Saturday 2 August 2008



Ole Gunnar Solskjaer aagwa OLD TRAFFORD!
MAN U 1 ESPANYOL 0
Akicheza dakika 25 za mwisho, leo Jumamosi, Agosti 2, 2008, Ole Gunnar Solskjaer aliagwa rasmi kuchezea MAN U katika mechi mahsusi iliyoandaliwa kwa ajili yake dhidi ya ESPANYOL ya Spain.
Katika mechi hii MAN U walipata bao lao la ushindi katika dakika ya 82 mfungaji akiwa chipukizi Frazier Campbell.
Ole Gunnar Solskjaer, umri miaka 35, alilazimika kustaafu soka Agosti 2007 baada ya kuumia goti.
Mechi ya kumuaga ilichezwa nyumbani kwa MAN U Uwanja wa OLD TRAFFORD na ilihudhuriwa na Watazamaji 68,868.
MAN U iliwakilishwa na wachezaji wafuatao [kwenye mabano ni wachezaji wa akiba walioingizwa pamoja na dakika waliyoingia]:
Van der Sar (Kuszczak 46); Simpson, Ferdinand (Brown 46), Vidic (Evans 62), Evra (Silvestre 46); Gibson (O’Shea 62), Fletcher, Scholes, Nani (Campbell 46); Giggs, Tevez (Solskjaer 68)

THURAM ASTAAFU SOKA KWA UGONJWA WA MOYO!!!!!!
Lilian Thuram, beki wa zamani wa Ufaransa, ametangaza kustaafu soka kwa sababu ya kuwa na ugonjwa wa moyo.
Thuram, mwenye umri wa miaka 36, alitegemewa kujiunga Klabu ya Ufaransa Paris St-Germain mwezi Juni mwaka huu lakini akagunduliwa ana maradhi ya moyo kwenye ukaguzi wa kawaida wa afya wa kabla ya kusaini mkataba.
Thuram, ambae alikuwemo kwenye kikosi cha Ufaransa kilichonyakua Kombe la Dunia mwaka 1998, alitangaza kustaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Ufaransa mara tu Ufaransa ilipotolewa kwenye mashindano ya EURO 2008
Juni mwaka huu.

ADEBAYOR KUBAKI ARSENAL,
GALLAS KUBAKI NAHODHA
Imethibitishwa kwamba mshambuliaji Emmanuel Adebayor amepewa mkataba mwingine ambao una nyongeza ya mshahara kufikia Pauni 70,000 kwa wiki na hivyo kuzima zile tetesi anataka kufuata nyayo za wenzake waliohama Arsenal akina Alexander Hleb, Mathieu Flamini na Gilberto Silva.
Wakati huohuo Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amethibitisha William Gallas ataendelea kuwa Nahodha wa Arsenal kwa msimu ujao.


Baada ya Arsenal kuporomoka vibaya kiuchezaji wakati LIGI KUU UINGEREZA inaelekea ukingoni habari zilizagaa kwamba Gallas atatemwa unahodha kwenye msimu huu unaokuja.


BLACKBURN WAMSAINI MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA CHILE
Meneja wa Blackburn, Paul Ince, ametamka kwamba klabu yake imempata Mchezaji Bora wa Chile kiungo Carlos Villanueva [miaka 22] kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka kwa Klabu ya Audax Italiano ya Chile.
Mchezaji huyu anategemewa ataziba pengo lililoachwa na David Bentley aliehamia Tottenham hivi juzi.

