Saturday 28 June 2008


MBINU ZA FAINALI: Germany vs Spain
MIFUMO:
Kocha wa Ujerumani Joachim Low itabidi aamue aufuate mfumo upi: ama ule wa 4-5-1 uliowaua vizuri Wareno lakini ulishindwa kufanya kazi vizuri katika mechi na ‘Wapiganaji wa Kituruki’ au fomesheni yake ya kila siku ya 4-4-2.
Nae Kocha wa Spain Luis Aragones yeye ametumia 4-4-2 katika mechi zote za EURO 2008 isipokuwa mechi ya Nusu Fainali dhidi ya Urusi alipolazimika kumtoa pacha mwenza wa Fernando Torres, David Villa alieumia, na kumwingiza staa na kiungo wa Arsenal Cesc Fabregas na hivyo kubadilisha fomesheni na kuwa 4-5-1.
Mfumo huo ulifanikiwa sana na Spain ikaibuka mshindi 3-0 na hivyo watalaam wengi wanahisi ndio utakaotumiwa kwenye fainali.
UBORA:
Ushujaa na moyo thabiti wa kiume wa kutokata tamaa kihistoria ndio nguzo ya Ujerumani. Daima wao wanaamini filimbi ya mwisho ndio inaamua mshindi. Na ndio maana wanaitwa ‘MASHINE YA KIJERUMANI’.
Ubora wa Spain uko kwenye utaalam na ufundi wao wa kusakata kandanda linalodhihirisha vipaji vya hali ya juu. Pamoja na hayo wana mfumo bora wa uchezaji ambao umewafanya wawe hawajafungwa katika jumla ya mechi 21 mpaka sasa.
UDHAIFU:
Germany ilionekana mchovu na ngome yao ilipwaya kwa muda mrefu katika mechi ya Nusu Fainali na Uturuki. Kipa Jens Lehmann, miaka 38, alionyesha kabisa kuwa zama zake zimekwisha na ndio maana ametemwa na Arsenal.
Spain hawana nguvu kwenye mipira ya juu ya vichwa kote kwenye ulinzi na ushambuliaji na hili, ingawa halijawaletea athari kwenye EURO 2008, ndio utakuwa mwanya wa Ujerumani.
NGOME:
Kipa wa Ujerumani na walinzi wanne wa nyuma wana uzoefu mkubwa ingawa walipwaya kwenye mechi ya Uturuki. Walinzi wa kati Per Mertesacker na Christoph Metzelder ni imara kukabili senta fowadi wa aina ya Torress ingawa wanapata shida kuwasimamisha viungo wanaoshambulia wa aina ya Fabregas na Andres Iniesta.
Defensi ya Spain haijapwaya. Kipa Iker Casillas na beki wa kati Carles Puyol bado hawajaifungisha timu huku beki wa kulia Sergio Ramos ameonekana mwepesi sana kupanda juu kwenda kushambulia.
VIUNGO:
Michael Ballack hakung’ara siku alipocheza na Uturuki lakini yeye ni mchezaji mkubwa na ni dhahiri atajituma kwenye mechi hii kubwa ambayo atasaidiwa na viungo wa pembeni mawinga Bastian Schweinsteiger na Lukas Podolski huku Torsten Frings akitegemewa kuongeza moto wa injini ya ‘MASHINE YA KIJERUMANI’.
Pasi zenye uhakika na usahihi za viungo wa Spain pamoja na kuingizwa ‘mpishi’ Fabregas ndicho kilichowaua Warusi. Na kama viungo hao watacheza kama hivyo basi patashika ipo.
MASHAMBULIZI:
Miroslav Klose, ambae amefunga goli moja moja katika mechi zake mbili za mwisho, anaanza kupamba moto kama ule uliomfanya awe Mfungaji Bora katika Kombe la Dunia mwaka 2006. Pia, uwezo wake wa kufunga magoli ya vichwa na udhaifu wa ngome ya Spain kwenye mipira ya juu ndio silaha kubwa ya Ujerumani.
Kumkosa David Villa, ambae ndie anaongoza kufunga magoli EURO 2008, kutamfanya Fernando Torres awe mshambuliaji pekee akisaidiwa na viungo Fabregas na Iniesta.Hata hivyo karata ya trufu ya Spain ni mshambuliaji Daniel Guiza ambae n mfungaji bora wa La Liga huko Spain na ambae bila shaka ataingizwa kipindi cha pili.

