Saturday 5 July 2008

RUSHWA SERIE A ITALIA!
Wachezaji watano wa Serie A, LIGI YA JUU huko Italia, wameshtakiwa kwa kupanga matokeo ya mechi ambayo ilihusisha timu za Atalanta na timu iliyoshushwa daraja Livorno. Mashtaka hayo yanahusu mechi zote mbili za timu hizo za nyumbani na ugenini za msimu uliopita ulioisha mwezi Mei.
Mchezaji wa Atalanta Gian Paolo Bellini na aliekuwa Nahodha wa Livorno David Balleri wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga matokeo. Ndugu wawili na wachezaji wa Livorno Emanuele na Antonio Filippini pamoja na mchezaji mwingine wa timu hiyo Alessandro Grandoni wameshtakiwa kwa kosa la kutotoa taarifa kwa wahusika kuhusu maovu hayo.
Timu hizo zilitoka sare 1-1 tarehe 23 Decemba 2007 na mechi ya marudiano ya tarehe 4 Mei 2008 Atlanta walishinda 3-2.
Klabu zote hizo mbili zipo pia matatani mbele ya vyombo vya soka.
Soka ya Italia si ngeni kwa tuhuma za rushwa na kupanga matokeo mechi.
Mwaka 2006, Klabu maarufu za Lazio, Fiorentina na AC Milan zilinyang’anywa pointi kwa kupanga matokeo na Juventus wakashushwa daraja.

RONALDO KUPASULIWA!
Cristiano Ronaldo anategemewa kufanyiwa operesheni ya kisigino wiki ijayo na hii inamaanisha atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita kuanzia hapo na hivyo kuukosa mwanzo wa msimu mpya wa LIGI KUU UINGEREZA ambao utaanuliwa rasmi tarehe 10 Agosti 2008 kwa pambano la kugombea NGAO YA HISANI kati ya Bingwa wa LIGI KUU, Manchester United, na Bingwa wa Kombe la FA, Portsmouth kwenye Uwanja wa Wembley.
LIGI KUU yenyewe inaanza rasmi tarehe 16 Agosti 2008 kwa Man United kupambana na Newcastle.
Kwa sasa Ronaldo yuko kwenye likizo na hatakuwa na timu yake kwenye ziara ya Afrika ambako Man United itatembelea Afrika Kusini na Nigeria mwishoni mwa Julai.
Siku za hivi karibuni utata mkubwa umekuwa ukimzunguka Ronaldo kuhusu hatma yake ambako amehusishwa kuhamia Real Madrid na hata ikabidi Man United waripoti mbinu za Real Madrid kumrubuni Ronaldo kwa FIFA na klabu hiyo itoe kauli kali ‘hauzwi’.
Jana tena Man United wamesisitiza msimamo kuwa hauzwi na kuziita tarifa kuwa anahama ni UPUMBAVU na VICHEKESHO VITUPU.
Hata dada yake Ronaldo amethibitisha Ronaldo hana mpango wa kuhama Man United.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
ADEBAYOR KWENDA BARCELONA?
Wakati Ronaldo bado ni fumbo kuna taarifa za chinichini ambazo zimepewa uzito mkubwa kuwa Klabu ya Barcelona ishakubaliana na Arsenal kumnunua Adebayor kwa Pauni Milioni 30.
Mchezaji huyu alinunuliwa na Arsenal kwa Pauni milioni 5 hivi miaka miwili nyuma toka Klabu ya Monaco na msimu uliopita aliifungia Arsenal mabao 30.
Arsenal inasemekana wamekubali shingo upande kumuuza hasa kufuatia ukweli kwamba mchezaji mwenyewe anataka kuhama kwa sababu tu hamna njia yeyote mshahara wake wa Pauni 35,000 kwa wiki unaweza kupandishwa kwani Klabu ya Arsenal ina kanuni kwamba mishahara ya wachezaji ina viwango maalum huku wengi wakiwa kwenye daraja la Pauni 50,000 kwa wiki.
Inategemewa Adebayor akiwa Barcelona atapata mshahara wa zaidi ya Pauni 100,000 kwa wiki.


Friday 4 July 2008



UHAMISHO LIGI KUU.................................


Middlesbrough wamemsajili Mshambuliaji wa Sparta Rotterdam ya Uholanzi Marvin Emnes kwa Pauni za Kiingereza milioni £3.2m.
Emnes, miaka 20, amesaini mkataba wa miaka minne baada ya kukubaliana na Middlesbrough malupulupu binafsi na kufaulu vipimo vya kiafya. Mchezaji huyo aliezaliwa mjini Rotterdam huichezea Timu ya Taifa ya Uholanzi ya vijana wa chini ya miaka 21 na msimu uliopita aliteuliwa Mchezaji Bora wa Klabu yake Sparta Rotterdam
.