Friday 1 August 2008

ARSENAL KUIKWAA TIMU YA MENEJA WA ZAMANI UINGEREZA STEVE McCLAREN!!!!
UEFA wametangaza timu zitakazopambana kwenye Raundi ya Tatu ya Mtoano katika mashindano ya LIGI YA KLABU BINGWA ZA ULAYA baada ya kupigwa kura.
Katika raundi hii mechi zitachezwa tarehe 12 na 13 Agosti na marudiano ni tarehe 26 na 27 Agosti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Arsenal imepangwa kukutana na timu ya Uholanzi FC Twente inayoongozwa na aliekuwa Meneja wa Timu ya Taifa ya Uingereza Steve McClaren ambae alitimuliwa kazi hiyo Novemba 2007.
Liverpool itakutana na Standard Liege ya Ubelgiji.
Mechi zimepangwa kama ifuatavyo:
Anorthosis au Rapid Vienna v Olympiakos

Vitoria Guimaraes v IFK Gothenburg au BaselShakhtar

Donetsk v Domzale au Dinamo Zagreb

Schalke 04 v Atletico Madrid

Aalborg au Modrica v RANGERS au Kaunas

Barcelona v Beitar Jerusalem au Wisla Krakow

Levski Sofia v Anderlecht au BATE

Standard Liege v LIVERPOOL

Inter Baku au Partizan v Fenerbahce au MTK Budapest

FC Twente v ARSENAL

Spartak Moscow v Drogheda au Dinamo Kiev

Juventus v Tampere au Artmedia

SK Brann au Ventspils v Marseille

Fiorentina v Slavia Prague

Galatasaray v Steaua Bucharest

Panathinaikos au Dinamo Tbilisi v Sheriff Tiraspol au Sparta Pragu

Washindi 16 wa mechi hizi watajumuika na timu nyingine 16 ambazo ni Mabingwa wa Nchi na washindi wa pili wa ligi za nchi [Timu kutoka Uingereza ni Mabingwa Man U na washindi wa pili Chelsea] kufanya jumla ya timu 32 zitakazogawanywa makundi manane ya timu 4 kila moja zitakazocheza mtindo wa ligi.Mechi hizi za makundi zitaanza tarehe 16 Septemba na kumalizika Desemba 10.
SOKA: OLYMPIC BEIJING 2008
Mashindano ya OLIMPIKI ambayo safari hii yanachezwa nchini China na yanajulikana kama OLYMPIC BEIJING 2008 yataanza wiki ijayo kwa michuano katika michezo ya kila aina.
Katika soka mechi zitaanza kuchezwa tarehe 7 Agosti 2008 na timu zilizofuzu kuingia OLYMPIC BEIJING 2008 ni:
-AFRICA: CAMEROON, NIGERIA, IVORY COAST
-ASIA: AUSTRALIA, JAPAN, CHINA, JAMHURI YA KOREA
-ULAYA: UBELGIJI, UHOLANZI, ITALIA, SERBIA
-MAREKANI KASKAZINI & KATI: HINDURAS, USA
-OCEANIA: NEW ZEALAND
-MAREKANI KUSINI: ARGENTINA, BRAZIL
Timu hizi zimegawanywa katika makundi manne ya timu 4 kila kundi na zitacheza kwa mtindo wa ligi na timu mbili za juu zitaingia raundi inayofuata.
Makundi ni:
KUNDI A: IVORY COAST, ARGENTINA, AUSTRALIA, SERBIA
KUNDI B: UHOLANZI, NIGERIA, JAPAN, USA
KUNDI C: CHINA, NEW ZEALAND, BRAZIL, UBELGIJI
KUNDI D: KOREA, CAMEROUN, HONDURAS, ITALY
Kufuatana na taratibu za FIFA, wachezaji wanaoruhusiwa kucheza michuano hii ni lazima wawe chini ya umri wa miaka 23 ingawa kila timu inaruhusiwa kuwa na wachezaji watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 23.
Wachezaji nyota na maarufu ambao wataonekana uwanjani kwenye michuano hii ni pamoja na Ronaldinho, Anderson, Pato [wakiwakilisha Brazil], Riquelme, Lionel Messi, Macherano [Argentina], Ryan Babel [Uholanzi].
BAADA YA KUTOLEWA JELA SASA FA YAMSHITAKI BARTON!
Chama cha Soka Uingereza FA kimemtaka mchezaji wa Newcastle Joey Barton, ambae juzi tu alitolewa jela baada ya kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi 6 baada ya kumjeruhi kijana mmoja nje ya hoteli mjini Liverpool, ajitetee kwanini hatua za nidhamu zisichukuliwe dhidi yake kwa kumshambulia na kumjeruhi mchezaji mwenzake mazoezini wakati alipokuwa akichezea Timu ya Manchester City.
Tukio hilo la Joey Barton kumpiga na kumuumiza mchezaji mwenzake Mfaransa Ousmane Dabo [pichani ni Ousmane Dabo na Joey Barton] lilitokea mwezi Mei 2007 na lilifikishwa Mahakamani tarehe 1 Julai 2008 ambako alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi minne baada ya kukiri kosa.
Hukumu hii ilitoka wakati tayari Barton alikuwa jela akitumia kifungo chake cha miezi 6 kwa kujeruhi.
Endapo atapatikana na hatia basi FA inaweza kumfungia kwa muda mrefu na kumpiga faini.
Klabu ya Newcastle imelalamikia hatua hii ya FA na kuhoji uhalali wa wao kuadhibiwa kwa kosa lililotendeka wakati mchezaji anamilikiwa na klabu jingine. Wakati Barton anatenda kosa hilo alikuwa ni mchezaji wa Manchester City na mfarakano huo ndio uliomfanya ahamishiwe Newcastle. Vilevile, Newcastle imelalamika kwa nini Barton ashitakiwe takriban miezi 15 baada ya kosa lenyewe kutendeka.
ARSENAL NA LIVERPOOL KUJUA WAPINZANI WAO WA LIGI YA MABINGWA ULAYA LEO!!!!
LEO IJUMAA TAREHE 1 AGOSTI 2008 saa 7 mchana zitapigwa kura kuamua timu zipi zitakutana kwenye Raundi ya Tatu ya Mtoano wa LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA.
Timu zilizoingia Raundi hii zimegawanywa makundi mawili ambamo Timu za KUNDI LA KWANZA zitacheza na Timu za KUNDI LA PILI.