DAVID VILLA KUIKOSA FAINALI!
Mshambuliaji wa Spain, David Villa, ambae ndie anaongoza kwa kufunga magoli kwenye Fainali za EURO 2008, hatocheza mechi ya fainali dhidi ya Ujerumani baada ya kuumia musuli za pajani kwenye mechi ya Nusu Fainali ambayo Spain waliipiga Urusi 3-0.

**********************************************************************************
THURAM ana tatizo la moyo!

Veterani wa Ufaransa, Lilian Thuram, ambae aliiwakilisha Ufaransa EURO 2008 na kutangaza kung'atuka timu hiyo mara tu baada ya kutolewa nje ya mashindano hayo walipofungwa 2-0 na Italy, ametangaza ana ugonjwa wa moyo.
Thuram, mwenye umri wa miaka 36, ambae alikuwa kwenye harakati za kuhama Barcelona na kujiunga na PSG ya Ufaransa, amesema amegundulika na ugonjwa kama ule uliomuua kaka yake aliefariki akicheza mpira wa vikapu.
Thuram alianzia kucheza soka la kulipwa klabu ya Monaco mwaka 1990 na alihamia Italy mwaka 1996 alikochezea timu za Parma na Juventus kisha kujiunga na Barcelona mwaka 2006.
Thuram alieiwakilisha Ufaransa mara 142, na ambae ndie mwenye rekodi ya kucheza mechi nyingi timu hiyo, alinyakua Kombe la Dunia 1998 na EURO 2000 akiwa na Ufaransa.


ADEBAYOR: ''nikihama klabu itanufaika!''

Mshambuliaji wa Arsenal Emmanuel Adebayor amekiri hajui atakuwa klabu ipi msimu ujao ingawa anasema ikiwa Arsenal italipwa Pauni milioni 50 wakati wamlinunua yeye kwa Pauni milioni 10 tu bila shaka klabu inapata faida.
Nyota huyo aliefunga goli zaidi ya 30 msimu uliopita alinunuliwa toka Klabu ya Monaco kwa dau la Pauni milioni 7 na siku za karibuni ameonekana kuwa na kauli kigeugeu hasa baada ya Inter Milan kutamka mchezaji huyo ndie yupo nambari wani kwenye listi ya wachezaji wanaotaka kuwasajili.

*********************************************************************************

MSHAMBULIAJI ELMANDER WA SWEDEN ATUA BOLTON
Johan Elamander, miaka 27, alieichezea Sweden kwenye EURO 2008, ametua Bolton Wanderers akitokea Toulouse ya Ufaransa.
Meneja wa Bolton Greg Megson amethibitisha taarifa hizo na kuongeza mchezaji wa kimataifa wa Norway Daniel Braaten atahama Bolton kwenda Toulouse.

*********************************************************************************

MAN CITY WAMSAINI MBRAZIL JO.

Klabu ya Manchester City imemsaini Mbrazil Jo kutoka CSKA Moscow ya Urusi kwa Pauni milioni 19.

Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 21 aliichezea Timu ya Taifa ya Brazil Juni, 2006 kwenye mechi ya ufunguzi wa Uwanja wa Wembley dhidi ya Timu ya Taifa ya Uingereza.

Jo amefunga goli 30 katika mechi 53 alizochezea CSKA Moscow na anategemewa kusaini mkataba wa miaka minne.

Thursday 26 June 2008

FAINALI: GERMANY V SPAIN!


SPAIN WAIBUGIZA URUSI 3-0!


Uhispania wakicheza kandanda safi hasa baada ya kuingizwa nyota wa Arsenal Cesc Fabregas baada ya kutolewa David Villa katika dakika ya 34 na hasa kipindi cha pili waliwashindilia Urusi 3-0 magoli yote yakipatikana kipindi hicho cha pili.
Xavi alifunga bao la kwanza dakika ya 50 baada ya kazi nzuri ya Iniesta na Fabregas alimtengenezea vizuri Danny Guiza aliefunga bao la pili dakika ya 73. Na ni Fabregas tena aliepika bao la tatu katika dakika ya 82 lililofungwa na David Silva.
Ni ukweli kabisa alieleta ushindi ni Cesc Fabregas kwani ndie alieonekana dhahiri akiiunganisha timu kwa ubora wa hali ya juu kabisa!
Sasa Uhispania itakwaana na 'MASHINE YA KIJERUMANI' kwenye FAINALI hapo Jumapili uwanjani ERNST HAPPEL STADION mjini Vienna, Austria.
Russia: Akinfeev, Aniukov, Vasili Berezutsky, Ignashevich, Zhirkov, Semak, Zyryanov, Semshov (Bilyaletdinov 56), Saenko (Sychev 57), Pavluchenko, Arshavin.
Akiba: Gabulov, Malafeev, Yanbaev, Alexei Berezutsky, Adamov, Ivanov, Shirokov, Bystrov.
Kadi: Zhirkov, Bilyaletdinov.
Spain: Casillas, Sergio Ramos, Marchena, Puyol, Capdevila, Iniesta, Xavi (Alonso 69), Senna, Silva, Villa (Fabregas 34), Torres (Guiza 69).
Akiba: Palop, Reina, Albiol, Fernando Navarro, Santi Cazorla, Sergio Garcia, Arbeloa, Juanito, De la Red.
Magoli: Xavi 50, Guiza 73, Silva 82.
Watazamaji: 50,000
Refa: Frank De Bleeckere (Belgium).


