa hii imethibitishwa na Meneja wa Chelsea Scolari ambae amesema hatochezi mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Wigan tarehe 16 Agosti 2008 lakini inawezakana akacheza mechi ya pili na Tottenham tarehe 31 Agosti 2008.
Scolari ametamka Niicolas Anelka atacheza nafasi ya Drogba.

Sunday 3 August 2008


Mshambuliaji wa Misri atua UINGEREZA kwa KISHINDO
Mshambuliaji wa Zamalek na Timu ya Taifa ya Misri Amr Zaki ameanza kuichezea Timu ya Wigan iliyo LIGI KUU UINGEREZA kwa nyota njema baada ya kufunga goli la tatu na la ushindi walipoifunga SHEFFIELD UNITED 3-2 katika mechi ya kirafiki.
Amr Zaki yuko WIGAN kwa mkopo kutoka ZAMALEK ya Misri.



Ferguson kumpa nafasi chipukizi Frazier Campbell
Meneja wa MAN U, Sir Alex Ferguson, amesema chipukizi Frazier Campbell atapewa nafasi kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha MAN U kwa sababu ana uwezo wa kufunga, mwepesi, mpiganaji mzuri na amethibitisha hayo baada ya kung’ara katika ziara ya Afrika ya hivi karibuni.
Frazier Campbell, miaka 20, jana alifunga goli la ushindi katika mechi ya kumuaga nyota wa MAN U, Ole Gunnar Solskjaer, hapo jana dhidi ya Espanyol ya Spain. MAN U ilishinda 1-0.

Vilevile, chipukizi huyu alikuwa mmoja wa wachezaji walioisaidia sana Hull City kupanda daraja na kuingia LIGI KUU UINGEREZA wakati alipoichezea timu hiyo kwa mkopo msimu ulopita.
Ferguson alitamka: ‘Ni mwepesi na ana bidii sana. Hapo baadae atakuwa nyota hapa. Tunategemea kupata kibali cha Manucho [Mchezaji mshambuliaji toka Angola] atasaidia kuimarisha safu ya washambuliaji. Campbell na Manucho ni muhimu kwani tuna upungufu safu hii. Tuna Washambuliaji wawili tu- Rooney na Tevez.’
Powered By Blogger