KUNDI LA KWANZA: Liverpool; Barcelona; Arsenal; Schalke; Juventus; Mshindi kati ya Rangers au Kaunas; Marseille; Steaua Bucharest; Mshindi kati ya Panathinaikos au Dinamo Tbilisi; Mshindi kati ya IFK Gothenburg au Basle; Olympiacos; Mshindi kati ya Fenerbahce au MTK Hungaria; Shakhtar Donetsk; Mshindi kati ya Anderlecht au BATE; Fiorentina; Spartak Moscow.
KUNDI LA PILI: Atletico Madrid; Mshindi kati ya Sheriff Tiraspol au Sparta Prague; Mshindi kati ya Drogheda au Dynamo Kiev; Levski Sofia; Slavia Prague; Galatasaray; Mshindi kati ya Inter Baku au Partizan Belgrade; Victoria Guimaraes; Mshindi kati ya Domzale au Dinamo Zagreb; Mshindi kati ya Beitar Jerusalem au Wisla Krakow; Standard Liege; Twente Enschede; Mshindi kati ya Tampere au Artmedia Bratislava; Mshindi kati ya Aalborg au Modrica; Mshindi kati ya Brann au Ventspils; Anorthosis Mshindi kati ya Famagusta au Rapid Vienna

Hii ina maana vigogo kama Liverpool, Barcelona, Arsenal, Juventus na kadhalika hawawezi kukutana kwa kuwa wote wako KUNDI LA KWANZA.
Katika raundi hii mechi zitachezwa tarehe 12 na 13 Agosti na marudiano ni tarehe 26 na 27 Agosti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Washindi 16 wa mechi hizi watajumuika na timu nyingine 16 ambazo ni Mabingwa wa Nchi na washindi wa pili wa ligi za nchi [Timu kutoka Uingereza ni Mabingwa Man U na washindi wa pili Chelsea] kufanya jumla ya timu 32 zitakazogawanywa makundi manane ya timu 4 kila moja zitakazocheza mtindo wa ligi.
Mechi hizi za makundi zitaanza tarehe 16 Septemba na kumalizika Desemba 10.