LIPPI ATEULIWA TENA KUWA MENEJA WA ITALY
Marcello Lippi alieiongoza Italia kuchukua Kombe la Dunia mwaka 2006 huko Berlin, Ujerumani amechaguliwa tena kuwa Meneja wa Italy kuchukua nafasi ya Roberto Donadoni alieachia ngazi kufuatia Italy kutolewa kwenye Robo Fainali ya EURO 2008 na Spain kwa penalti 4-2 baada ya dakika 120 za mchezo kuwa suluhu 0-0.
Lippi, umri miaka 60, hajafanya kazi yeyote tangu alipojiondoa madarakani mara baada ya Italy kunyakua Kombe la Dunia huo mwaka 2006.



LIGI KUU UINGEREZA YAMTEUA REFA 'MTOTO'!
Bosi wa Marefa nchini Uingereza Keith Hackett ametangaza kumchagua Stuart Attwell, mwenye umri wa miaka 25, kuwa miongoni mwa Marefa watakaochezesha LIGI KUU UINGEREZA msimu wa 2008/9 unaoanza tarehe 16 Agosti 2008.
Keith Hackett amethibitisha Refa huyo ndie atakuwa Refa mdogo kupita wote kuchezesha LIGI KUU. Refa huyu aliaanza kazi ya urefa mwaka 1998 na mwaka 2007 alipata promosheni na kuingizwa kwenye Listi ya Marefa wa Taifa huko Uingereza.

NANI KUINGIA FAINALI KUPAMBANA NA ‘MASHINE YA KIJERUMANI’?
LEO: NUSU FAINALI- SPAIN V RUSSIA!
Andrei Arshavin wa Urusi ameibuka na kuwa lulu kwenye michezo ya EURO 2008 hasa baada ya kuiongoza Urusi kuibamiza Uholanzi 3-1 kwenye Robo Fainali na kuifungisha virago Sweden 2-0 kwenye mechi ya KUNDI D.
Kama leo, kwenye mechi ngumu ya Nusu Fainali dhidi ya Uhispania, atafanikiwa kuwa shujaa kwa kuiongoza Urusi kuingia fainali kupambana na ‘MASHINE YA KIJERUMANI’ basi, bila shaka, ataibuka na tuzo ya Mchezaji Bora wa EURO 2008.
Lakini wengi wanashangazwa mbona kabla ya michuano hii dunia ilikuwa haijamskia huyu nyota Andrei Arshavin mwenye miaka 27? Warusi wanajibu haraka kwamba kosa ni kuwa katika miaka ya hivi karibuni Urusi ilikuwa haina mafanikio kwenye mechi za kimataifa ingawa wao walimtambua Andrei Arshavin ni moto tangu yuko mdogo.
Leo Andrei Arshavin ana kibarua kikubwa kwani kwanza anakutana na Uhispania timu ambayo tayari ishaifunga Urusia kwenye michuano hii ilipobamizwa 4-1 kwenye mechi za makundi katika kundi lao KUNDI D ingawa Andrei Arshavin hakucheza mechi hiyo kwani alikuwa kafungiwa. Pili timu ya Uhispania imesheheni mastaa kama vile Torres, Villa, Fabregas nk ambao wanatambulika dunia nzima.
Vikosi vya timu hizi mbili havina majeruhi wala athari za kufungiwa wachezaji.
Refa kwenye mechi hii ni Mbelgiji Frank De Bleec
kere.