Galatasaray wanadai wamemsaini Harry Kewell ingawa Klabu yake ya Liverpool haijathibitisha. Tovuti ya Klabu hiyo ya Kituruki imesema Kewell, miaka 29, amesaini mkataba wa miaka mitatu baada ya Meneja wa Liverpool Rafael Benitez kukataa kumuongezea muda.
Kewell yupo Liverpool kwa miaka mitano sasa ingawa muda mwingi ni majeruhi.

Fulham wamempata mlinzi kutoka Finland aitwae Toni Kallio, umri miaka 29, kwa mkataba wa kudumu wa miaka miwili baada ya kuja hapo Januari mwaka huu kwa mkopo. Mchezaji huyo alitokea Klabu ya Uswisi BSC Young Boys.





BEKI WA USWISI AJIUNGA LIVERPOOL
Liverpool wamemsaini mlinzi wa Timu ya Taifa ya Switzerland Philipp Degen kutoka klabu ya Kijerumani Borussia Dortmund. Mchezaji huyo mwenye miaka 25 ni beki wa kulia na itabidi agombee namba hiyo na mabeki wengine wawili wa kulia Alvaro Arbeloa na Steve Finnan.
Degen amesaini mkataba wa miaka mine na alikuwa mchezaji wa akiba kwenye EURO 2008 iliyoisha hivi juzi.
CRESPO SASA RASMI NJE CHELSEA!
Mshambuliaji Hernan Crespo amehama rasmi Chelsea baada ya mkataba wa Muargentina huyo kuisha.
Crespo, umri miaka 33, alijiunga Chelsea 2003 na akapelekwa AC Milan kwa mkopo mwaka mmoja baadae. Akarudi tena Chelsea msimu wa 2005/06 na kuisaidia kunyakua Ubingwa wa LIGI KUU UINGEREZA.
Baada ya msimu huo akarudishwa tena kwa mkopo AC Milan na inasemekana sasa atasaini mkataba wa kudumu na Inter Milan baada ya Bosi wake wa zamani Jose Mourinho kuteuliwa Meneja wa Inter Milan
.

Sunday 29 June 2008

SPAIN BINGWA EURO 2008

tangu 1964 hawajachukua kombe lolote!

Torres aizima Ujerumani!

Mshambuliaji wa Liverpool Fernando Torres alitumia kosa la Philipp Lahm, shujaa wa Ujerumani kwenye Nusu Fainali na Uturuki, kufunga bao la ushindi na kuwapa Spain nchi ambayo haijashinda kombe lolote kwa miaka 44, Kombe la EURO 2008!

Wenger ataka Ronaldo abaki!
-Na Adebayor adengua!
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger anaamini ni muhimu kwa Manchester United kuhakikisha Cristiano Ronaldo anabaki Old Trafford ili kupinga juhudi zisizo halali za Real Madrid kumchukua.
Wenger ameusifia msimamo wa Man United wa kukataa kuzungumza na mtu yeyote kuhusu uhamisho wa Ronaldo kwa sababu anataka LIGI KUU UINGEREZA iimarike zaidi na zaidi. Vilevile amesisitiza Real Madrid wamevunja sheria kwa kujaribu kumrubuni Ronaldo.
Alipoulizwa kama yeye binafsi anataka Ronaldo ahamie Spain alijibu:"Hapana, hapana hata kidogo! Mie nataka kuwe na msimamo. Nataka LIGI KUU UINGEREZA iwe bora duniani na nataka nijue nikiwafunga Man United, nikiwafunga Chelsea, basi nazifunga timu bora duniani!’’
Wakati huo huo, Arsene Wenger amesisitiza Emmanuel Adebayor atabaki Arsenal msimu ujao kwa sababu ana mkataba na klabu hiyo. Adebayor mwenyewe na vyombo vya habari lukuki vimekuwa vikisema anahama ingawa haijulikani waziwazi anahamia wapi.
REFA ROBERTO ROSETTI- Mtaliano atakaechezesha FAINALI!
Germany wanamkumbuka Refa huyu hasa baada ya kipigo kitakatifu walichokipata kwenye mechi ya kirafiki tarehe 28 April 2004 walipobamizwa na Romania 5-1.
Hata hivyo Roberto Rosetti alikuwa Refa hivi karibuni tu wakati Germany waliposhinda ugenini 2-1 dhidi ya Czech Republic kwenye mechi za mitoano ya awali kuwania nafasi za kuingia Fainali za EURO 2008.
Spain nao wana hisia tofauti na Mtaliano huyu.
Roberto Rosetti alikuwa Refa kwenye Kombe la Dunia 2006 Spain walipofungwa 3-1 na France katika Robo Fainali. Kwenye mechi za mitoano ya awali kuwania nafasi za kuingia Fainali za EURO 2008 Roberto Rosetti alikuwa mwamuzi kwenye mechi ya Spain walipowatoa Sweden 3-0.
Leo, Roberto Rosetti atawapa bahati nani?