Thursday 31 July 2008



UHAMISHO LIGI KUU UINGEREZA: Tottenham wamnunua Bentley
Tottenham wamemsaini kiungo David Bentley kutoka Blackburn Rovers kwa thamani ya Pauni milioni 18.
Mwenyekiti wa Blackburn Rovers John Williams ametamka kuwa Bentley alipasi vipimo vya afya siku ya Jumatano na Klabu ya Tottenham leo itatoa tamko rasmi kuhusu uhamisho huu.
Bentley [23], ambae pia huchezea Timu ya Taifa ya Uingereza, aliingia Blackburn mwaka 2006 akitokea Arsenal na ameifungia Blackburn magoli 13 katika mechi 102 za LIGI KUU UINGEREZA. Pia ameshaichezea Timu ya Taifa ya Uingereza mara 6.
Tottenham mpaka sasa imeshawauza Paul Chimbonda, Teemu Tainio, Steed Malbranque [wote wamehamia Sunderland] na Kipa Paul Robinson alieenda Blackburn. Na mpaka sasa imewanunua mshambuliaji Giovani Dos Santos, kiungo Luca Modric na Heurelho Gomes.
.......................Na Newcastle wamchukua Bassong
Mlinzi wa Klabu ya Ufaransa Metz, Sebastien Bassong ambae pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa ya Vijana chini ya miaka 21, amejiunga na Newcastle.
Bassong alikuwemo kwenye kikosi cha Newcastle kinachojitayarisha kwa msimu ujao ingawa alikuwa hajahama rasmi.
Sasa imethibitishwa Bassong ni mchezaji halali wa Newcastle.

Wednesday 30 July 2008


ARSENAL WAMSAJILI BISCHOFF
Arsenal wamethibitisha kwamba wamemsaini Kiungo wa Klabu ya Ujerumani Werder Bremen Amaury Bischoff, mwenye miaka 21, ambae ingawa alizaliwa Ufaransa huichezea Timu ya Taifa ya Vijana wa chini ya miaka 21 ya Ureno.
Bischoff hakuwa akichezeshwa mara kwa mara alipokuwa Werder Bremen lakini Arsene Wenger anaamini ana kipaji kitakachoisaidia Arsenal hapo baadae.
Bischoff atavaa jezi namba 28 akiwa Arsenal na inasadikiwa ataziba mapengo yaliyoachwa na Viungo Mathieu Flamini, Gilberto na Alexander Hleb waliohama timu.

UHAMISHO LIGI KUU UINGEREZA WAPAMBA MOTO!!!!!!!!!!!
Malbranque apimwa afya Sunderland................Atakuwa mchezaji wa tatu toka Tottenham kutua Sunderland!
Steed Malbranque, kiungo mwenye umri wa miaka 28, leo amepimwa afya yake Klabuni Sunderland na endapo mambo yataenda sawa basi atakuwa mchezaji wa tatu kutoka Tottenham kuchukuliwa na Sunderland ndani ya wiki moja.
Wengine waliokwenda Sunderland kutoka Tottenham wiki hii ni beki Pascal Chimbonda na kiungo Teemu Tainio.
Ilitegemewa vilevile beki mwingine wa Tottenham Younes Kaboul angekwenda Sunderland lakini sasa inaelekea atajiunga na Portsmouth.

Stoor atua Fulham!
Fulham imemnunua mchezaji wa Kimataifa wa Sweden Fredrik Stoor kwa mkataba wa miaka mine kutoka Klabu ya Norway ya Rosenberg.
Stoor ni beki wa pembeni na alicheza mechi zote za Sweden kwenye EURO 2008.