Germany 3-2 Turkey
GOLI DAKIKA YA MWISHO LAWAUA WATURUKI!
RADI ZAKATISHA MATANGAZO!
Beki wa kushoto Philipp Lahm alifunga bao la ushindi katika dakika ya mwisho ya mchezo na kuwaingiza Ujerumani FAINALI ya EURO 2008 ambapo watakutana na Uhispania au Urusi wanaocheza leo.
Uturuki iliyoonekana dhahiri ni timu bora ilipata bao la kwanza dakika ya 22 lililofungwa na Uqur Boral lakini Ujerumani ikasawazisha dakika ya 27 kwa goli la Schweinsteiger.
Miroslav Klose akafunga kwa kichwa goli la pili la Ujerumani kwenye dakika ya 79 na Mturuki Senturk akasawazisha dakika ya 86.
Wengi wakiamini dakika za nyongeza 30 zitachezwa, Wajerumani walicheza soka safi lililoishia kwa beki wa kushoto Philipp Lahm kufunga kwenye dakika ya 89.
Hakika Waturuki walikufa kishujaa kwani mbali ya kuwa na majeruhi wengi na wachezaa kadhaa kufungiwa ilikuwa wazi walitawala mchezo. Pengine bahati haikuwa yao kwani ‘Mwingereza’, mchezaji wa zamani wa Sheffield United Colin Kazim-Richards ambae siku hizi hujiita Kazim Kazima baada ya kuamua kuchezea Uturuki kwa kuwa na damu ya Kituruki, alipiga shuti dakika ya 12 lililompita Kipa Jens Lehmann na kugonga mwamba. Na tena dakika ya 22 aligonga mwamba!
Wapenzi wengi katika pembe kadhaa za dunia walikosa matangazo ya TV kwa muda baada ya radi na mvua kukatiza matangazo.
Germany: Lehmann, Friedrich, Mertesacker, Metzelder, Lahm, Hitzlsperger, Rolfes (Frings 46), Schweinsteiger, Ballack, Podolski, Klose (Jansen 90).
Akiba: Enke, Adler, Fritz, Westermann, Gomez, Neuville, Trochowski, Borowski, Odonkor, Kuranyi.
MAGOLI: Schweinsteiger 27, Klose 79, Lahm 90.
Turkey: Rustu, Sarioglu, Topal, Zan, Balta, Aurelio, Kazim-Richards (Metin 90), Altintop, Akman (Erdinc 81), Boral (Karadeniz 84), Senturk.
Akiba: Zengin, Cetin, Emre, Gungor, Nihat.
KADI: Senturk.
MAGOLI:
Boral 22, Senturk 86.
WATAZAMAJI: 40,000
REFA: Massimo Busacca (Switzerland).

Tuesday 24 June 2008

Liverpool waanza kujenga uwanja mpya
Klabu ya Liverpool imeanza ujenzi wa uwanja mpya kwa gharama ya Pauni £350 milioni jirani na Uwanja wa sasa wa Anfield.
Klabu hiyo imeruhusiwa kuanza ujenzi huku mkataba wa hati miliki ya ardhi wa miaka 999 ukiendelea kujadiliwa na serikali.
Kibali hicho kinaruhusu ujenzi wa uwanja utakaoingiza watazamaji 60,000 na kinaweza kupanuliwa kufikia watu 73,000 baadae. Ufunguzi wa uwanja huo mpya unategemewa kuwa Agosti, 2011.
Hadi sasa klabu inayoongoza kwa kuwa na uwanja mkubwa unaoingiza watu wengi ni Manchester United na uwanja wao Old Trafford ukipakia watu 76,000, Arsenal na Emirates watu 60,000, Newcastle na wa kwao St James Park watu 52,000, Manchester City na The City of Manchester Stadium watu 47,000, Liverpool na Anfield watu 45,000 huku Chelsea na Stamford Bridge yao watu 42,000.
Paul Ince atambulishwa rasmi Meneja Blackburn Rovers
Mwenyekiti wa Blackburn Rovers John Williams amemtangaza rasmi Paul Ince kuwa Meneja mpya wa klabu yake kuchukua nafasi ya Mark Hughes aliehamia Manchester City.Ince, mwenye umri wa miaka 40, amepewa mkataba wa miaka mitatu na anaweka rekodi ya kuwa Meneja wa kwanza 'mweusi' katika historia ya LIGI KUU UINGEREZA.
Blackburn Rovers ilipata kibali maalum kutoka FA, ambacho ni Chama cha Soka Uingereza, kumtumia Paul Ince bila ya yeye kuwa na LESENI YA UKOCHA YA UEFA PRO.
Leseni hii inahitajika kwa Mameneja wote wa ligi za juu za nchi nyingi Ulaya.Ili kupata leseni hii inabidi upate masomo maalum ya zaidi ya masaa 240 na kawaida huchukua mwaka mmoja kuhitimu. Mkataba wa Paul Ince na Blackburn Rovers una kipengele kwamba lazima Ince ahitimu hiyo LESENI YA UKOCHA YA UEFA PRO
Chama cha Kandanda Ureno chakanusha ripoti zinazomhusu Scolari juu ya Ronaldo!
Jana usiku Chama cha Kandanda Ureno kimetoa taarifa kupinga kauli zilizosemekana zimetolewa na Meneja wa Timu ya Taifa ya Ureno Luiz Felipe Scolari anaeachia ngazi rasmi kazi hiyo na kujiunga na Chelsea tarehe 1 Julai 2008
Taarifa hiyo inatamka: "Luiz Felipe Scolari amekataa moja kwa moja kwamba alihojiwa au kutamka chochote kuhusu Ronaldo na uvumi wa kuihama klabu yake. Anasikitika sana kuhusishwa na uongo na uvumi huu ambao unatangazwa bila kuthibitisha ukweli uko wapi’’
JUMATANO, JUNI 25: NUSU FAINALI YA 1: Germany v Turkey
UWANJA: St Jakob-Park, Basel, SWITZERLAND