FAINALI: misuli v ustadi!


Bila shaka Euro 2008 imetupa utamu hasa baada ya kuuzoea ule uhondo wa LIGI KUU UINGEREZA iliyomalizika Mei. Kweli tumeshuhudia mechi 30 zilizojaa ufundi, ari, utata, vipaji na leo tupo kwenye mechi ya mwisho-FAINALI, kati ya Ujerumani na Uhispania.
Leo ni mashindano kati ya Nguvu asilia na Akili kichwani! Ni patashika ya Misuli ya Ujerumani na Ustadi wa Uhispania!
Ujerumani wakiongozwa na Meneja ‘kijana’ Joachim 'Jogi' Low, umri miaka 48, ambae hupenda kuvaa ‘kileo’ na Spain wana meneja ‘mzee’ Luis Aragones, miaka 69, ambae wengi humtambua ni mkorofi na haogopi kusema kitu chochote!
Meneja wa zamani wa Uingereza Graham Taylor ananena: "Kimkakati, ni vita kati ya mchezo wa pasi fupifupi na wepesi wa Spain dhidi ya mpira wa moja kwa moja wa Ujerumani ambao daima wao vita mbele tu!"
Graham Taylor anaongeza: "Spain wanajua kucheza aina moja ya mchezo tu! Kushambulia! Kiuchezaji wanafanana na Arsenal na hivyo ikiwa Ujerumani watawaachia waje kushambulia tu na kuwavizia kwa mashambulizi ya kushtukiza, Ujerumani watapotea! Nguvu ya Ujerumani ni mipira ya juu na mipira ya juu ni udhaifu mkubwa wa Spain!"





njia ya kuingia fainali!
GERMANY- KUNDI B
-GERMANY 2 POLAND 0
-GERMANY 1 CROATIA 2
-GERMANY 1 AUSTRIA 0
ROBO FAINALI
GERMANY 3 URENO 2
NUSU FAINALI
GERMANY 3 TURKEY 2
SPAIN- KUNDI D
SPAIN 4 RUSSIA 1
SPAIN 2 SWEDEN 1
SPAIN 2 GREECE 1
ROBO FAINALI
SPAIN 0 ITALY O [4-2 kwa penalti]
NUSU FAINALI
SPAIN 3 RUSSIA O
NAHODHA WA UJERUMANI HATIHATI KUCHEZA!
Michael Ballack aumia mazoezini!

Spain mfumo wawachanganya!
Nahodha wa Germany Michael Ballack yuko kwenye hatihati ya kutocheza Fainali ya Euro 2008 baada ya kupata maumivu mguuni na kusababisha akose mazoezi Ijumaa na Jumamosi.
Kuikosa mechi hii kwa Ballack, mwenye umri wa miaka 31, kutakuwa pigo kubwa kwa Ujerumani kwa kumkosa Nahodha wao na vilevile kwa Ballack binafsi kwani mwaka 2002 aliikosa Fainali ya Kombe la Dunia alipofungiwa kucheza kutokana na kadi.
Kwa upande wa Spain, zaidi ya kumkosa mfungaji bora wa EURO 2008, David Villa, ambae ni majeruhi na hachezi fainali, timu haina tatizo kubwa isipokuwa kuamua mfumo upi watautumia- ama 4-5-1 ukimfanya Fabregas awe kati pamoja na viungo wengine wanne huku Fernando Torres akiwa mshambuliaji pekee au wacheze 4-4-2 na hivyo Fabregas awe benchi na timu iwe na washambuliaji wawili yaani Torres na Daniel Guiza.
Huo ndio mtihani unaoikabili Spain ambayo haijachukua kombe lolote kubwa tangu mwaka 1964 waliponyakua Kombe la Mataifa ya Ulaya.
USO KWA USO
Germany na Spain zimeshakutana mara 19 huku Wajerumani wakishinda mara 8 na Spain mara 5.
Katika Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa Ulaya washakutana mara 5 Ujerumani ikishinda mara 3 na Spain mara 1 tu.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ni kwenye mechi ya kirafiki Februari 2003 na Spain walishinda 3-1.
Powered By Blogger