Ben Haim aenda Man City!
Beki Myahudi Tel Ben Heim amehamia Manchester City kutoka Chelsea kwa dau ambalo halikutangazwa. Ben Heim alijiunga Chelsea msimu uliopita lakini uchezaji wake ulikuwa wa nadra kwani alishindwa kupata namba ya kudumu kwani Chelsea siku zote walikuwa wakiwapanga John Terry na Ricardo Carvalho.
SAHA KUHAMISHWA MAN UNITED?
Luis Saha ni mchezaji kipenzi wa mashabiki wengi wa Man U hasa kwa umahiri na ustadi wake wa kushambulia na kufunga magoli lakini wengi wanahuzunika sana kwa jinsi anavyoandamwa na maumivu ya mara kwa mara na kumfanya acheze kwa nadra sana.
Luis Saha alicheza mechi 24 tu msimu uliopita alioandamwa mfululizo na majeruhi hasa goti lililomsumbua muda mrefu sana.
Inasemekana Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson, ameshakata tamaa kuhusu Saha na yuko tayari kumuuza.
Tayari Klabu za Fulham, Bolton, Roma, Paris St Germain na Monaco zinapigana vikumbo kumnunua ingawa wengi wanaamini ataenda kwa Kepteni wa zamani wa Man U, Roy Keane, kwenye timu ya Sunderland.
Kuuzwa kwa Saha kunaonekana hakuepukiki hasa ikizingatiwa Man U inamuwania Dimitar Berbatov wa Tottenham ingawa vilevile inadaiwa washambuliaji wengine wanatajwa kuwemo kwenye listi ya wachezaji wanaowindwa na Man U.
Listi hiyo ina majina ya Roque Santa Cruz wa Blackburn Rovers, Klaas Jan Huntelaar wa Ajax na hata Thierry Henry yumo!!

KINDA WA MAN U AJIUNGA BURNLEY
Mchezaji chipukizi wa Man U, Chris Eagles, ambae aling’ara katika ziara ya Afrika ya Man U ya hivi juzi alipofunga magoli katika mechi dhidi ya Kaiser Chiefs huko Afrika Kusini na Portsmouth mjini Abuja, Nigeria, amehamia timu ya Burnley inayochezea kwenye LIGI YA COCA COLA ambayo ni ligi chini tu ya LIGI KUU UINGEREZA.
Chris Eagles, mwenye umri wa miaka 22, alieanza kuichezea Man U tangu akiwa na miaka 14 ameshindwa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Man U na muda mwingi aliishia kupelekwa kucheza kwa mkopo kwa timu nyingine.
Timu alizowahi kucheza kwa mkopo ni Watford, Sheffield Wednesday na Klabu ya Uholanzi ya NEC Nijmegen.

LEE CATTERMOLE AENDA WIGAN
Kiungo wa Middlesbrough, Lee Cattermole, miaka 20, anaechezea Timu ya Taifa ya Uingereza ya Vijana wa chini ya miaka 21, amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Wigan kwa dau ambalo halikutangazwa.
Mpaka sasa Wigan imeshanunua wachezaji Olivier Kapo na Daniel de Ridder kutoka Birmingham City na imemchukua mchezaji wa Misri mshambuliaji Amr Zaki kutoka Klabu ya Zamalek kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Tuesday 29 July 2008

UHAMISHO.....ni rasmi sasa!!!!!!!

ROBBIE KEANE YUKO LIVERPOOL!!

Robbie Keane wa Tottenham amehamia Liverpool kwa dau la Pauni milioni 20. Keane amesaini mkataba wa miaka mitano na atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 80,000 kwa wiki.
Liverpool ni Klabu ya sita kwa Keane baada ya kuzichezea Klabu za Wolves, Coventry, Inter Milan na Leeds kabla ya kuhamia Tottenham mwaka 2002.

...............................DIOUF YUKO SUNDERLAND!!!

Nae Msenegali machachari, El Hadji Diouf, rasmi ametua Sunderland kwa uhamisho wa Pauni milioni 2 na nusu kutoka Bolton. Diouf, miaka 27, aliingia Bolton mwaka 2005 akitokea Liverpool.
Tayari Meneja wa Sunderland Roy Keane ameshawasaini wachezaji wawili kutoka Tottenham ambao ni Teemu Tainio na Pascal Chimbonda.