Kocha wa Ujerumani Joachim Low amesema kiungo Torsten Frings anaweza kucheza mbali ya kuvunjika mbavu katika mechi za makundi na kuikosa mechi ya ROBO FAINALI ambayo waliifunga Ureno. Ukiacha hilo, Ujerumani wana kikosi chao kamili bila ya majeruhi au athari nyingine.
Uturuki wanakabiliwa na majeruhi wengi pamoja na wachezaji kadhaa kufungiwa kwa kuwa na kadi na hivyo wanaweza wakawa na kikosi chenye wachezaji 13 tu wa mbele kuwakabili Ujerumani.
Juhudi zao za kujaribu kukata rufaa ili Kipa nambari wani na Nahodha wao Volkan Demirel afunguliwe baada ya kufungiwa mechi mbili baada ya kadi nyekundu kwenye mechi na Czech Republic zimekataliwa na UEFA.
Meneja wa Uturuki Fatih Terim amesema inawezekana akamchezesha kipa wa tatu wa akiba Tolgan Zengin kwenye mechi hii: "Anaweza kuingia mwisho kabisa wa mechi kwenye ulinzi kama beki wa nyuma kabisa au mshambuliaji wa mbele kabisa."
Uso kwa uso
Ujerumani na Uturuki washakutana mara 17 huku Ujerumani akishinda mechi 11 na kupoteza 3 tu.
Waturuki hawajafungwa na Ujerumani katika mechi tatu zao za mwisho kukutana ambazo walishinda mbili na kutoka droo moja.
Ushindi wa mwisho wa Ujerumani dhidi ya Waturuki ulikuja Mei 1992 waliposhinda 1-0 kwenye mechi ya kirafiki.
Mara ya mwisho kukutana kwenye mashindano makubwa ilikuwa kwenye Kombe la Dunia mwaka 1954 nchini Uswisi na wakati huo ikiwa inaitwa Ujerumani Magharibi [wakati huo kulikuwa na Ujerumani mbili-moja Magharibi na nyingine Mashariki] na Ujerumani ilishinda 4-1 and 7-2 katika mechi mbili za mashindano hayo.
Mechi ya mwisho kabisa kukutana ni katika mechi ya kirafiki Oktoba 2005 mjini Instanbul, Uturuki na Uturuki walishinda 2-1.
Waamuzi
Refa: Massimo Busacca, Wasaidizi: Matthias Arnet, Stephane Cuhat (Wote kutoka Uswisi),
Refa wa akiba: Peter Frojdfeldt (Sweden)
Real wang’aka hawawezi kuvunja benki kwa Ronaldo!
Nae Carlos Queiroz adai: "Manchester United ni spesho, Ronaldo atabaki!!"
Ramon Calderon, Rais wa Real Madrid, amegeuka na kudai hawawezi kuvunja benki ili kumnunua Ronaldo.
Imekuwa ikivumishwa kwamba Real wako tayari kuvunja rekodi ya dunia ya kumnunua mchezaji na kuwalipa Manchester United Pauni za Kiingereza milioni 80 ili kumnunua Cristiano Ronaldo.

Real kwa sasa ndio wanaoshikilia rekodi hiyo ya kumnunua mchezaji kwa bei ghali sana pale walipomnunua Zinedine Zidane mwaka 2001 kwa Pauni za Kiingereza milioni 46.
Hata hivyo Ramon Calderon amekataa na kudai hamna ‘ishu’ ya Ronaldo kwa sababu kwanza Manchester United hawataki kumuuza na pili wao hawawezi kumnunua mchezaji yeyote yule kwa dau hilo.
Wakati huohuo, Wareno wawili wenzake Ronaldo ambao wako pamoja nae Manchester United wameibuka na kumsihi abaki Manchester.
Mchezaji Nani amekaririwa akisema: ‘Ni dhahiri nataka abaki. Alinisaidia sana nilipowasili Man U.’
Nae Meneja msaidizi wa Man U Carlos Queiroz ana matumaini kuwa mapenzi ya Klabu ya Manchester United kwa Ronaldo yatamfanya abakie Old Trafford klabu aliyojiunga mwaka 2003 akitokea Sporting Lisbon ya Ureno.
"Manchester United ni spesho," Queiroz aliiambia Redio ya Kireno iitwayo Renascenca. "Kwa sababu hiyo tunajua namna ya kumzunguka na kumfariji Cristiano kwa upendo na kila hali inayobidi na hali hii hawezi kuipata kwingine kokote.’

Italy wamtimua Donadoni!!!!!!
Shirikisho la Kandanda la Italia limemtimua Meneja wa Timu ya Taifa ya Italia Roberto Donadoni kufuatia timu hiyo kutolewa kwenye Nusu Fainali ya EURO 2008 na Uhispania.
Uhispania ilishinda kwa penalti 4-2 baada ya dakika 120 za mchezo kuwa suluhu 0-0.
Inasemekana Marcello Lippi alieiongoza Italia kuchukua Kombe la Dunia mwaka 2006 huko Berlin, Ujerumani kama Meneja atarudia tena kazi yake aliyoiacha tangu wakati huo.
WATURUKI WANA MOYO WA KIJERUMANI: Ballack akiri!
Nahodha wa Ujeruman Michael Ballack anaamini wapinzani wao kwenye NUSU FAINALI ya EURO 2008 itakayochezwa kesho Uturuki wana moyo wa kijasiri wa Kijerumani na hivyo mechi hiyo itakuwa ngumu sana kwao.
Ingawa Ujerumani wanapewa nafasi kubwa ya kushinda, Ballack ambae ni mchezaji wa Klabu ya Chelsea anakiri: "Wana moyo, imani na umadhubuti wa Kijerumani! Hawakati tamaa na ndio maana wamefunga magoli mengi mwishoni mwa mechi –kitu ambacho ni Ujerumani pekee hukifanya katika mashindano makubwa."
Hata hivyo kikosi cha Uturusi kina hali ngumu sana na huenda wakalazimika kumchezesha Kipa wa akiba Tolga Zengin kama mchezaji wa mbele kutokana na wachezaji sita muhimu kuwa majeruhi wakiwa pamoja na mshambuliaji nyota Nihat Kahveci wakati Kipa nambari wani Volkan Demirel, Tuncay Sanli, Arda Turan na Emre Asik wamefungiwa.

***********************************************************************************
Ronaldo aenda likizo na kuacha fumbo!
Mapaparazi, hasa wa Kihispania wanaoshabikia Ronaldo kuhamia Real Madrid, wamepigwa bumbuwazi baada ya nyota huyo kuingia mitini na kwenda likizo ya wiki tatu kuanzia jana bila ya ufafanuzi kuhusu hatma yake.
Wengi walitegemea jana kutakuwa na habari za kuvunja shoka lakini walipigwa butaa waliposikia Ronaldo sasa anaenda mapumzikoni.
Wakati Ronaldo anaanza likizo ya wiki tatu mapaparazi sasa watawaandama Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson na Mkurugenzi Mkuu wa klabu David Gill mara tu watakaporudi toka likizo zao wiki ijayo ili kudadisi mambo.