......................PENGO LA DIOUF BOLTON LAZIBWA!!!!!!!!!!!!!!

Baada ya kumpoteza Diouf, Bolton tayari wamepata mtu wa kuziba pengo baada ya kumsajili Winga Mdachi ambae ni mzaliwa wa Ghana Mustapha Riga kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mustapha Riga aliichezea Timu ya Taifa ya Uholanzi ya Vijana wa chini ya miaka 21 na ametokea Klabu ya Spain Levante ambayo msimu uliopita imeshuka daraja.

Monday 28 July 2008




UHAMISHO LIGI KUU UINGEREZA

Mshambuliaji wa Everton Andy Jonhson yuko njiani kuhama na inasemekana leo amepimwa afya yake kwenye Klabu nyingine ya LIGI KUU UINGEREZA Fulham.

Nae Robbie Keane wa Tottenham anaripotiwa kuwa atachukuliwa na Liverpool kwa dau la Pauni milioni 20. Mazungumzo ya uhamisho huu yanadaiwa yako hatua za mwisho.
Inasemekana Keane atasaini mkataba wa miaka mitano na atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 80,000 kwa wiki.
Vilevile inadaiwa tayari ashapimwa afya yake na kinachongojwa tu kwa sasa ni pande zote husika kutia saini mkataba na kuutangaza rasmi.

Na wakati huohuo, Msenegali machachari wa Klabu ya Bolton, El Hadji Diouf, leo yupo Sunderland akikaguliwa afya yake kabla hajasaini mkataba wa uhamisho wa Pauni milioni 2 na nusu.
Diouf, miaka 27, aliingia Bolton mwaka 2005 akitokea Liverpool.
Tayari Meneja wa Sunderland Roy Keane ameshawasaini wachezaji wawili kutoka Tottenham ambao ni Teemu Tainio na Pascal Chimbonda.
Roy Keane anadaiwa vilevile yuko mbioni kuwasaini wachezaji wengine wawili kutoka Tottenham na wanaotajwa ni Steed Malbranque na Younes Kabul.
MUNTARI ATUA INTER MILAN
Mchezaji wa Ghana na Timu ya LIGI KUU UINGEREZA Portsmouth, Sulley Muntari, miaka 23, amesaini mkataba wa miaka minne kwenye Klabu ya Italia Inter Milan.
Muntari ni mchezaji wa pili kusainiwa na Meneja mpya wa Inter Milan Jose Mourinho.

Wa kwanza ni Winga kutoka Klabu ya Roma Roberto Mancini.
BARTON AFUNGULIWA JELA!
Mchezaji kiungo wa Newcastle Joey Barton [pichani akitoka geti la jela leo asubuhi] ameachiwa kutoka jela baada ya kutumikia kifungo cha siku 74 katika adhabu yake ya kufungwa miezi 6 baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga na kumjeruhi kijana mmoja nje ya hoteli mjini Liverpool Desemba 27 mwaka jana.
Barton alilakiwa nje ya geti la gereza na rafiki yake mmoja na alikataa kuongea na waandishi habari.
Jana Meneja wa Newcastle, Kevin Keagan, alitamka Joey Barton ataendelea kuichezea klabu hiyo ili kumpa nafasi kujirekebisha kinyume na fikra za wengi kuwa atafukuzwa klabuni.
Wakati akiwa kifungoni, Barton alipatikana na hatia katika kesi nyingine alipompiga na kumjeruhi mchezaji mwenzake wakati akiwa Manchester City.
Mfaransa Ousmane Dabo alipigwa na Barton kwenye mazoezi na kitendo hicho kilisababisha ahamishwe Manchester City na kwenda Newcastle.
Barton alikwepa jela kwenye kesi hii baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi minne.

MAN U WASHINDA TENA AFRIKA!!!!!!!!!!!!!!!!