Monday 23 June 2008


WAAMUZI WA NUSU FAINALI NA FAINALI Euro 2008 WATAJWA!
UEFA imetangaza waamuzi watakaochezesha mechi za NUSU FAINALI na FAINALI za EURO 2008.
Tangu mashindano haya yaanze UEFA ilikuwa ikipanga Refa na Wasaidizi wake wakitoka nchi moja katika kila mechi na utaratibu huu ndio utakaoendelea katika mechi zilizobaki.
NUSU FAINALI
JUMATANO June 25 Germany v Turkey
Refa: Massimo Busacca,
Wasaidizi: Matthias Arnet, Stephane Cuhat (Wote kutoka Uswisi),
Refa wa akiba: Peter Frojdfeldt (Sweden)
ALHAMISI June 26 Russia v Spain
Refa: Frank De Bleeckere,
Wasaidizi: Peter Hermans, Alex Verstraeten (Wote kutoka Ubelgiji),
Refa wa akiba: Kyros Vassaras (Greece)
JUMAPILI June 29 FAINALI
Refa: Roberto Rosetti,
Wasaidizi: Alessandro Griselli, Paolo Calcagno (Wote kutoka Italia),
Refa wa akiba: Peter Frojdfeldt (Sweden)

Pele aporwa na vibaka!
Pele, Mbrazil veterani na nyota maarufu sana duniani, alitishiwa bastola na vibaka na kuporwa mkufu wa dhahabu, simu na saa karibu na mji wa Santos, Brazil tarehe 13 Juni 2008.
Pele, jina kamili Edison Arantes do Nascimento, mwenye miaka 67 alikuwa abiria kwenye gari dogo akielekea nyumbani kwake na gari hiyo ikalazimishwa kusimama na genge la vibaka wasiopungua 10 waliokuwa wamebeba bastola na visu.
Vibaka hao baada ya kumpora ndio wakagundua kumbe ni Pele wakaamua kumrudishia baadhi ya vitu.
Pele, ambae aliisaidia sana Brazil kunyakua Vikombe vitatu vya Dunia kati ya vitano ambavyo inavyo, hakuripoti tukio hilo Polisi.
Taifa la Brazil linamtambua kisheria Pele kama ni ‘HAZINA YA TAIFA’ na Kamati ya Olympiki ya Dunia mwaka 1999 ilimpigia kura kwamba ndie MWANAMICHEZO BORA WA KARNE!

Spain 0-0 Italy

Italia wang'oka kawa penalti 4-2

Spain kukutana tena na Urusi!

Spain wamewatoa Italy 4-2 kwa penalti na kuingia NUSU FAINALI ya EURO 2008 kucheza na Urusi ikiwa ni mara ya pili kwa Spain na Urusi kukutana katika mashindano haya.
Mechi ya kwanza ilikuwa kwenye KUNDI D wakati Urusi ilipobamizwa 4-1 ingawa Warusi wanaweza kujipa moyo kwamba katika mechi hiyo staa wao mkubwa Andrei Arshavin hakucheza kwani alikuwa kafungiwa.
Mechi kati ya Spain na Italy ilikuwa ngumu na nafasi zilikuwa chache na hata dakika 120 hazikutoa mshindi.
Katika penalti Kipa wa Spain Iker Casilla alikuwa shujaa kwa kuokoa penalti za Daniele de Rossi na Antonio di Natale.
Ushindi huu wa Spain utakuwa mtamu sana kwa Wahispania hasa wakikumbuka katika mashindano makubwa matatu yaliyopita, yaani Kombe la Dunia mwaka 1986 na 2002 na Euro 1996, walitolewa Robo Fainali - na mara zote kwa penalti na tarehe ikiwa hiyohiyo moja, yaani tarehe 22 Juni kama ya jana!

NUSU FAINALI
JUMATANO
25 JUNI
UJERUMANI V UTURUKI
ALHAMISI
26 JUNI
URUSI V SPAIN
FAINALI
JUMAPILI
29 JUNI
MSHINDI WA UJERUMANI V UTURUKI V URUSI V SPAIN


Sunday 22 June 2008




Blackburn wamteua Paul Ince kuwa Meneja


Blackburn Rovers imetangaza kuwa bosi wa MK Dons Paul Ince ndie atakuwa Meneja wao mpya kuchukua nafasi ya Maark Hughes aliehamia Manchester City.
Ince, mwenye umri wa miaka 40, amepewa mkataba wa miaka mitatu na anaweka historia ya kuwa Meneja wa kwanza 'mweusi' katika historia ya LIGI KUU UINGEREZA
.