MAN U 2 PORTSMOUTH 1

Wakicheza mechi yao ya pili ndani ya siku mbili barani Afrika, MAN U leo wameifunga timu ya LIGI KUU UINGEREZA PORTSMOUTH mabao 2-1 katika UWANJA WA TAIFA mjini Abuja, Nigeria.

Jana, Man U walicheza Pretoria, Afrika Kusini na kuwafunga wenyeji wao Kaiser Chiefs 4-0 na kutwaa Kombe la VODACOM.

Katika mechi ya leo, mabao ya Man U yalifungwa na Chris Eagles na Carlos Tevez. Bao la Portsmouth lilifungwa na Jermaine Defoe.

Timu hizi zitakutana tena katika mechi ya kufungua pazia msimu mpya wa mwaka 2008/9 wa Uingereza kwa kushindania NGAO YA HISANI Uwanja wa Wembley, tarehe 10 Agosti 2008.

Timu hizi zinakutana kwa sababu Man U ni Bingwa wa LIGI KUU na Portsmouth ndie alieshinda Kombe la FA.

Sunday 27 July 2008

Keegan ampa mchezaji mfungwa Barton nafasi kujirekebisha!!!!
Meneja wa Newcastle Kevin Keegan amesisitiza ni haki na ubinadamu kumpa Mchezaji wake alie jela nafasi ya kujirekebisha kwa kumruhusu kuendelea kuichezea Newcastle atakapofunguliwa.
Kiungo Joey Barton alihukumiwa kifungo cha miezi 6 jela baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia na kumjeruhi kijana mmoja nje ya hoteli mjini Liverpool. Adhabu yake hiyo inaisha wiki ijayo na hatua ya Keegan kumsamehe imezima dhana na uvumi kuwa mchezaji huyo mwenye historia ya ukorofi atafukuzwa.
Wakati akitumikia kifungo hiki cha miezi 6 Barton alipatikana na hatia ya kumjeruhi mchezaji mwenzake kwenye kesi nyingine wakati alipokuwa Manchester City. Mfaransa Ousmane Dabo alipigwa na Barton kwenye mazoezi na kitendo hicho kilisababisha ahamishwe Manchester City na kwenda Newcastle. Barton alikwepa jela kwenye kesi hii baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi minne.

MAN U WAUA BONDENI!
Man U jana walitwaa Kombe la Vodacom kwenye Uwanja wa Loftus huko Pretoria, Afrika Kusini walipowabamiza Kaiser Chiefs kwa mabao 4-0.
Wakichezesha timu yenye mchanganyiko wa chipukizi na mastaa wao wa kila siku, Man U walifunga mabao kupitia mkongwe Giggs, dakika ya 40, staa Rooney, dakika ya 57, machipukizi Cleverley, dakika ya 62 na Frazier Campbell, dakika ya 86.
Leo, Man U wako nchini Nigeria watakapokumbana na timu nyingine ya LIGI KUU UINGEREZA Portsmouth kwenye mechi ya kirafiki.
CHIMBONDA AHAMIA SUNDERLAND.
Beki Mfaransa wa Tottenham, Pascal Chimbonda, amekuwa mchezaji wa pili wa Tottenham kuhamia Sunderland baada ya kiungo Teemu Tainio kufanya hivyo siku tatu zilopita.
Kabla ya kwenda Tottenham, Chimbonda alikuwa akichezea Wigan.

***************************************************************************************
KIPA WA BLACKBURN BRAD FRIEDEL AENDA ASTON VILLA.
Kipa mkongwe Mmarekani, Brad Friedel, umri miaka 37, amehamia Klabu ya Aston Villa akitokea Klabu yake ya siku nyingi Blackburn Rovers aliyoichezea kwa miaka minane na jumla ya mechi 287.
Juzi, Blackburn walimnunua aliekuwa Kipa nambari wani wa Uingereza Paul Robinson kutoka Tottenham.
Powered By Blogger