WAFUNGAJI BORA NA MAGOLI WALIYOFUNGA
4 David Villa - Spain
3 Hakan Yakin - Switzerland
3 Roman Pavlyuchenko - Russia
3 Lukas Podolski - Germany
2 Arda Turan - Turkey
2 Andrei Arshavin - Russia
2 Michael Ballack - Germany
2 Zlatan Ibrahimović - Sweden
2 Ivan Klasnić - Croatia
2 Nihat Kahveci - Turkey

KIKOSI CHA UTURUKI MASHAKANI
Kipa wa akiba huenda akacheza mbele

UEFA wametamka hawawezi kuwaruhusu Uturuki kuita wachezaji wapya kuja kwenye EURO 2008 kufuatia timu yao kukabiliwa na majeruhi wengi na wengine kufungiwa mechi kutokana na kadi.
Hali hii inamaanisha huenda Uturuki wakalazimika kumchezesha Kipa wa akibaTolga Zengin kama mchezaji wa mbele.
UEFA imesisitiza kanuni zinatamka wazi huwezi kuita mchezaji mpya baada ya mechi ya kwanza ya EURO 2008 na wameongeza wangeita kikao cha dharura pale tu timu ingebakiwa na wachezaji wanane tu.
Uturuki wanakutana na Ujerumani Nusu Fainali siku ya Jumatano.
Meneja Fatih Terim amesema wachezaji sita muhimu ni majeruhi wakiwa pamoja na mshambuliaji nyota Nihat Kahveci wakati Kipa nambari wani Volkan Demirel, Tuncay Sanli, Arda Turan na Emre Asik wamefungiwa.
Scolari – Ronaldo ana ndoto na Real
Bosi mpya wa Chelsea anategemea nyota wa Man United kuhama
Luiz Felipe Scolari amesisitiza Manchester United hawawezi kumzuia Cristiano Ronaldo asihamie Real Madrid.
Kocha huyo anaeiacha Timu ya Taifa ya Ureno Julai 1 na kuhamia Chelsea wapinzani wa Man United kwenye LIGI KUU anadai anamfahamu vizuri Ronaldo na ndio maana amesisitiza Ronaldo atahama.
Kauli hii ya Mbrazil huyo inadhirisha zaidi kile wanachoamini Man United kuwa Scolari ni mchochezi mkubwa anaemshawishi Ronaldo kuhama ili kuibomoa Man United ili yeye apate upinzani hafifu akiwa kwenye timu yake mpya ya Chelsea.
Mpaka sasa Man United wamesisitiza Ronaldo hauzwi na hawaingia kwenye majadiliano na yeyote kuhusu kuuzwa nyota huyo
.

Netherlands 1-3 Russia
Urusi, wakiongozwa na Meneja Mholanzi Guus Hiddink, jana waliwaendesha mchakamchaka Uholanzi timu iliyodhaniwa bora kwenye EURO 2008 na kuwabwaga kwa mabao 3-1 kwenye kandanda iliyochezwa dakika 120.
Roman Pavlyuchenko aliwawafungia Urusi bao la kwanza lakini Ruud van Nistelrooy alisawazisha na mpira ukingia dakika za nyongeza.
Dimitri Torbinski na Andrei Arshavin wakahakikisha ushindi kwa Urusi kwa kupachika bao la pili na la tatu.
Bosi wa Urusi Guus Hiddink aliisifia timu yake: "Sitaki kutumia maneno makubwa. Lakini ni maajabu. Nasikia fahari kwa vijana wangu. Kwa nguvu, utaalam na mbinu tuliwazidi Waholanzi wenzangu!'
MECHI YA LEO:
ROBO FAINALI: Spain v Italy
Kocha wa Uhispania Luis Aragones atakirudisha kikosi chake cha kwanza kwenye mechi hii ya Robo Fainali dhidi ya Italia alichokipumzisha kwenye mechi ya kukamilisha ratiba ambayo waliwafunga Ugiriki 2-1.
Italia wana tatizo kubwa la kuwakosa viungo Gennaro Gattuso na Andrea Pirlo ambao wote wana kadi na hawaruhusiwi kucheza mechi hii. Badala yake Alberto Aquilan na Massimo Ambrosini wanategemewa kuanza huku Daniele De Rossi na Simone Perrotta pia wana nafasi kubwa ya kucheza.

NUSU FAINALI
JUMATANO
25 JUNI
UJERUMANI V UTURUKI
ALHAMISI
26 JUNI
URUSI V SPAIN/ITALIA
Powered By Blogger